Katika mada ngumu kuzijadili barani Afrika kwa sasa ni pamoja na Umoja wa Afrika, haki ya uhuru wa nchi na mataifa kujitawala na umakini unaohitajika katika hayo yote.
Nikiwa shule ya msingi, nilielezwa jinsi jamii za Kiafrika zilivyokuwa na haki ya uhuru wa kujitawala kupitia himaya zao za utawala wa kijadi kabla ya mwingiliano wa jamii hizo na wageni kutoka nchi za mbali.
Huko Mali, tunaambiwa kuwa hapo zamani Afrika ilishakuwa na mataifa huru yaliyojitawala, ikiwemo himaya za Ajuran, Bachwezi na Dagbon; Mali, Songhai na Bono; na pia Buganda, Oyo, Lunda na Ashanti kwa uchache.
Wageni walipoanza kufika Afrika, waliwakuta mabibi na mababu zetu wakizalisha, wakifanya siasa, wakiwa na mifumo ya elimu na wakifanya siasa katika viwango vya ubora wa hali ya juu kabisa. Hata masuala ya ulinzi na usalama wa mipaka, raia na mali zao ulikuwepo kwa ubora kabisa.
Nikiwa sekondari, nilijifunza jinsi Wahehe wa Kalenga na Tosamaganga walivyopanga na kutekeleza masuala ya uhusiano wa kimataifa kwa kutembelea sehemu za mbali kama Tabora na hata Buganda na Ankole.
Aidha, tunafahamu kuwa taifa la Wanyamwezi lilikuwa na utaratibu wa kwenda kununua silaha hata za moto kutokea kwa wenzao wa Bunyoro na Buganda ambao walikuwa wameanza kuwa nazo kabla yao.
Ni bahati mbaya sana kuwa wageni walipowasili Afrika hawakutaka kujifunza kutoka kwa wenyeji kwa lolote.
Badala yake, walileta taratibu, mifumo na ustaarabu waliotoka nao Ulaya na maeneo mengine na kuanza kuvipandikiza katika jamii za Waafrika kwa nguvu tena bila kujali wala kuwianisha na yale waliyoyakuta.
Tazama maendeleo makubwa yaliyokuwa yamefikiwa Afrika katika nyanja kama za sayansi, elimu na sanaa. Michoro mbalimbali kama iliyowahi kuonekana Isimila, Olduvai na kwingineko katika iliyokuja kuwa Tanganyika baada ya karne kadhaa ilichorwa na Waafrika kwa elimu yao wenyewe.
Huko Afrika Kaskazini, jamii zilikuwa zimepiga hatua kubwa katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Mto Nile mapema katika miaka ya 3100 BC.
Kufikia mwaka huo, Mfalme Menes wa Misri alishaweza kuunganisha maeneo ya kusini na kaskazini na kuunda Shirikisho la Himaya ya Misri. Watimbuktu na Wamorocco walikuwa nao wana vyuo vikuu katika miaka mingi sana kabla wageni ‘hawajavumbua’ na kufika Afrika.
Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Al Karaouine kilianzishwa huko Fes, Morocco katika miaka ya 859 AD kikiwa ni cha pili baada ya kile kikongwe zaidi cha Timbuktu kilichoanza miaka ya 982 BC.
Vyuo vikuu vingine vikongwe Afrika ni pamoja na Al-Azhar (Misri, 972 AD); Fourah Bay (Sierra Leone, 1927) na Cape Town, Afrika Kusini (1829). Kwa hakika bara la Afrika halikuwa na ‘kiza totoro’ kama walivyolielezea Wazungu walipowasili hapa.
Umakini unahitajika
Ni kwa sababu hiyo, inafaa kuwa makini sana katika kujadili mada zinazohusiana na utaifa na mahusiano ya watu katika bara la Afrika kabla na baada ya ukoloni. Dhana kuwa mipaka ya mataifa ya Afrika iliasisiwa na wakoloni katika mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 – 1885 ni potofu kupitiliza.
Taifa kama la Morocco na jamii yake ambayo mchanganyiko wa makabila, rangi na dini mbalimbali lilikuwepo kabla ya mwaka 800 AD.
Mjadala wa Morocco pana kama unavyojulikana kule Rabat na Casablanca ni dhana yenye mantiki ya eneo lililokuwa likikaliwa na jamii zilizounda taifa la Morocco miaka mingi kabla wavumbuzi, wamisionari na wakoloni hawajafika Afrika.
Dhana hii imekuja kuanza kupotoshwa katika miaka ya 1970 wakati jamii ya Wasahara ilipoanza kudai kutaka kuunda nchi yao nje ya mataifa yaliyopo na ambayo jamii hiyo imekuwa sehemu yake kwa karne na karne.
SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?
Kwa faida ya wasiojua masuala ya Maghreb, Wasahrawi ni jamii ya watu ambao wanatokea katika eneo la Jangwa la Sahara ambalo linazikumba nchi nyingi tu za eneo la Maghreb.
Kwa maana hiyo, Wasahrawi, kwa asili yao, wanapatikana katika nchi za Algeria, Tunisia, Chad, Mauritania na kwa kiasi fulani Cameroon.
Kumuona au kumsikia Msahrawi anayeishi Algeria, Tunisia au Mauritania anajiita mkimbizi wa Morocco ni sawa na Mmaasai akiwa Kenya akajiita mkimbizi wa Tanzania! Ukweli ni kwamba kwa Wamaasai, Kenya ni nyumbani kama ilivyo Tanzania.
Ni bahati mbaya nyingine kuwa mipaka ya nchi waliyoichora wakoloni wakiwa Ujerumani ilikosa umakini kiasi cha kukatisha katikati ya jamii ndugu za Afrika, ikiwa ni pamoja na Wajaluo, Wakamba, Wamaasai, Washona na jamii nyingine nyingi ambazo ubaguzi wa mipaka ya wakoloni umeshindwa kuua udugu wao wa damu.
Ndiyo maana viongozi wa Afrika wapatao 32 waliokuwepo katika mkutano ulioanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) – sasa Umoja wa Afrika (AU) – walitafakari sana jambo hili la matatizo ya mipaka ya kikoloni Afrika na namna ya kuweza kuyamaliza kwa kuiunganisha Afrika yote ili iwe nchi moja, yenye mataifa, jamii, makabila na rangi mbalimbali.
Nikisikiliza hotuba ya Rais wa Ghana wa wakati huo Kwame Nkrumah, yeye alitaka jambo la msingi iwe ni kuunda shirikisho la mataifa ya Afrika kutoka Cape mpaka Cairo ili hatimaye mipaka ya ndani ya Afrika waliyoichora wakoloni ipoteze maana au ife kabisa.
Nkrumah alitaka kuanzishwe shirikisho la Mataifa ya Afrika lenye Katiba moja ya Serikali moja, mpango mmoja wa kiuchumi na maendeleo ukihusisha soko la pamoja, sarafu na Benki Kuu moja, na mfumo mmoja wa mawasiliano bara zima.
Aidha, Nkrumah alitaka mfumo mmoja wa sera ya mambo ya nje ya Afrika nzima, jeshi moja la ulinzi la wananchi wa Afrika na uraia mmoja kwa waafrika wote kiasi ambacho utaifa na makabila au dini zetu vingebaki kuwa katika kumbukumbu ya tunu ya jadi zetu kwa ajili ya kile Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikiita kutambikia, basi.
Wengine waliokuwa na uelekeo wa mawazo ya umoja kamili wa Afrika walikuwa ni pamoja na mwenyeji wa mkutano, Mfalme Haile Selassie I wa Ethiopia, Ahmed Ben Bella wa Algeria, Rais Ahmadou Ahidjo wa Cameroon na Rais Modibo Keita wa Mali.
Bahati mbaya nyingine ilikuwa ni kwamba kuwepo kwa viongozi ambao walikuwa wamekwishaonja asali ya Urais au Uwaziri Mkuu kwa nchi 32 zilizowakilishwa, pamoja na wale waliokuwa wanaendelea na mapambano ya kutafuta uhuru ili nao wakapigiwe saluti na mizinga 21, kulififisha msimamo wa kuamua kuunda Serikali ya Shirikisho katika mkutano ule wa Mei 1963.
Hii ndiyo imepelekea kufuatwa kwa ushauri uliotaka Umoja wa Afrika ufikiwe pole pole, hatua kwa hatua, jambo ambalo limekuwa gumu sana hivi leo.
Dhana ya utaifa, uraia
Inanisikitisha kuwa leo Afrika imejaa migogoro na mivutano inayotokana na uwepo wa mipaka bandia barani pamoja na mkanganyiko uliopo kati ya dhana ya utaifa na ile ya uraia.
Kwa maoni yangu, utaifa ni hali ya kuwa sehemu ya jamii fulani ya watu ambao wana historia, utamaduni na asili moja. Kwa upande mwingine, uraia ni hadhi ambayo mtu mmoja mmoja anaipata kutokana na kuthibitika kuwa yeye ni sehemu ya mipaka ya nchi husika.
Upo wakati mwingi ambapo watu wa taifa moja wanaweza kuwa na uraia wa nchi tofauti na vivyo hivyo watu wa nchi moja wanaweza kuwa na kutoka mataifa au jamii tofauti tofauti.
Kwa akili yangu, taifa linaunganishwa na lugha, utamaduni, asili, jadi na mila wakati nchi inaunganishwa na siasa, vitambulisho na vyeti wa kuzaliwa na kusajiliwa.
SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiwango Gani Waafrika Wanaweza Kujitatulia Matatizo Yao Wenyewe?
Hapa ndipo ninadiriki kusema kuwa Afrika tumepotoka kwa kuchanganya mambo haya mawili pasipo kuyaweka bayana kuwa ni tofauti. Kwa mfano, taifa la Waafrika ni taifa moja miaka yote bila kujali makazi yako ni Goma au Yaounde au hata Soweto.
Wasahrawi walioko Algeria, Tunisia, Mauritania au hata Mali ni sawa sawa kabisa na wale walioko Morocco. Kwa kuwa asili, jadi, mila, tamaduni na lugha yao inapaswa kufanana.
Itashangaza, na kwa kweli inashangaza, kuwa jamii moja inaweza kuhitilafiana, kugawanyika na hata kuuana kwa sababu ya tofauti ya mahali wanakoishi.
Kwa mtazamo wangu, Mwafrika aliyeko Burundi na Bamako wana udugu wa damu kabisa na Mwafika aliyeko Cuba, Puerto Rico na Marekani.
Sasa swali langu ni, je, kwa nini tumeruhusu Waafrika waanze kujimega na kujitangazia kutaka kuunda nchi huru kwa sababu tu wao ni taifa moja? Kwani kila taifa lazima liwe na nchi yake?
Je, haiwezekani tukaenda na msimamo wa waasisi wa OAU – na baadaye AU – kwamba Afrika ni mataifa mengi lakini lazima tuwe nchi moja?
Hizi vurugu za vikundi vya jamii zenye asili ya taifa moja kutaka kijenga na kuanzisha nchi yao siyo dalili za utumwa mpya?
Nchi ya kisasa lazima ijisikie fahari kuwa na mchanganyiko wa mataifa kwa maana ya kabila, dini, rangi na asili tofauti tofauti ili warefu wachangamane na wafupi, wanene waoane na wembamba na weupe wazae na weusi ili kupata maji ya kunde.
Nimetembea sana Afrika na kushuhudia matatizo makubwa kutokana na uelewa potofu wa dhana ya utaifa na uraia. Ukienda Cameroon utakuta watu wa jamii au taifa la Ambazonia wameunda vuguvugu la kudai kujitenga na Cameroon na kuanzisha nchi yao ya Ambazonia.
Huko, wamefikia hatua mbaya mpaka kuunda Jeshi la Ulinzi la Watu wa Ambazonia, jambo ambalo linakiuka msingi wa kuwa taifa. Taifa halihitaji kuwa na jeshi lake kwa kuwa kazi ya kulinda mipaka ni kazi ya kiserikali inayopaswa kuwa jukumu la nchi au dola.
SOMA ZAIDI: Uhasama Kati Ya Mataifa Ya Afrika Mashariki Unaipeleka Wapi Jumuiya Hiyo?
Tukianza kuwa na jeshi la Wanyakyusa, jeshi la Wazulu na jeshi la Wa-Ibo tutakuwa tumeruhusu fujo, vita na vurugu kila uchao kati ya taifa na taifa na baadaye kati ya watu wa taifa moja na jingine.
Nimepata kutembelea pia Mombasa, Kenya wakati fulani nikaambiwa kuwa kulikuwa na vuguvugu la kutaka Mombasa iwe jamhuri huru kwa kigezo kuwa jamii hiyo ilikuwa na inaendelea kuwa sehemu ya jamii za Pwani ikishirikiana na kuoleana na Zanzibar, Pemba, Tanga na Comoro.
Sasa swali ni je, kwani ukiwa Mombasa na mjomba wako akawa Zanzibar kuna shida gani? Ni lazima mlioko Mombasa mjitenge na Kenya ili ndipo muendelee kuwa shangazi wa mtu aliyeko Tanga?
Kwa mtazamo wangu, huu ni upotofu wa kimaono kuhusu dhana ya utaifa na dhana ya uraia.
Kwingineko, jamii ya Azawad wanataka kujitenga na nchi ya Mali; vijana wa Ki-Ibo wanapambana na vikosi vya Serikali ya Nigeria wakitaka jamii ya Wa-Ibo ipewe haki ya kuunda Serikali yao; jamii ya Wa-Cabinda imeanzisha mapambano yanayoitwa FLEC mahsusi kupigania haki ya jamii yao kujitenga na Angola na kuunda dola yao ya wana-Cabinda.
Hata ndani ya Algeria ambako kuna Wasahrawi wanaopambania kutaka kuunda Serikali yao kuna mapambano yanayoendelea kati ya wa-Algeria wa asili ya Kabylie yakiongozwa na vuguvugu la MAK kutaka kujitenga na dola ya Algeria.
Mwanzilishi wa MAK, Ferhat Imazinghen Imula, au kwa jina jingine Ferhat Mehenni, anaishi mafichoni nchini Ufaransa na mamlaka za Algeria zimelitangaza vuguvugu la MAK kuwa ni kundi la kighaidi kufuatia fununu kuwa wanachama wake walipanga kutega mabomu ya magari katika jiji la Algiers na miji mingine.
Zaidi ya yote, Algeria imesaini hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Mehenni ili aweze kushitakiwa.
Je, kama Algeria ni muumini wa dhana ya haki ya vikundi vya kijamii kuunda dola yake, kwa nini isimruhusu Ferhat Mehenni aendelee na harakati zake kwa kuwa ameshaiongoza MAK kuandika katiba itakayokuwa sharia mama ya nchi ya Kabylia?
Kwa ujumla, hata Zimbabwe kulikuwa na harakati za watu wa kabila la Wamatabele kutaka kuunda dola yao ya Matabele kule Bulawayo kufuatia walichokiita unyanyasaji na uvunjaji wa haki za wana-Matabele ikiwemo mauaji ya halaiki ya Gukurahundi ambapo watu wao wasiopungua 20,000 waliuwawa kati ya mwaka 1983 na 1987.
Serikali ya Zimbabwe haijawahi kutoa fursa kwa wana wa Bulawayo na maeneo yanayounda Matabeleland kama Gwanda, Matobo, Bulilima na Tsholotsho kujitenga na kuunda dola yao huru. Kwa nini?
Unyeti wa madai ya Wasahrawi
Hii ndiyo sababu naamini kuwa suala la mgogoro wa Wasahrawi walioko ndani na nje ya mipaka ya Morocco ni jambo nyeti lakini linalohitaji tafakuri ya mbinu mbadala za kuweza kutatua mgogoro ambao unaendelea kufukuta tangu miaka ya 1970.
Kwa maoni na uelewa wangu, njia ya SADR – kama nchi ya Sahrawi inavyojulikana – kuendeleza mapambano ya kutambulika kama nchi huru imeonekana kuleta shida ya kimtazamo na kimkakati. Kwa mfano, hivi SADR inataka kuundwa katika eneo lipi haswa?
Kama ni ndani ya mipaka ya Morocco, je, kwa nini ndani ya Morocco wakati eneo la Jangwa la Sahara wanakopatikana watu wa jamii ya Wasahrawi ni pana kuliko mipaka ya Morocco?
SOMA ZAIDI: Afrika Na Demokrasia Bado Mguu Ndani, Mguu Nje
Na je, kwa nini Wasahrawi walioko Algeria wanasemekana wako katika kambi za wakimbizi wakati nchi ya Algeria pia kiasili ina Wasahrawi? Nini kinamtofautisha Msahrawi wa Algeria na yule wa Morocco na Tunisia au Mauritania?
Je, ni wote hawa wanaishi katika makambi ya wakimbizi au ni wale waliotokea Bir Lehlou, Morocco pekee? Kama ni hivyo, huo si unakuwa ubaguzi wa moja kwa moja?
Nashauri kuwa mjadala wa suala la mgogoro wa Wasahrawi walioko eneo lote la Maghreb na malalamiko yao juu ya haki zao zinazovunjwa ubaki katika vikao vya Umoja wa Mataifa ili lijadiliwe na kupatiwa suluhu ya kudumu.
Mapambano ya nguvu hayatazaa tija hata kidogo kama ilivyokwisha thibitika katika miaka yote iliyopita tangu mgogoro uanze miaka ya 1970 wakati Hispania ilipoachia ngazi kama mkoloni wa eneo la Sahara na Equatorial Guinea.
Kwa wasiofahamu, umahiri mdogo wa OAU katika kushughulikia mgogoro huu ulisababisha Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua hatamu ya utatuzi wake kwa njia ya mazungumzo kuanzia mwaka 1988.
Kutokana na hilo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) limekuwa likiendendelea na juhudi za kutafuta suluhu ya suala la Sahrawi kwa njia ya mazungumzo ya kidiplomasia kwa lengo la kupata maridhiano yatakayokubalika kwa pande zote chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa UN na mjumbe wake maalum.
Tayari juhudi za UN zimepata uungwaji mkono wa Jumuiya ya Kimataifa kama vile Uamuzi Namba 693 wa AU wa mwaka 2018 ukiunga mkono UN kuwa ndiyo chombo pekee cha kushughulikia suluhu ya mgogoro wa Sahrawi.
Hilo la mazungumzo ya mezani limekubaliwa na kuungwa mkono kidunia na tangu hapo nyaraka zote za UNSC zinatambua washiriki wote wa mazungumzo hayo ambao ni Morocco, Algeria, Mauritania na ‘Polisario.’
Na tayari hadi wakati huo Morocco imewasilisha mpango wa kugatua madaraka kwa eneo la Sahrawi kuweza kujitawala kama watu huru ndani ya mipaka ya nchi hiyo.
Chini ya mpango huu wa Morocco unaofanana sana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuunda Tanzania, Sahrawi itakuwa na mamlaka yake kamili ya kiutawala, Bunge lake na mfumo wake wa utoaji haki (Mahakama).
Kwa kujifunza kutoka Tanzania, Morocco itakuwa mithili ya Tanzania na Sahara kama Zanzibar jambo litakalodumisha umoja na mshikamano wa taifa hilo ndani ya mipaka ya Morocco badala ya madai ya kuimega Morocco vipande vipande.
Hiyo inaenda kinyume na ndoto za waasisi wa Umoja wa Afrika waliotaka, hatimaye, Afrika iungane na kuwa nchi moja yenye mataifa, makabila, rangi na dini mbalimbali mchanganyiko wakiishi kwa amani, utulivu na mafanikio makubwa.
Hii ndiyo njia pekee ya suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Sahara na ndiyo maana kwa kutambua hilo Jumuiya ya Kimataifa imeanza kuunga mkono uelekeo huu na kwa kuanzia nchi zilizounga mkono hoja kuwa Morocco ni nchi na himaya moja ni pamoja na Marekani na nchi nyingine kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya ikiwemo Hispania (mtawala wake wa zamani), Ujerumani, Uholanzi, Poland na Hungary kwa sasa.
Aidha, asilimia zaidi ya 40 ya nchi za Afrika tayari zimefungua balozi ndogo katika majimbo ya kusini (eneo la Sahara). Hii inaenda sambamba na mkataba wa Vienna wa mahusiano ya kidiplomasia na kutambua uelekeo mpya wa suluhu ya amani ya Morocco na wasahrawi.
Nje ya utaratibu huo, sioni hoja za msingi zinazojengwa katika misingi ya taaluma na uhalisia wa mahusiano ya kimataifa bali vurugu.
Tusiingie katika mkumbo wa kulaani upande wowote katika mgogoro wa Sahara bila kuufahamu vizuri maana kinachohitajika kutoka kwetu ni ushirikiano na wadau wa mgogoro huu katika kutafuta suluhu siyo kuchochea utengano wao!
Mungu ibariki Afrika!
Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.