Fahamu Kuhusu Tausi, Mfumo Mpya wa Ukusanyaji Mapato Serikalini

Unatajwa kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji mapato na kuepusha upotevu.

Dodoma. Mkurugenzi wa TEHAMA, Ofisi ya Rais TAMISEMI mkoani Dodoma Erick Kitali, ameeleza kwamba mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ujulikanao kama Tausi utasaidia kupunguza urasimu uliokuwepo hapo awali kwenye ukusanyaji wa mapato.

Kitali alitoa tathmini hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake mjini hapa hivi karibuni kuhusu mfumo huo unaotajwa kubuniwa na wataalam wa ndani ya nchi.

Ukipewa jina la ndege huyo mzuri anayepatikana nchini Tanzania, Tausi umebuniwa baina ya kubainika uwepo wa changamoto mbalimbali kwenye mfumo uliokuwa unatumika hapo awali, ikiwa ni pamoja na uzoefu wa mlipa kodi.

“Mfumo huu utasaidia kupunguza muda, kuondoa urasimu uliokuwepo kwa baadhi ya sehemu,” Kitali alisema kwenye mahojiano hayo. “Na sehemu nyingine tulikuwa tunaambiwa kwamba kuna rushwa tumepunguza kwa sababu hukutani moja kwa moja na mwananchi.”

SOMA ZAIDI: Nini Kifanyike Kuboresha Mfumo wa Kodi 2023?

Pamoja na mambo mengine, mfumo wa Tausi humsaidia mteja kufanya malipo kwa kutumia VISA, MasterCard na namba ya malipo kutoka Mfumo wa Malipo wa Kielektroniki wa Serikali (GePG).

Mfumo huo pia humsaidia mteja kujihudumia mwenyewe, hali ambayo haimlazimu tena kwenda ofisi za halmashauri kuomba, au kulipia, tozo, ushuru, leseni, faini au vibali mbalimbali badala yake anaweza kufanya mwenyewe kupitia dirisha la mteja, au Taxpayer Portal

Kabla ya ujio wa mfumo huo, Serikali ilikuwa inatumia mfumo wa LGRCIS, au Local Government Revenue Collection Information System, ambao Kitali alisema kwenye mahojiano yake na The Chanzo kwamba ulipaswa ubadilishwe ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.

Akizungumzia kuhusu namna wananchi walivyoupokea mfumo huo mpya, Kitali alisema mpaka sasa muitikio ni mkubwa.

“Kwa sababu wananchi walikuwa wanapata changamoto ya kupoteza muda mwingi sana kwenda kufuatilia huduma,” alisema. “Ule urahisi wa kufanya malipo mbalimbali ya Serikali umesaidia wananchi kuwa na muitikio mkubwa.” 

“Umeongeza uaminifu kwa wananchi kwa Serikali yao kwa sababu wana uhakika na fedha wanayoilipa inakwenda moja kwa moja kwenye Serikali,” aliongeza Kitali. “Pia, mfumo huu umesaidia fedha zinazokusanywa [na halmashauri] zinapelekwa benki kwa wakati.”

SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini

Kitali alisema kwamba faida nyengine kwa upande wa Serikali inayotokana na matumizi ya mfumo huo ni kwenye eneo zima la usimamizi wa mashine za ukusanyaji wa mapato, yaani POS. 

“Tulikuwa tuna changamoto, saa nyingine usijue zipo ngapi,” alisema afisa huyo. “Lakini sasa hivi, kwa kutumia mfumo huu, tumeboresha hilo eneo [na] kuhakikisha kwamba POS zote ambazo zipo kwenye halmashauri tunajua zipo ngapi, zinatumiwa na nani na zimekusanya kwa kipindi gani.”

Kitali alisema kwamba matarajio ya Serikali kwa sasa ni kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi, akisema kwamba huduma bora husaidia kuongeza mapato serikalini. 

“Wito wetu kwa wananchi ni kwamba tunaomba waendelea kuutumia mfumo huu na panapotokea changamoto yoyote basi watujulishe,” alisema mtaalamu huyo. 

“Na uzuri tulichokifanya, watalaam wetu wa halmshauri wamefundishwa [kuutumia huu mfumo], maafisa bishara [na] maafisa fedha wanaufahamu mpaka ngazi ya mkoa,” aliongeza Kitali.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Jackline Kuwanda

One comment

  • paul christopher

    12 March 2023 at 11:19 AM

    Kwa system hiyo ,mfumo utasaidia Sana mwananchi ,kuondokana na changamoto za rushwa,kufaidisha mmtu binafsi kuliko serikali ,na kupunguza kupoteza mda ,/kutumia mda mrefu kwa kitu kidogo

    Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2023 © All Rights Reserved