Dar es Salaam. Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, ifanyiwe marekebisho ili maamuzi ya kumnyima dhamana mtuhumiwa yatolewe na Mahakama, Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania imependekeza.
Tume hiyo, iliyowasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan hapo Julai 15, 2023, imependekeza pia kutungwa kwa sheria mahususi ya dhamana itakayoainisha mfumo, mamlaka, na utaratibu wote wa dhamana ili kuliweka suala la dhamana kwenye sheria moja na kupunguza mamlaka zinazoshughulikia dhamana.
Suala la dhamana limekuwa moja kati ya masuala ambayo yamekuwa yakizua utata na mjadala mkubwa kuhusu mfumo wa haki jinai nchini, huku wadau mbalimbali wakilalamika kuhusu sheria zilizopo kushindwa kuruhusu dhamana kwa baadhi ya makosa.
Kwenye kazi yake, tume hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman ilisikia malalamiko haya kutoka kwa wananchi, huku mapendekezo kadhaa yakitolewa juu ya namna ya kuboresha utaratibu wa dhamana nchini.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Uchunguzi Mali Zilizotaifishwa Chini ya Utaratibu wa Kukiri Kosa
Baadhi ya wadau, kwa mfano, walipendekeza kwamba makosa yote nchini yawe na dhamana kama ilivyo kwa nchi nyingine ikiwa ni pamoja na Kenya. Hili ni pendekezo ambalo wadau wengi wa haki jinai nchini Tanzania wamekuwa wakipendekeza.
“Hata hivyo, wadau wengine walipendekeza kuwa makosa makubwa kama vile ugaidi, mauaji, uhaini, ubakaji na ulawiti wa watoto chini ya miaka kumi ndiyo yaondolewe dhamana lakini makosa mengine yote yawe na dhamana,” tume imeandika kwenye muhtasari wa ripoti yake.
Tume ilibaini pia kwamba makosa tangulizi, yaani predicate offence ya utakasishaji wa fedha haramu na taratibu za dhamana zilizopo katika Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, zimeonekana kuchangia washtakiwa wengi kukosa dhamana.
Kosa tangulizi linaelezwa kwamba ni uhalifu ambao ni sehemu ya uhalifu mkubwa uliofanyika. Kwa mfano, kwenye makosa ya utakasishaji fedha, kosa tangulizi linaweza kuwa ni aina yoyote ya uhalifu unaozalisha pesa.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Mkakati wa Kitaifa Kubaini, Kuzuia Uhalifu Tanzania
Tume imekubaliana na maoni ya wadau kwamba kwenye makosa kama ya ugaidi hayapaswi kuwa na dhamana kutokana na uzito wa kosa na adhabu yake, uwezekano mkubwa wa mtuhumiwa kuharibu ushahidi, au kuingilia upelelezi na wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa.
Hata hivyo, tume imeitaka Serikali, bila kuathiri masharti ya mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeingia kuhusu kudhibiti makosa makubwa ya kupangwa na makosa ya uhujumu uchumi, kurekebisha tafsiri ya makosa tangulizi ya kosa la utakasishaji fedha haramu.
Tume inaamini kwamba kufanya kutapunguza washtakiwa wengi kukosa dhamana kutokana na tafsiri hiyo kuwa pana.
Tume pia imetaka jedwali linaloainisha makosa ya uhujumu uchumi katika Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, lipitiwe upya.
Lengo la kufanya hivyo ni kuweka kigezo cha thamani ya mali au fedha inayohusika na kesi hiyo ili kudhibiti mamlaka na kutathmini endapo makosa yote yaliyobainishwa kwenye jedwali hilo yanapaswa kuendelea kuwa ya uhujumu uchumi.
SOMA ZAIDI: Wakuu wa Mikoa, Wilaya Wasiwe na Mamlaka ya Kukamata Watu, Tume Yashauri
Tume pia imeshauri Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20, irekebishwe ili mashauri ya makosa yasiyo na dhamana yaanze kusikilizwa ndani ya muda maalumu utakaowekwa kisheria.
Tume imependekeza kwamba ikiwa mashauri hayajaanza kusikilizwa ndani ya muda huo, dhamana itolewe isipokuwa kama mahakama itaona kuna sababu za msingi za kumnyima dhamana mshtakiwa huyo.