The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ni Fedheha Klabu Zetu Kushtakiwa FIFA

Kunahitajika kanuni ya kulazimisha mizozo yote itatuliwe ndani kwanza kabla ya kupelekwa nje.

subscribe to our newsletter!

Ukitafuta sentensi “FIFA yaifungia… kusajili” kwenye mtandao wa Google, majibu yatakuja mengi kuhusu klabu za soka za Tanzania kuzuiwa kusajili kutokana na kushindwa kutimiza vipengele vya mikataba wakati wa kuachana na wachezaji wao.

Majibu hayo ya adhabu za FIFA—Shirikisho la Kimataifa la Soka—kwa siku za karibuni yanazihusisha klabu za Young Africans (Yanga), Tabora United, Biashara United na Singida Fountain Gate (zamani Singida Big Stars) ambayo taarifa yake ilitangazwa wiki iliyopita.

Na taarifa zote hizo huhusu wachezaji wa kigeni wanaokuja kusakata soka nchini na baadhi ya makocha kutoka nje. Taarifa hizo za adhabu hazijahusu wachezaji wetu wazawa wala makocha.

Nicholas Gyan, kiungo raia wa Ghana ndiye aliyesababisha FIFA itoe adhabu hiyo kwa Singida baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipa mishahara yake ya miezi kadhaa pamoja na marupurupu.

Na kutokana na kasi ya kusajili wachezaji wa kigeni kuwa kubwa, hatua hizi za wachezaji kupeleka madai yao FIFA hazitaisha kwa kuwa inalingana na kasi ya kuachana nao kwa sababu tofauti.

SOMA ZAIDI: Kelele kwa Mangungu ni za Kukariri, Tatizo ni Kubwa Simba

Moja kati ya sababu hizo ni mchezaji kuisha kiwango au kutoonyesha kiwango kilichosababisha anunuliwe kutoka nje na pengine viongozi kudanganywa kuhusu kiwango cha mchezaji kumbe ni wale wa kuangalia kwenye mtandao wa YouTube kumbe uwanjani ni sifuri.

Suala hapa si wachezaji kudai haki zao, suala ni kwa nini wakimbilie FIFA na kwa nini ni wachezaji wageni tu? Kwamba wachezaji wazawa hulipwa haki zao zote wakati wanapoachwa, hawajui haki zao, au ni gharama kudai haki zao?

Jukumu la TFF

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo jukumu lake kubwa ni pamoja na kushughulikia masuala kama hayo ya haki na maslahi ya wachezaji kulingana na mikataba yao.

Siku hizi hii kamati haikutani mara kwa mara labda wakati msimu unapokaribia kuanza tu kwa ajili ya masuala ya usajili. Ni nadra sana kusikia hii kamati imekutana kujadili hoja ya mchezaji aliyeachwa na klabu fulani na kutoa uamuzi.

Ni kama vile wachezaji hawawasilishi malalamiko yao ya mikataba kwenye kamati hii, labda kutokana na ahadi nono wanazopewa wakati wanaachwa, au kuhofia kujenga uhasama na klabu walizozitumikia na ambazo wanazipenda.

SOMA ZAIDI: Mamelodi Wametoa Somo kwa Yanga, Simba

Lakini kucheza soka ni ajira na hivyo ajira inapokuwa na mambo yanayoathiri ujira, ni tatizo la kimsingi ambalo linatakiwa liwasilishwe kwa vyombo husika ili litatuliwe na kumuwezesha mchezaji kuishi maisha ya matamanio yake.

Awali wachezaji walikuwa na mwamko huo wa kuwasilisha madai yao TFF na kutolewa uamuzi na kwa nafasi yangu ya zamani pale ya Katibu Mkuu, niliwahi kusimamia kwa mafanikio utekelezaji wa amri ya kamati hiyo ya hadhi ya wachezaji hadi wote wakalipwa stahiki zao bila ya kuwepo na athari kubwa kiuchumi kwa klabu.

FIFA huwa wanajua kuwa kila nchi ina mfumo wake wa utoaji haki kwa kuweka vyombo huru vya maamuzi. Inapofikia wahusika hawakubaliani na maamuzi ya vyombo hivyo, ndipo huenda FIFA kwa ajili ya uamuzi wa mwisho ndani ya mfumo wa soka. 

Ndiyo ukishindwa hapo unaweza kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS).

Kwa maana hiyo, mchezaji, au kocha, ambaye amenyimwa haki zake kwenye klabu iliyomtimua, hutakiwa kwanza amalize mchakato wa humu ndani kabla ya kwenda FIFA.

SOMA ZAIDI: Kanuni za Ridhaa Zinaondoa Ushindani wa Haki Kwenye Soka. Bodi ya Ligi, TFF Ziziondoe

Na iwapo atapitiliza FIFA bila ya kutumia kwanza mfumo wa haki wa ndani, mlalamikiwa anaweza kutoa hoja kwamba mlalamikaji hakuanzia katika vyombo vya ndani vya maamuzi, hoja ambayo inaweza kukubaliwa bila ya matatizo.

Siyo geresha

Kwa maana hiyo, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji haikuundwa kama geresha, bali kama chombo kinachoweza kusimamia na kutoa haki kwa wanafamilia wa soka ambao wameathiriwa na uongozi mmoja wa klabu, vyama na hata shirikisho lenyewe.

Na mara mchezaji anapowasilisha malalamiko yake, ni kazi ya sekretarieti kuwasiliana na klabu au chombo kinacholalamikiwa kwa ajili ya kuitaairifu hoja iliyo mezani. 

Hii husaidia klabu au chombo hicho kufanya mawasiliano ya haraka na mlalamikaji ili kama kuna uwezekano, suala hilo limalizwe mapema kabla ya kufikia uamuzi wa kuizuia klabu kusajili.

Hii husaidia masuala mengi kumalizwa kwa njia za kiungwana na kujenga imani kwa wachezaji, hasa wazawa kuwa kuna chombo kinachoweza kufanya maamuzi kuhusu haki zao iwapo zitakiukwa. Na hii itawezesha wachezaji kuwa makini zaidi na mikataba yao.

SOMA ZAIDI: AFL Yaanza kwa Kishindo Huku Ikiacha Maswali Mengi

Inaweza kuwa ni vigumu kwa wachezaji wageni kwa kuwa mara wanapoachwa na wakakosa klabu za kuwasajili hapa nchini, huenda nje kutafuta klabu nyingine na hivyo kimbilio rahisi kwao huwa ni FIFA. 

Lakini kama kamati itakuwa imara na kutoa haki kama inavyostahili, hata wachezaji wageni watakuwa na imani nao na masuala yote yataamuliwa humu ndani badala ya kwenda kutia aibu nje.

Naelewa wakati ule kuna wachezaji kadhaa, hasa kutoka Kenya, waliokuwa wakiwasilisha madai yao TFF na yakasikilizwa na kutolewa uamuzi na pale klabu zilipogoma kutekeleza au kutoa ushirikiano kwa TFF ndipo walipokwenda FIFA ambako walipata haki zao.

Kujenga imani

Hivyo, ni muhimu kuirejeshea Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji nguvu zake za kusimamia haki za wachezaji ili kuondoa fedheha ya nchi kwa klabu zake kushtakiwa kila mara FIFA wakati uwezo wa kutatua matatizo hayo upo. 

Pia, umauzi huo utasaidia kujenga imani kwa wachezaji wetu wazawa kuwa kuna chombo kinachoweza kutoa haki iwapo klabu zitakiuka mikataba.

SOMA ZAIDI: Makosa ya Waamuzi ni Tatizo la Soka Siyo Klabu Zinazolalamika

Naamini wako wachezaji wengi ambao mikataba yao ilikuwa mizuri, lakini hawakutimiziwa maslahi yao kama ilivyokubaliwa lakini wanashindwa kudai haki zao kwa kudhani kwamba kuna gharama kubwa kwenda FIFA, au kuhofia kukiuka makubaliano ya mdomo yenye ahadi lukuki.

Najua linaweza kuwa si tatizo la kamati, lakini kuna umuhimu wa masuala ya ndani kushughulikiwa ndani kwanza na natumaini mikataba ya wachezaji hueleza hivyo kuhusu jinsi ya kutatua matatizo ya kimkataba. 

Kunahitajika kanuni ya kulazimisha mizozo yote itatuliwe ndani kwanza kabla ya kupelekwa nje ili wanafamilia wa soka waikimbilie kamati kwanza.

Kushtakiwa kila siku FIFA ni aibu na fedheha kwa nchi na hasa pale klabu zetu zinaposhindwa katika kila kesi. 

Ni aibu hata kwa TFF kutangaza maamuzi ya FIFA ya kuzifungia klabu kusajili kama ilivyokuwa kwa Singida wakati shirikisho lilipotangaza kumbe pande hizo mbili zilishamalizana mapema.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts