The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watendaji Wasio Waadilifu Watajwa Kuchochea Migogoro ya Ardhi Zanzibar

Ingawaje Rais Mwinyi ameahidi kuunda tume kushughulikia kesi za migogoro ya ardhi visiwani humo, Wazanzibari ambao wamekuwa wakihangaika na kesi hizo miaka nenda rudi hawana imani kama tume hiyo itakuwa na msaada kama itaundwa na watendaji wale wale ambao uadilifu wao ni wa kutiliwa mashaka.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kwa Salma Salum Khalfan, mkazi wa Wete, Pemba, hatua ya Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi kutangaza kuunda tume maalum ya kushughulikia kesi za ardhi visiwani humo haitakuwa na faida yoyote kama itaundwa na Wazanzibari wale wale anaodai wanakosa uadilifu kwenye utendaji wao wa kazi.

Dk Mwinyi alifichua nia yake hiyo mnamo Februari 28, 2022, wakati wa mkutano wake wa kila mwisho wa mwezi na waandishi wa habari kufuatia swali kutoka kwa mwandishi wa habari aliyetaka kujua mipango ya Serikali ya kukabiliana na kesi za muda mrefu zinazohusisha masuala ya ardhi.

“Kwenye [sekta ya] ardhi kuna mambo mengi ya hovyo,” alisema Rais huyo wa awamu ya nane wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Mambo mengi mabaya yapo. Kuna watu wamenyang’anywa [ardhi] wenye haki. Kuna watu waliopewa [ardhi] hawana haki. Kuna maeneo ya Serikali ya wazi yamegawiwa. Kuna tume tunaiunda, na hiyo tume nataka tuhakikishe kwamba inafanya kazi ya uhakika.”

Lakini kama kuna funzo moja ambalo Salma, 53, amejifunza kwenye miaka 20 ya kupigania haki yake ya umiliki wa mashamba matano yenye ukubwa kati ya ekari tatu mpaka nane yaliyopo Ukunjwi, Pemba, ni kwamba watendaji wenye uadilifu Zanzibar ni wachache sana kiasi ya kwamba hadhani Rais Mwinyi anaweza kupata watu wa kuwaweka kwenye tume hiyo.

“Labda [Rais Mwinyi] achukue watu kutoka Tanzania Bara,” Salma, ambaye licha ya Mahakama Kuu ya Zanzibar kuamuru apewe mashamba hayo bado hajayapata, anaiambia The Chanzo. “Hakutakuwa na matokeo yoyote ya maana kama tume hiyo itaundwa na Wazanzibari. Sisi Wazanzibari ndiyo tunakandamizana wenyewe kwa wenyewe. Hakutapatikana suluhu kama sisi ndiyo tutaunda hiyo tume.”

Jinamizi linalowakosesha watu usingizi

Hakuna neno bora zaidi linaloelezea migogoro inayohusisha kesi za ardhi Zanzibar zaidi ya lile la jinamizi. 

Maelfu ya Wazanzibari wanashindwa kupata usingizi kwa kutokujua hatma ya kesi zao ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miaka kadhaa kwenye ofisi mbalimbali za maaumzi bila kupatiwa ufumbuzi wa kina.

Ni ngumu sana kuongea na Wazanzibari watatu kuhusiana na kesi za ardhi visiwani humo bila kukutana na mtu ambaye si muhanga wa jambo hilo. 

Kesi za ardhi Zanzibar ni nyingi sana kiasi ya kwamba zimeongoza miongoni mwa malalamiko yaliyokabidhiwa kwa Rais Mwinyi kupitia mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama Sema na Rais Mwinyi, zikiambatana na kero za maji na umeme.

Wakati wa swali lake kwa Rais Mwinyi, mwandishi wa habari wa siku nyingi Zanzibar Salum Said Salum alimueleza mkuu huyo wa nchi kwamba kwenye Wizara ya Ardhi kuna uozo unaohitaji kusafishwa.

“Nina nyaraka zaidi ya kumi hapa [ambazo zinaonesha kwamba] kesi zinachukua miaka 24 bila kutolewa uamuzi,” alieleza Salum. “Nyumba hiyo hiyo moja, watu wa Wizara ya Ardhi wanaibadilisha namba mara nne. Kughushi kumekuwa kama mchezo wa kucheza nage katika Wizara ya Ardhi.”    

Ukosefu wa uadilifu

Jamila Mahmoud Juma ni Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) ambaye chama chake kimekuwa kikitoa msaada wa kisheria kwa wanawake wengi wanaopigania haki zao za umiliki wa ardhi visiwani humo.

Wakati wa mazungumzo na The Chanzo kwa njia ya simu hivi karibuni, Jamila, ambaye pia ni muhanga wa jaribio la kudhulumiwa ardhi yake, alibainisha kwamba kitu kikubwa walichobaini wao kama ofisi wakati wa ufuatiliaji wa kesi zinazohusiana na migogoro ya ardhi ni ukosefu wa uadilifu miongoni mwa watendaji waliokabidhiwa jukumu la kutatua kesi hizo. 

“Tumekuwa tukiishauri Serikali kuweka watu ambao ni waaminifu kwa sababu kuna watu wachache katika taasisi za Serikali ambao sio waaminifu katika kuhakikisha kwamba watu wanapata haki zao,” anasema Jamila. “[Watu hawa] wanakuwa ni wepesi wakishapewa rushwa kidogo wapo tayari kubadilisha hata hizo hati.”

The Chanzo ilimuuliza Harus Mpatani, Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), ambaye shirika lake limekuwa likipokea kesi mbalimbali zinazohusiana na migogoro ya ardhi kama anaweza kuainisha vyanzo vikuu vya migogoro ambayo imekuwa ikiripotiwa Zanzibar.

Harus alibainisha vyanzo vitatu ambavyo kwa mujibu wa utafiti wao migogoro mingi huanzia. Vyanzo vyenyewe ni kudhulumiana ardhi katika ngazi ya familia; kesi zinazohusisha wananchi na wawekezaji; pamoja na watu kukabidhiana ardhi kiholela bila ya kuingia makubaliano yoyote ya maandishi.

Tunaaminiana sana hapa

“Hapa Zanzibar tumekuwa na utamaduni wa kuaminiana sana,” anasema Harus. “Kwa hiyo, tumekuwa tukishauri kwamba kuaminiana huku ni lazima kuambatane na maandishi. Kuwepo na makubaliano ya maandishi yatakayosaidia endapo kama kutaibuka tatizo la kisheria.”

Akieleza hatua inayopaswa kuchukuliwa kuepusha migogoro hii kuendelea kutokea, Harus anashauri: “Tuendelee kuelimisha watu wetu. Tuendelee kutoa elimu kwa jamii juu ya taratibu zinazopaswa kufuatwa pale mtu anapotaka kumiliki ardhi. Hiyo itasaidia kupunguza migogoro hii.” 

Lakini kwa Salma, mama anayeendelea kupigania haki yake ya umiliki wa mashamba matano huko Pemba, anatoa ushaui huu kwa watendaji wa Serikali waliopewa dhamana ya kutatua migogoro ya ardhi huko Zanzibar: “Inabidi [watendaji hawa] watazame nani mwenye haki na nani hana haki badala ya kutazama nani ana pesa na nani hana pesa au nani tunamjua na nani hatumjui.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *