Search
Close this search box.

Uchaguzi Tanzania 2024 Na 2025: Tuna Nini Cha Kujifunza Kwa Majirani?

Tunaweza kujifunza matumizi mazuri kwenye uchaguzi. Kwangu mimi, kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu mwaka 2025 ni ufujaji wa pesa za walipa kodi.

subscribe to our newsletter!

Wakati watanzania tukijiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, nimepitia makabrasha yangu ya nilichojifunza nikiwa mwangalizi wa Uchaguzi katika nchi kadhaa Afrika na kutamani tungejifunza chochote kutoka kwenye taratibu za uchaguzi katika nchi hizo, tukianza na majirani zetu tulionao Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mambo hayo yangezingatiwa, Uchaguzi wa Tanzania katika miaka ijayo ungepata heshima kubwa na tungeshuhudia mwitikio mkubwa zaidi wa wapiga kura kuliko tulivyoshuhudia miaka iliyopita. Naandika haya kwa Imani kuwa watanzania, ambao wenye nchi watachukua hoja hizi na kuzitumia katika kujenga utetezi wa maboresho ya Kisheria, kisera, kimfumo na kiutendaji katika uchaguzi unaokuja mwakani 2024 na mwaka unaofuata, 2025.

Kurahisisha mfumo wa uandikishaji wapiga kura

Kwanza kabisa naamini tunaweza kujifunza kuhusu uandikishaji wapiga kura. Katika uzoefu wangu, nimegundua kuwa nchi zilizoweza kuandikisha wapiga kura wengi ni nchi zenye mfumo mzuri na rahisi wa kuandikisha wapiga kura wapya na kuhuisha taarifa za waliokwishajiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

SOMA: Uchaguzi Umekuwa Kichocheo Kikubwa cha Marekebisho ya Katiba Tanzania

Kwa sababu hiyo, natamani Tanzania tujifunze kuwa na mfumo mchanganyiko wa uandikishaji wapiga Kura ili ifike siku mtanzania anayetimiza umri wa kupiga kura ifikapo uchaguzi ujao aweze kuchagua njia atakayotumia kujiandikisha kuwa Mpiga Kura. Njia ya kwanza ni njia ambayo tayari tunaitumia.

Kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2015, watanzania wanayo fursa ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura angalau mara mbili ndani ya miaka mitano kati ya uchaguzi mmoja na mwingine.

Tatizo hapa ni kwamba uandikishaji huu ni mahsusi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pekee. Uchaguzi wa serikali za Mitaa utafanyika kwa uandikishaji mpya wa wapiga kura kabla ya siku ya kupiga kura. Mara nyingi, uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za Mitaa hufanyika siku chache kabla ya upigaji kura.

Niliwahi kuambiwa kuwa katika maeneo fulani ya nchi yetu, uandikishaji uliwahi kufanyika siku yenyewe ya kupiga kura. Hii inatia mashaka juu ya uwepo wa daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa vile kama unaandikisha mpaka siku ya kupiga kura, inatia mashaka juu ya uhakiki wa taarifa za mpiga kura unafanywa lini na nani kama upo?

SOMA: Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo

Je wanaojiandikisha huku wakiwa si wakazi wa eneo husika wanaweza kujulikana vipi na nani atawabaini wakati hakuna fursa ya kukagua daftari la wapiga kura?

Upatikanaji wa takwimu za wapiga kura

Jambo la wazi hapa ni kuwa takwimu za wapiga kura Tanzania kwa upande wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa siyo wazi hata kidogo. Hivi nikiuliza hapa, watanzania waliopiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2019 ni wangapi nani anaweza kutoa majibu?

Kwa upande wa Uchaguzi Mkuu, takwimu za wapiga kura walioandikishwa katika daftari la Kudumu la wapiga Kura zinajulikana wazi. Kwa mfano, kwa mwaka 2015, Tume ya Taifa ilikuwa inao wapiga Kura 23,161,440 ikiwa ni jumla ya wapiga Kura 22,658,247 wa Tanzania Bara na wapiga kura 503,193 kwa upande wa Zanzibar.

Idadi hii iliongezeka mwaka 2020 kwa jumla ya wapiga kura wapya 6,560,587 na kufikia jumla ya wapiga kura 29,754,699 ambao kati yao 29,188,347 walikuwa ni kutoka Tanzania Bara na waliosalia 566,352 walitokea Zanzibar. Hata ukitaka kujua umri wa wapiga Kura walio katika daftari la Kudumu inakuwa ni rahisi.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wapiga kura waliokuwa katika daftari la wapiga kura hadi kufikia siku ya uchaguzi wa mwaka 2020 walikuwa katika makundi matatu ya umri. Kundi la kwanza lilikuwa la wapiga kura vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 35 ambao idadi yaoilifikia 15,745,499 (53%).

Kundi la pili lilikuwa la wapiga kura wa makamo ambao wana umri kati ya miaka 36 hadi 50 ambao walifikia 7,664,343 (26%) na kundi la tatu ni lawapiga kura wazee ambao wanaanzia umri wa miaka 51 na kuendelea ambao idadi yao ilikuwa ni 5,778,505 (19%).

Jambo la kujifunza kutoka Afrika Kusini ni kwamba takwimu zikichanganuliwa kwa makundi mengi zaidi zinaleta picha nzuri zaidi ya aina ya wapiga kura waliotarajiwa kupiga kura. Kwa mfano, kwa uchaguzi mkuu unaokuja mwakani 2024, Afrika Kusini imeshaandikisha 26,894,466 ambao wako katika makundi yafuatayo na idadi yao katika mabano: Miaka 18 – 19 (wanawake 240, 271; wanaume 184, 784); miaka 20 – 29 (wanawake 2,248,075; wanaume 1,848,238).

SOMA: Je, Miswada Mipya ya Sheria za Uchaguzi Imekidhi Matarajio ya Wananchi?

Miaka 30 – 39 (wanawake 3,615,780; wanaume 3,111,938); miaka 40 – 49 (wanawake 3,099,424; wanaume 2,809,666); miaka 50 – 59 (wanawake 2,479,580; wanaume 2,022,026); miaka 60 – 69 (wanawake 1,767,711; wanaume 1,286,192); miaka 70 – 79 (wanawake 921,499; wanaume 564,095); na umri wa zaidi ya miaka 80 (wanawake 495,287; wanaume 199,900).

Kwa ujumla, wanawake waliojiandikisha katika daftari nchini Afrika Kusini ni zaidi ya wanaume kwa kiasi cha takribani milioni 3. Idadi hii ya wapiga kura ni zaidi ya kura zote zilizompa ushindi Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera mwaka 2020.

Mwitikio wa wapiga kura

La kujifunza pia ni kuhusu mwitikio wa wapiga kura kujitokeza kwenda kupiga kura. Katika nchi yetu, mwitikio umekuwa ukishuka badala ya kupanda. Hii imedhihirika zaidi katika chaguzi za miaka ya karibuni. Kwa mfano, mwitikio wa wapiga kura ulishuka kutoka asilimia zaidi ya 70% mwaka 1995, 2000 na 2005 hadi 42% na 50% pekee mwaka 2010 na 2020.

Wakati mwitikio ukishuka Tanzania, kwa nchi kama Gambia, mwitikio wa kupiga kura uliweza kupanda kutoka asilimia 59% tu  mwaka 2016 hadi asilimia 90% mwaka 2021. Aidha, kwa jirani zetu Kenya mwitikio uliweza kupanda pia kwa takribani mara dufu kutoka 39% ya mwaka 2017 hadi 64% katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Hii ilitokana na matumaini mapya ya ushindani yaliyojengeka miongoni mwa wakenya baada ya kuanza kutumika rasmi kwa Katiba Mpya ya Kenya ya Mwaka 2010, ikiwemo Imani iliyoongezeka kwa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi ya Kenya (IEBC).

Kwa Tanzania, malalamiko ya Wananchi kuhusu haja ya Katiba Mpya ili kuizaa Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itaaminika machoni pa wagombea na wapiga kura yamefumbiwa macho hadi tunakaribia kufanya uchaguzi mwingine pasipo Tume Huru kikatiba. Ni vyema kujifunza kuwa Katiba Mpya italeta matumaini mapya Tanzania.

Mgombea binafsi

Katika ziara zangu za uangalizi wa Uchaguzi barani Afrika nimebaini pia kuwepo kwa wagombea huru au binafsi wasiolazimishwa kudhaminiwa na chama chochote cha siasa pia kunaongeza hamasa ya Mchakato wa Uchaguzi. Nikiwa Nchini Gambia kuangalia uchaguzi nilitembelea majimbo yote 53 na Kata 100 kati ya 120 zinazounda Nchi hiyo.

SOMA: Mambo Kumi Muhimu Kuboresha Muswada wa Tume ya Uchaguzi Tanzania

Nilichogundua ni kuwa kulikuwa na wagombea wapatao 85 wasiowakilisha chama chochote katika vyama 19 vilivyo na usajili wa kudumu nchini humo. Jumla ya wagombea wote wa nafasi ya Ubunge walikuwa ni 251 na baada ya upigaji kura kukamilika, Tume Huru ya Uchaguzi ya Gambia iliwatangaza wabunge wapatao 12 wasiodhaminiwa wala kuwakilisha chama chochote cha siasa.

Maeneo ya mijini ndiyo yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya ushindi wa wabunge binafsi kama vile: Banjul (2); Foni (5); Busurubala (1); Sabach (1); Kiang (1); Janjanbureh (1) na Niani (1). Uganda pia ina wabunge binafsi 73 kati ya bunge la watu 529 lililotokana na uchaguzi wa mwaka 2021.

Wabunge hao binafsi wameongezeka ikilinganishwa na uchaguzi wa miaka ya nyuma kama ifuatavyo: 2016 (66); 2011 (43) na 2006 (40). Ingawa mfumo wa mgombea binafsi si maarufu sana katika ngazi ya urais duniani, Rais George Washington wa Marekani alipata na kutumikia urais wake kama mtu binafsi bila kuwakilisha chama hadi alipomaliza kipindi chake mwaka 1796.

Yatosha kujifunza kuwa mfumo wa mgombea binafsi kwa sasa hauepukiki na ni lazima tuanze kuutumia hata kama tutapaswa kupambana na changamoto zake.

Matumizi ya teknologia

Kuhusu matumizi ya teknolojia, tuna mifano mingi ya kujifunza. Nchini Afrika Kusini, mwananchi ambaye atakuwa ametimiza umri wa kupiga kura ifikapo siku ya uchaguzi ujao anaweza kujiandikisha kupiga kura kwa moja ya njia mbili: Kujiandikisha yeye mwenyewe kwa kutumia simu au computer yake au kwenda kujiandikisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inapopita kuandikisha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi ya Kenya, Mkenya aliyetimiza umri wa kupiga kura anaweza kujiandikisha kidigitali au kusubiri Tume itakapopita. Kwa Tanzania, nimeona kuwa matumizi ya TEHAMA yamekwishaanza. Ukiingia kwenye tovuti ya Tume unaweza kuboresha taarifa zako au kuhama kituo chako kwa kutumia mtandao katika tovuti ya Tume.

SOMA: ‘Kidole Kimoja Hakivunji Chawa’: Uchaguzi Mkuu wa Nigeria 2023 na Mambo Makuu ya Kujifunza Tanzania

Hata hivyo jambo ambalo tunaweza kujifunza ni kuanza kuruhusu vitu viwili zaidi. Kwanza, kuweza kujiandikisha kama mpiga kura mpya kupitia tovuti ya Tume au kuweza kujiandikisha kupitia mfumo wa wakala wa uandikishaji wapiga kura utakaoanzishwa na Tume. Mfumo huo unaweza kufanana na ule wa usajili wa laini za simu ambao TCRA wameuanzisha na kufanikiwa sana kwa kushirikiana na mitandao ya simu.

Haitakuwa ngumu hata kidogo kuiga mfumo huo kwenye uandikishaji wapiga kura ili ifikie mahali mtu anaweza kwenda kwenye mwavuli wa usajili laini za simu na kujiandikisha kupiga kura. Kwa kuhitimisha, nadhani tunaweza kujifunza matumizi mazuri kwenye uchaguzi. Kwangu mimi, kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu mwaka 2025 ni ufujaji wa pesa za walipa kodi.

 Katika Nchi jirani ya Kenya, kura zinazopigwa katika siku ya Uchaguzi Mkuu ni sita: Rais na Makamu wake; Mbunge; Diwani; Seneta, Mbunge Mwanamke na Gavana. Hata Uganda, mpiga kura anachagua watu 7 kwa mpigo: Rais; Wabunge wa Majimbo (353); Wabunge wanawake(146); Wabunge wanajeshi (10); Wawakilishi wa wafanyakazi(5); Wawakilishi wa vijana(5); Wawakilishi wa Watu wenye Ulemavu (5) na Wawakilishi wa Wazee (5).

Pia wanachagua viongozi wa ngazi za halmashauri au Parish kama wanavyoziita. Je sisi tunashindwa nini kuchagua kwa mkupuo Rais na Makamu wake; Mbunge wa Jimbo; Wabunge Wanawake; Diwani na viongozi wa serikali za vijiji, mtaa au kitongoji? Kwa nini tusijifunze kuunganisha uchaguzi huo wa ngazi zote ili tuokoe mabilioni ya fedha za walipa kodi?

Tukiamua, tunaweza !

Deus Kibamba Ni mtafiti Na mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa. Pia, ni Mhadhiri wa Masuala ya Diplomasia na Sheria za Kimataifa katika Chuo Cha Diplomasia cha Dkt Salim Ahmed Salim, Kurasini, Dar es Salaam. Anapatikana kwa nambari: +255 788 758 581 na barua pepe: dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

2 Responses

  1. Maoni yako ni mazuri kwani hata mimi nimekubaliana nayo. Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ikinzingatia ushauri huu ni hakika itaandika historia nyingine katika bara la Afrika.Historia ya kwanza ni kisiwa cha amani na uvumilivu,Historia ya pili ni hii ya kukuza na kuimarisha demokrasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *