The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Kidole Kimoja Hakivunji Chawa’: Uchaguzi Mkuu wa Nigeria 2023 na Mambo Makuu ya Kujifunza Tanzania

Ifike wakati wanasiasa wa Afrika waone umuhimu wa kushirikiana.

subscribe to our newsletter!

Wahenga waliwahi kunena kuwa kidole kimoja hakivunji chawa! Wengine waliongeza kwamba mtaka yote kwa pupa hukosa yote! Uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini Nigeria hapo Februari 25, 2023, umedhihirisha kuwa lisemwalo lipo na kama halipo linakuja.

Rais mteule Bola Ahmed Tinubu ataapishwa rasmi kuchukua mikoba ya urais wa Nigeria ifikapo Mei 29, 2023, baada ya matokeo ya uchaguzi wa majimbo yote 36 ya Nigeria utakaofanyika Machi 18, 2023, kupatikana na kutangazwa.

Ingawa uchaguzi huja na kishindo kokote duniani, Nigeria kulikuwa na kishindo kikubwa zaidi mwaka huu wa 2023. Nchi yenye idadi ya watu wanaofikia milioni 223.8 kwa takwimu za mwanzoni mwa mwaka 2023, Nigeria ina  wapiga kura wapatao milioni 93.4 waliojiandikisha kupiga kura kumchagua Rais wa taifa hilo kubwa barani Afrika.

Kwa wachambuzi wa siasa kama mimi, ilitarajiwa kuwa mwitikio wa wananchi kwenda kupiga kura ungekuwa mkubwa sana, ikizingatiwa matatizo lukuki yanayolikabili taifa hilo.

Hata hivyo, kwa mshangao mkubwa, jumla ya kura zote zilizohesabiwa ni milioni 25 pekee, ikiwa ni takribani robo ya wapiga kura wote waliojiandikisha. Je, kuna shida gani zilizopelekea mwitikio kuwa mdogo kiasi hicho?

Je, watu wanaokaribia robo tatu ambao hawakupiga kura waliishia wapi? Je, aliyetangazwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho ana uhalali kiasi gani wa kuunda Serikali ikizingatiwa kura kiduchu alizozipata katika uchaguzi huo? Nini kifanyike ili wananchi wengi zaidi waweze kupiga kura katika miaka ijayo?

Jambo moja kubwa la kujifunza kutokana na uchaguzi wa Nigeria ni kwamba wanasiasa lazima wajifunze kushirikiana.

Laiti mgombea wa chama cha PDP, Atiku Abubakar, ambaye ameshika nafasi ya pili katika uchaguzi huu kwa kupata kura milioni 6.98, angeungana na mgombea wa tatu Peter Obi wa chama cha Labour, jumla ya kura ambazo wangevuna ingekuwa ni zaidi ya milioni 13, wakimpita kwa mbali mgombea aliyetangazwa mshindi Bola Tinubu wa chama cha APC ambaye ameshinda kwa kura milioni 8.7 pekee.

Kwa wasiofahamu, Atiku Abubakar na Peter Obi walikuwa pamoja katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019, huku ndugu Obi akiwa mgombea mwenza wa Abubakar kupitia chama cha PDP.

SOMA ZAIDI: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Miaka 63 ya ‘Uhuru wa Migogoro’

Matokeo ya mwisho yaliwapatia kura milioni 11.2 ambazo safari hii wamezitawanya katika vyama viwili baada ya Obi kuanzisha ‘chama cha mtandaoni’ cha Labour. Laiti wangekuwa bado pamoja, wawili hawa wangeshinda uchaguzi kwa hesabu za mwaka huu au hata kwa hesabu za jumla ya kura walizozipata mwaka 2019.

Tinubu mwenyewe ameshinda kutokana na kubahatika kuwa mgombea wa umoja wa vyama vya Progressives ambao unatokana na wanasiasa wengi wakongwe ambao waliamua kujiunga pamoja wakitokea vyama mbalimbali na kuanzisha APC mwaka 2013.

Harakati za urais za Tinubu

Tinubu alianzia siasa katika chama cha Social Democratic Party mwaka 1992, akichaguliwa kushika wadhifa wa Seneta wa Lagos Magharibi kwa mwaka mmoja kati ya 1992 na 1993. Wakati huo, Atiku Abubakar, ambaye alikuwa naye chamani, aliamua kuanza kuutafuta urais.

Baadaye Tinubu alihamia chama cha Alliance for Democracy kuanzia 1998 hadi 2006 ambako alifanikiwa kugombea na kupata Ugavana wa Lagos, akitumikia tangu Mei 1999 hadi Mei 2007.

Baadaye, Tinubu alibaini kuwa mafanikio ya kisiasa hayawezi kuja akiwa na vyama vidogo vidogo na aliamua kuungana na wenzake wengi waliotokea vyama mbalimbali kuanzisha vuguvugu kubwa la mageuzi nchini Nigeria na kulisajili kama chama cha APC.

Hata akiwa huko, Tinubu aliendeleza dhana ya umoja kwa kuvumilia alipoambiwa asubiri kidogo kugombea urais wakati ambapo Jenerali Muhammadu Buhari alikuwa anagombea uchaguzi wa mwaka 2015 na baadaye akamalizia kipindi cha pili mwaka 2019.

Wakati Tinubu akisimamia umoja na uvumilivu, mwanasiasa mwenzake Atiku Abubakar ambaye walikuwa naye APC kuanzia mwaka 2014 hakuwa mvumilivu na aliamua kuingia katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za kuusaka urais, akishindana na Jenerali Buhari na akapoteza nafasi.

Badala ya kuvumilia kidogo, Abubakar aliamua kuhama chama na kurejea tena chama cha PDP kuanzia mwaka 2017 ili kuvizia kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2019.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Sawa Kwa Wasahrawi Kudai Kujitawala?

Kwa bahati mbaya, PDP kilikuwa kimepoteza nguvu baada ya wanasiasa wengi wazuri kuhamia APC na Abubakar alishindwa na Rais Buhari katika uchaguzi wa 2019.

Endapo idadi ya uchaguzi ambao mgombea anaweza kugombea ingekuwa na ukomo, Jenerali Muhammadu Buhari asingeruhusiwa kugombea urais mwaka 2015, ikizingatiwa kuwa alishawahi kugombea kupitia chama cha ANPP mwaka 2003 na 2007 akiangushwa na Olusegun Obasanjo na Umaru Yar’Adua mtawalia na mwaka 2011 kupitia chama cha CPC akiangushwa na Goodluck Jonathan.

Wakati Buhari anagombea na kushinda urais mwaka 2015 alikuwa anafanya hivyo kwa mara ya tatu mfululizo. Watu wengi nchini Nigeria na kwingineko Afrika wanaanza kupata fikra kuwa mifumo ya uchaguzi itapaswa kuweka ukomo wa idadi ya vipindi ambavyo mtu mmoja anaweza kugombea hata kama hajashinda.

Ukomo wa vipindi vya urais

Kuweka ukomo wa vipindi vya urais pekee inaonekana kuwa haitoshi kwa kuwa mtu mmoja kuruhusiwa kuendelea kugombea zaidi ya mara tatu katika taifa la watu milioni 223 kama Nigeria ni ukosefu wa utaratibu mzuri.

Sambamba na ukomo wa vipindi vya kugombea, kuna pendekezo kuwa kuwepo kwa ukomo wa umri wa kugombea kikatiba ili mwananchi aliyefikia miaka 65 asiruhusiwe tena kugombea nafasi ya urais au Makamu wa Rais.

Hatua hii inaonekana kushabikiwa sana na vijana kote nchini Nigeria, huku ikidhaniwa kuwa itapelekea kutoa nafasi kwa watu ambao akili bado zina ubunifu kuweza kuongoza nchi.

Hata hivyo, mawazo haya ni mwiba mkali kwa mwanasiasa kama Peter Obi ambaye katika umri wake wa sasa wa miaka 62 anaweza asiruhusiwe tena kugombea urais mwaka 2027 kwa vile atakuwa amevuka miaka 65.

SOMA ZAIDI: Maswali Muhimu Uchaguzi Mkuu wa Kenya Ukielekea Mahakamani

Kwingineko, Babu Atiku Abubakar ambaye naye ana matumaini ya kugombea tena mwaka 2027 anaweza akaungana na wazee wenzake kupinga mabadiliko ya sheria kuweka ukomo wa umri kwa wagombea. Je, Tanzania tunalo la kujifunza katika hilo?

Ni vyema pia kujifunza kuwa siasa nzuri lazima ziwe na ukomo. Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakipigania ukomo wa kikatiba kwa mtu mmoja kushika nafasi ya urais na kwa hili wamefanikiwa.

Kwa sasa, Katiba ya Nigeria inaruhusu mtu kushika nafasi hiyo kwa vipindi visivyozidi viwili vya miaka minne, basi. Rais Buhari mwenyewe hakuruhusiwa kikatiba kuweza kuomba tena ridhaa ya kuongoza Nigeria kama Rais baada ya muhula wake kuisha mwaka 2023.

Ukomo mwingine unaopiganiwa Nigeria ni ukomo wa umri. Katika hili, kazi bado pevu kwa vile ni utamaduni wa miaka kwa wanasiasa wa Nigeria kupenda kugombea uongozi hadi wakiwa ajuza.

Rais mteule Bola Ahmed Tinubu anaanza kipindi chake cha kwanza cha urais akiwa ni babu wa miaka 70 na kikatiba ana miaka hadi nane ya kuwa ikulu. Aidha, Rais Muhammadu Buhari ataongoza taifa hilo hadi akiwa na umri wa miaka 80 atakapokabidhi madaraka kwa Tinubu mwezi Mei mwaka huu.

Makamu wa Rais wa zamani Atiku Abubakar amegombea urais mwaka huu kwa mara ya sita akiwa na umri wa miaka 77. Mara ya kwanza alipojaribu bahati yake ilikuwa ni mwaka 1993 wakati huo akiwa na umri wa miaka 47 kupitia chama cha SDP wakiwa pamoja na Bola Tinubu.

Tangia hapo, Abubakar amejaribu bahati yake bila mafanikio mwaka 2007 kupitia chama cha Action Congress. Mwaka 2011 akijaribu katika hatua ya kura ya maoni ndani ya chama cha PDP na kushindwa na Rais wa wakati huo Goodluck Jonathan.

Bila kukata tamaa, Abubakar alijaribu tena mwaka 2014 baada ya kuwa amejiunga na chama kipya cha akina Tinubu ambapo Abubakar alipoteza katika hatua ya kura za maoni huku Jenerali Buhari akiibuka kidedea.

SOMA ZAIDI: Jumuiya ya Madola Imepoteza Dira, Muelekeo. Hiyo Inaiathiri Vipi Afrika?

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Abubakar alihama tena na kurejea chama cha PDP ambako alifanikiwa kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais ambapo Rais Buhari alishinda.

Akiwa ameamua kusalia katika chama cha PDP, Abubakar alitaraji kuwa angegombea na kushinda urais mwaka huu wa 2023 lakini ni bahati mbaya kwake kuwa mgombea wa chama cha Rais Buhari cha APC, Bola Tinubu ndiye ametangazwa kuwa Rais mteule atakayeapishwa na kuchukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo mwezi Mei mwaka huu.

Funzo usimamizi wa uchaguzi

Kuna jambo pia la kujifunza kuhusu usimamizi wa uchaguzi. Katika nchi yenye idadi ya watu milioni 223, watu wengi wangetaraji kuwa Tume Huru ya Uchaguzi ya Nigeria (INEC) ingefanya juhudi ili kuhakikisha kuwa wapiga kura wengi iwezekanavyo waliojiandikisha wanapiga kura.

Ni bahati mbaya sana kuwa idadi ya kura zilizokidhi vigezo vya kuweza kuhesabiwa imeishia kuwa milioni 25 pekee. Kiwango hiki cha mwitikio wa wapiga kura wa asilimia 26.7 ni kiwango duni sana kuwahi kutokea barani Afrika.

Hata ndani ya Nigeria yenyewe, kiwango hiki kimepungua kwa zaidi ya asilimia nane kutoka kiwango cha mwitikio katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019. Mbaya zaidi, mwenendo unaonesha kuwa mwitikio umeendelea kupungua kila uchao katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Kwa mfano, uchaguzi wa Mwaka 2011 ulishuhudia mwitikio wa wapiga kura wa asilimia 53.68 huku miaka minne baadaye kiwango kilishuka na kufikia asilimia 43.65 na mwaka 2019 kiwango cha mwitikio kilizidi kuporomoka hadi kufikia asilimia 34.75.

SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?

Imekuwa ni masikitiko makubwa kwamba Tume ya Uchaguzi haikufanya juhudi zozote za kupandisha ari ya wapiga kura na kiwango cha mwitikio na badala yake mwaka huu mwitikio umeporomoka zaidi na kufikia asilimia 26.71 pekee.

Nimejiuliza sana kuhusu kiwango cha ufanisi cha Tume ya Uchaguzi na nimegundua kuwa kiko chini mno.

Kwa ushauri wangu, nadhani tume itapaswa kupanguliwa na kusukwa upya ili waingie makamishna na wafanyakazi wenye ari mpya ya kuweza kuhamasisha wananchi wa Nigeria kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi ujao wa mwaka 2027.

Kiukweli, hamasa ndogo pia imedhihirika kupitia idadi ya kura walizovuna wagombea. Kwa mara ya kwanza tangu 1993, nimeshuhudia kura kiduchu mno zikimpa ushindi mgombea wa urais. Jambo la kujifunza hapa ni kuwa wanasiasa hawapaswi kuachiwa huru kuchezea Katiba ya nchi.

Endapo masharti ya Katiba yangebaki kama yalivyokuwa miaka 10 iliyopita, mgombea wa urais angepaswa apate kura nyingi zaidi ya alizopata Tinubu ili atangazwe mshindi. Ushindi wake umekuwa kiduchu zaidi kuliko ushindi wa mgombea yoyote tangu kurejea kwa demokrasia ya uchaguzi nchini Nigeria mwaka 1993.

Kwa mfano, wagombea walioshinda urais miaka iliyopita na kura walizopata ni kama ifuatavyo: kura milioni 18.7 (Olusegun Obasanjo, 1999); kura milioni 24.4 (Olusegun Obasanjo, 2003); kura milioni 24.6 (Umaru Yar’Adua, 2007); kura milioni 22.4 (Goodluck Jonathan, 2011); kura milioni 15.4 (Muhammadu Buhari, 2015); na kura milioni 15.1 (Muhammadu Buhari, 2019).

Ushindi wa Bola Tinubu wa kura milioni 8.7 mwaka 2023 unakaribia kulingana na ushindi wa Moshood Abiola katika uchaguzi wa kwanza wa zama mpya za demokrasia ya uchaguzi Nigeria uliofanyika mwaka 1993 ambapo Abiola, aliyegombea kupitia chama cha SDP, alipata kura milioni 8.34 ambao kwa kipindi hicho hazikuwa haba ikizingatiwa pia kuwa idadi ya wapiga kura ilikuwa bado ndogo.

Kazi na dawa?

Kijamii, nimejifunza pia kuwa wanasiasa ni watu wa ‘kazi na dawa.’ Pamoja na hekaheka zote hizi za kisiasa, wagombea wote walioshindana katika uchaguzi wa Rais mwaka 2023 ni watu wa familia na wana matatizo ya kibinadamu kama raia wengine.

SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiwango Gani Waafrika Wanaweza Kujitatulia Matatizo Yao Wenyewe?

Kwa mfano, wakati Atiku Abubakar akikabiliwa na tuhuma za kuwa na familia kubwa juu ya wastani nchini Nigeria, Rais mteule Bola Tinubu bado hajaweza kuusahaulisha umma wa Nigeria na dunia nzima kuhusu tuhuma zilizomkumba akiishi Marekani katika miaka ya ‘90 kwamba alikuwa akijihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.

Vivyo hivyo, Abubakar naye aliwahi kuwa na tuhuma za vitendo vya rushwa nchini Marekani kiasi cha kutoweza kuzuru nchi hiyo kwa miaka mingi na pale Serikali ya Marekani ilipoulizwa juu ya ukweli wa tuhuma hizo, Washington ilisema kuwa inahitaji ridhaa ya Atiku Abubakar mwenyewe ili kumwaga ukweli wa mambo juu ya kwa nini asingeweza kusafiri kwenda Marekani.

Kwa tafsiri ya watu wengi, ilionekana kuwa kuna siri nzito juu ya kilichokuwa kimemsibu Atibu wakati alipokuwa huko ughaibuni.

Ukiachilia mbali masuala ya kashfa, wanasiasa wakuu wa Nigeria wana vijimambo vya kifamilia kama mimi na mtu mwingine yeyote.

Kwa upande wa Makamu wa Rais mstaafu Abubakar, kumekuwa na mambo ya hapa na pale kuhusu taarifa za familia yake. Kwa utafiti wangu, Bwana Abubakar amewahi kuwa na wake rasmi zaidi ya wanne na talaka kadhaa.

Kwa mfano, mkewe wa kwanza Bi Titilayo Albert aliolewa kisiri mwaka 1971 kutokana na kwamba familia ya Atiku haikuwa imeridhia ndoa hiyo. Hilo lilimfanya Titi aishi kinyemela na Atiku kwa miaka kadhaa hadi mwaka ya 1979 wakati ambapo Atiku aliamua kuoa mke mwingine kwa jina la Ladi Yakubu na kumtangaza kama mke wa pili akimrasimisha Titilayo Abubakar kama mke rasmi wa kwanza.

Kwa bahati mbaya, Atiku alikuja kutalikiana na Ladi baada ya kuzaa naye watoto kadhaa. Hapo kati, Abubakar aliongeza mke mwingine, mwana mfalme Rukkaiya Atiku-Abubakar ambaye ndoa yake ilifungwa mwaka 1983.

SOMA ZAIDI: Afrika Na Demokrasia Bado Mguu Ndani, Mguu Nje

Huku na huku, Atiku alibaini kuwa idadi ya wake wanne anaoruhusiwa kwa mujibu wa dini ya Kiislamu walikuwa hawajatimia na akaamua kumuoa Bi. Jenifer Iwemjiora Douglas ambaye naye aliutangazia umma wa Nigeria na dunia nzima ilipofika tarehe Februari 1, 2022, kuwa ameachana na Atiku kutokana na tofauti zao juu ya masuala kadhaa ya kifamilia, ikiwemo kuishi kwake Uingereza, umiliki wa nyumba na mali zilizoko Nigeria na nyingine Dubai pamoja na tofauti nyingine zilizoshindwa kutatulika kwa mazungumzo.

Kwa bahati nzuri, wakati hayo yakiwa yanaendelea, Atiku alikuwa ameshafanya maamuzi ya kumuoa Fatima Shettima na kufanya hadi leo kuendelea kuwa na wake rasmi wanne na watoto zaidi ya 28.

Akihojiwa na vyombo vya habari wakati fulani juu ya ukubwa wa familia yake, Atiku aliwahi kusema kuwa yeye aliishi na alikuwa bila kaka wala dada na hakutamani wanawe waje waishi kwa upweke kama alioishi yeye.

Kwa hakika, wanasiasa ni binadamu kama tulivyo wengine na wana upande wa shilingi ambao ni wa maisha ya kawaida ya mtaani.

Wanasiasa na bata

Maisha binafsi ya Bola Tinubu nayo yamenifunza mambo machache. Kwanza, kwamba wanasiasa ni watu wa bata. Baada ya maisha ya awali na masomi nchini Nigeria na Marekani, Tinubu alipata mahusiano kadhaa wa kadha ambayo yalimpatia watoto watatu, kwa uchache: Kazeem Olajide (1974); Folashade (1976) na Oluwaseyi (1985).

Baada ya kuanza kufikiria siasa za Ikulu, Tinubu aliamua kufunga rasmi pingu za maisha na mwanasiasa mwenzake na mbunge Oluremi Tinubu mwaka 1987. Huku nako, Tinubu amebahatika kupata watoto watatu.

Kwa bahati mbaya, Olajide alifariki Jijini London mwishoni mwa Oktoba 2017 na iliwashangaza wengi kuwa mtoto wa wanasiasa mkubwa kama Bola Tinubu alianza kuzua utata juu ya siyo tu chanzo cha kifo chake bali pia umri wake halisi.

Kuhusu uchaguzi wa mwaka 2023, Nigeria imetuachia mambo mengi ya kutafakari. Kwa mfano, uchaguzi uliogharibu kiasi kikubwa cha fedha jumla ya Naira bilioni 305 (zaidi ya Shilingi trilioni 1.5 za Kitanzania) umewezaje kuwa na kasoro nyingi kama ilivyojitokeza?

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Nigeria, Mahmood Yakubu na tume yake wanawezaje kujitetea kuhusu watu wengi walioshindwa hata kuona majina yao na vituo walivyopangiwa kwenda kupiga kura? Nini kilipelekea vituo vilivyo vingi kuchelewa kufunguliwa au kutofunguliwa kabisa?

 

Ni kwa nini tume haikuweza kupanga muda au siku mbadala ya kuwapa fursa wananchi walioshindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kuweza kufanya hivyo? Je, kushindwa kufanya kazi kwa mifumo na vifaa vya kidigitali (BVAS na BVR) hata baada ya kuvinunua kwa mabilioni ya pesa kunaiambia nini Afrika juu ya utegemezi wetu kwenye teknolojia kutoka nje ambayo mara zote imetuangusha?

Rais mteule Tinubu anarithi nchi yenye matatizo lukuki, ikiwemo mpasuko wa kimajimbo, kiitikadi na kikabila. Je, anapaswa kufanya nini ili kujenga Nigeria iliyo moja na yenye umoja?

Na mwisho, je, Tanzania tunajifunza nini kutokana na uchaguzi wa Rais nchini Nigeria na maisha ya wanasiasa waliogombea uchaguzi huo?

Mungu ibariki Afrika!

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts