Watoto hujifunza kutokana na matendo ya wazazi wao. Hivyo basi, watoto wakilelewa kwenye familia yenye mifarakano na kutokuelewana baina ya wazazi wao, mara nyingi watarithi tabia hizo.
Na kinyume chake ni ukweli, kwamba endapo kama watoto watalelewa kwenye familia zenye mahusiano mazuri na majibizano yenye kuheshimiana, nao watathamini umuhimu wa mahusiano. Tatizo kubwa linalopelekea mahusiano kuzorota ni mawasiliano dhaifu.
Udhaifu wa mawasiliano tunaozungumzia ni pamoja na kukaripiana, kutukanana, kununiana na hata kusonyana mbele za watoto wenu. Hili laweza kuwa tatizo la mahusiano yenu, lakini kwa nini muwahusishe watoto? Kwani ugomvi lazima ufanyike sebuleni? Hakuna faragha kama chumbani mkakaa na kuzozana?
Kupaziana sauti mbele ya watoto wako inawaletea watoto madhara mbalimbali ikiwemo nidhamu ya uoga na kutojiamini na hivyo kumyima fursa ya kuwa mdadisi na kudhoofisha uwezo wa akili yake kukua kadiri ya umri wake.
SOMA ZAIDI: Shule ya Kwanza ya Mtoto ni Nyumbani
Kwa maneno mengine, unamdumaza mwanao kwa wewe kutohusiana vyema na mzazi mwenzio. Wewe ni mama au baba kwa mtu na si vinginevyo. Hivyo, majina mnayoitana mkiwa na mihasira yenu yanawaondolea uhalisia na heshima mbele za watoto wenu.
Inawezekana kabisa mzazi mwenzako ni mkorofi na hajali kama kuna mahitaji ya watoto na familia kwa ujumla. Ingawa tunatambua umuhimu wa kushirikiana katika kulea watoto, busara inahitajika katika kuhusiana na mwenza mkorofi wa namna hii katika ndoa.
Haingii akilini kwa baba au mama kumcharaza viboko mwenza wake wa ndoa/mzazi mwenza kisa kakosea. Sasa unamcharaza viboko ili ajifunze ama unabomoa mahusiano yenu na maisha ya watoto wenu bila ya wewe kujua?
Suala lingine linaloathiri maadili ya watoto amabalo ni la kimahusiano katika familia ni ubinafsi uliokithiri kwa baadhi ya wazazi. Kuna wazazi ambao wanaishi kwa sheria ndani ya nyumba kwa kuwazuia wenzi wao na watoto kutotumia baadhi ya miliki zilizomo ndani ya nyumba zao.
SOMA ZAIDI: Namna Sita Mzazi Anavyoweza Kuhakikisha Malezi Bora Kwa Mtoto
Kwa mfano, kama baba hayupo TV, Radio, nakadhalika. haviwashwi ama akiwepo basi wote mnaangalia anachotaka yeye na hakuna mjadala juu ya hili. Bado yote haya ni kutowaheshimu wenzi wao wa maisha.
Dharau unazomfanyia mwenzio mbele ya watoto wenu unajenga maisha ya watovu wa nidhamu. Watoto wanaokuzwa katika namna hii hawatoweza kuwaheshimu watoto wenzao na hata watu wazima, ikiwemo waalimu.
Matokeo yake watoto hawa itawawia vigumu kusoma darasani na mara nyingi wataishia mitaani kuhangaikia matumbo kwa kugaagaa kuganga njaa ukubwani. Ikiwa huna mahusiano mema na mkubwa mwenzio, vipi utakuwa na mahusiano na watoto wenu?
Watoto pia wanakumbana na changamoto kama ilivyo kwa watu wazima na wanahitaji mtu wa kuwasikiliza na kuwapa ushauri wa namna ya kuzitatua changamoto hizo.
Kutokana na kukosekana kwa mahusiano na mawasilianao mazuri baina ya wazazi na watoto wao, watoto wanapata wakati mgumu kujenga ukaribu na wazazi.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Kumjengea Mtoto Tabia ya Kujitegemea Mapema
Pindi wanapopata changamoto, hasa katika kipindi cha balehe kwa kuogopa kuwahusisha wazazi wao, watoto wengi hutumbukia katika matatizo makubwa kama kutumia madawa ya kulevya na mimba za utotoni.
Kuna wazazi ambao kwao ni mwiko kuongea na watoto wao ana kwa ana na badala yake husikiliza mahitaji ya watoto kupitia mzazi mwenza! Matokeo yake mtoto akipatwa na matatizo, wazazi hawa mara nyingi huishia kuwalaumu wenza wao ambao eti wameshindwa kulea. Mmeshirikiana kuzaa. Shirikianeni kulea!
Familia nzuri na yenye amani hujengwa kutokana na uhusiano thabiti wa wanafamilia, hasa baba na mama. Familia ya namna hii inayo mazingira muafaka kwa makuzi ya watoto.
Ubora wa mawasiliano, uchaguzi wa maneno ya kusema hasa uwapo na hasira mbele za watoto ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo ya watoto. Kutofautiana katika mahusiano kupo, lakini ugomvi wa maneno kati yenu ufanyeni faraghani.
Inawezekana!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.
One Response
Mungu awabariki nimejifunza mengi kuhusu malezi ya mtoto