The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Teuzi za Watu Wasio Waadilifu Zinawapa Motisha Viongozi Kutumia Vibaya Ofisi za Umma

Teuzi hizo zinatoa taswira ya ubovu wa mifumo yetu ya kisiasa – na uadilifu kutokea juu kwenda chini.

subscribe to our newsletter!

Imekuwa siyo ajabu hapa nchini kwetu Tanzania kusikia mtu anayetuhumiwa kwa uhalifu ameteuliwa kushika ofisi ya umma. Tumeona teuzi nyingi ambazo zinabishaniwa, kwamba, mtu huyu ama yule, kwa historia yake, hakufaa kushika ofisi ya umma, lakini mamlaka za uteuzi huwateua licha ya uwepo wa ukinzani mkali kutoka kwa wananchi.

Suala hili limejirudia sana na limenisukuma kurejea ufahamu wangu kuhusu maadili ya viongozi wa umma. Kuna dhana kwamba maadili ni suala la mtazamo tu. Lakini ukweli ni kwamba tuna sheria na miongozo hapa nchini kwetu zinazohusu maadili inayoelekeza kiwango fulani cha maadili kwa viongozi wa umma.

Lakini ‘kiongozi wa umma’ ni nani haswa? Viongozi wa umma wametajwa katika kifungu cha nne cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, sura ya 398. Kwa mfano, Rais wa Tanzania na Zanzibar, Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu wao, Spika wa Bunge na Naibu wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, na Wabunge ni viongozi wa umma.

Pia, wamo Majaji, Mahakimu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mabalozi, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala. Kuna Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Katibu wa Bunge, Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Polisi na Makamanda wa Polisi Mikoa, na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa.

Kwenye orodha pia wapo Mkuu wa Usalama wa Taifa, Mkuu wa Magereza, Mkuu wa TAKUKURU, Mameya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Tume zote wenye ajira ya kudumu, Wakuu wa Mashirika ya Umma, Makamishna wa Kodi, Makamishna na Wakurugenzi katika Wizara.

SOMA ZAIDI: Tusiruhusu Uholela wa Matumizi ya Mamlaka ya Kipolisi

Watu wote wenye nyadhifa zilizotajwa hapo juu ni viongozi wa umma kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, wanalazimika kukidhi na kukiishi kiwango fulani cha maadili katika utekelezaji wa majukumu yao. Hiyo ni kabla, wakati wa, na baada ya kushika mamlaka katika ofisi ya umma.

Maadili ya umma

Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inampa Rais jukumu la kusimamia mageuzi katika maadili ya umma. Lengo ni kujenga uadilifu na imani ya umma kwa viongozi na maamuzi yao. Rais anatajwa kwa sababu ni mkuu wa utumishi wa umma. Ana nafasi ya kuteua, kufuta kazi, na kusikiliza rufaa za maadili ya viongozi, na watumishi, wa umma.

Kwa hiyo, Rais hatamteua mtu katika nafasi ambayo ana maslahi binafsi; atazingatia uzoefu na utaalamu. Rais atabainisha kanuni za maadili ili kuzuia mgongano wa kimaslahi kwa viongozi wa umma, kabla, wakati na baada ya kushika ofisi ya umma.

Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kifungu cha sita, imetaja viashiria vya maadili, ikiwa ni pamoja na kuwa mkweli, kuwa na kiasi, huruma na kujihoji. Kiongozi wa umma anatarajiwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha maadili, uadilifu na imani ya umma anaouongoza. Anatakiwa kuwa na busara na aepuke upendeleo katika maamuzi.

Kiutendaji, viongozi wa umma wanatakiwa kuwa wazi kuhojiwa na umma kuhusu matendo yao, kwa mfano, kupitia wanahabari. Viongozi wanatarajiwa kufanya kazi na maamuzi kwa kuzingatia sheria na maslahi ya umma.

SOMA ZAIDI: Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki

Viongozi wa kisiasa wanatakiwa kutangaza mali zao kama ilivyoelekezwa katika sheria, na kuepuka kutumia nafasi na upendeleo wao kwa maslahi binafsi.

Teuzi zinazobishaniwa

Kuna mengi ya kuandika kuhusu maadili. Lakini nataka kujiuliza, kwa nini, licha ya kuwa na sheria nzuri, angalau katika maandishi, bado tuna visa vya viongozi ambao teuzi zao zinabishaniwa sana?

Utaafikiana na mimi kwamba kumekuwa na teuzi kadhaa ambazo zimezua mjadala; zile zilizozua maswali kuhusu uhalali wa ‘mteuliwa’ kushika ofisi ya umma kwa kukosa uadilifu ama historia ya nyuma.

Kwa mfano, uteuzi wa watu wenye tuhuma za uhalifu, au matumizi mabaya ya ofisi. Kwa kiongozi wa umma, tuhuma pekee inatosha kukunyima fursa ya kushika ofisi fulani, hususani kama unalindwa, ama umewekewa, kinga ya kutowajibishwa.

Tumeona watu kama Paul Makonda, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ambaye ana tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi. Mathalani, mnamo Machi 18, 2017, alidaiwa kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds Media. 

SOMA ZAIDI: Mahakama Imdhibiti DPP Kuondokana na Kero ya Futa Kesi, Kamata, Shitaki Upya

Makonda alifanya tukio la uvamizi akiwa na watu wenye silaha ambao hawakuvaa sare za jeshi lolote, picha za CCTV kuhusu tukio hilo zinaonesha. Inadaiwa Makonda alikwenda kwenye kitu hicho cha habari mashuhuri nchini kushinikiza maudhui anayoyapenda yachapishwe na kurushwa hewani.

Makonda alifaa kushitakiwa. Lakini Serikali ya wakati huo ilimlinda. Serikali mpya imemlinda na sasa imemzawadia Ukuu wa Mkoa wa Arusha. Rais ameona kwamba watu wa Arusha, na heshima zao, wanastahili kiongozi mwenye makandokando aina ya Makonda. Hii inaudhi sana!

Makonda hakabiliwi na tuhuma ya uvamizi pekee. Anatuhumiwa pia kwa kutumia vibaya ofisi ya umma na kujilimbikizia mali kwa dhuluma. Serikali ya Marekani imemuwekea zuio la kuingia nchini humo kufuatia tuhuma walizozidhibitisha za kudhulumu uhai wa binadamu, pamoja na uhalifu mwingine.

Kuna kumbukumbu chungu nzima za Makonda ama akiwafokea watu wa chini yake, akitoa lugha za matusi, au makatazo yasiyoungwa mkono na sheria yoyote nchini Tanzania.

Kuna mfano mwingine wa Biswalo Mganga ambaye, akiwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), alitumia vibaya ofisi yake. Suala hata Rais Samia Suluhu Hassan alilitaja akirejea uendeshwaji holela wa zoezi la plea bargain kwa makosa ya jinai. Katika zoezi hilo, Mganga alikusanya pesa kiholela, na nyingine, kwa mujibu wa Rais, zimeonekana katika akaunti binafsi za benki huko nchini China.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?

Mganga anadaiwa kutumia vibaya ofisi kwa kufungua kesi nyingi za jinai bila kuzingatia maslahi ya umma. Licha ya kuwapotezea muda na kuwatesa watuhumiwa kwa kuwatupa jela, kuna masuala ya rushwa na uporaji wa mali zao. Rushwa ilitumika kama nyenzo ya watu kurejesha uhuru wao.

Kwenye ripoti yake maalumu kuhusiana na suala hilo, iliyotolewa Machi 29, 2023, CGA alipendekeza Mganga achunguzwe kwa matumizi mabaya ya ofisi. Hata hivyo, Rais, badala ya kumchunguza Mganga, alichagua kumzawadia heshima na hadhi ya Jaji wa Mahakama Kuu!

Na sasa Biswalo, licha ya tuhuma zinazomnyima sifa za kuwa kiongozi wa umma, anakaa katika usukani wa kutoa haki. Suala hili halileti maana kabisa na halikufaa kutokea.

Upendeleo

Kuna visa vya kutosha vya watu wanaoteuliwa katika ofisi za umma ambao hawakutakiwa hata kufikiriwa kushika nafasi hizo maana teuzi za viongozi inaaminika zinafuata utaratibu fulani. Zilitakiwa pia kufanyika kwa uwazi na ushindani – bahati mbaya hatuna utaratibu huu hapa nchini kwetu.

Kwa kutazama uteuzi wa Makonda na Mganga, utaona teuzi zinafanyika kwa upendeleo bila kujali sifa za kushika ofisi za umma. 

SOMA ZAIDI: Profesa Mussa Assad: Ufisadi Umeshamiri Kwa Sababu Mafisadi Hawaadhibiwi

Kwa upande mwingine, teuzi za watu wasio waadilifu zinawapa motisha viongozi kutumia vibaya ofisi za umma bila kuhofia uwajibikaji, na zinatoa taswira ya ubovu wa mifumo yetu ya kisiasa – na uadilifu kutokea juu kwenda chini.

Rais wa Tanzania hawezi kukwepa kuhusishwa na teuzi mbovu. Labda kwa kuwa tumekuwa na historia ya kuongozwa na watu ambao hawajachaguliwa, ama viongozi ambao mamlaka yao ya kisiasa hayana uhalali wa kisiasa, na kwa hiyo hawaoni sababu ya kufuata sheria hata kidogo, isipokuwa pale ambapo zinawanufaisha wao binafsi.

Kwa kuwa maisha ya kisiasa ni mafupi, viongozi wengi wa umma hutumia rasilimali za umma kujitajirisha kadri wawezavyo. Ushahidi wa haya unawekwa hadharani kila mwaka katika ripoti za CAG.

Nilipanga kutafakari maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa sheria. Lakini inaonekana kuna mengi ya kujitazamisha, ikiwemo wajibu wetu kama wananchi kwenye kusimamia utekelezaji wa sheria hizo. 

Nitaendelea!

Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 responses

  1. Kwa hakika hili ni suala linalopaswa kutazamwa kwa umakini sana. Kabla ya mtu kuteuliwa kwenye wadhifa wowote wa serikali hata kwa maofisa wa ngazi za chini, na hususan kwenye idara zinazohusiana na mambo nyeti (Mambo ya ndani, Mambo ya Nje, Mahakama, WIzara ya Fedha na bila shaka TRA, Vyombo vya habari nk) ilikuwa lazima afanyiwe uchunguzi (vetting) kwa kipindi kisichopungua mwaka. Kabla, au kutokana na matokeo hasi ya uchunguzi huo, ofisa aliyekuwa tayari ameajiriwa hakuruhusiwa kushughulikia nyaraka za siri, na kama matokeo ni ya kuonyesha kuwa hakuwa muadilifu, basi, hakuajiriwa au alihamishiwa mahali pasiposhughulikia masuala nyeti. Na kama alishaachishwa kazi hakuweza kuajiriwa tena katika ofisi za serikali. Hivi leo ni kama suala la uadilifu halina nafasi tena katika kupima kufaa au kutofaa kwa muombaji wa kazi au mteuliwa kwenye ajira ya serikali – Wizara, Idara au Shirika. Ndiyo sababu wezi wanaitwa, “wanaume” na waadilifu wanaitwa “wajinga”. Kama mtu anaajiriwa ikifahamika wazi kuwa si muadilifu kwa njia yoyote, basi yule anayemteua angeweza kuhusishwa na makosa ya mteuliwa – kama kweli suala la uadilifu lingekuwa sehemu ya utamaduni wa utendaji serikalini au popote pale ambapo maslahi ya wananchi yanaweza kuaathirika. Hili nalo lingefaa kuwekwa kwenye katiba mpya.

    1. Nakubaliana na wewe kabisa. Kuna haja ya matengenezo makubwa kifalsafa, kijamii na kiutendaji. Visa vya watu(mishi) kukosa uadilifu ni vingi kuliko matokeo chanya ya utumishi. Tunahitaji kuandika historia mpya katika uga wa uwajibikaji.

      Asante kwa kusoma

  2. Niccolo Machiavelli kwenye Kitabu chake cha The Prince anasema kwamba Politics has nothing to do with Morals na akaendelea kusema kwamba “the Means will determine the Ends”. May be kwenye Republics unlike Monarch, accountability ingekuwa na nguvu kwa sababu Powers are from the People and those in powers must be accountable to the Voters! Pengine ni muhimu zaidi kuimarisha taaaisi za Uwajibikaji kuliko kuwa na Strong men” by paraphrasing Baraka Obama – Former US 🇺🇲 President

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts