The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tuache kutumia Tanganyika na Utanganyika kisiasa

Watu wanaoibua suala la Serikali ya Tangayika hawaijui vizuri historia yetu au wanajua ila kwa makusudi wameamua kuupotosha umma.

subscribe to our newsletter!

Hivi karibuni nchini Tanzania kumekua na wimbi kubwa la wanaharakati na wanasiasa ambao wamekuwa wakijaribu kwa nguvu kubwa kuibua mjadala kuhusu Tanganyika, huku mjadala mkubwa ukielekezwa kwenye haja na umuhimu wa wa kurudisha mamlaka ya Tangayika. 

Kigezo wanachotumia wanaharakati na wanasiasa hawa ni kwamba kwa vile ni nchi mbili zilizoungana kutengeneza hiki tunachokiita Tanzania, yaani Tangayika na Zanzibar, na kwa vile Zanzibar wana Serikali yao, basi na Serikali ya Tanganyika nayo iwepo.

Nasikitika kusema kwamba watu wanaoibua suala la Serikali ya Tangayika na kupigia kelele uwepo wake ni ama hawaijui vizuri historia yetu, au wanaijua ila kwa makusudi tu wameamua kupuuzia historia hiyo kwa ajili ya kutimiza azma zao za kisiasa.

Zao la ukoloni

Ili tuelewe tumefikaje fikaje hapa tulipo ni lazima tuelewe tulipo toka. Tuanze na chimbuko la eneo ambalo lilikua likifahamika kama Tangayika. Ifahamike kwamba Tangayika ni zao la ukoloni kwa asilimia mia. Kabla ya ukoloni hakukuwepo na eneo linaloitwa Tangayika na hakukuwepo watu wanaoitwa Watanganyika. 

Eneo hili tunaloliita Tanganyika leo lilizaliwa kutokana na Mkutano wa Berlin uliofanyika kati ya mwaka 1884 na 1885, pale ambapo mataifa makubwa ya Ulaya yalikaa chini na kujigawia maeneo ya bara la Afrika. Kitendo hiki kilifahamika kama The Scramble for Africa

Lengo la mkutano huu lilikua ni kuzizuia nchi za Ulaya kupigana vita kwa ajili ya kugombania maeneo mbalimbali ya bara la Afrika na lengo hilo, kwa kiasi kikubwa, lilifanikiwa. Katika Mkutano wa Berlin, Ujerumani ilijitwalia eneo la Afrika Mashariki na wakaliita German East Africa, yaani Afrika Mashariki ya Ujerumani.

SOMA ZAIDI: Jinsi Sakata la Ndizi Kuzuiliwa Kuingia Zanzibar Lilivyoibua Mjadala wa Muungano

Eneo hilo lilijumuisha Tanzania Bara, tunayoiita Tanganyika leo, Burundi pamoja na Rwanda iliyoundwa rasmi mwaka 1885. Makao makuu ya koloni hili yalikua ni Bagamoyo mpaka yalipo hamishiwa Dar es Salaam mnamo mwaka 1891. 

Koloni hili lilidumu mpaka mwaka 1919 pale Ujerumani iliposhindwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na makoloni yake kugawiwa kwa nchi za Ulaya zilizoshinda. Uingereza nao wakawa na British East Africa, yaani Afrika Mashariki ya Uingereza iliyojumuisha Kenya na Uganda. 

Kwa makubaliano kati ya Mjerumani na Mwingereza, wawili hawa waliamua kuheshimu utawala wa Sultani wa Zanzibar ambayo ilijumuisha visiwa vya Zanzibar na ukanda wa bahari wa Afrika Mashariki kwenye pwani ya Mto Tana na Mto Minengani.

Mjerumani alipoweka sahihi kutawala eneo la Tanganyika hakuingia makubaliano na mamlaka ya Tangayika ambayo haikuepo bali aliingia mkataba na makabila mbalimbali ndani ya eneo tunaloliita Tangayika. 

Tawala za kikabila

Karl Peters, kwa niaba ya Ujerumani, kwa mfano, aliingia mkataba na tawala za makabila kama vile Usambara, Usangara, Nguru, Useguha na Ukami ambayo yalikua ndani ya eneo ambalo leo tunaita Tanganyika. 

Hivyo, kabla ya 1885, hakukua na utawala wowote wa umoja ndani ya eneo tunaloliita Tangayika bali kulikua na tawala mbalimbali za kikabila. Mjerumani alitawala eneo hili kwa miaka 34, kutoka 1885 mpaka 1919, na mpaka hapo bado hakuna jina, wala mamlaka, inayoitwa Tangayika. 

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyopelekea kuanguka kwa mamlaka ya Ujerumani, eneo la Afrika Mashariki ya Ujerumani ikagawanywa kati ya Uingereza na Ubelgiji. 

SOMA ZAIDI: Kikosi Kazi cha Mwinyi Chataka Mamlaka Zaidi kwa Z’bar Ndani ya Muungano

Ubelgiji wakachukua Rwanda na Burundi na eneo lililobaki akapewa Mwingereza na kuiita Tanganyika. Hivyo, neno Tanganyika linaanza kutumika mwaka 1920. Kabla ya hapo hakukuwahi kua na taifa, wala nchi, ya Tanganyika. 

Makabila ndani ya iliyoitwa Tanganyika hayakuwahi kuwa wamoja, wala kua chini ya tawala moja, kabla ya Mjerumani na Uingereza. 

Hivyo, taifa na mamlaka tunayoiita Tanganyika ilidumu kwa miaka 44 tu kati ya mwaka 1920 mpaka 1964. Hii ni tofauti na utaifa na mamlaka ya Zanzibar uliodumu kwa miaka 108 kati ya mwaka 1856 mpaka 1964.

Ndani ya eneo tunaloliita Tangayika kulikua na mataifa mbalimbali yenye uongozi, lugha, mila na desturi zao. Hili ndilo lililopelekea Mwalimu Nyerere kuvunja tawala za kichifu mwanzoni kabisa mwa utawala wake. 

Ujenzi wa utaifa

Nyerere alitambua kwamba Tangayika ni kitu kipya na bila adui mkoloni basi hakuna utaifa wa Tangayika. Alitambua mapema kwamba baada ya kumuondoa mkoloni basi watu watarudi katika utaifa wao wa awali na kulikua na hatari ya Tangayika kumegeka.

Nguvu ya utaifa wa makabila yetu yapo hadi leo hii ndiyo maana wote tuna utambulisho wa makabila yetu. Hata falme zetu za kikabila zilikua zikijulikana kama mataifa. Kwa mfano, taifa la Wachagga, taifa la Wasambaa, nakadhalika. 

SOMA ZAIDI: Nini Hasa Kilipelekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?

Utambuzi wa makabila yetu bado una nguvu na ndiyo maana tunaweza kutambuana kwa makabila yetu kutokana na majina yetu ya kikoo na lafudhi zetu. Hata Kiswahili, ambacho leo ni lugha ya taifa, haikua lugha inayozungumwa na idadi kubwa ya watu wakati tunapata uhuru. 

Serikali ikaweka jitihada maalum ya kukitumia Kiswahili ili kujenga umoja wa kitaifa ambao ungetishiwa na kila mtu kuongea lugha yake. Hali hii ni tofauti kabisa na wenzetu wa Zanzibar. Hivyo, utaifa wa tunachokiita Tangayika haukudumu zaidi ya miaka mitatu, yaani kutoka 1961 mpaka 1964.

Lengo la kuweka historia hiyo fupi ni kujaribu kuweka bayana wanachokipigania wale wanaodai mamlaka ya Tangayika ndani ya Muungano au wengine kwenda mbali zaidi na kudai Zanzibar yenye mamlaka kamili ndani ya Muungano!

SOMA ZAIDI: Je, Zanzibar Inaweza Kuwa na ‘Mamlaka Kamili’ Ndani ya Jamhuri ya Muungano?

Kwa nini ilichaguliwa Serikali mbili badala ya tatu au moja? Ni kwa sababu lengo lilikua ni kuja kua na Serikali moja. Ila kwa sababu ya nguvu ya historia na utaifa wa Zanzibar, kuiondolea mamlaka Zanzibar isingekua rahisi. 

Hilo halikua gumu kwa upande wa Tangayika kwa sababu ya uhalisia wa wakati huo ambao ni kwamba hisia za Utangayika hazikua kali ndani ya Watangayika. 

Utangayika ulikua bado ni mgeni na mbichi ndani ya hao waliokua wanaitwa Watangayika na ndiyo maana kuondoa mamlaka ya Tanganyika na neno Tangayika haikua na ukakasi hata wakati ule. 

Leo hii tunataka kusema hisia zetu za utaifa wa Tangayika ni mkali kuliko wale waliokuepo mwaka 1964? Hiyo siyo kweli hata kidogo. Tuache kutumia Tanganyika na Utanganyika kisiasa!

Tusije kulalamika

Tutambue kwamba tukishamaliza kuidai hiyo mamlaka ya Tangayika iliyovunjwa mwaka 1964 basi baada ya hapo tusiwalaumu wale watakaoanza kudai mamlaka za kichifu ambazo zilivunjwa mwaka 1962. 

Pale ambapo Tangayika itakaporudishwa na maeneo mbalimbali ndani ya hiyo Tangayika zitakapoanza kudai utaifa wao uliokuepo kabla ya kitu kinachoitwa Tangayika kuwepo, basi tusije tukalalamika. 

Tusije tukalalamika pale ambapo Wasambaa watadai utawala wa koo ya Kimweri uridishwe au pale ambapo Wahehe watadai utawala wa koo ya Mkwawa uridishwe. Pale ambapo Wachagga watadai utawala wa koo ya Marealle uridishwe, tusije tukalalamika. 

Pale ambapo watu watadai mamlaka zote zilizovunjwa ili kujenga tunachokiita Tangayika ndiyo tutaelewa mzimu wa tunachokidai utatutafuna na hata hao wanaoidai Tangayika kwa sababu za kisiasa hawatakua na pakukimbilia!

Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *