The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Ubadhirifu Serikalini Unaweza Kudhibitiwa? Wataalamu Wanaamini Hivyo

Wataka kuwekwe mifumo imara itakayohakikisha uwajibikaji Serikalini.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wataalamu wa masuala ya usimamizi wa fedha za umma wanaamini kwamba ubadhirifu Serikalini unaweza kudhibitiwa endapo tu kama mamlaka husika zitaweka mifumo imara itakayohakikisha uwajibikaji wa watendaji watakaobainika kutokuwa waadilifu.

Wakizungumza wakati wa mjadala ulioandaliwa na Policy Forum, asasi ya kiraia inayosimamia uwazi na uwajibikaji Serikalini, hapo Aprili 28, 2023, jijini hapa, wataalamu hao wamebainisha kwamba kuendelea kukithiri kwa ufujaji wa fedha za umma kunatokana na kutokuwepo kwa mifumo imara inayohakikisha uwajibikaji Serikalini.

Mjadala huo ni sehemu ya mazungumzo mapana yanayoendelea nchini Tanzania hivi sasa tangu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere afichue upotevu wa kiwango cha juu wa fedha za umma kwenye idara na mashirika kadhaa ya Kiserikali.

Kwenye ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 aliyoikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan hapo Machi 29, 2023, Kichere alibaini mambo kadhaa yanayohusiana na usimamizi usio sawa wa fedha za umma, akibainisha mapendekezo kadhaa ya namna hali hiyo inavyoweza kuzuiwa isijirudie kwenye mwaka wa fedha unaofuata.

Akichangia kwenye mjadala huo uliofanyika katika hoteli ya Four Points by Sheraton, CAG mstaafu Ludovick Utouh alisema kwamba ifike mahala watendaji wanaobainika kuwa wabadhirifu wachukuliwe hatua kali za kisheria badala ya kuhamishiwa kwenye idara nyingine ya Serikali.

Maumivu binafsi

“Kuwe na utaratibu wa kurudisha ile pesa iliyoibiwa,” alisema Utouh ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIBU, asasi ya kiraia inayohusika na masuala ya uwajibikaji. “Kwa sababu, kama mtu amewakwapulia mabilioni, ukimsimamisha kazi si ndiyo unampa nafasi ya kwenda kuzitumbua zile pesa?”

Pendekezo hili la kuwawajibisha watendaji pia liliwahi kutolewa na CAG mstaafu Profesa Mussa Assad ambaye alishauri kwamba ili kuhakikisha utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, watendaji wa Serikali wanapaswa kulazimishwa kuyatekeleza mapendekezo hayo.

Profesa Assad, ambaye kwa sasa ni Naibu Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), alitoa pendekezo hilo wakati wa mahojiano na runinga ya AZAM TV baada ya CAG Kichere kubainisha kwenye ripoti yake kwamba kati ya mapendekezo 6,947 aliyoyatoa kwenye ukaguzi wake wa 2020/2021, ni mapendekezo 2,506 tu, sawa na asilimia 36, ndiyo yaliyotekelezwa.

SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini

“Kwanza ni maumivu binafsi,” Assad alisema alipoulizwa Serikali ifanye nini kuhakikisha mapendekezo ya CAG yanatekelezwa. “Kama mkuu wa shirika hujatekeleza mapendekezo, basi unatakiwa kuwajibika, nchi nyingine zinafanya hivyo.”

“[Kwa] mfano, usipotekeleza mapendekezo ya CAG basi mshahara wako utapunguzwa kwa asilimia tano hadi asilimia 10 kila mwezi, hiyo inamaanisha ikimalizika miezi 10 hutakuwa na mshahara kabisa.

“Pia, watu hao [wasiotekeleza mapendekezo] wanaweza kuingizwa katika ‘blacklist,’ yaani wanakuwa katika orodha ya watu ambao wanaonekana hawafai, hivyo wanakuwa hawapati nafasi nyingine Serikalini,” Profesa Assad alibainisha kwenye mahojiano hayo.

Njia nyingine ambazo Utouh amependekeza na ambazo anaamini kama zitatekelezwa zitasaidia kudhibiti ubadhirifu Serikalini ni nafasi za wakuu wa mashirika ya umma yenye lengo la kuzalisha faida zipatikane kwa njia za kiushindani badala ya uteuzi kama ilivyo hivi sasa.

Pia, Utouh anataka ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iwekwe hadharani kama vile ambavyo ya CAG huwekwa hadharani kwa ajili ya kujadiliwa, akisema hatua hiyo ni muhimu kwani itachochea uwazi na uwajibikaji Serikalini.

SOMA ZAIDI: Fahamu Kuhusu Tausi, Mfumo Mpya wa Ukusanyaji Mapato Serikalini

“Kwa nini hii ripoti imekabidhiwa kwa Rais na haijawekwa wazi kwa umma kama ilivyo kwa ripoti ya CAG iliyokabidhiwa kwa Rais kwenye tarehe hiyo hiyo?,” alihoji Utouh. “Sisi tunadhani ripoti hii nayo itolewe kwa umma kwa ajili ya kujadiliwa.”

Utamaduni wa upigaji

Pengine kinachowauma wananchi walio wengi ni kuona ni kwa namna gani ripoti zilezile za ubadhirifu wa kupitiliza zinaripotiwa na CAG kila mwaka kwenye taarifa zake za ukaguzi.

Hali hii ya kujirudia kwa taarifa hizi imewafanya baadhi ya wadadisi kuhoji endapo kama ufisadi unatokana na udhaifu wa Serikali au ni sehemu ya tatizo pana la kijamii?

Akiandika kwenye The Chanzo kuhusiana na ripoti ya CAG kwa mwaka 2020/2021, mchambuzi Njonjo Mfaume alisema ubadhirifu Serikalini ni matokeo ya kuwa na jamii inayotukuza ufisadi.

“Jambo la msingi hapa ni kuwa vita dhidi ya ufisadi na rushwa lazima ipiganwe kwa mbinu tofauti,” aliandika Mfaume, akisisitiza umuhimu wa elimu kwa umma. “Ni kurahisisha tatizo gumu na kujidanganya kudhani kuwa ukali wa viongozi pekee utaondoa ufisadi.”

SOMA ZAIDI: Ripoti ya CAG: Je, Ufisadi Unatokana na Udhaifu wa Serikali au ni Tatizo la Kijamii?

Dhana hii ya kujengeka kwa “utamaduni wa upigaji” katika jamii aliibua pia Mkurugenzi Mtendaji wa Policy Forum Semkae Kilonzo kwenye mjadala huo uliofanyika hoteli ya Four Points ambapo alibainisha kwamba vita dhidi ya ufisadi haiwezi kukoma kwa kufukuzwa kwa mtendaji wa idara fulani tu ya Serikali aliyebainika kuwa mbadhirifu.

Mtazamo huo ulitokana na baadhi ya hatua ambazo Rais Samia amechukua kufuatia ripoti hiyo ya ukaguzi, hatua ambazo zimemuhusisha yeye akisimamisha kazi watendaji waandamizi wa idara zilizotajwa na CAG kuhusika katika upotevu mkubwa wa fedha za walipa kodi.

“Sawa tunaweza kusema hiyo ni mifano ya hatua lakini kwangu mimi naona kama haijitoshelezi kwa maana ya kwamba huwezi ukamfukuza mkurugenzi wa taasisi fulani ya umma lakini ili ubadhirufu utokee, au wizi utokee, waziri au mkurugenzi peke yake hatoshi,” Kilonzo alisema.

SOMA ZAIDI: Nini Kifanyike Kuboresha Mfumo wa Kodi 2023?

“Kuna mifumo pale na wataalamu wa kucheza na mifumo ni wale waliopo chini. Kuna utamaduni fulani hizi taasisi zetu za umma wa kusema kwamba watakaowajibishwa ni wale waliopo juu, wenye dhamana za kisiasa, sisi huku huwa hatuguswi,” aliongeza.

Kuvunja utamaduni huu imekuwa ni moja ya vitu ambavyo wadau kadhaa wamekuwa wakijaribu kupendekeza namna zinazoweza kufanikisha lengo hilo.

‘Lifestyle audit’

Mmoja kati ya watu hawa ni Mwenyekiti wa chama cha upinzani CHADEMA Freeman Mbowe ambaye amependekeza kufanyika kwa kitu alichokiita ‘lifestyle audit’ ya watendaji wa Serikali kama sehemu ya juhudi za kitaifa za kupambana na ufisadi nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu hapo Aprili 14, 2023, Mbowe alisema kwamba ufisadi nchini Tanzania umefikia katika viwango ambavyo kufanya uhakiki wa mahesabu tu ya kifedha haitoshi bali kunahitajika kufanyika kwa uhakiki wa mitindo ya maisha ya viongozi wa Serikali.

“Lazima tuanze kufanya uhakiki wa mtindo wa maisha,” alisema Mbowe kwenye hafla hiyo. “Huyu mtu anaishi maisha haya, kipato chake kipoje? Hili jambo [la ufisadi] halipaswi kuwa jambo la kufanya mzaha. Ni suala la maisha yetu.”

SOMA ZAIDI: Mbowe Ataka Hatua Zaidi Zichukuliwe Kukabiliana na Ufisadi

Mbowe pia aliwakosoa waandishi wa habari nchini, akisema bado hawajachukia sana mambo ya ufisadi yanayotokea nchini, akisema endapo kama watachukia vya kutosha, wana uwezo wa kuzuia tabia hiyo kuendelea kulitesa taifa.

Tathmini hii iliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) Dastan Kamanzi ambaye kwenye mjadala huo ulioandaliwa kwa ushirika wa Policy Forum na WAJIBU alisema kwa sasa Tanzania ina uandishi wa habari wa uwajibikaji kwa kiwango kidogo sana.

Kamanzi alisema kazi ya uandishi wa habari haitakiwi kuwa ni tukio la siku moja tu kuripoti alichosema CAG na kuacha mpaka pale CAG atakapokuja tena na ripoti yake ndiyo waandishi wa habari wafanye habari kuhusu uwajibikaji.

Mtaalamu huyo amesema kazi ya kufichua ubadhirifu Serikalini inapaswa iwe ni kazi ya kila siku ya vyombo vya habari, kitu ambacho kwa mtazamo wake anaona hakifanyiki kwa kiwango cha kuridhisha nchini Tanzania kwa sasa.

“Kwa hiyo, utagundua kwamba uandishi wa habari ambao ni wa kukosoa, ambao unalenga kuwajibisha Serikali na kuwafanya umma uweze kuwa na maamuzi ya busara, nitakwambia kwamba tuna uandishi wa namna hiyo mdogo sana,” alisema.

Lukelo Francis ni Mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts