The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waondolewa Kusomea Chini ya Miti Baada ya Ripoti ya The Chanzo

Ni wanafunzi wapatao 55 wa Kituo cha Tucheze, Tujifunze cha Fukuchani, Unguja, ambao wanadaiwa kusomea chini ya miti kwa miaka 13.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Mamlaka visiwani hapa zimewahamisha wanafunzi wapatao 55 katika Kituo cha Tucheze, Tujifunze cha Fukuchani, wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini, Unguja baada ya ripoti ya The Chanzo iliyoonesha kwamba wanafunzi hao wamekuwa wakisoma chini ya miti kwa kukosa madarasa kwa muda wa miaka 13 sasa.

Vituo vya Tucheze, Tujifunze, au kwa kifupi kama TuTu, ni vituo vilivyoanzishwa na Serikali ya Zanzibar katika maeneo mbalimbali ya sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwawezesha wazazi kuwapatia watoto wao elimu ya maandalizi karibu na pale wanapoishi.

Wanafunzi hao ni miongoni mwa wanafunzi 3,559 wanaosoma kwenye vituo 69 vya TuTu vinavyoendeshwa na Serikali katika wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini, kisiwani Unguja. Kuna vituo kama hivyo 269 Zanzibar nzima, vyenye jumla ya watoto 18,748.

The Chanzo ilifika katika kituo hicho mnamo Juni 11, 2023, na kushuhudia watoto hao wenye umri kati ya miaka mitatu na mitano wakiwa wamekaa kwenye mabusati kwa ajili ya masomo, ikiwa ndiyo masomo yameanza baada ya kusitishwa kwa takriban miezi mitatu kupisha mvua zilizokuwa zikinyesha.

SOMA ZAIDI: Kwa Miaka 13 Jamii Hii Imeshuhudia Watoto Wake Wakisoma Chini ya Miti. Sasa Yaitaka Serikali Kukomesha Kero Hiyo

Wazazi ambao watoto wao wanasoma kwenye kituo hicho, pamoja na walimu wao, waliilamikia The Chanzo kwamba hali hiyo inaathiri usomaji na ufundishaji, wakiitaka Serikali iingilie kati kuwaepusha watoto hao na adha hiyo.

Wazazi na walimu walitoa wito kwa mamlaka na wasamaria wema wengine kuwasaidia kwenye jitihada zao za ujenzi wa madarasa ili hatimaye watoto hao wasome kwenye mazingira salama na tulivu ambao umeshindwa kukamilika kutokana na wazazi na walezi kushindwa kumudu gharama zake.

Wiki moja tangu The Chanzo ichapishe habari hiyo hapo Septemba 5, 2023, mamlaka katika wilaya ya Kaskazini A ambapo kituo hicho kipo zinaripotiwa kuchukua uamuzi wa kuwahamisha watoto hao kwenye eneo hilo na kuwapeleka Shule ya Msingi ya Kidagoni iliyopo umbali wa kilomita tano kutoka kilipo kituo hicho.

Hatua hiyo ilikuja baada ya wanakijiji kufanya kikao na maafisa elimu kutoka wilayani ambapo iliamuliwa kwamba watoto hao wahamie kwenye shule hiyo ya jirani wakati jitihada za kukamilisha ujenzi wa shule hiyo zikiendelea.

SOMA ZAIDI: Haya ni Lazima Yazingatiwe Ili Upangaji, Upanguaji Safu Katika Sekta ya Elimu Zanzibar Uweze Kuzaa Matunda

 Ni wanafunzi wapatao 55 wa Kituo cha Tucheze, Tujifunze cha Fukuchani, Unguja, ambao wanadaiwa kusomea chini ya miti kwa miaka 13.

Fatima Haruna Haji, mwalimu wa watoto hao, ameishukuru The Chanzo kwa kuibua kadhia yao hiyo, akisema kwamba siku zote wamekuwa wakilalamikia jambo hilo lakini mamlaka husika hazikuonesha utayari wa kulishughulikia.

“Tushasema sana juu ya hali hii kwenye kijiji chetu ila mara hii tumeona utofauti maana hadi viongozi wamekuja,” Fatima aliiambia The Chanzo iliyomkuta kwenye shule hiyo waliyohamishiwa akiwa na wanafunzi wake. 

“Hakukuwa na kiongozi hata mmoja aliyekuwahi kuja hapa ila mara hii hadi Mbunge kaja na kumuomba Rais asaidie ujenzi huu nae akiwa atasaidia pia,” aliongeza Fatima.

Hata hivyo, wazazi wa watoto hao wamesema kwamba watoto wao kulazimishwa kutembea umbali wa kilomita tano haiwezi kuwa ni suluhu ya kudumu, wakizitaka mamlaka husika kukamilisha ujenzi wa shule ambayo jamii hiyo imeanza kujenga lakini imeshindwa kuikamilisha.

Wananchi wameweza kujenga kozi tano za shule hiyo lakini wameshindwa kuukamilisha ujenzi huo, wakiomba Serikali na wasamaria wengine wawasaidie kuukamilisha. 

The Chanzo ilitaka kufahamu ni kiasi gani cha fedha wanajamii hao wanahitaji ili kukamilisha ujenzi huo, lakini walishindwa kujibu, wakisema hawajafanya tathmini bado.

Wanakijiji waliiambia The Chanzo kwamba kijiji hicho kilipokea ugeni wa maafisa kutoka Wizara ya Elimu na Ufundi wa Amali Zanzibar ambapo, mbali na kuongea nao, walipima, huku wakiwaahidi wananchi kuwa ujenzi utaanza mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba.

SOMA ZAIDI: Inachoweza Kufanya Zanzibar Kuhakikisha Watoto Wanaorudishwa Skuli Hawarudi Mitaani

Mbali na ugeni huo, wanakijiji pia walitembelewa na Mbunge wa Kijini (Chama cha Mapinduzi – CCM) Yahaya Ali Khamis kuzungumzia kadhia hiyo, kikao ambacho wanakijiji wanaamini kwamba kisingefanyika kama The Chanzo isingeibua suala hilo.

“Siku hizi hadi tuseme kwenu [waandishi], viongozi watoke kwenye mitandao ndo wanakuja, ila kuja wao wenyewe hawawezi kuja, sasa hiyo siyo nzuri maana wanatusahau,” Mwatima Said Pandu, mmoja kati ya wanakijiji hao, aliiambia The Chanzo.

“Sisi tuko tayari kubeba mchanga na hata matofali kukamilisha ujenzi [wa shule],” aliongeza mama huyo. “Maana kama siyo kwenda kule [Shule ya Msingi ya Kidagoni] basi watoto kipindi hiki cha mvua wasingesoma kwa sababu hawana pakwenda.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *