Search
Close this search box.

Mambo Kumi Muhimu Kuboresha Muswada wa Tume ya Uchaguzi Tanzania

Serikali haina budi iyarekebishe mambo hayo kuiwezesha nchi yetu ipate sheria nzuri zaidi inayoanzisha, kuisimamia, na kuongoza shughuli za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

subscribe to our newsletter!

Nimefanikiwa kuupitia kwa kina na kuuchambua Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama ulivyowasilishwa Bungeni Novemba 10, 2023, na kubaini mapungufu lukuki. Kwa nafasi yangu, nimeamua kuchangia mambo kumi muhimu katika kuuboresha Muswada huu ili uwe na tija kwa siasa za Tanzania. 

Kipekee, nimeamua kugusia maeneo ambayo yamekuwa chanzo cha mzozo kwa lengo kwamba yakikubalika na waheshimiwa wabunge, basi Serikali itashawishiwa kuyarekebisha ili nchi yetu ipate sheria nzuri zaidi inayoanzisha, kuisimamia, na kuongoza shughuli za Tume ya Taifa ya Uchaguzi. 

Muswada huu umewasilishwa kwa mara ya kwanza na unaruhusiwa kujadiliwa na kila mwenye kutaka kufanya hivyo kuanzia sasa hadi mwishoni mwa Januari 2024 ambapo wadau tutaalikwa kupeleka rasmi maoni Bungeni kabla ya Muswada huo kusomwa kwa mara ya pili. 

Miswada inayotumia hati ya kawaida kama huu husomwa mara tatu Bungeni kabla ya kupitishwa na kuwa sheria pale itakaporidhiwa na Rais.

Jina huumba

Jambo la kwanza nililoliona ni jina lisiloakisi lengo la kutungwa kwa sheria hii. Sheria hii inatungwa mahsusi kwa ajili ya kutengeneza Tume ya Uchaguzi itakayokuwa huru na huru kweli, isiyoingiliwa, kuelekezwa, kuagizwa wala kufokewa na mtu, chombo, taasisi au mamlaka yoyote.

SOMA ZAIDI: Je, Miswada Mipya ya Sheria za Uchaguzi Imekidhi Matarajio ya Wananchi?

Waswahili husema, jina huumba. Kwa nini tumeamua kubakiza jina lisiloendana na lengo kuu la utungaji wa sheria hii? Kwani tulikuwa hatuna Tume ya Taifa ya Uchaguzi mpaka kupelekea uhitaji wa kuiboresha tume hii? 

Kwa maoni yangu, kinachokosekana na kulalamikiwa na wadau wa demokrasia ya uchaguzi ni chombo mithili ya ‘mwamuzi huru wa mpira’ ambaye ataweza kupuliza filimbi akiona dhambi zimetendeka uwanjani bila kujali nani amefanya dhambi hizo. 

Uhuru wa tume humaanisha mambo mawili au matatu – kiini, muundo, na upatikanaji wa wajumbe na rasilimali watu na fedha. Katika yote haya, jina huumba, na ni kiashiria muhimu sana cha kujua tume ni huru au la. 

Nashauri jina la tume mpya liwe ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania. Dhana ya uhuru wa tume kama lengo kuu la kutungwa kwa sheria hii ijitokeze pia katika madhumuni na sababu mwishoni mwa sheria.

Muundo wa tume

Jambo la pili muhimu ambalo liliazimiwa na waliotoa wito wa kutungwa kwa sheria kuboresha mfumo wa usimamizi na uratibu wa uchaguzi ni haja ya kuiumba Tume ya Uchaguzi kama taasisi iliyo na muundo unaoakisi taasisi ya kisasa. 

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Umekuwa Kichocheo Kikubwa cha Marekebisho ya Katiba Tanzania

Katika hili, tume inapaswa kuwa na Kamisheni au Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wa Tume. Ni kutokana na mgawanyo huu ndipo tume itaweza kuwa taasisi huru, huku kila moja ya mihimili hiyo ya tume ukiwa na kazi zake. 

Kwa mfano, kazi kuu ya Kamisheni ni kuipa tume, na kusimamia, maono, ndoto na malengo. 

Wajumbe wa Kamisheni wanapaswa kuwa watu wenye maono juu ya jinsi bora ya kuendesha uchaguzi Tanzania katika namna ambayo walioshinda watatangazwa washindi, walioshindwa watakubaliana na matokeo tayari kwenda kuapishwa, na wachache walio na mashaka watafungua mashauri dhidi ya mashaka yao.

Endapo kama tume itasukwa vizuri na kuaminika, baadhi ya malalamiko yanaweza kuishia katika kamati za rufaa za Kamisheni badala ya kila kitu kwenda Mahakamani. 

Wajumbe wa Kamisheni ya tume watakutana mara nne tu kwa mwaka kwa lengo la kupokea, kujadili taarifa za uendeshaji wa tume, na kutolea maelekezo mahsusi. 

SOMA ZAIDI: Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo

Kamisheni ya tume lazima ijiepushe na mtego wa kuingia jikoni kuanza kushiriki kupika chakula yenyewe maana kufanya hivyo kunaiondolea mamlaka ya kuwawajibisha watendaji pale mambo yanapokwenda mrama. 

Kwa ushauri wangu, kiongozi mkuu wa Kamisheni atakuwa Mwenyekiti ambaye, yeye pamoja na makamu wake, watachaguliwa kidemokrasia katika mkutano wao wa kwanza baada ya kukamilika kwa mchakato wa usaili, uteuzi, na uapisho wao.

Chini ya Kamisheni, au Bodi, kunapaswa kuwa na Menejimenti ya Tume ikiongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni mwajiriwa wa Kamisheni na siyo mteule wa Mamlaka yoyote nyingine ya dola. 

Mkurugenzi wa Uchaguzi ndiye kiungo, au shingo, kati ya Kamisheni (kichwa) na Secretareti (mwili) wa Tume. Yeye ndiye mwajiriwa pekee wa Kamisheni na wengine wote atawaajiri yeye. 

Mkurugenzi ndiye Afisa Mtendaji Mkuu na Afisa Maduhuli wa Tume. Kwa nafasi yake kama kiungo, Mkurugenzi wa Uchaguzi ni Katibu wa Kamisheni, au Bodi, ya Tume. Mkurugenzi atakuwa ndiye Mkuu wa Menejimenti ya Tume, akiwa na jukumu la kuongoza utendaji wa tume wa kila siku, ikiwemo kutoa matamko ya tume.

SOMA ZAIDI: Cheo cha Naibu Waziri Mkuu, Gharama Kuendesha Serikali Zazua Gumzo Mabadiliko Baraza la Mawaziri. Uchaguzi Mkuu 2025 Watajwa

Utaratibu ambapo Mwenyekiti ndiye anazindua shughuli za uandikishaji wapiga kura, elimu ya uraia, mafunzo ya makarani, au ratiba ya kampeni siyo sawa na lazima ukomeshwe na sheria mpya.

Shughuli zote zitabuniwa, kuratibiwa, na kusimamiwa na secretarieti ya tume ambayo ndiyo yenye wataalamu walioomba kazi na kuajiriwa kwa vigezo vya kuijua kazi ya usimamizi wa uchaguzi chini ya uongozi shupavu wa Mkurugenzi. 

Wataalamu hawa wataendelea kusheheni uzoefu kutokana na shughuli zao ndani na nje ya tume hapa nchini na kwingineko watakakoalikwa kwenda kupeleka na kuchota uzoefu wa masuala ya uchaguzi. 

Ni kwa msingi huu, tabia ya kutumia Mwenyekiti katika shughuli za kila siku za tume itapaswa isiendelee. 

Mjumbe wa tume ambaye anajiona kuwa na utaalamu na uzoefu wa masuala ya uchaguzi kiasi cha kutamani kufanya kazi za kila siku atapaswa kujiengua kutoka kwenye Kamisheni na kuomba nafasi ya ajira katika Sekretarieti ya Tume ili akafanye kazi chini ya uangalizi wa Kamisheni ya Tume. 

SOMA ZAIDI: Wadau Wapendekeza Marekebisho Muhimu Yafanyike Katika Katiba ya Sasa Kuruhusu Kujiandaa na Uchaguzi

Ili kuleta uwazi wa majukumu ya vyombo mbalimbali katika tume, nashauri Muswada utumie neno ‘Kamisheni’ kumaanisha ngazi ya wajumbe wa tume yenye wajibu wa kuisimamia Secretarieti ya Tume. 

Pia, ni vema maneno Kamisheni, Secretarieti na Menejimenti yakapatiwa maana zake katika kifungu Nambari 2 cha Muswada huu ili yawe sehemu ya sheria itakapopitishwa.

Upatikanaji wa wajumbe

Zaidi ya hayo, kuna suala la upatikanaji wa wajumbe ambalo nimelisemea katika makala yangu yaliyopita. 

Kwenye makala hayo, nimeshauri kuwa Mkurugenzi wa Tume awe ni mwajiriwa wa Kamisheni ili kuepusha mgongano wa kimaslahi na kimamlaka pale Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Mkurugenzi wanapokuwa wote ni wateule wa Rais. 

Kwa maoni yangu, hata kiapo cha Mkurugenzi kisiwe cha Rais bali kiwe cha Tume, ambayo, kwa bahati nzuri, Mwenyekiti wake atakuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu, au ya Rufani, ambaye yupo kazini au mstaafu. 

SOMA ZAIDI: Sheria za Uchaguzi, Vyama vya Siasa Kufanyiwa Marekebisho?

Kwa ajili hiyo, Mwenyekiti anaweza vema kabisa kumwapisha Mkurugenzi kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Utaratibu ulioelezwa katika kifungu cha 5(4) cha Muswada wa namna ya kumpata Mkurugenzi una upungufu mkubwa.

Badala yake, Muswada ueleze kuwa baada ya kuteuliwa na kuapishwa kwao, wajumbe watakutana kama Kamisheni ya Tume na kuanzisha mchakato wa wazi wa uajiri wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, ambaye, baada ya kupatikana, atakuwa ndiye Katibu wa Kamisheni na Mtendaji Mkuu wa Tume. 

Kwa mantiki hiyo, kifungu Nambari 9(3) kinachomtaka Mkurugenzi wa Uchaguzi kuwa Katibu wa Kamati ya Usaili, kwa ajili ya kupata Wajumbe, ni batili, na itafaa kifutwe kwa vile kinakinzana na misingi ya utawala bora. 

Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni Katibu wa Kamisheni anakuwaje Katibu wa Kamati itakayoizaa Kamisheni? 

Yaani, Mkurugenzi anashiriki katika mchakato wa kuwapata wajumbe wa Kamisheni ya Tume halafu itarajiwe kuwa huyu atakuja kuwaheshimu wajumbe watakapoanza kazi ya kumsimamia na kumwajibisha? Hapana!

SOMA ZAIDI: ‘Kidole Kimoja Hakivunji Chawa’: Uchaguzi Mkuu wa Nigeria 2023 na Mambo Makuu ya Kujifunza Tanzania

Kamati ya usaili

Jambo moja kwenye Muswada ambalo limeshangiliwa na wadau ni uwepo wa Kamati ya Usaili itakayozaa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi. Hata hivyo, ukiangalia vema mchakato wa usaili wa waombaji wa nafasi ya ujumbe wa tume, unaona kuwa haujakaa vizuri. 

Ili kuleta uwazi, itapendeza kwamba mchakato wa usaili wa waombaji lazima uhusishe pia maoni ya Watanzania kuhusu uadilifu wa waombaji. 

Kinachoweza kufanyika hapo ni kuwa, mara baada ya kukamilisha usaili, Kamati ichapishe na kutangaza majina 11 ya waombaji waliosailiwa, kuchujwa, na kuonekana wana sifa katika vyombo vya habari ili Watanzania wenye taarifa nzuri na mbaya juu ya sifa za waombaji waweze kuzituma kwa Kamati ya Usaili. 

Baada ya siku 30, Kamati itapaswa kukaa ili kupitia maoni waliyopokea kuhusu ukubalifu wa wajumbe wanaopendekezwa kupelekwa kwa Rais kwa ajili ya kuteuliwa. 

Endapo baadhi ya wajumbe watakuwa wametajwa kuwa na sifa, au mwenendo, hafifu, au mbaya, basi Kamati inaweza kutengua mapendekezo yao na kuyaondoa majina hayo.

SOMA ZAIDI: Maswali Muhimu Uchaguzi Mkuu wa Kenya Ukielekea Mahakamani

Kwa uzoefu wa nchi nyingine, Uhuru wa Tume pia hupimwa kwa kigezo cha ulinzi wa ajira za wajumbe wa tume. Hapa Tanzania, kumekuwa na mjadala kama huo kuwahusu majaji pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). 

Kwa msingi wa ulinzi thabiti wa ajira, kifungu Nambari 8(2)(3) kina kasoro. Kwa mfano, hoja ya kifungu cha 8(2)(e) kwamba Rais anaweza kumuondoa madarakani mjumbe kwa sababu ya kupoteza uwezo wa kutenda majukumu yake, tabia mbaya, au kupoteza sifa za ujumbe, inaleta utata. 

Je, tabia mbaya ni kama ipi? Je, ni kwa vigezo vya nani? Je, kwa tafsiri ipi? 

Kutokana na utata huo, nashauri kuwa kifungu hiki kitamke kuwa Rais anaweza kuunda Kamati ya Uchunguzi ambayo itahusisha pia uwakilishi wa Jaji wa Mahakama na mjumbe wa Tume ya Uchaguzi kutoka nchi japo moja ya Jumuiya ya Madola. 

Kamati hii itachunguza endapo kama tuhuma dhidi ya Mjumbe wa Tume zina ukweli na kwamba upungufu wa uwezo au tabia hiyo mbaya vina athari kwa utendaji kazi wa mjumbe husika wa tume. 

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Kenya Umekwisha. Tanzania Imejifunza Nini?

Hii itaepusha uwezekano wa mjumbe, ambaye anafanya kazi yake vizuri, kutungiwa tuhuma za kutengenezwa ili kumchafua endapo inaaminika ana misimamo fulani isiyoyumbishwa.

Hoja za ziada

Kwa kuhitimisha, kuna mambo mengine matatu. Kwanza, suala la uhuru wa kifedha na kibajeti wa tume. Hili limepigiwa kelele kwa miaka mingi sana. 

Ilifika wakati tume ilikuwa inataka kufanya kazi ya uhuishaji wa daftari la wapiga kura, ikiwemo kuandikisha wapiga kura wapya, lakini changamoto ya rasilimali fedha ilionekana kuwakwamisha. 

Itafahamika kuwa baada ya kuombea pesa Serikalini, jukumu la idara zisizohuru za Serikali huwa ni kusubiri majibu na siyo vinginevyo. 

Ni kutokana na ukweli kwamba hili na mengine yanayoweza kujitokeza, nashauri kuwa kifungu cha 22 kirekebishwe ili kutamka bayana kuwa fedha za uendeshaji wa shughuli za tume zitatoka Mfuko Mkuu wa Hazina badala ya kuishia kusema kuwa zinatoka katika bajeti ya Serikali. 

SOMA ZAIDI: Ado Shaibu: Hivi Ndivyo Tanzania Inaweza Kupata Tume Huru ya Uchaguzi

Sambamba na hili la fedha, kifungu cha 23 kirekebishwe ili kuondoa dhana ya tume kusubiri kushauriana na Waziri husika katika kuandaa Muundo wa Utumishi wa Sekretarieti ya Tume. 

Mwisho, nimekagua, pasipo mafanikio, kifungu kinachohusu ofisi za tume, na nashauri kiwepo kifungu kipya kinachotamka kuwa tume itakuwa na ofsi zake yenyewe katika kila mkoa na wilaya nchi nzima.

Kama imewezekana kuiwezesha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikawa na ofisi hadi ngazi ya wilaya, tunashindwaje kuipa Tume ya Uchaguzi ofisi hadi ngazi ya jimbo? 

Nikiwa katika uangalizi wa uchaguzi nchini Kenya, nilibaini kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) ina ofisi katika kila mkoa kwenye mikoa kumi ya nchi hiyo, kuanzia Kakamega, Bungoma, Busia hadi jiji la Nairobi. Pia, tume ina ofisi katika kila jimbo la uchaguzi kwa majimbo yote 290 ya Kenya. 

Vivyo hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Uganda ina mtandao wa kudumu wa ofisi katika majimbo yake yote 353 ya kijiografia, zikitoa huduma za uandikishaji wapiga kura, uelimishaji, uratibu wa kampeni na usimamizi wa uchaguzi kwa ujumla wake. 

SOMA ZAIDI: Jinsi Uchaguzi Mkuu 2020 Ulivyoacha Simulizi za Majonzi Tarime

Nashauri kuwa Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi utamke bayana kuwa tume itakuwa na ofisi hadi katika ngazi ya kila Jimbo la Uchaguzi. 

Tukutane kwenye makala ijayo ambapo nitachambua na kujadili kwa kina Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani Tanzania.

Mungu ibariki Tanzania!
Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *