The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Laiti Kama Watawala Wetu Wangekuwa na Muda wa Kusoma Kazi za Fasihi

Isingekuwa rahisi kwao kufanya makosa wanayofanya, na wangefaidika sana na mafunzo yanayohusu uadilifu na uwajibikaji.

subscribe to our newsletter!

Kwa kuwa fasihi ni zao la lugha, bila ya shaka hufuatana na kuchagizana na mabadiliko ya mwanadamu kifikra na kimitazamo katika kukabili mabadiliko ya wakati na mazingira yake. 

Hivyo, fasihi imekuwa chombo kinachoendelea kukata mawimbi ya safari za jamii na mataifa yao kuelekea kwenye bandari za mifumo bora ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Inaelezwa, na ndivyo ilivyo, kuwa aina za mifumo ya maisha inayofuatwa na wanajamii, huamuliwa na siasa ya jamii hiyo. 

Sera, mipango, bajeti na maamuzi ya miradi ya maendeleo huchakatwa kupitia mfumo wa kisiasa kabla ya kuletwa kwa wananchi kwa ajili ya utekelezaji. Hivyo, mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu hutawaliwa na misingi ya kisiasa inayoongoza jamii inayohusika.

Si jambo la kushangaza kuona nchi inabadili na kuimarisha mifumo yake ya kiutawala, kiulinzi, kintelijensia, kidiplomasia, kisheria na jumla ya mifumo inayohusiana na uendeshaji wa siasa, kutokana na mafunzo yanayojadiliwa katika fasihi mbalimbali ulimwenguni. 

Kwa minajili hii ni wazi kwamba, nyimbo, filamu, riwaya, mashairi, tamthiliya na tanzu nyingine za kifasihi zinaweza kutumiwa katika kuimarisha siasa za nchi.

Fasihi na siasa

Fasihi kama taaluma na sanaa inayolenga kusawiri maisha ya mwanadamu na mustakbali wake, huchukua nafasi kubwa katika kutufunza kuhusu aina mbalimbali za uongozi na athari zake kwa mustawa wa jamii husika.

Tukiitupia macho nukuu hii kutoka katika riwaya ya Kufikirika, tunamuona Shaaban Robert akitufahamisha kuhusu uongozi bora. Uongozi unaolenga kivitendo kuboresha maisha ya wananchi kupitia sera na mipango madhubuti. 

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru wa Mwanafasihi, Fasihi Haiwezi Kuwa Chombo cha Ukombozi wa Umma

Hapa mwandishi anatueleza umuhimu wa Serikali imara, elimu kwa raia na kuwatumia kulingana na taaluma zao:

“Serikali ya Kufikirika ililazimisha sana ustadi wa watu wake katika kazi zake. Kwa hivi Wafikirika waliidilika katika njia nyingi sana. Nchi ilikuwa ina serikali imara, waongozi wa ubongo mzuri, mahakimu wa haki, waandishi bora, wanachuoni mufti, wasafiri na wagunduzi wavumilivu na wajasiri, mabaharia wa moyo mkuu na wenye kuthubutu na askari wa miili migumu, mishipa minene, kano 33 kavu zenye nguvu na shabaha nzuri …” (ukurasa 17).

Mafunzo haya adhimu na yaliyojaa hekima yanaakisi kwa kiwango gani katika siasa za jamii zetu? Tunashuhudia Serikali nyingi za Kiafrika zikilalamikiwa kwa ukosefu wa ajira na mikakati dhaifu ya kuinua maisha ya vijana. 

Kabla ya machozi ya kilio hiki kukauka, tunagundua wimbi la wasiyo na uwezo kupewa nafasi kwa misingi ya udugu, urafiki na mirengo ya kisiasa, huku kundi kubwa la wenye uwezo na umahiri katika utendaji, likizagaa mitaani bila ya kupatiwa nafasi ya kutumia uwezo na maarifa yao kwa maslahi ya taifa.

Shairi la Chunguzeni Walombele, katika diwani ya Mashairi ya Chekacheka, linatubainishia uongozi mbaya, uongozi unaozingatia zaidi maslahi ya wachache kuliko ya umma. Mshairi anasema katika beti hizi:

Mipango ingewajali,
haya yasingetupata,
Uroho kuwa awali,
wa mbele kuchotachota,
Kuihodhi yote mali,
yote wakaikamata,
Huu wao ufujaji,
ulozidi ukoloni.

Tazama yao majumba,
wenyewe waita vila,
Havihesabiki vyumba,
hesabu iso jumla,
Chini pia wamechimba,
kwa nguvu ya zetu hela,
Bwawa la kuogelea,
lenye nakshi za kisasa.

(ukurasa 16).

Uongozi wa mabavu, au kiimla, pia unaelezwa katika kazi za fasihi. Shaaban Robart ni mfano mzuri wa waandishi wanaotufundisha madhara ya uongozi wa namna hii katika riwaya yake ya Kusadikika. Anasema:

“Sheria za Wasadikika zilikuwa hazimwamuru mshitakiwa kujitetea juu ya ushahidi wa mshitaki. Aghalabu mashtaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo. Labda hii ndiyo sababu ya nchi yao kuitwa kusadikika. Kama mashtaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu, nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka kuwa salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi hii.”

SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

Baadhi ya kazi za fasihi hubainisha pia uongozi unaowapa hadhi na nafasi wasiyostahiki, kwa sababu ya uhusiano wao na watawala. Hapa nalikumbuka shairi la Kuna Nini Huko Ndani katika diwani ya Mashairi ya Chekacheka. Mshairi analalama:

Tumewaletea kuni, maharage hata unga,
Halafu mnatuhini, marafikizo mwahonga,
Mwataka tulale chini, mtutese mkiringa,
Hizo kofia nyeupe, tumewaazima sisi?

Fasihi huibua na kujadili matatizo kadhaa yanayotokana na watawala wa kisiasa. Miongoni mwayo ni pamoja na rushwa, uonevu, ukandamizaji, ulaghai, ubadhirifu wa mali ya umma, ufisadi, usaliti, ubinafsi na kadhalika. Hizi ni miongoni mwa kazi za fasihi ya Kiswahili zinazojadli dhamira hizo:

Kusadikika, Kufikirika (Shaaban Robert); Joka la Mdimu (A. J. Safari); Kivuli Kinaishi (Said Ahmed); Morani (E. Mbogo); Wasakatonge (M. S. Khatib); Mashairi ya Chekacheka (T. A. Mvungi); nyimbo kama Nipeni Maua Yangu (Roma); Sauti ya Watu, Amkeni (Nay wa Mitego).

Jambo la kusikitisha ni pale mifumo ya kisiasa inapojaribu kuwatia vikwazoni wasanii wa namna hii, na wakati mwingine kuzifungia kazi zao. Wanafasihi wanaoibua maovu ya kiutawala huhesabiwa kama maadui, ilihali huitumia fasihi kuwafunua macho watawala ili warekebishe mifumo na kutenda haki kwa manufaa na mustakbali wa taifa zima.

Mifumo ya siasa huwapa nafasi wanasiasa katika uandaaji na utungaji wa sharia. Lakini mara nyingi hushuhudiwa viashiria vya uatawala usiozingatia sharia. Kesi ya Karama katika Kusadikika inanikumbusha nukuu muhimu sana inayotanabahisha kuwa utii wa sheria ni muhimu katika kudhibiti haki na mnaadili katika jamii. 

Kalamu ya Shaaban Robert katika riwaya hiyo inamwaga wino mzito ukiwakilisha umuhimu wa viongozi kuzingatia sheria katika kusimamia haki za wanaowaongoza. Hapa, kupitia sauti ya Mfalme, anatueleza juu ya haki ya kusikilizwa kwa mshatakiwa:

“Muda huu ukiisha, hukumu inayostahili itatolewa kwa mshitakiwa. Wakati una mabawa kama ndege. Uvumilivu ukitumiwa siku sita ni sawa na saa sita. Kwa kuwa haifai kuonekana kuwa baraza haina saburi, haja ya mshitakiwa ya muda wa kueleza sababu za kuanzisha uanasheria katika nchi hii haina budi kukubaliwa. (ukurasa 10).

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunahitaji Kusoma Vitabu Vingi Zaidi vya Kiswahili?

Katika riwaya yake ya Kufikirika, Shaaban Robert anaeleza baadhi ya manufaa yanayoweza kupatikana katika jamii zinazoongozwa kwa kufuata na kutii sheria. Mwandishi anasema:

“Hapakuwa na mtu aliyeweza kuvunja sheria pasipo kupatilizwa. Wafikirika walihesabu kuvunjwa sheria kuwa si uhalifu mkubwa tu lakini ni dhambi vilevile iliyostahili laana. Sheria zao zilikuwa imara kama zilivyowezekana kufanywa. Zilikuwa si sheria dhaifu au halisi kama uzi wa buibui ambao hukatwa na nzi mkubwa na kunasa nzi mdogo tu. Imara ya sheria hizo ilikuwa mbele ya kila mtu pasipo mapendeleo; mkubwa kwa mdogo, mnguvu kwa mnyonge; na tajiri kwa masikini. Hata mfalme hakuweza kutenda dhara bila ya kulaumiwa na sharia.” (ukurasa 31).

Kutetea haki za wanyonge

Kazi nyingi za fasihi hujadili matatizo, migogoro na mikinzano kadha inayowapata watu wa tabaka la chini, kutokana na unyonyaji, ukandamizaji na usaliti unaofanywa na viongozi wao. Wakulima, wafanyakazi, wachimbaji wa migodini, makuli na wengineo hujadiliwa sana katika kazi za fasihi kwa namana ya kutetea haki zao.

Diwani kama vile Mashairi ya Chekacheka, Wasakatonge, Fungate ya Uhuru na Kimbunga; au riwaya kama Vutan’kuvute, Watoto wa Mama N’tilie na Takadini ni mifano ya kazi za fasihi ya Kiswahili zinazotetea maslahi ya wanyonge katika muktadha wa kisiasa na kiutawala.

Fasihi, kwa kujadili kwake masuala ya kisiasa na uongozi, hutia hamasa katika nyoyo za watu katika kuleta mabadiliko ya kisiasa katika jamii. Ndiyo maana misimamo ya wanafasihi wengi ni ya kimapinduzi hasa katika siasa.

Fasihi ya Kiswahili, kwa mfano, imechangia sana katika kuleta mabadiko kutoka katika ukoloni kwenda kwenye uhuru. Kwa mfano, riwa za Kufikirika, Kusadikika, Vutan’kuvute na kadhalika. 

Zipo fasihi zilizotetea ujamaa, demokrasia, haki, uadilifu na kuchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya kiutawala na kisiasa katika jamii. Chunguza nyimbo za siasa na tenzi za mikutano ya hadhara namna zinavyotia mushawasha na kariha katika nyoyo za wanachama na wanasiasa.

SOMA ZAIDI: Laiti Kama Ningepata Nafasi ya Kumhoji Shaaban Robert

Pamoja na uwezo wa fasihi kubeba dhima ya kisiasa katika miktadha tafauti, bado fasihi ya Kiswahili haijapewa nafasi ya kutosha na wanasiasa na hata jamii nzima. Wanafasihi na kazi zao hutumika sana katika masuala ambayo wanasiasa wenyewe wameyaridhi. 

Pale fasihi inapokwaza maslahi yao, hata ikiwa kwa nia njema ya mabadiliko, mifumo ya kisiasa haisiti kuchukua hatua kandamizi dhidi ya wasanii na kazi zao.

Aidha, kazi nyingi za fasihi zimejiweka kando katika kuibua maovu na misuguano ya kisiasa inayoikabili jamii. Mapenzi, upelelezi, udaku, kusutana, vijembe, ngono na masuala mengine yasiyo na uzito wa kiukombozi, yamechukua nafasi kubwa katika dhima na dhamira za kazi nyingi za fasihi ya Kiswahili kwa sasa.

Hali hii inasababishwa na uhuru hafifu wa wanafasihi, udhamini, kutojiamini kwa baadhi ya wanafasihi, fasihi kuingiliwa na mamlaka za kiutawala, mwelekeo wa udhibiti badala ya uthibiti, tamaa ya kipato, umaarufu wa haraka na nyingine nyingi.

Ipo haja ya kubadilisha mwelekeo kwa wanafsihi na mamlaka zinazosimamia sanaa nchini. Wanafasihi wapewe uhuru stahiki wa kuchangia mawazo yao kupitia kazi zao kwa mintarafu ya kukosoa na kushauri namna bora ya kuimarisha mifumo yetu ya kisiasa ambayo hushikilia kwa kiasi kikubwa dira ya maisha ya jamii na taifa kwa ujumla.

Fasihi ikiachwa ipenye katika mianya inayotoa fursa za ubadhirifu, rushwa, uhujumu uchumi, ufisadi na ulaghai wa kisiasa, naamini itaziba mianya hiyo. Hatimaye itashauri njia bora za kukabiliana na mikwamo na misuguano inayosababishwa na siasa za kidhalimu, kifisadi, chuki na zisizojali maslahi mapana ya jamii.

Fasihi inaweza kuwa tanga madhubuti, ambalo manahodha wakiamua kulipindua, lina uwezo wa kulifikisha jahazi katika bandari ya kisiwa cha ‘Amani ya Kisiasa’ na kutuokoa na gharika ya mkondoni. Ni vyema kutanabahi alfajiri kabla jua halijatusonga mafichoni.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Allah amuongoze zaidi katika kazi yako. Akuzidishie weledi na uthubutu katika kuipeleka jamii kwenye mwangaza

  2. Allah akuongoze zaidi katika kazi yako. Akuzidishie weledi na uthubutu katika kuipeleka jamii kwenye mwangaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *