Chama cha ACT-Wazalendo, mbia na mshiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, hivi karibuni kimetishia kujitoa kwenye Serikali hiyo.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema chama chao, baada ya kufanya tafakuri ya kina kuhusu mwenendo wa SUK, kimeonyesha kutoridhika na mwenendo huo na kuweka bayana nia yake ya kujitoa.
Hii siyo mara ya kwanza kwa ACT-Wazalendo kuonyesha ghadhabu juu ya mwenendo wa SUK. Licha ya kero zilitokana na uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo wengi waliwaonya ACT-Wazalendo kutoingia katika SUK, chama hicho kiliafikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) masuala matatu kama masharti ya wao kujiunga na Serikali hiyo.
Mambo hayo yalikua ni pamoja na kuachiwa kwa wafungwa na wanachama wa ACT-Wazalendo waliokamatwa wakati wa uchaguzi; kuundwa kwa tume yenye hadhi ya kijaji kuchunguza maovu ya uchaguzi; na mwisho marekebisho ya kimfumo kwenye uendeshaji wa uchaguzi.
Ikimbukwe kwamba kati ya mwaka 2016 na 2020 Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kilikua mbia wa kwanza kwenye SUK 2010, kilikataa kujiunga na Serikali baada ya kususia uchaguzi wa marudio.
Nimetathmini siasa za maridhiano Zanzibar na kufanya utafiti kuhusu mifumo ya demokrasia shirikishi ambayo inatumika katika mataifa yenye migawanyiko mikubwa kwenye masuala kama ukabila, dini, rangi ama historia.
SOMA ZAIDI: Mustakabali wa Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar
Mfumo wa demokrasia shirikishi unaazimia kutatua historia za chuki na migawanyiko kupitia mfumo wa kugawana madaraka. Mara nyingi demokrasia shirikishi hutekelezwa kupitia Serikali za Umoja wa Kitaifa, Serikali za Mseto, au ugavi wa madaraka kisawia.
Makubaliano haya yanaweza kufanyika kupitia maelewano ya kimaridhiano na wakati mwingine maelewano yanawekwa katika sheria na Katiba za nchi. Kwa Zanzibar, maelewano haya yaliridhiwa na mabadiliko ya kikatiba mwaka 2010 baada ya kura ya maoni.
Tathmini yangu ya kiutafiti iliimarisha tafiti nyingi kuhusu mustakabali ya serikali za umoja wa kitaifa duniani – kwamba zina changamoto za uendelevu. Hapa nitaainisha sababu nne za kwa nini SUK Zanzibar imefeli na kwa nini ni wakati wa kutafakari mbinu mbadala za ushiriki wa upinzani katika Serikali.
Moja, miongoni mwa tafiti zangu imebaini kwamba tatizo kubwa katika serikali za umoja wa kitaifa ni kushindwa kujikita katika misingi ya jamii ya walio wengi. Kama ilivyokua kwa mataifa ambayo yamejaribu demokrasia shirikishi kama vile Kenya, Zimbabwe, Ivory Coast na kadhalika, SUK ziliundwa kwa maridhiano ya makada wa juu, au elites kwa kimombo.
Vilevile kwa Zanzibar, SUK ilijikita katika mgawanyo wa madaraka na siyo mgawanyo wa mamlaka. Hata katika SUK ya sasa ambayo ina mawaziri wawili – Nassor Ahmed Mazrui (Afya) na Omar Said Shabaan (Biashara ya Maendeleo ya Viwanda) kutoka ACT-Wazalendo ni dhahiri waliteuliwa kukidhi takwa la kikatiba na sio mgawanyo wa mamlaka.
SOMA ZAIDI: Je, Matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Yanakinzana na Yale ya Demokrasia ya Vyama Vingi?
Ukitizama nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ambayo kikatiba ni nafasi ya pili mara baada wa Rais wa Zanzibar, utaona haina mamlaka hata kidogo. Makamu wa Pili wa Rais, ambaye kikatiba anatoka katika chama kilichoshinda uchaguzi, anaoneka ana mamlaka zaidi ya Makamu wa Kwanza. Hii ilidhihirika wazi katika kipindi cha kwanza cha SUK (2010-2015) na inaendelea mpaka hivi sasa.
Mbili, moja ya makubaliano baina ya ACT-Wazalendo na CCM baada ya uchaguzi wa 2020 ilikua ni kuleta marekebisho kwenye mfumo wa uchaguzi, kutathmini historia ya dhulma pamoja na fidia za waathirika wa uchaguzi. Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, aliahidi atatekeleza madai haya ya ACT-Wazalendo.
Suala la tathmini ya historia ya dhulma na ukosefu wa haki lilijadiliwa sana na watu ambao wanafahamu umuhimu wake katika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa. ACT-Wazalendo waliamini kwamba CCM watabadilika na kuyaridhia madai yao. Ukweli ni kwamba CCM wasingethubutu kuyaangazia madai ya dhulma za kihistoria.
Tatu, Serikali za umoja wa kitaifa mara nyingi hudhoofisha msingi wa uwajibikaji wa viongozi wa Serikali kwa sababu hakuna upinzani. Ubia kati ya Serikali na upinzani unapunguza kukemewa kwa maovu ya Serikali kwa njia ya kibunge.
Kati ya 2010-2015, Ismail Jussa pamoja na baadhi ya viongozi wa CUF walibaki bila nyadhifa serikalini na kubaki kama back benchers – dhana inayotokana na mfumo wa kibunge nchini Uingereza ambayo inamaanisha wabunge, ama wawakilishi, wenye uhuru wa kuzungumza bila hofu ya kuwajibishwa na vyama vyao.
SOMA ZAIDI: Kikosi Kazi cha Mwinyi Chataka Mamlaka Zaidi kwa Z’bar Ndani ya Muungano
Akina Jussa waliweza kubaki kama sauti ya ukosoaji kwenye SUK. Ila kwa sasa uwajibishwaji wa Serikali umepungua kwenye SUK. Ila kusema ukweli ACT-Wazalendo hawana uwakilishi wa nguvu kama ilivyokua CUF kwenye SUK ya kwanza.
Nne, mhimili wa maridhiano Zanzibar uliasisiwa na dhamira ya kumaliza miongo ya chuki baina ya Wazanzibari. Mchakato wa majadiliano na kujenga maridhiano ulihitimishwa kwa kushikana mkono baina ya Rais Amani Karume na Maalim Seif Shariff Hamad Novemba 5, 2009.
Japo kulikua na kamati ya maridhiano ambayo ilifanya kazi nyuma ya pazia, maudhui ya maridhiano yalibebwa na Karume na Maalim Seif. Baada ya Maalim Seif kufariki 2021, maridhiano yameyumba. Maalim Seif pamoja na Karume walikua ishara ya maridhiano.
Bila shaka wapo wale ambao bado wanaamini katika maridhiano Zanzibar ila mihimili imekosekana. Na kama nilivyosema hapo juu, SUK imeshindwa kusambaza maridhiano kwenye ngazi ya kijamii.
Tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, SUK itaendelea kudhoofika na dhana ya maridhiano Zanzibar inaweza ikafa. Ili kuimarisha umoja na mshikamano, ni lazima kuwepo na mjadala wa mustakali wa maridhiano na mageuzi ya kimfumo wa uchaguzi Zanzibar.
Nicodemus Minde ni mtafiti wa masuala ya siasa za muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia nminde96@gmail.com au kupitia X @decolanga. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
2 responses
Makala nzuri Daktari
Mtazamo wako unaeleweka na madhaifu uliyoainisha yako sahihi kabisa