Search
Close this search box.

Uhodari wa Mwanamke ni Zaidi ya Siku ya Wanawake Duniani

Kama jamii tunawajibu wa kuwajibika na kuhakikisha mwanamke anajivunia kuwa mwanamke. Kama ambavyo wanawake wametutunza na kuzitunza familia zetu, nasi kama jamii tunajukumu adhimu la kuwatunza.

subscribe to our newsletter!

Shamrashamra, sherehe na shangwe za siku ya wanawake sasa zimeshapoa. Kama kulikuwa na kivumbi, sasa tuko kwenye ule wakati wa shwari, kwani lile vumbi limeshatua na hali imetulia tuli.

Zile zawadi za kuharibika ama zimeshaharibika au zimeshatumika; vya kuliwa vimeshaliwa na kutoka; picha za tambo zimeshatumwa zote na zimesharudiwa; nyimbo zilizotungwa zimeshapumzishwa kusubiri mwakani na siku nyinginezo za maadhimisho ya kufanania. Wale walioadhimisha kwa miradi, nao watakuwa wameshaandika ripoti zao na kuzituma kwa mabwana wakubwa.

Zaidi ya wiki moja sasa imeshapita, tumerudi kwenye hali ya ukawaida. Vitenge na sare zimerudi masandukuni. Ikiwa sasa ile mihemko ya huba, sifa na pongezi pongezi imetulia, pengine ni muda muafaka wa kutafakari kuhusu siku ya wanawake na kutathmini kuhusiana na hali na mustakabali wa mwanamke nchini.

Haihitaji kuwa mwanafalsa, au mwanasayansi, kujua kwamba mwanamke ni chanzo na kiini cha jamii; yaani mwanamke ndiyo msingi wa jamii. Haihitaji kuwa mwanazuoni kiimani, au kidunia, ili kukubaliana nami kwamba, mwanamke ni nguzo kuu ya maisha ya mwanadamu katika sayari hii.

Je, si kweli sote tumetoka kwa mwanamke? Si kweli sote, kama si wengi wetu, tumelelewa na kukuzwa na mwanamke? Hivyo basi, si kweli sote kama jamii, msingi wetu ni uzao wa mwanamke?

SOMA ZAIDI: ‘Siyo Uhuni’: Wanawake Jasiri wa Kizanzibar Walioingia Kwenye Sekta ya Uongozaji Watalii

Ieleweke, hata hivyo, kwamba sina maana kwamba mwanaume hana nafasi katika haya ninayoyasema, hapana! Wala nisingependa kuingia kwenye mjadala wa namna hiyo; lengo langu kuu ni kutukumbusha tu hoja ambayo ni dhahiri kabisa kwamba nguzo kuu, na siyo ya pekee, ya maisha ya mwanadamu, na jamii kwa ujumla, ni mwanamke.

Uhodari wa mwanamke

Ni wazi kwamba wengi wetu katika kuiadhimisha siku hii ya mwanamke tuliipa uzito kwa sababu hizi hizi za kuashiria ukuu, umuhimu na uhodari wa mwanamke, katika maisha ya mwanadamu na ustawi wa jamii.

Pamoja na hayo, tulimsherehekea mwanamke kwa uzuri wake wa kimaumbile, kimatendo na kimienendo; ujasiri, uchapakazi na umadhubuti wake kama mpambanaji; uwezo na umahiri wake wa kumudu nafasi ya ulezi na shughuli za utafutaji; werevu, weledi na ubunifu wake katika maendeleo; na upendo, uwezo na upekee wake katika kuhakikisha ustawi wa jami.

Hakika, Machi 8 ni siku muhimu sana. Ni siku ambayo tunapaswa kuisherehekea na kuzisherehekea kofia zote, zinazoashiria nafasi na majukumu ya mwanamke. Tarehe hii pia ni muhimu katika kukumbuka na kuenzi karne na karne ya mapambano ya wanawake, katika mapambano dhidi ya madhila ya unyonyaji, ukandamizaji na ubaguzi.

Siku hii ya wanawake duniani inalenga kuendeleza mapambano ya yaliyoasisiwa na kushamiri miaka ya mwanzo ya 1900; na vivyo hivyo yanatusisitiza kuendelea kudai haki sawa kwa wote katika kila nyanja – kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Madhila 

Pamoja na kwamba tumepiga hatua kubwa, tangu wanawake kukatazwa “kisheria” kupiga kura, kwenda shule, kumiliki mali, kufanya kazi, kutoka eneo moja kwenda eneo lingine, na kadhalka, bado mwanamke wa kileo anakabiliwa na changamoto lukuki.

SOMA ZAIDI: Siku ya Wanawake Duniani: Kesho Yenye Usawa Inaanza na Leo Yenye Ujumuishi

Nikiwa kama mwanamke mwanasiasa, ninayo mengi ninayoweza kueleza na kushuhudia kuwa ninakabiliana nayo; nayo hayo hayanikabili mimi tu. Hali ni hivyo hivyo kwa wanawake wenzangu, wengi, kama siyo wote, tuliopo katika siasa.

Tunaonekana kama vyombo vya starehe, tunapuuzwa na kuchukuliwa kama watu tusioelewa mambo na hata kuonekana wahuni katika jamii zetu. Unyanyapaa tunaokabiliana nao haulezeki!

Si mitandaoni, majukwaani au mitaani, hatuna tunakopata ahueni. Kote huko, sisi tunachukuliwa kama raia nambari mbili au vikaragosi. Isivyo bahati, hali iko hivyo hivyo kote katika jamii zetu na katika kila nyanja. Hakuna penye ahueni kwa mwanamke.

Cha kustaajabisha, wakati madhila dhidi ya wanawake yalipokuwa yakitokea zamani tulisingizia ujinga na tamaduni duni; leo hii, licha ya jamii kuwa imeerevuka kuliko maelezo na kuweza kuboresha tamaduni zake, bado wanamke yuko kwenye hatari kila leo kuliko jana.

Katika ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2022, iliyochapishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wanawake wanaelezwa kuwa asilimia 33 ya wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ndiyo kundi la pili linaloathiriwa sana na ukatili, nyuma ya kundi la watoto, ambalo linaathiriwa kwa asilimia 47.

SOMA ZAIDI: Wanawake Wajitosa Kwenye Sekta ya Madini Licha ya Changamoto Wanazopitia

Wakati ikielezwa kuwa mwanamke ni muathirika wa ukatili, takwimu za Serikali zinaonesha hali kuzidi kuwa tete kwa mwanamke kutokana na kuendelea kuwepo kwa uhalifu wa makosa dhidi ya binadamu, maadili ya jamii na kuwania mali. 

Isitoshe uhalifu huo umeongezeka kutoka kuwa na matukio 43,771, yaliyoripotiwa kwa mwaka 2021/22, hadi kuwa na matukio 45,455, yaliyoripotiwa katika kipindi cha cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023.

Takwimu hizo zinaenda mbele na kueleza kuwa makosa hayo yameongezeka kutokana na watu kujichukulia sheria mkononi, migogoro ya ardhi na mirathi, ubakaji, ulawiti, mmomonyoko wa maadili, tamaa ya mapenzi na imani za kishirikina. 

Bila shaka, kwa kurejea tathmini ya ripoti ya LHRC, ongezeko hili la uhalifu na makosa haya, ni dhahiri linawaathiri zaidi wanawake na watoto kuliko kundi lingine lolote kwenye jamii.

Wajibu wa jamii

Kama jamii tunawajibu wa kuwajibika na kuhakikisha mwanamke anajivunia kuwa mwanamke. Kama ambavyo wanawake wametutunza na kuzitunza familia zetu, nasi kama jamii tunajukumu adhimu la kuwatunza.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kujenga Jamii Yenye Mtazamo Chanya Kwa Wanawake wa Makundi Maalumu?

Hapa simaanishi kuwatunza kwa chocolate na mitoko maalum, au date; simaanishi kuwatunza kwa fedha na vito na vitu vya thamani; simaanishi kuwatunza kwa mashairi na nyimbo; vivyo hivyo simaanishi kuwatunza kwa marashi, vitenge, abaya, batiki. 

Nimaanisha kuwatunza kwa hayo niliyoyataja pekee inapowezekana, bali kuwatunza kwa kuhakikisha wanapata na kuzifurahia haki zao.

Tunajukumu, kama jamii, kuhakikisha kwamba tunakabiliana na, miongoni mwa mambo mengine, vitendo vya ukatili wa kiuchumi dhidi ya wanawake, vilivyoelezwa kwenye ripoti ya LHRC: wasiwasi kuhusu upatikanaji, matumizi, na umiliki wa ardhi hususani kwa wanawake wanaoishi vijijini; changamoto ya wanawake na wazee kunyang’anywa mali na wanawake kuzuiwa kutumia kipato cha familia, hasa maeneo ya vijijini; wajane kutolewa kinguvu nyumbani, kufukuzwa na kunyang’anywa mali; wanawake na wasichana kunyimwa haki ya kurithi na kumiliki mali… Orodha ni ndefu!

Mapambano ya mwanamke kutaka uhuru kamili kiuchumi; usawa na haki katika kila nyanja; na kutokomezwa kwa ukatili wa kijinsia katika sura zake zote, si jukumu la wanawake pekee yake. Ni jukumu la jamii kwa ujumla na Machi 8 inapaswa, miongoni mwa mambo mengine, kutukumbusha haya.

Hata hivyo, licha ya umuhimu wa siku hiyo na pamoja kwamba siku ya wanawake duniani inatoa fursa ya kipekee ya kusherehekea mchango wa wanawake katika jamii; ni muhimu tukakumbuka kwamba uhodari wa mwanamke huzidi mipaka ya siku hiyo moja.

SOMA ZAIDI: Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’

Binafsi, nikimtizama mwanamke ninaona ni mtu anayepaswa kusherehekewa, kuzingatiwa na kuthaminiwa na thamani yake kuonekana siku zote. Kwa fahari kubwa, ninamuona mwanamke kama kito cha thamani kinachopaswa kutunzwa na kuheshimiwa kila siku.

Pamoja na kuthamini pongezi na yote yaliyofanyika Siku ya Wanawake Duniani na wiki husika; ninasisitiza kwa heshima na upendo ulio mkuu kabisa, tunapaswa kudumisha thamani ya mwanamke kila siku. Kwa kufanya hivyo, tunajenga jamii yenye usawa na haki kwa wote – wanaume kwa wanawake.

Kwa umoja na heshima kwa wanawake kila mahali!

Monalisa Joseph Ndala ni mwanachama wa ACT Wazalendo na mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia monalisandalla@gmail.com au X kama @monalisandala. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *