Dodoma: Haikuwa rahisi kwa Alice Chalo ,43, kujiingiza kwenye shughuli ya uchimbaji wa madini ujenzi akiwa mwanamke pekee kufanya kazi katika mgodi mpya uliopo kata ya Chamkoroma, wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Ugumu wa maisha ulimfanya mama huyu wa watoto watano kujiingiza kwenye uchimbaji wa madini hayo mwaka 2016 baada ya kutelekezwa na mume wake tangu mwaka 2001. Kabla ya hapo alikuwa akijishughulisha na shughuli za kilimo.
“Kazi hii si rahisi, tunafanyia shida tu” anasema Alice, “Tufanyaje?”
“Maana nikisema niuze mboga haziendi, naona bora nifanye kazi hii hapa.” aliendelea huku akiwa ndani ya shimo akiendelea na kazi.
Ni umbali wa takribani Kilomita 48 kutoka Kongwa mjini mpaka mahali yalipo machimbo haya ya madini ujenzi katika kata ya Chamkoroma ambapo The Chanzo ilikutana na Alice, Novemba 26, 2023.
Ni eneo ambalo limezungukwa na mashimo mengi ya wachimbaji wa madini ujenzi yenye urefu wa hadi futi sita.
Alice ambaye ni mrefu kiasi akiwa amevaa gauni la kitenge na kitambaa kichwani chenye rangi ya waridi, huku akiwa kashikilia nyundo mkononi, beleshi na mfuko wa kuhifadhi nguo zake za kazi. Hakuwa na vifaa vyovyote vya usalama wakati wa kazi.
SOMA ZAIDI: Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’
Anakiri kuwa ni kazi ngumu kwake, hana chaguo zaidi ya kuendelea kupambana kulingana na hali aliyonayo. Hutumia muda wa masaa saba hadi nane kwa siku hapo mgodini.
“Kwa kuwa mawe ni magumu wakati mwingine napata kiasi kigodo, na wakati mwingine huwa nakosa” anasema Alice “muda mwingine naweza kupata robo, nusu hadi kilo kwa siku”
Kilogram moja ya madini ujenzi haya akiuza anapata shilingi 70,000, nusu ni shilingi 35,000 na robo ni kati ya shilingi 15,000 mpaka 20,000.
Kipato hiki kimemuwezesha Alice kuweza kujikimu yeye na familia yake licha ya ugumu wa kazi yenyewe.
“Pamoja na kwamba sijajenga bado lakini baadhi ya mambo inanisaidia kama vile kuhudumia watoto. Lakini [kwa sasa] sina kitu kutokana na ajali niliyoipata.”
Kama ilivyo kwa kazi yoyote ile haikosi changamoto. Changamoto kubwa ambayo alipitia na hajaisahau ni ajali ya kufukiwa na kifusi mwaka 2021 wakati akiwa kwenye shimo akichimba.
“Mchanga ulitoka mbele yangu ukanifukia mwili mzima. Nikafukuliwa na nikatolewa na wachimbaji wenzangu” anasimulia Alice “Nilipotolewa nikawa siwezi kukaa, kusimama siwezi [na] kulala siwezi. Nikaja kubebwa mgongoni nikarudishwa nyumbani.”
Tukio hili lilimfanya akae nyumbani kwa muda wa miaka miwili bila ya kufanya kazi yoyote mpaka mwaka huu aliporudi tena kazini.
Hakuna Kazi ya Mwanaume au Mwanamke pekee
Wakati wengine wakiingia kwenye kazi hii kutokana na ugumu wa maisha, kama ilivyo kwa Alice, ni tofauti kwa Rachel Joseph Njau ,51.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kujenga Jamii Yenye Mtazamo Chanya Kwa Wanawake wa Makundi Maalumu?
Mchimbaji huyu wa madini ya Tanzanite kutoka Mirerani anayemiliki mgodi wake anasema, amejiingiza kwenye uchimbaji wa madini kwa kuwa ni kazi anayoipenda na haikumuhitaji kuwa na cheti chochote cha elimu.
“Nilikuwa naipenda kazi hii toka nikiwa na miaka sita. Hivyo kuingia kwenye uchimbaji kwangu ilikuwa ni rahisi sana,” anasema Rachel “Isitoshe baba yangu ni mchimbaji alikuwa anamiliki migodi sita.”
Rachel ambaye ni mama wa watoto wawili anasema kazi hii imeweza kumsaidia kuendesha maisha yake pamoja na changamoto zinazojitokeza.
“Unapochukua uthubutu, kujiamini, na kuipenda kazi yako lazima uone urahisi.”
Mbali na kuwepo kwa vikwazo ,Rachel anasema wanawake wasichague kazi, hakuna kazi ya mwanaume au mwanamke, muhimu ni kujiamini na kuipenda kazi unayoifanya.
“Tanzania ni nchi iliyobarikiwa sana, tutazalisha mabilionea wanawake kila mkoa kama wanawake watashiriki ipaswavyo kwenye hii sekta”
Kwa mujibu wa Kituo cha Uzalishaji Madini Afrika, takriban asilimia 40 hadi 50 ya wanawake kwenye sekta ya madini Afrika wanajitajhidi kuvunja dhana ya kwamba sekta ya madini ni ya wanaume pekee.
Afisa kutoka EACOP Fatuma Mssumi akizungumza kwenye Jukwaa la Uziduaji la mwaka 2023 amesema, mbali na wanawake kujengewa uwezo na kubadilishwa mitazamo yao, jamii inapaswa pia kutambua kuwa sekta ya madini ni ya watu wote wanawake na wanaume.
SOMA ZAIDI: Wanawake Ziwa Victoria Wabainisha Changamoto Zinazowarudisha Nyuma
“Iwapo utamuona mwanamke ameenda kutafuta fursa katika sekta hii usimshangae,” anasema Fatuma. “Tubadilike tuone kwamba hii sekta ni ya watu wote. Na hii tunaomba sana kwa upande wa Serikali, lakini vilevile na asasi mbalimbali kutoa elimu kwenye jamii.”
Ukiwa muoga huwezi kutoboa
Rehema Mahega ,46, mkazi wa Shinyanga anayejishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu na anayefanya kazi katika mgodi wa Mwime uliopo Kahama anasema, kazi ya uchimbaji madini ni rahisi kama mwanamke akijitambua na kutoa dhana ya kwamba mwanamke ni kiumbe dhaifu.
“Ukiwa mtu muoga muoga huwezi kutoboa,” anasema Rehema alipoongea na The Chanzo Novemba 19, 2023.
“Kwa sababu ule mfumo dume wa mwanzo ilikuwa unatusumbua sana. Kiasi kwamba ilikuwa mwanamke anapewa nafasi ya kuwa mama lishe kwenye migodi unawapelekea chakula wale ili waweze kuendesha mambo yao.”
Mama huyu mwenye watoto watano alianza na biashara ya kuuza mazao, ilipofika mwaka 2019 aliingia kwenye sekta ya uchimbaji madini rasmi. Aliona kuna uwezekano mkubwa wa kupata fedha, tofauti na biashara nyingine.
Mbali na kupata mafanikio kadhaa kwenye kazi hii, Rehema anasema wanawake wanaofanya kazi kwenye sekta ya madini mara nyingi wanajikuta wakiishiwa mitaji.
SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni
“Maana zile kazi wakati mwingine ni hamsini kwa hamsini. Hamsini kupata na hamsini kukosa. Wakati mwingine unaweza kufanya kazi watu wakakudhulumu unajikuta umepoteza muda wako.”
Tafiti zinaonesha kuwa wanawake ni asilimia 25 tu ya nguvu kazi inayojishugulisha kwenye sekta ya uziduaji kwa namna moja au nyingine.
Unyanyasaji wa kijinsia kwenye sekta ya madini
Unyanyasaji kwenye maeneo ya migodi umekuwa ukiripotiwa. Mfano mwanamke aliyefahamika kwa jina la mjomba Hussein [ Pili Hussein] alilazimika kujifanya mwanaume ili kuepukana na unayanyasaji wa kijinsia unaofanyika kwenye migodi alipoenda kuchimba madini.
Pili Hussein ni mwanamke wa kwanza kuingia ndani ya mgodi wa Tanzanite inayotajwa kuwa mirefu sana. Kipindi hicho Sheria za madini zilikuwa haziruhusu wanawake kwenda chini ya migodi. Sababu kubwa kulikuwa na kesi nyingi zinazowatokea wanawake ikiwemo kubakwa.
”Wanawake wahakuruhusiwa kwenye maeneo ya migodi hiyo, nikajitosa kama mwanaume shupavu na mwenye nguvu. Nilichukua suruali ndefu na kuzikata zikawa kama kaputula ili kufanana na mwanamume Hivyo ndivyo nilivyofanya.” alinukuliwa Pili katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari.
Naye Mkurugenzi wa Women in Mining Operatation, Mhandisi Lightness Salema ambaye anafanya kazi ya uongezaji thamani wa madini ya vito anasema kwamba, wanawake kwenye migodi wamekuwa wakipitia changamoto kubwa ukilinganisha na wanaume.
SOMA ZAIDI: Sekta Isiyo Rasmi Yadaiwa Kutokuwa Rafiki Kwa Wanawake wa Kitanzania
Mara kadhaa, ameshuhudia wanawake wakienda na watoto kwenye migodi. Hugonga mawe kwa mikono, hufanya uchenjuaji kwa mikono. Hufanya hivyo kwa kuwa hawajapata vifaa vya kisasa kwa ajili ya uchimbaji.
“Wao asubuhi wanaamka tu kwenda kwenye migodi anafanya kile anachokikuta anapata faida ndogo sana,” anasema Lightness alipoongea na The Chanzo Novemba 23,2023.
“ Wengi unakuta kwa siku wanaingiza shilingi elfu mbili au tano na kuendelea lakini ametokwa jasho kubwa sana.”
Lightness anasema wapo wanawake wanaolazimishwa kufanya ngono zembe wakiwa migodini. Yote hayo yanatokana na kukosa maarifa ya kitu ambacho wanakitafuta kwenye sekta ya madini.
“Kuna maeneo mengine ya migodi wanawake hawaruhusiwi kabisa kuingia. Wanaamini mwanamke akishuka kwenye madini atasababisha madini kupotea. Yaani ni kama nuksi.”
Asasi za Kiraia zinavyopambana kumwinua mwanamke sekta ya uziduaji
Anasema shida iliyopo ni kwamba hakujatengenezwa mpango mkakati wa kitaifa wa kumkomboa mwanamke kwenye sekta ya madini. Kiasi ya kwamba kila mtu anaruka kwenye kona yake.
Hali hiyo ilimfanya aanzishe Chama cha Wanawake Wachimbaji wa Madini na Uongozeji Thamani. Lengo likiwa ni kumuinua mwanammke, kubadilika kifikra na kuwa na uwezo wa kuzalisha na kupata faida kubwa kupitia madini na kutoa huduma kwa namna tofuati.
SOMA ZAIDI: Fatma Taufiq: Wanawake Tunahitaji Ukombozi wa Kiuchumi
“ [Lakini pia] Kumsaidia kupata elimu ya uchimbaji. Elimu ya kuongeza thamani na jinsi ya kupanga bei, kubuni miradi mbalimblai tofuati na madini kuweza kujipatia kipato.”
Akiongea kwenye Jukwaa la Uziduaji mwaka huu, Katibu Mtendaji taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na kuendeleza uchimbaji mdogo Tanzania (FADev), Mhandisi Theonistina Mwasha amesema wamekuwa wakiwajengea uwezo wanawake wa kujiamini na kujitambua. Kwamba wapo katika jamii ya namna gani, na jamii inafikiria nini juu yao.
katika kuwajengea uwezo, waliona kwamba kwa mtu mmoja mmoja kunaweza kuwa na hofu, wakaona vikundi vianzishwe ili kuwaondoa kwenye kufanya kazi mmoja mmoja.
“Unajua mwanamke ukimkuta kwenye maeneo ya uchimbaji mdogo, wale wa mwanzoni hawakwenda kufanya faida,” alisema Mwasha .“ [Wanawake] wamekwenda kuhakikisha watoto wao wamepata chakula. Ni maisha halisi kwa wanawake wengi huko vijijini.”
SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Ajenda Kuu ya Wakulima Wadogo Wanawake Barani Afrika
Wanawajengea msingi wa kuweza kutoka hapo walipo, na kutambua kuwa wanaweza kufanya kazi hiyo na wakapata faida.
“ Baada ya hapo ikaonekana ni muhimu waweze kupata mafunzo na pia kuongezewe ujuzi. Wengi walio kwenye jamii ya uchimbaji mdogo [hasa vijijini] walikuwa wanajiona duni, wanajidharau.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma, unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com