Timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, itashiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) mwezi ujao nchini Ivory Coast, ikiwa ni mara ya tatu tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo makubwa barani.
Fainali hizo ni za mwaka 2023 lakini zimepangwa kufanyika Januari mwakani kutokana na hali ya hewa ya Ivory Coast kuwa ya joto kubwa katikati ya mwaka kama ambavyo hufanyika kila mwaka. Hata fainali zilizopita nchini Cameroon zilisogezwa mbele kwa sababu kama hizo.
Fainali hizo zitashirikisha nchi 24, takriban nusu ya idadi ya mataifa yote 54 ya Afrika, tofauti na ilivyokuwa awali wakati fainali hizo zilipokuwa zinashirikisha nchi 16 tu na hivyo kuwa ngumu kwa mataifa mengi kufuzu.
Ni fainali kubwa ambazo zinakusanyisha wachezaji nyota kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Wako ambao walitakiwa na mataifa makubwa ya Ulaya kutokana na kuzaliwa huko au kuwa na wazazi wenye asili ya nchi hizo, lakini wameona fahari kuja Afrika kuchezea nchi zao za asili na hivyo kuongeza ushindani mkubwa.
Mbali na hao, wako wachezaji nyota wanaotamba katika ligi kubwa za Ulaya kama akina Sadio Mane, Mohamed Salah, Victor Osimhen, ambaye hivi karibuni alitwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka, Riyad Mahrez, Wilfred Nditi, Thomas Partey, Mbwana Samatta, Nicholas Jackson, Mohamed Kudus, Jonathan Bamba, Sofian Amrabat na Houssein Aouar.
SOMA ZAIDI: Michezo ni Muhimu Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa Mafanikio
Na wapo nyota wengine wengi wanaosakata soka ndani ya bara la Afrika, lakini wakiwa nje ya nchi zao kama Percy Tau, Simon Msuva, Fagrie Lakay na Pacome Zouzoua.
Hao pamoja na wengine wengi ndiyo watakaoongeza chachu, ushindani na uzuri wa fainali hizo kubwa kwa ngazi ya taifa zitakazoanza Januari 13 na kumalizika Februari 11.
Tanzania haijawahi kuvuka hatua ya makundi ya fainali hizo tangu ilipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1980 na baadaye mwaka 2019 wakati fainali hizo zilipofanyika Misri.
Wakati kufuzu kumepunguzwa ugumu kutokana na idadi ya washiriki kufikia takriban nusu, kufanya vizuri kumekuwa tatizo kubwa zaidi kutokana na nyota wengi kuona umuhimu wa kushiriki fainali hizo na kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kuwalinda.
Zamani klabu ziliweza kuwazuia wachezaji wao kujiunga na timu zao za taifa, hasa katika kipindi kama hiki ambacho ligi za Ulaya zinaendelea, lakini tangu FIFA iboreshe kanuni zake, hilo haliwezekani tena, labda mchezaji mwenyewe astaafu kuchezea taifa lake.
Maana yake ni kwamba ushindani unaendelea kuwa mkubwa na hivyo uwezekano wa kufanya vizuri unakuwa mdogo kama timu itakuwa haijajiandaa vizuri kukabiliana na mataifa makubwa kisoka barani Afrika na yenye wachezaji nyota wanaotamba duniani.
SOMA ZAIDI: Timuatimua ya Makocha Imekuwa Mtindo Ligi Kuu
Tanzania imepangwa kundi moja na Morocco, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia. Kwa maana nyingine, Tanzania ndiyo taifa dogo kwa rekodi. Morocco, DRC na Zambia zishawahi kutwaa kombe hilo, huku timu kutoka Afrika Kaskazini ikiandika historia ya kuwa taifa la kwanza la Afrika kufuzu kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana nchini Qatar.
Maandalizi muhimu
Kwa hiyo, wakati tukiitakia kila la heri Tanzania katika mashindano hayo, ni muhimu pia kuikumbusha kuhusu maandalizi ambayo ndiyo muhimu kujenga timu ambayo inastahili kuombewa kila la heri.
Hatujasikia programu ya Tanzania kuelekea fainali hizo, yaani imepanga kuweka kambi wapi, kucheza mechi ngapi za kirafiki, itaweka makazi yake sehemu gani ikiwa Ivory Coast na kwa ujumla motisha kwa msafara mzima.
Kocha Carlos Alberto Pereira alisema baada ya kuiwezesha Brazil kutwaa ubingwa mwaka 1994 kuwa kama kuna kitu alitaka kisikosewe wakati wa fainali hizo ni malazi, taratibu za kuingia hotelini na kupoteza muda uwanja wa ndege.
Alisema si kitu kizuri kwa wachezaji kutumia muda mrefu eneo la mapokezi wakisubiri kupangiwa vyumba, wakati wanahitaji kupumzisha akili kwa ajili ya michezo iliyo mbele yao. Kwa hiyo, alihakikisha malazi yao yanaandaliwa mapema kiasi kwamba wachezaji wanapofika hpotelini, hawachukui dakika 10 wote wanakuwa wameshaingia vyumbani.
SOMA ZAIDI: Hongera Hersi Said, Kazi ni Kuziamsha Klabu Afrika
Hii ni sehemu inayoweza kuonekana ndogo sana, lakini muhimu kisaikolojia. Tunaweza kuwa hatujafikia huko, lakini kuna mambo mengi ambayo yalitakiwa yawe yamefanyika mapema kiasi kwamba vyombo vya habari vingeanza kudodosa kilichoko huko ambako wabeba bendera wetu watakuwa.
Katika kikosi cha awali cha wachezaji 53, nimeona kuna sura mpya nyingi ambazo zinahitaji muda wa kutosha na wazoefu ili kujenga maelewano ya kawaida ya kijamii kabla yay ale ya uwanjani.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeipanga Januari 3 kuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha majina 27 ya mwisho kwa ajili ya fainali hizo, hivyo kuna muda mfupi umesalia kabla ya kocha Adel Amrouche kupata wachezaji hao na kutuma majina CAF. Atakuwa na siku zisizozidi kumi kuchambua wachezaji aliowaita na kuwachuja kabla ya siku ya mwisho.
Kujipima nguvu
Cha muhimu zaidi ni programu ya mechi za kujipima nguvu kabla ya kuwa tayari kimashindano. Labda hiki ni kipindi kibaya kwa kuwa kina muda mfupi wa maandalizi kabla ya fainali zenyewe.
Iwapo fainali zinafanyika majira ya joto, huwa ni rahisi kwa kuwa karibu kila eneo ligi zinakuwa zimemalizika na hivyo timu kuwa na hata mwezi mzima wa kujiandaa na hivyo kucheza mechi za kutosha; kuanzia na timu nyepesi, ngumu na kumaliza na nyepesi.
SOMA ZAIDI: CHANETA Imetufikirisha Kuhusu ‘Goli la Mama’
Hata hivyo, hiyo haizuii kuwa na mechi nzuri za maandalizi badala ya kwenda kujaribisha wachezaji kama ilivyokuwa katika mechi ya mwisho ya Taifa Stars jijini Dar es Salaam wakati Amrouche alipojaribu wachezaji kadhaa katika mechi muhimu ya mashindano.
Fainali za AFCON 2023 ni vita ambayo nchi inahitaji kutumia kila silaha yenye ufanisi kushinda. Hatutarajii kuona timu ikiwa na wachezaji wanaojaribiwa na kuibua hisia za kuwatafutia soko wachezaji badala ya kutafuta ushindi kama zilivyoibuka nchini Misri.
Bila shaka hisia hizo hazikuwa za ukweli, lakini tatizo ndiyo lililoibua tuhuma hizo. Tuna uhakika hilo haliendi kutokea. Kila la heri timu yetu katika maandalizi ya AFCON 2023 na fainali zenyewe.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.