Mwezi Februari mwaka huu wa 2024 tumeshuhudia tena mbio za matrathoni za Kilimanjaro ambazo hufanyika kipindi hiki kila mwaka, zikijumuisha wanariadha kutoka kote nchini na nje, hasa kutoka Kenya.
Mbio hizi ni za muda mrefu kulinganisha na mbio nyingine za marathoni ambazo sasa ni utitiri unaotumiwa na mashirika kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao kama vile biashara, hisani na kuelimisha wananchi kuhusu baadhi ya matatizo yaliyoko kwenye jamii, kama vile magonjwa na vitu vinginevyo.
Huwezi kuyalaumu haya mashirika, au taasisi, kwa kuona mbio za marathoni ndiyo njia nzuri, au rahisi, ya kufanikisha malengo yao, kwa sababu zimeona jamii inahamasika huko.
Karibu kila mwezi, kwa mwaka uliopita wa 2023, tulishuhudia mbio za marathoni zikiendeshwa kwa umahiri mkubwa na wa hali ya juu ambao hata Chama cha Riadha (AT) chenyewe hakiwezi kufikia viwango hivyo.
Mbio kama zile zinazoandaliwa na benki za NMB na CRDB zimekuwa za kiwango cha juu sana, zikiendeshwa kwa weledi na usasa, kiasi kwamba kama zingeshirikisha wanariadha mahiri, na kama zimesajiliwa vizuri, rekodi ya dunia ingeweza kuvunjwa hapa, iwe Kilimanjaro ambako mbio hizo ni za muda mrefu, Dar es salaam, ambako ndiko kuna utitiri, au Dodoma na Mbeya.
SOMA ZAIDI: Mpira wa Miguu Sasa ni Sekta Muhimu, Uratibiwe
Lakini hatuoni makubwa kwa upande wa wahusika wenyewe wa riadha, zaidi ya viongozi na maofisa wake kuhusishwa kwa kiwango kikubwa katika maandalizi.
Sidhani kama AT imekaa chini na kutafakari jinsi ya kujinufaisha na mbio hizo kwa kuongea na waandaaji na kuwaambia mapendekezo yao ya jinsi ya kufanikisha malengo ya waandaaji na mipango ya maendeleo ya Chama cha Riadha.
Uratibu
Kwa mfano, mbio nyingi zinazofanyika Dar es Salaam huanzia na kuishia Uwanja wa Farasi, Oysterbay ambako AT haiwezi kufanya kitu kingine zaidi ya kuratibu ushiriki wa wanariadha.
Uwanja wa Farasi ni mzuri sana kwa shughuli za promosheni za waandaaji na wadau wake na pengine ni sehemu ambayo unaweza kupata washiriki wengi wa mbio za kujifurahisha, hasa wanasiasa, wakurugenzi watendaji wa mashirika na kampuni, pamoja na wale ndugu zetu maarufu; wasanii na watu wa mitandaoni.
Bahati mbaya sana, pamoja na kwamba hili ni taifa lenye wendawazimu wa soka, wachezaji si watu maarufu kwenye shughuli kama hizo!
SOMA ZAIDI: Baraza la Michezo Lifikirie Kuandaa Olimpiki Yetu Kwanza
Kwa hiyo, Uwanja wa Farasi utawezesha washiriki kufanya mazoezi ya kupasha joto mwili, kuanza na kumaliza mbio, lakini kikubwa ni vyakula na vinywaji ambavyo huvuta maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.
Kadiri washiriki wa mbio za kujifurahisha wanavyokuwa wengi, ndivyo waandaaji wanavyoona malengo yao yamefanikiwa, huku wale wanariadha, hasa wa mbio kama za kilomita 10 na 21, wakiwa wachache na ambao muda wao haujawahi kustua anga za ridha, si tu duniani bali hata Afrika.
Hayo ni mambo yanayokuja taratibu lakini kama wahusika wenyewe wa riadha wataiona fursa hii na kuitumia vizuri.
Mashindano hayafanyiki
Ni miaka mingi sasa AT wanashindwa kuandaa mashindano makubwa ya riadha ambayo huhusisha michezo mingi kama mbio fupi, kuruka juu na chini, kurusha mkuki, kurusha tufe, kurusha kisahani, mbio za masafa ya kati na marathoni zenyewe ambazo hufanyika siku ya mwisho ya mashindano.
Ni dhahiri kuwa hiyo michezo mingine haiwezi kufanyika kwenye Uwanja wa Farasi au sehemu nyingine Tanzania ambako mbio za marathoni huanzia na kuishia. Sehemu hizo hazina miundombinu inayoweza kutumiwa kwa michezo kama kurusha tufe na mkuki, au mbio fupi na za kuruka vihunzi.
SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Idhibiti Uahirishaji Mechi Kiholela, Kuhama Viwanja
Bahati mbaya ni kwamba hadi sasa viwanja vyenye hadhi ya kutumika kwa ajili ya michezo yote ya riadha ni Uwanja wa Benjamin Mkapa na Amaan wa Zanzibar, vingine havijawekwa vizuri kwenye sehemu za kukimbilia na hivyo si rafiki kwa wanariadha.
Uwanja wa Uhuru ndiyo kabisa haufai kwa michezo mingine ya riadha kwa sababu sehemu ya kukimbilia imewekwa lami.
Hapa kunahitajika uwezo mkubwa wa kujenga hoja utakaowawezesha waandaaji hawa kuunganisha matukio yao na ya AT.
Wanahitaji kuwashawishiwa kubadili sehemu ya kumalizia mbio zao za marathoni na kutumbukiza fedha katika michezo mingine ili lengo lao litangazwe mfululizo kwa muda wa wiki nzima ya mashindano, likiambatana na vitu halisi, yaani michezo yenyewe tofauti na matangazo matupu ya redioni na kwenye televisheni.
Si kwamba AT itumie kila mbio za marathoni kufanikisha michezo ya taifa, bali iandae mpango mkakati utakaowashawishi viongozi wa mashirika haya, au taasisi, kuona kuna thamani ya kuunganisha shughuli zao na michezo rasmi ya taifa, ambayo kwa kawaida hufanyika katikati ya mwaka kuwezesha wanariadha ambao ni wanafunzi kushiriki wakati wakiwa likizo.
Tunahitaji kuona vijana wengi wakijitokeza kwenye michezo mingine ambayo pengine wana uwezo nayo zaidi, badala ya kuamini kuwa fani zinazoweza kuwatoa ni mpira wa miguu na muziki tu.
Kenya yaonesha njia
Kenya walikuwa wafalme wa mbio ndefu na za masafa ya kati, lakini sasa wamepanua wigo kutokana na chama chao cha riadha kuona mbali na kutekeleza mikakati yake. Januari mwaka huu wa 2024, Chama cha Riadha cha Kenya (KA) kiliandaa mashindano makubwa ya riadha kwenye Uwanja wa Nyayo.
SOMA ZAIDI: Sheria, Kanuni za Uchaguzi TFF Ziangaliwe Sasa
Tofauti na miaka mingine, macho ya wengi yalielekezwa kwenye mbio za mita 200, ambako mshindi wa mbio za mita 100 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola, Ferdinand Omanyala, alipata changamoto kutoka kwa Mark Otieno, hiyo ikionyesha ni mabadiliko makubwa kimtazamo katika riadha nchini Kenya.
Mbali na mashindano hayo, kwa sasa Kenya inapeleka wanariadha wake wa mbio fupi kushiriki mashindano ya dunia katika mchezo wa kupokezana vijiti, kama ilivyokuwa mapema mwezi huu wakati timu ya Kenya iliposhiriki mashindano ya dunia ya mbio za ndani.
Yote hayo ni matokeo ya Chama cha Riadha cha Kenya kuwa na mwendelezo wa uandaaji wa mashindano yake, ambayo huvuta nyota wake wanaotamba duniani katika mbio tofauti.
Huku kwetu Tanzana ni nadra sana wanariadha wetu nyota kama akina Felix Simbu, Magdalena Shauri, Andrew Rhobi, Jacqueline Sakilu na Augustine Paulo kusikia wameingia kutia joto mashindano yetu labda marathoni, na wengine hawawezi kwa kuwa hakuna jukwaa la kushindania.
Kwa hiyo, hawa waandaaji wa mbio za marathoni kwa ajili ya malengo tofauti na mchezo wa riadha, wanaweza kuhamasishwa kuweka juhudi hizo katika mashindano rasmi ya kitaifa.
SOMA ZAIDI: Serikali Itafakari Hili la Mafunzo ya Wachambuzi wa Soka Tanzania
Lakini kwa kuwa ni mashirika yanayoendeshwa kwa taratibu maalum za kitaasisi na yanataka kuona thamani ya fedha katika kila wanachofanya, hasa yanapotoa fedha, viongozi wa AT hawana budi kukuna vichwa na kuangalia watawezaje kuweka thamani kwenye mashindano yao ili hawa wakubwa waunganishe mikakati yao na mashindano rasmi ya kitaifa ili nao washiriki kuendeleza michezo.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.