The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vyombo vya Habari Viache Kuwakataa Wanafunzi wa Mafunzo kwa Vitendo

Tunasema wanafunzi wanahitimu wakiwa hawajaiva, lakini wataivaje kama wananyimwa nafasi za mafunzo kwa vitendo?

subscribe to our newsletter!

Mwaka 2019 nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nikisomea uandishi wa habari katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) chuoni hapo.

Baada ya kumaliza muhula wa pili wa masomo, nilitakiwa kwenda kutafuta eneo la kazi kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa njia ya vitendo, jambo ambalo ni lazima kwa wanafunzi wote.

Nilichohitaji ilikuwa ni kufanya mafunzo yangu katika chombo cha habari. Nilichukua jitihada za kusambaza barua za utambulisho tunazopewa na chuo kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya hapa Dar es Salaam na hata mikoani ili niweze kupata nafasi ya kujiunga nao kwa kipindi cha takribani miezi mitatu hivi. 

Nakumbuka zoezi hilo nililianza mapema sana, yaani miezi kama minne hivi, kabla ya muda wa kuanza mafunzo hayo kufika, nikitarajia kwamba hadi muda utakapofika nitakuwa tayari nimepata sehemu ya kwenda. 

Mambo yakageuka kuwa kinyume chake, huku muda ukifika niende kwenye mafunzo lakini sehemu sijapata. Nilijaribu kufuatilia sehemu nilizopeleka maombi sikupata majibu yoyote. 

SOMA ZAIDI: Waandishi Mwanza Watathmini Hali ya Uhuru wa Habari

Basi ikanibidi nirudi Mlimani Media, ambacho ni chombo cha habari cha SJMC kinachotumiwa muda wote na wanafunzi kwa ajili ya mafunzo, kitu ambacho sikuwa nimetaraji wala hayakuwa malengo yangu kwa sababu nilihitaji kupata uzoefu wa nje. 

Pale tulikuwa wanafunzi takribani 100, wengi wao wakiwa ni wenzangu tuliokuwa tunasoma darasa moja. Hao wote tulibaki hapo baada ya kukosa nafasi kwenye vyombo vya habari ambavyo wengi walipenda kwenda huko. 

Suala la wanafunzi kukataliwa kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye vyombo vya habari halikuwa la kwanza kwetu sisi na wala halikuishia hapo. 

Mpaka ninapoandika makala hii bado changamoto hiyo imeendelea kuwepo, hali inayowapa wakati mgumu wanafunzi wa masuala ya uandishi wa habari nchini kote. 

Kulipia fedha 

Simon Eriyo ni Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi kutoka SJMC kwa mwaka 2023/2024 ambaye amenieleza kwamba amekuwa akipokea malalamiko ya wanafunzi kukumbana na changamoto ya kutopata nafasi pale wanapoomba kufanya mafunzo kwenye vyombo vya habari.

SOMA ZAIDI: TGNP Yataka Wanahabari Kuchochea Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi

Eriyo ameenda mbali zaidi na kunieleza kwamba wapo ambao pia wamekuwa wakikutana na changamoto ya kutakiwa walipe kiasi fulani cha fedha ili waweze kukubaliwa kufanya mafunzo hayo, jambo ambalo mara zote limekuwa likiwapa wakati mgumu wanafunzi wengi.  

“Bila chochote kitu, hakuna kuzingatiwa,” Eriyo, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka pili wa SJMC anayesomea mahusiano kwa umma pamoja na masoko, alisema. “Chochote kitu namaanisha kiasi kidogo cha fedha, kesi za namna hiyo nimezipokea.”

“Hii ni changamoto kubwa kwa sababu mwanafunzi ni lazima afanye mafunzo kwa vitendo, haijalishi kapata au hajapata [sehemu],” aliongeza Eriyo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amenithibitishia pia kupokea malalamiko ya wanafunzi wa uandishi wa habari kutakiwa kulipa pesa kwenye vyombo vya habari ndipo wapate nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo.

“Hayo malalamiko nimekutana nayo,” Balile aliniambia nilipozungumza naye kwa jia ya simu. “Ninayakuta kwenye semina, ndiyo shida ninayoipata. Lakini ukiuliza ni nani, kwa mfano, aliyekwambia ulipe? Hawasemi! Lakini kwenye semina wanasema wanadaiwa pesa.”

SOMA ZAIDI: Je, Wanahabari Walipe Vyanzo Vyao Vya Habari?

Hata hivyo, Balile, ambaye pia ni Mhariri wa gazeti la Jamhuri, alijaribu kuutetea uamuzi wa vyombo vya habari kutopokea wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo, akisema unachangiwa na uwepo wa idadi kubwa ya wanafunzi kuliko uwezo wa vyombo vya habari kuhimili.

“Idadi ya wanafunzi imekuwa kubwa kuliko uwezo wa vyombo vya habari,” alisema Balile. “Wanafunzi wanaotakiwa kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo hawapungui 1,000 hadi 1,500 kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, kuna shida kidogo ya watu kuongezeka.”

Uwezo mdogo 

Dastan Kamanzi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) ambaye amebainisha umuhimu wa wanafunzi kupata nafasi hizi, akisema vyombo vya habari vina wajibu wa kufanya hivyo. 

Hata hivyo, Kamanzi, ambaye shirika lake limekuwa mstari wa mbele kuchochea uandishi wa habari wa tija nchini Tanzania, amesema wanafunzi wengi wameonekana kuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi, kitu kinachowatia hofu wahariri kwamba itawachukua muda mrefu kuwafundisha kazi.

“Watu wengi huwa wanalalamika kuwa wanafunzi wanaotoka vyuoni wana uwezo mdogo,” anasema Kamanzi. “Kwa hiyo, watu wengine huwa wanaona watachukua muda mwingi kuwafundisha, na kwa hiyo watakuwepo tu kama wanawapotezea muda.” 

SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?

Lakini haijalishi ni visingizio gani wahariri na vyombo vyao vya habari wanaweza kuja navyo kuhalalisha wanafunzi kunyimwa nafasi ya mafunzo kwa vitendo, vitendo hivi siyo vizuri na ni lazima suluhu ya kudumu ipatikane kwa ustawi wa tasnia yetu ya habari hapa nchini.

Kukosa weledi

Malalamiko ya waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla kutokidhi kiu ya wanajamii yamekuwa yakiongezeka kila uchao, huku waandishi wakitupiwa lawama za kukosa weledi na maadili katika kufanya kazi zao. 

Wakati ni kweli shule na vyuo vya uandishi wa habari vinawajibu wa kuwanoa wanafunzi wao kiweledi ili kukidhi kiu ya wanajamii, ukweli unabaki kwamba mafunzo kwa vitendo yana mchango mkubwa katika kumfunda mwandishi kuweza kufanya kazi ambayo jamii inamtegemea kuifanya.

Wanafunzi wakipata misingi imara ya uandishi, wakafanya kazi kwa vitendo kwa kuzingatia maadili, kanuni na sheria huenda tasnia yetu ikaja kuheshimishwa hapo baadaye.

Ni muhimu sana kwa wadau wa habari nchini kulipigia kelele suala hili na kuvikumbusha vyombo vya habari na wahariri wao wajibu walionao wa kutengeneza kizazi kipya cha waandishi wa habari kitakachoipa tasnia yetu heshima inayostahiki na kuchangia maendeleo kwenye taifa letu.

SOMA ZAIDI: Vyuo vya Uandishi wa Habari Virejee Mitaala Mara kwa Mara

Ni muhimu kwa vyombo vya habari na wahariri wao kukumbushwa kwamba kulalamika tu pekee kwamba wanafunzi wanaohitimu kwenye shule na vyuo vya uandishi wa habari “hawajapikika” haitoshi bali watambue kwamba wao pia wana wajibu wa “kuwapika” waandishi wanaotaka kuwaona sokoni.

Kwa pamoja, hakuna litakaloshindikana katika jitihada zetu za kuikuza na kuiheshimisha tasnia ya habari Tanzania ili iweze kutoa mchango unaotegemewa kwenye jamii!

Lukelo Francis ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia lukelo@thechanzo.com. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

 1. Chombo cha habari ninachofanyia kazi kama Mhariri wa Habari, tunapokea wanafunzi wa field wengi sana, mathalani mwaka huu tulikuwa nao 20 ambao ni wengi kuliko waandishi wetu, ila asilimia kubwa ya wanafunzi hawajitambui wanataka nini na hawana intereest na uandishi wa habari wa gazeti bali walitaka kutangaza kwa ajili ya kusikika na kuonekana zaidi, wachache sana wanajitambua.

  Wengi huwa na udhuru kwa wiki atahudhia field mara mbili ya tatu baada ya hapo anapotea, udhuru zao nyingi ni kufiwa, kuugua, kuuguliwa na mwisho anataka umjazie fomu yake kwa matokeo mazuri.Mathalani nilipokea wanafunzi wawili kutoka UDOM niliwaona wiki ya kwanza na ya mwisho wanataka kujziwa fomu.Katika kundi la hivi karibuni kulikuwa na wanafunzi watano kutoka SJMC kati yao wawili wao wana udhuru kila siku kama haumwi, basi anauguliwa au kafiwa, na mmoja alihudhuria field wiki moja tu na kwa vitukio vingi na alikuja kwa kuchelewa, SASA jiulize chombo gani au mhariri gani atavumilia watu wa hivi?hapo hatujazunguzia mavazi, uharibifu wa mali za ofisi au vifaa vilivyopo kama vinatosheleza.

  Chumba cha habari kinajiendesha kwa kukimbizana na muda hivyo ni ngumu kuhudumia wanafunzi wengi na wanaopata fursa hubaribia wenzao na kuua moyo wa wanaojitoa kuwasaidia.
  Ni MUHIMU sana vyuo viwajenge wanafunzi sana kimasomo, kimaadili, kiutendaji na kuwaeleza wajitambuee wanapikuja maeneo ya kazi na pale sio chuoni kwamba ataweza kufanya anavyojisikia, pia wajue tuna ratiba zetu za kazi na tunakimbizana na matokeo kama waajiriwa.

  Kazi njema

 2. Chombo cha habari ninachofanyia kazi kama Mhariri wa Habari, tunapokea wanafunzi wa field wengi sana, mathalani mwaka huu tulikuwa nao 20 ambao ni wengi kuliko waandishi wetu, ila asilimia kubwa ya wanafunzi hawajitambui wanataka nini na hawana intereest na uandishi wa habari wa gazeti bali walitaka kutangaza kwa ajili ya kusikika na kuonekana zaidi, wachache sana wanajitambua.

  Wengi huwa na udhuru kwa wiki atahudhia field mara mbili ya tatu baada ya hapo anapotea, udhuru zao nyingi ni kufiwa, kuugua, kuuguliwa na mwisho anataka umjazie fomu yake kwa matokeo mazuri.Mathalani nilipokea wanafunzi wawili kutoka UDOM niliwaona wiki ya kwanza na ya mwisho wanataka kujaziwa fomu.Katika kundi la hivi karibuni kulikuwa na wanafunzi watano kutoka SJMC kati yao wawili wao wana udhuru kila siku kama haumwi, basi anauguliwa au kafiwa, na mmoja alihudhuria field wiki moja tu na kwa vitukio vingi na alikuja kwa kuchelewa, SASA jiulize chombo gani au mhariri gani atavumilia watu wa hivi?hapo hatujazunguzia mavazi, uharibifu wa mali za ofisi au vifaa vilivyopo kama vinatosheleza.

  Chumba cha habari kinajiendesha kwa kukimbizana na muda hivyo ni ngumu kuhudumia wanafunzi wengi na wanaopata fursa hubaribia wenzao na kuua moyo wa wanaojitoa kuwasaidia.
  Ni MUHIMU sana vyuo viwajenge wanafunzi sana kimasomo, kimaadili, kiutendaji na kuwaeleza wajitambuee wanapikuja maeneo ya kazi na pale sio chuoni kwamba ataweza kufanya anavyojisikia, pia wajue tuna ratiba zetu za kazi na tunakimbizana na matokeo kama waajiriwa.

  Kazi njema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *