The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Kusiathiri Haki Zingine za Wanajamii

Ulinzi wa mazingira usifanyike kwa gharama za maisha na haki za wanajamii.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Maelezo yanayofuata yametolewa kutoka sauti kwenda kwenye maneno kutoka kwenye mahojiano maalum ambayo The Chanzo imefanya na Dk Baruani Mshale, mtaalamu wa masuala ya maliasili na mabadiliko ya tabianchi. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji.

Suala la muingiliano baina ya maendeleo pamoja na mazingira, ni suala ambalo mdahalo wake umekuwapo, na siyo mdahalo tu kwa maana ya mdahalo, ni suala ambalo ni kweli lipo, kwa sababu kama ambavyo tu katika ngazi ya dunia, tumeona kwamba maendeleo ya kasi ya binadamu yamepelekea uharibifu wa kiasi kikubwa wa mazingira, ikiwemo haya mabadiliko ya tabianchi ambayo tunakabiliana nayo sasa. 

Ina maana hata sisi Tanzania, kadri tunavyotaka kufanya shughuli ambazo zitatuletea maendeleo yetu, kuanzia kipato cha kaya mpaka kipato cha kitaifa, lazima tuzingatie, tuangalie kwamba mbinu tunazozitumia haziwi na athari hasi katika mazingira yetu, au kuongeza tatizo na mabadiliko ya tabianchi.

Na hili limekuwa ni eneo moja wapo ambalo limeleta tafrani sana ndani ya nchi lakini pia na kimataifa. Ndani ya nchi, tunafahamu namna ambavyo, kwa mfano, Serikali katika jitihada za kuhifadhi mazingira huwa inafikia mahali watu wa maeneo fulani wanaondolewa ili kuweza kuhifadhi yale maeneo kwa sababu za kimazingira. 

Watu wa Ngorongoro hivi karibuni, kwa mfano, kuongezeka kwa idadi pale Serikali inasema kwamba wanaharibu mazingira nakadhalika. 

​​SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Ni Nini? Mtaalam Afafanua

Lakini tukija katika ngazi za kimataifa, nchi zilizoendelea, zimekuwa zikitulaumu, na hii ilikuwa ni mjadala zaidi katika miaka 20 iliyopita, kwamba sisi ambao tuko kwenye nchi zinazoendelea basi tuhakikishe kwamba maendeleo yetu hayasababishi matatizo zaidi katika mazingira. 

Hiyo imeleta hali ya kutokuelewana baina ya hizi pande mbili za dunia, nchi zinazoendelea na nchi ambazo zimeendelea, kwamba kwa nini wao walichafua mazingira, waliharibu mazingira, na kupelekea mabadiliko ya tabianchi, halafu sasa hivi watuzuie sisi kuweza kufanya ile shughuli wakati watu wetu wanahitaji chakula, tunahitaji nishati, tunahitaji mahitaji mengine mengi tu? 

Pamoja na kwamba hatua hizi zinasababisha athari kwenye mazingira lakini hatuwezi tukasema kwamba kizazi chetu sasa hivi kife ili kupisha kizazi cha wenzetu ambao wako katika nchi zilizoendelea waweze kuendelea kuishi vizuri kwa sisi kutokufanya vitu ambavyo vitatusababishia kutuletea maendeleo. 

Huo mjadala ulikuwepo kwa kutokukubaliana baina ya pande mbili ndiyo kukapelekea, kadiri miaka ilivyokuwa inaenda, na kuweza kufikia makubaliano hasa katika ngazi za kimataifa kwamba basi lile jukumu la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wapewa zaidi wale ambao wana uwezo na ndiyo walisababisha hili tatizo kuliko sisi ambao tunatokea katika nchi ambazo hatusababishi tatizo kwa kiasi kikubwa, lakini sisi ndiyo ambao tunaathirika zaidi. 

SOMA ZAIDI: Nini Hupelekea Mabadiliko ya Tabianchi?

Kwa hiyo, hiyo ikapalekea, kwa mfano, katika Jumuiya ya Kimataifa kuna ile jumuiya ambayo inajulikana kama United Nations Framework Convention on Climate Change (UNFCCC), ambao ni mpango wa kushughulika na kukabiliana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi, kuja na mbinu ambazo zitatumika kwa nchi zinazoendelea na katika nchi zilizoendelea.

Maendeleo safi

Moja wapo ilikuwa inaitwa ni Clean Development Mechanism (CDM), yaani maendeleo ambayo ni safi katika muktadha wa mazingira. Na maendeleo haya ni, kwa mfano, badala ya kutumia balbu hizi za taa ambazo zinatumia nishati nyingi, kuwezeshwa kutumia balbu ambazo hazitumii nishati nyingi. 

Na kunakuwa na utaratibu wa zile nchi ambazo zinatumia mfumo huo mpya kuweza kufidiwa kwa kuacha kutumia ile teknolojia ambayo ni haribifu, teknolojia ambayo ina athari kwenye mazingira, watakapotumia teknolojia ambayo ni safi zaidi kuweza kufidiwa, kifedha, kutokana nakiasi ambacho kimepimwa cha hewa ukaa ambacho kimezuiwa kwenda kwenye anga kwa sababu ya kutumia teknoloji ambayo ni safi. 

Na kwamba ni jukumu la nchi zilizoendelea kuzisaidia nchi zinazoendelea kuweza kutumia hizo teknolojia, au mifumo, ambayo haitakuwa na athari hasi katika mazingira.

Eneo jingine ilikuwa ni katika kupunguza na kuzuia hewa ukaa itokanayo na ukataji wa misitu, ukataji wa miti na misitu. Miradi ile ya Tanzania ambayo ilijulikana kwa jina MKUHUMI ilifanyiwa majaribio na ikaonesha uwezekano wa kuchangia katika maendeleo na maisha ya watu katika maeneo yetu katika nchi zinazoendelea. 

SOMA ZAIDI: Nini Kinadhihirisha Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania?

Lakini vilevile, kuchangia katika kupunguza kiasi cha hewa ukaa ambacho kinazalishwa. Kwa hiyo, malumbano haya baina ya mazingira na maendeleo yamekuwepo lakini pamekuwa na mbinu tofautitofauti ambazo zinatumika kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha maisha yetu bila kuchafua mazingira. 

Na sisi tunakuwa katika nafasi ya kuweza kuchukua ile fursa badala ya kurudia makosa ya wenzetu tunajifunza kutokana na makosa yao na kutumia zile teknolojia kadri zilivyo, ambavyo ziko sasa, na tuweze kuepusha matatizo kwenye mazingira.

Changamoto

Lakini kuna changamoto na siyo kwamba haya masuala yanafanyika kiurahisi tu. Kwa sababu, kwa mfano, Tanzania tuna makaa ya mawe na hivi karibuni, nadhani, watu watakuwa wanafahamu kwamba nchi za Ulaya wanataka kuzuia, sikumbuki ni mwaka gani haswa, nadhani ni kuanzia mwaka 2027 ndiyo wataanza kuleta hizo sera za kuzuia magari ambayo yanatumia petroli na dizeli badala yake wawe wanatumia magari yanayotumia nishati mbadala zaidi. 

SOMA ZAIDI: Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Huathiri Maisha, Uchumi wa Watanzania

Kama hiyo itafanyika, ina maana sisi gesi yetu asilia, makaa ya mawe tunayozalisha, tutakosa wa kwenda kumuuzia. Sasa kusikia kwamba nchi zingine watazuia kuagiza au kununua gesi asilia au makaa ya mawe kunapelekea nchi ambazo zina hayo makaa ya mawe au zina mafuta asilia kuzalisha kwa wingi sasa hivi na kuuza kwa kuhofia kwamba baadaye watakosa wa kumuuzia.

Kwa hiyo, hiyo inaweza ikawa, pamoja na kwamba kuna nia nzuri ya kuondokana na hizi teknolojia ambazo zinachafua mazingira, lakini kwa sababu za kiuchumi kuona sasa hii gesi makaa ya mawe tutamuuzia nani, inapelekea yazalishwe mengi sasa hivi na kutumika kwa wingi na kuharibu mazingira. 

Kiasi kwamba hata zile faida zitakazokuja kupatikana baadaye za kuachana nayo zikawa ni kidogo tofauti na hii athari ambayo imesukumwa kutokana na kusikia kwamba hakutakuwa na soko la wapi tutauza hayo makaa ya mawe. 

Haki za wanajamii

Lakini vilevile kingine ambacho naweza nikakizungumzia hapo ni kwamba, kwenye huu mjadala wa mazingira na maendeleo umepelekea kuibua kitu kingine ambacho ni kuangalia masuala haya ya mabadiliko ya tabianchi katika lenzi ya masuala ya haki na usawa ambayo inaitwa climate justice

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Apangua Hoja za Wanaopinga Uwepo wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi

Kwamba mbinu zozote zinazotumika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zisipelekee athari hasi kwa jamii za watu katika maeneo tofauti duniani. Kama tunasema kwamba misitu isikatwe, tufahamu kwamba wanaokata ile misiti wanakata kwa sababu wanahitaji kujikumu kimaisha, wanahitaji na wao kuishi, wanahitaji chakula, nakadhalika. 

Je, tunapowaondoa kwa nguvu kutoka katika yale maeneo, tunawapa kitu gani mbadala? Wanaweza kweli kuishi maisha ambayo ni maisha yenye hadhi na stahiki kama binadamu? Au tunawalazimisha kuishi maisha ambayo ambayo hayana utu, hayana heshima, kwa sababu tu tunasema tunataka kutunza mazingira?

Kwa hiyo, hili eneo la climate justice inatusaidia kuweza kuangalia mbinu tofauti tofauti ambazo zinatumika katika kukabiliana na masuala haya ya mabadiliko ya tabianchi ziweze kuhakikisha kwamba hazipelekei athari hasi kwa jamii tofauti tofuati duniani.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi?

Tusiseme sisi tunataka kuhifadhi halafu tunaathiri maisha ya watu wengine. Hiyo inakuwa siyo sawa. Huwatendei haki wale watu katika ngazi ya nchi na pia katika ngazi ya kimataifa kuangalia nchi zilizoendelea na nchi ambazo zinaendelea. 

Hapo ndipo ambapo tunaweza tukasema kwamba jamii ya kimataifa ndiyo ipo kwa sasa na kila mbinu yoyote ambayo inapendekezwa, pamoja na kuangaliwa kwamba itatatua vipi tatizo la mabadiliko ya tabianchi, itakuwa na faida gani kwenye mazingira, nakadhalika. 

Lakini imeshakuwa wazi sasa hivi kwamba ni lazima pia kuweza kuangalia itakuwa na athari gani kwa jamii za watu. Kama itakuwa na athari hasi, hata kama itakuwa na athari ambazo zitakuwa ni chanya kwenye kwenye mazingira, lazima iangaliwe tena upya ili isiathiri maisha ya watu.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *