The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hizi Hapa Habari 10 Zilizofuatiliwa Zaidi Kwenye Kurasa za The Chanzo 2022

Ni habari zilizopigiwa kura na waandishi wa habari wenyewe wa The Chanzo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Tangu kuanzishwa kwake miaka miwili iliyopita, The Chanzo imekuwa ikichapisha habari zinazolenga kuwafanya Watanzania wazidi kuielewa nchi yao na yanayotokea ili kuwaweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufanya maamuzi kuhusiana na hatma ya taifa lao.

Waandishi weledi na mahiri wa chombo hicho cha habari waliosambaa katika maeneo mbalimbali ya nchi – Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Mtwara na Zanzibar – wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii kuwapatia Watanzania maana zilizojificha nyuma ya vichwa vya habari.

Mwaka huu wa 2022 unaokwenda kuisha umeshuhudia waandishi hawa, wengi wao wakiwa ni vijana wadogo lakini wenye uthubutu wa kusimama baina ya watawala na watawaliwa, wakichapisha habari nyingi ambazo zimechochea mijadala kuhusiana na mambo mengi yanayolihusu taifa la Tanzania.

Tunakuwekea hapa orodha ya habari 10 bora zilizochapishwa na The Chanzo kwa mwaka huu, habari ambazo zimechaguliwa na kupigiwa kura na waandishi wa habari wenyewe wa chombo hicho cha habari:

Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani

Hii ni habari iliyopigiwa kura na waandishi wengi wa habari wa The Chanzo kama habari bora kabisa ambayo chombo hicho cha habari imechapisha kwa mwaka huu wa 2022.

Ni habari iliyotokana na uchunguzi wa Najjat Omar, mwandishi wa The Chanzo kutokea Zanzibar, kuhusiana na vijana kupotea katika mazingira ya kutatanisha visiwani humo.

Uchunguzi wa mwandishi huyo ulibaini kwamba vijana wengi wanaoripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha visiwani humo wanaripotiwa kwenda kujiunga na vikundi vya kigaidi.

Ni habari iliyolifanya gazeti la Uingereza la The Guardian kuifanyia mwendelezo habari hiyo, na kumfanya Najjat kutokea kwenye jarida la kimataifa kwa mara ya kwanza katika fani yake hiyo ya uandishi wa habari aliyoianza miaka takriban tisa iliyopita.

Unaweza kuisoma habari hiyo kwa ukamilifu hapa.

Kama Ngorongoro Ingeongea: Wamaasai, Ardhi na Serikali

Katikati ya juhudi za Serikali kutaka kuwahamisha wenyeji wa Ngorongoro ikidai zoezi hilo ni muhimu kwa ajili ya kutunza hadhi na urithi wa dunia ambao eneo hilo limepatiwa, sauti za wenyeji wa eneo husika zilikuwa ni nadra sana kusikika.

Ni katika mazingira hayo ambapo timu ya waandishi wa habari wa The Chanzo ilisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Ngorongoro, Arusha na kutumia siku mbili kuzungumza na wenyeji wa Ngorongoro kupata mtazamo wao kuhusiana na suala husika.

Wenyeji wa Ngorongoro, wengi wao wakiwa ni Wamaasai, walieleza kwa nini hatua ya kuwahamisha na kuwapeleka Tanga ni shambulio dhidi ya haki zao za msingi za kibinadamu, ikiwemo haki yao ya kuabudu na ile ya kiutamaduni.

Unaweza kutazama makala hiyo hapa.

Serikali Wilayani Mbozi Yadaiwa Kuhamisha Wananchi kwa Nguvu Kupanua Hifadhi ya Kimondo

Hii ni habari iliyofanywa na mwandishi wa The Chanzo kutokea Mbeya Asifiwe Mbembela iliyohusu uamuzi wa Serikali kuwahamisha kwa nguvu wanakijiji wa kijiji cha Isela, wilayani Mbozi, mkoani Mbeya kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Kimondo.

Wananchi takriban 1,300 walikuwa wanategemewa kuathiriwa na zoezi hilo lililokuwa linasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). 

Mwandishi wa The Chanzo alikwenda kwenye kijiji husika, akikuta wengi wamekimbilia porini kwa usalama wao, na kuongea nao kupata maoni yao juu ya hatua hiyo ya NCAA, na kuandika habari hiyo.

Unaweza kuisoma habari hiyo hapa.

Haya ni Baadhi ya Madhila Wanayopitia Wafanyakazi wa SBC Tanzania

Habari hii inahusu uchunguzi wa The Chanzo kwenye moja ya makampuni makubwa ya vinywaji baridi nchini Tanzania, ile ya SBC Tanzania, inayozalisha vinywaji kama Pepsi, Mirinda Nyeusi nakadhalika, kuhusu ukiukwaji wa sheria za kazi katika kiwanda chake kilichopo Dar es Salaam.

Ni habari iliyotokana na taarifa ambazo The Chanzo ilipatiwa na mmoja wa wafanyakazi kiwandani hapo kuhusiana na madai ya udhalilishaji unaofanywa na uongozi wa kampuni hiyo dhidi ya wafanyakazi wake.

Mwandishi wa The Chanzo Lukelo Francis ndiye aliyefanya habari hiyo ambayo ilipelekea Serikali kuingilia kati, ambapo kikao kati yake, chama cha wafanyakazi na baadhi ya wawakikilishi wa wafanyakazi kiwandani hapo kilifanyika na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto hiyo.

Unaweza kuisoma habari hiyo hapa.

‘Upigaji’ wa Kutisha Dar es Salaam Zaidi ya Bilioni 26.9 Zatafunwa Kati ya 2018 na 2021 

Hii ni habari iliyotokana na uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/2021 ambayo ilibainisha kupotea kwa takribani Shilingi bilioni 26.9 katika halmashauri ya Ilala, jijini Dar es Salaam. 

The Chanzo iliifanya habari hiyo kupitia mtandao wa Twitter na kuonesha ni jinsi gani maafisa wa halmashauri hiyo ‘walipiga’ fedha hizo kati ya Julai 2019 na Juni 2021, ‘upigaji’ ambao kwa kiasi kikubwa uliwezeshwa kwa kughushi risiti na kuchezea mifumo.   Wiki chache baada ya The Chanzo kuchapisha habari hiyo, Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa, mnamo Julai 11, 2022, alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halamshauri ya jiji la Ilala, Jumanne Shauri na watumishi wengine tisa. 

Majaliwa alisema watu hao wanapaswa kupisha uchunguzi kwa tuhuma za ubadhirifu wa Shilingi bilioni 10 ambazo zilikusanywa na hazikuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.

Unaweza kusoma habari nzima hapa.

Surviving on Brown Envelops: Tanzania’s ‘Volunteer’ Radio Journalists in Limbo

Habari hiyo iliyochapishwa kwa lugha ya Kiingereza (The Chanzo huchapisha kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili) inaangazia maswaibu wanayopitia waandishi wa habari nchini Tanzania ambao kutokana na kulipwa kidogo, au kutokulipwa kabisa, kunawafanya wategemee hongo kutoka kwa watu wanaowafanyia habari.

Ikiandikwa na mwandishi wa habari wa kujitegemea Mweha Msemo, habari hiyo ilibainisha namna mazingira magumu ya ufanyaji kazi miongoni mwa waandishi wa habari Tanzania, hususan wale wa redio za kijamii, kunawalazimisha wafanye kazi kinyume na maadili yao ya kazi.

Ni mara chache sana waandishi wa habari, ambao ni wazuri kwenye kuonesha matatizo ya watu wengine, huwa tayari kuonesha matatizo ya kwao. Ni moja kati ya vitu vinavyoifanya habari hii kuwa kubwa na ya muhimu.

Unaweza kuisoma habari hiyo hapa.

Nini Kinachochea Mauaji Holela Yanayoendelea Kuitesa Tanzania?

Hii ni habari iliyolenga kuwapatia Watanzania baadhi ya majibu juu ya maswali yao mengi yaliyotokana na uwepo wa wimbi kubwa la mauaji ambayo yamehusishwa na wivu wa mapenzi na imani za kishirikina.

Wimbi hilo la mauaja siyo tu liliwaacha Watanzania wengi wakiwa na maswali lukuki bali pia liliwafanya viongozi waandamizi wa Serikali kukosa namna bora ya kulidhibiti na hivyo kupelekea kuundwa kwa tume maalum ya kuchunguza suala hilo.

Kwenye habari hii, The Chanzo inajaribu kujibu baadhi ya maswali kuntu juu ya suala hilo, ikifanya hivyo kutokana na uchambuzi wake wa matukio mbalimbali ya mauaji yaliyokuwa yakiripotiwa nchi nzima.

Habari kamili inapatikana hapa.

People Go Missing in Tanzania. Authorities Seem Not To Care Much About It

Hii ni habari iliyoangazia kupotea kwa watu katika mazingira tatanishi nchini Tanzania, huku mamlaka zinazohusika zikionekana kutokufanya kazi kama ambavyo wananchi wangezitarajia zifanye kwenye mazingira kama hayo.

Inahusiana na kupotea kwa vijana watano jijini Dar es Salaam na vijana wengine wawili mkoani Mara, kwa zile kesi zinazojulikana, ambao licha ya familia zao kuiangukia kila idara inayohusika ya Serikali bado zimeshindwa kujua kama vijana wao wako hai au wamefariki.

Unaweza kusoma habari kamili hapa.

Ulawiti Unavyowajaza Hofu Wazazi Kuhusu Hatma ya Watoto wa Kiume Tanzania  Kuanzia

Ulawiti ni janga jingine lilioitesa Tanzania kwa mwaka huu wa 2022. Habari hii ililenga kupaza sauti juu ya suala hilo linaloumiza vichwa vya watu wengi nchini, ikiwa ni sehemu ya kutafuta suluhu ya muda mrefu juu yake.

Ikifanywa na mwandishi wa habari wa The Chanzo kutokea Dodoma, Jackline Kuwanda, habari hiyo ilijikita kwenye kuchambua tatizo husika, pamoja na kutafuta majibu kuhusiana na maswali mbalimbali waliyonayo Watanzania kutoka kwa wadau wanaojihusisha na utetezi wa ustawi wa watoto nchini.

Unaweza kuisoma habari husika hapa.

Plastic Waste Pickers: The Shunned and Scorned Environmental Warriors of Tanzania

Hii ni habari nyengine kutoka kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea Mweha Msemo ambayo inajikita katika kuangazia maswaibu wanayoyapitia watu wanaojishughulisha na uokotaji chupa za plastiki katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Watu hawa wanaofanya kazi muhimu ya kudumisha usafi kwenye mitaa yetu, hawapewi thamani na heshima wanayostahiki, habari hiyo inaonesha. Wengi wao huonekana ni wendawazimu, waliopoteza mwelekeo wa maisha au vibaka.

Lakini mitaa yetu ingekuwaje kama isingekuwa kwa watu hawa wanaopita mitaani na kuokota chupa tunazozitupa baada ya kuzitumia?

Habari kamili inapatikana hapa.

Tukiwa tunaelekea mwaka 2023, The Chanzo itaendelea kuwa chombo cha habari cha kuaminika nchini Tanzania, kinachochapisha habari zinazohusu maisha ya watu ya kila siku, kutoka kwa watu wenyewe.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts