Kila ifikapo Novemba 3 ya kila mwaka, dunia huadhimisha siku inayojulikana kama Siku ya Afya Moja Duniani, au One Health Day kwa kimombo. Lakini je, ni watu wangapi kati yetu tunafahamu kuhusu kitu kinachoitwa Afya Moja, achilia mbali maadhimisho yake?
Basi niruhusu nieleze kwa uchache dhana hii na nikuoneshe umuhimu wake kwenye maisha yetu ya kila siku. Afya Moja imekuwa ikitafasiriwa kama mbinu shirikishi yenye kuhusisha sekta na taaluma mbalimbali ili kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuboresha afya.
Afya Moja inatambua uhusiano na mwingiliano uliopo kati ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira yao.
Mbinu hii imeridhiwa kimataifa na mashirika na wadau mbalimbali, ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WAOH), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Programu ya Kimataifa ya Mazingira (UNEP).
Hii ni kutokana na umuhimu wake katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Kufungamanisha Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii?
Ingawaje mbinu hii ya Afya Moja kwa kiasi fulani ni mbinu mpya, dhana yenyewe imekua ikitumika tangu miaka ya 1800 baada ya wanasayansi kugundua mfanano katika usambaaji wa magonjwa kati ya binadamu na wanyama.
Hata hivyo, dhana hiyo haikupewa uzito sana mpaka karne ya 20 baada ya mwanasayansi Calvin Schwabe kuvumbua wazo la ‘One Medicine,’ yaani Dawa Moja, akionesha mwingiliano wa kimatibabu kati ya wanyama na binadamu.
Schwabe alisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kutibu, kuzuia, na kudhibiti magonjwa yenye kuathiri binadamu na wanyama kwa pamoja.
Dhana ya Afya Moja imeshika kasi zaidi katika kipindi cha miongo miwili iliyopita baada ya kuungwa mkono na wadau mbalimbali, ikiambatana na matukio muhimu yenye lengo la kuitangaza zaidi, hususan kwa upande wa afya ya umma na wanyama.
Kuongezeka kwa magonjwa
Lakini kuongezeka kwa magonjwa yatokayo kwa wanyama pia kumeufanya umuhimu wa mbinu ya Afya Moja kuwa wazi zaidi kwa wadau wengi duniani.
Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, asilimia 75 ya magonjwa yanayozuka na kuambukiza upande wa binadamu yametajwa kutoka kwa wanyama. Magonjwa haya ni kama vile Ebola, Kimeta, Brusela na kichaa cha mbwa.
Ukweli ni kwamba, kwa kila magonjwa 10 anayoambukizwa binadamu, angalau sita yametoka kwa wanyama!
Pia, kuathirika kwa afya ya mazingira kutokana na uchafuzi inaweza kuwa chanzo kingine cha vimelea vya magonjwa, na hivyo kuhatarisha zaidi afya ya binadamu.
SOMA ZAIDI: Tutafakari Namna Bora ya Kuhakikisha Afya za Watu Wetu
Idadi ya watu vilevile inaongezeka kwa kasi kubwa, huku dunia hivi sasa ikikisiwa kuwa na jumla ya watu bilioni nane.
Hivyo, ili kuweza kutoa huduma stahiki za afya, maji na chakula ni muhimu sana kushirikisha sekta mbalimbali na kufanya kazi kwa pamoja kwa uratibu.
Mbinu hii ya Afya Moja kwa sasa imekua ikitumika katika kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya ya umma, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na magonjwa yanayoambukiza na yale yasiyoambukiza.
Changamoto nyengine ni kama vile usugu wa vimelea vya magonjwa, kuhakikisha usalama wa chakula na afya ya mazingira ambapo kwa kiasi kikubwa imeonesha ufanisi japo bado kuna mambo mengi zaidi ya kuzingatia.
SOMA ZAIDI: Wananchi Waishio Bonde la Mto Msimbazi Hatarini Kupata Tatizo la Usugu wa Dawa
Hali ikoje Tanzania?
Kama nchi, Tanzania imekua mstari wa mbele katika kupokea na kufuata misingi ya Afya Moja.
Kwa mara ya kwanza kabisa, mbinu ya Afya Moja ilitekelezwa katika mlipuko wa Homa ya Bonde la Ufa, au Rift Valley Fever kwa kimombo, hapo 2006 na 2007, japo hakukuwa na uratibu rasmi.
Mnamo mwaka 2013, Afya Moja ilirasimishwa kupitia kile kilichoitwa Agenda ya Kitaifa ya Afya Moja, au the National One Health Agenda, ambayo ilizinduliwa na aliyekua Makamu wa Rais wa wakati huo, Dk Gharib Bilal.
SOMA ZAIDI: Tusiruhusu Binadamu Atenganishwe Na Afya Yake
Mwaka 2015 pia, mkakati wa miaka mitano wa Afya Moja, yaani National One Health Strategic Plan, 2015-2020, uliandaliwa ambao ulizinduliwa rasmi mwaka 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Hatua hii ilienda sambamba na kusimikwa rasmi kwa dawati la uratibu wa Afya Moja katika Idara ya Menejimenti ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa kutambua umuhimu wa uratibu wa shughuli za Afya Moja, mwaka huu wa 2022, dawati limebadilishwa na kuwa ‘One Health Section’ ambapo itakua na mkurugenzi wake ili kuongeza ufanisi zaidi.
Pia, kwa mara ya kwanza, Tanzania imefanya tathmini ya kiuchumi ya utekelezaji wa Afya Moja katika kukabili milipuko ya magonjwa, ambapo imeonekana kuwa na matokeo chanya zaidi ukilinganisha na kama ingefanywa na sekta moja moja.
Wadau wa maendeleo, yakiwepo mashirika mbalimbali ya kimataifa yaliyopo nchini, yamekua na mchango mkubwa sana katika utekelezaji wa mbinu ya Afya Moja kwa kuchangia rasilimali fedha na utaalam.
Safari bado ndefu
Hata hivyo, pamoja na kwamba kama nchi tunajitahidi katika kukumbatia na kutekeleza mbinu ya Afya Moja, bado hatujafika mbali sana, hususan katika ngazi za chini, mathalan kwenye jamii.
Uelewa wa wadau, hususan wananchi wa kawaida na watendaji wa Serikali wa ngazi za chini, bado ni mdogo sana.
Pia, ushirikishwaji bado ni wa sekta chache ambapo mara nyingi huwa ni wataalam wa sekta ya afya, mifugo, wanyamapori na kilimo.
Wadau muhimu kama vile Mamlaka ya Hali ya Hewa, watalaamu wa sayansi jamii, mazingira, wauza maduka ya madawa, viongozi wa kisiasa na wanajamii kwa ujumla, wamekuwa wakiachwa nyuma.
SOMA ZAIDI: Daktari Bingwa Muhimbili Awasihi Watu Kuacha Kutumia Kuni, Mkaa Kupikia
Ili mbinu ya Afya Moja iweze kuwa na ufanisi na matokeo chanya zaidi, ni muhimu kwa Serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine, kuhakikisha inafika katika ngazi za chini za utendaji.
Kinachohitajika kufanyika hivi sasa ni kuwajengea uwezo wataalam wa kada mbalimbali ambazo zinahusika kwa namna moja au nyingine kwenye kusimamia afya ya umma pamoja na miongozo itakayowasaidia katika kutumia mbinu hii ya Afya Moja.
Pia, Serikali haina budi kuongeza ushirikishwaji wa sekta nyingi zaidi kwani afya ya binadamu kwa sasa ni zaidi ya kujikinga na magonjwa.
Ni matumaini yangu kuwa kupitia Afya Moja tutaweza kudhibiti hatari mbalimbali za kiafya kwa binadamu na mazingira yake kwa wakati na kwa gharama ndogo.
Hiyo itasaidia kupunguza, au kuzuia, madhara ambayo yangeweza kusababishwa na vihatarishi mbalimbali.
Dk Janeth George ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na mtafiti wa masuala ya Afya Moja. Pia, huchambua mifumo ya afya. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia jnthgrg10@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kwa ufafanuzi zaidi.
2 responses
Makala hii ni muhimu sana imenijengea uelewa, nadhani jamii haina uwelewa wa kutosha kuhusa Afya Moja. Endelea kutupa elimu ili nasi tuisambaze kwa watu wa karibu yetu.
Ahsante Dr. Janeth
Asante sana kwa kunielewesha juu ya Afya moja