Afrika ipo katika kipindi cha joto kubwa la kuipokea, kwa mara nyingine tena, moja ya nchi zenye uchumi mkubwa na ushawishi duniani, Urusi.
Urusi, hata hivyo, haipo Afrika kusambaza sera za kikomunisti au kutafuta ushirika na mataifa yenye siasa za mwelekeo huo kama ilivyokuwa mwanzoni mwa miaka ya 1960. Taifa hilo la Mashariki mwa Ulaya lipo Afrika kufanya biashara na kuongeza nguvu ya ushawishi kupitia mwamvuli wa ulinzi na usalama.
Hali ya usalama barani la Afrika, hususan katika ukanda wa Sahel na Afrika ya Kati, imeendelea kuwa ya kutoridhisha kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na makundi ya kigaidi. Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania, na Niger ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa sana na mdororo huu wa usalama.
Hali hii imewapelekea wananchi katika nchi hizi kuzishinikiza Serikali zao kuongeza jitihada katika kupambana na ugaidi, hali iliyozilamisha Serikali hizo kuomba msaada kwenye mataifa mbalimbali. Ufaransa lilikuwa moja kati ya mataifa ya awali kuombwa msaada na mataifa hayo iliyowahi kuyatawala.
Kama kudhihirisha nia yake ya kusaidia, Ufaransa ikapeleka takribani wanajeshi 4,500 kulinda amani katika ukanda huo uliopewa jina la ‘G5 Sahel’ kupitia ‘Operation Barkhane.’ Hata hivyo, uwepo wa Ufaransa kwenye ukanda huo umechangia kwa kiwango kidogo sana kuimarisha hali ya ulinzi katika ukanda huo.
Mapinduzi ya kijeshi
Kuzorota kwa hali ya usalama kukaanza kuangusha Serikali katika nchi za ukanda huo, huku wanajeshi wakipindua kwa kisingizio cha kuimarisha hali ya usalama kwenye nchi hizo.
Mnamo Mei 24, 2021, kwa mfano, Rais Bah Ndaw wa Mali alipinduliwa na jeshi lake likiongozwa na Makamu wake, Kanali Assimi Goita. Nchini Burkina Faso nako mtiririko wa mapinduzi ya kijeshi yametokea, hoja ikiwa ni ile ile kwamba Serikali nchini humo imeshindwa kuimarisha hali ya usalama.
Kwa namna hali inavyoonekana hivi sasa, wananchi wengi kutoka nchi hizi wameonekana kuweka matumaini yao kwa Serikali hizi mpya za kijeshi kwenye mapambano dhidi ya ugaidi. Hata hivyo, Serikali hizi za kijeshi pia zina sifa moja inayofanana: chuki dhidi ya mkoloni wao wa zamani Ufaransa, na mapenzi kwa Urusi.
SOMA ZAIDI: Jumuiya ya Madola Imepoteza Dira, Muelekeo. Hiyo Inaiathiri Vipi Afrika?
Urusi inakisiwa kuanza kuingia kwenye ukanda huu angalau mwaka 2018 pale kundi la wanajeshi mamluki linalofanya kazi sambamba na Serikali ya Urusi chini ya kampuni ya Wagner lilipelekwa nchini Afrika ya Kati (CAR) kwa lengo la kile kilichoitwa “kulinda viongozi na Serikali” ya Rais Faustin-Archange Touadera.
Kipindi hicho, Serikali ya Touadera ilikuwa inakumbwa na vitisho vya vurugu na mapinduzi kutoka kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Francois Bozize.
Wagner wakafanikiwa kutekeleza majukumu hayo yaliyoshindwa na jeshi la Umoja wa Mataifa (MINUSCA) pamoja na jeshi la Ufaransa kwa zaidi ya miaka tisa. Mafanikio haya yalipaisha sifa kundi hili la Wagner barani Afrika.
Ushindi zaidi kwa Wagner
Mnamo mwaka 2021, Serikali ya Mali chini ya Kanali Assimi Goita ilialika “wakufunzi” wa kijeshi kutoka Urusi ambao Serikali ya Ufaransa ilidai ni wanajeshi mamluki kutoka kikundi cha Wagner.
Hatua hii ilileta msuguano baina ya nchi hizi mbili kiasi cha kupelekea kufukuzwa kwa Balozi wa Ufaransa nchini humo.
Februari 2022 Serikali ya Ufaransa ikatangaza kuondoa majeshi yake nchini Mali na hatua hiyo ilipokelewa kwa shangwe na wananchi wa Mali, huku wakishangilia wakiwa wamebeba bendera ya Urusi. Hii ilikuwa ni ishara ya kupokelewa nchi ya Urusi kama mbadala wa Ufaransa katika sekta ya ulinzi na mapambano dhidi ya ugaidi.
SOMA ZAIDI: Nini Maana ya Ukimya wa Afrika Kwenye Mgogoro wa Urusi na Ukraine?
Wimbi hili lilienda na kufika nchini Burkina Faso ambapo wananchi wake waliipokea Urusi sawa na ilivyopokelewa nchini Mali.
Mapokeo haya yaliziudhi nchi nyingi za Magharibi kiasi cha Marekani kutangaza kuitoa Burkina Faso kama mnufaika wa mkataba AGOA, kwa kosa la “kutokukidhi sifa” ya utawala wa sheria na demokrasia.
Kura ya turufu?
Kujikita katika sekta ya ulinzi na usalama inaonekana kuwa ndiyo karata itakayoipa Urusi kura ya turufu na kuendelea kubaki Afrika kwa muda mrefu, ikizingatiwa migogoro katika bara la Afrika inaongezeka kila uchwao.
Nchi za Chad, Sudan, na Libya zimekuwa zikiripotiwa kushirikiana na Urusi kwenye masuala ya usalama.
Kufanikiwa kupenya kuwa sehemu ya maamuzi katika Serikali hizi za ukanda wa Sahel kunatengeneza njia ya kuwa na ushawishi katika eneo zima la nchi za Afrika Magharibi ambazo zimekuwa pia zikiathiriwa na hali ya ukosefu wa amani katika ukanda huo.
Huko nchini Libya, kiongozi anayetawala mashariki mwa nchi hiyo, Jenerali Khalifa Haftar, amekuwa mshirika wa karibu na Serikali ya Urusi kwa kuendelea kumpa wataalam na silaha za anga.
SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?
Ushirikiano huu unautesa nchi za Magharibi na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Ulaya (NATO) kwa kuwa mji wa Tripoli upo Maili 600 kutoka mji wa Rome, Italia.
Hivyo, Urusi kuishika Libya kutaweka vizuizi vya operesheni nyingi za kijeshi za NATO barani Afrika kupitia mlango wa Libya-Italia. Pia, kutaiweka Ulaya katika mkondo wa wasiwasi kwa kuwa Urusi atakuwa anazidi kusogea mlangoni kwake.
Hivyo, endapo Urusi atafanikiwa Libya, kutampa kura ya turufu kwenye majadiliano ya usalama wa bara la Ulaya hasa nchi za magharibi, suala ambalo inaonekana itakuwa ni mwelekeo wa njia ya kuidhoofisha NATO.
Kupenya huku kwa Urusi barani Afrika kunaonekana kama ni njia ya kutengeneza na kulinda viongozi na maslahi yao, hususan ikizingatiwa uwezo wake wa kulinda viongozi kama ilivyo katika nchi ya Afrika ya Kati (CAR).
Lakini pia ikumbukwe Urusi ilishalalamikiwa na Marekani juu ya kushiriki na kumwezesha Rais Donald Trump kushika madaraka. Ikiwa ni kweli Urusi walifanikiwa kuuchezea mfumo wa uchaguzi wa Marekani, vipi kuhusu chaguzi hizi za mataifa ya Afrika?
SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiwango Gani Waafrika Wanaweza Kujitatulia Matatizo Yao Wenyewe?
Mwezi Julai 2023, Afrika yote itakusanywa Jijini St. Petersburg, Urusi katika mkutano wa Russia-Africa Economic and Humanitarian Forum ambao mataifa haya yatakutana pamoja kujadiliana kuhusu mashirikiano ya kiuchumi na misaada ya kibinadamu.
Mkutano huu unatarajiwa kuongeza maeneo zaidi ya mashirikiano ukiendeleza maeneo yaliyokubaliwa katika mkutano wa kwanza wa Oktoba 2019.
Awamu hii kunatarajiwa kuwepo na makubaliano makubwa zaidi hasa ikizingatiwa na mafanikio ya nchi hiyo barani Afrika katika sekta za ulinzi, usalama, biashara na uwekezaji yaliyopatikana kwa zaidi ya miaka minne.
Maslahi binafsi ya viongozi
Serikali nyingi za Afrika hitaji lao limekuwa siyo kuandaa, kutekeleza, na kusimamia maendeleo ya wananchi wao bali kuhakikisha wanalinda maslahi yao na washirika wao wa kiutawala wa nje na ndani.
Kwa kuwa nchi ya Urusi imeshadhihirisha kwamba inaweza kulisimamia hilo, ni wazi viongozi wengi barani Afrika wanaweza kuwa “wateja wa huduma” hii mujarab inayotolewa na nchi hii.
SOMA ZAIDI: Afrika Na Demokrasia Bado Mguu Ndani, Mguu Nje
Hata hivyo, ni vyema kutambua kuwa mataifa ya Ulaya pamoja na Marekani yaliingia Afrika kupitia njia inazoingia nazo Urusi sasa hivi, hasa kupitia chaguzi au mapinduzi.
Mataifa hayo yakawalinda viongozi wa Afrika kwa kutumia vyombo vya ulinzi, asasi za kiraia, propaganda za maendeleo, uchumi wa vitu, vyama dhaifu na pandikizi vya upinzani, vyombo vya habari, mikopo, na mipango ya matumaini ya maendeleo isiyotekelezeka.
Kinachopiganiwa na mataifa haya makubwa kwa sasa siyo ustawi wa Afrika bali ni nguvu ya umiliki wa mataifa hayo kwenye dunia ya sasa.
Afrika inatumika kama karata ya ushindi. Kwa mataifa haya makubwa, Afrika ni kama kete tu kwenye mchezo. Hivyo, itoshe kusema kuwa Afrika itaendelea kuchezewa mpaka pale itakapopata akili!
Ezra Nnko ni mwana-Majumui wa Kiafrika na mchambuzi wa uchumi, siasa na sera za kimataifa. Anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917 na +255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
2 responses
Ezra. Andiko zuri sana nimestafidi na kutafakari sana
Ni makala makini. Hasa pale unapobainisha kwamba “Serikali nyingi za Afrika hitaji lao limekuwa siyo kuandaa, kutekeleza, na kusimamia maendeleo ya wananchi wao bali kuhakikisha wanalinda maslahi yao na washirika wao wa kiutawala wa nje na ndani”. Kwangu mimi siyo jambo baya Urusi kutafuta washirika wa kibiashara, kiusalama na kiulinzi barani Afrika. Tatizo ni pale ambapo watawala wetu wanapoingia kwenye makubaliano na mataifa haya ya nje bila kuwa na masilahi yao ya kitaifa ya kimkakati. Lazima tujijengee utayari na uwezo wa kuyatafsiri vizuri malengo na nia halisi ya mahusiano yetu na mataifa haya makubwa ya dunia.