The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima

Akianza kufahamika kama mshairi kwenye miaka ya 1950 na kufahamika zaidi alipohamia Dar es Salaam miaka ya 1960, Andanenga alifariki Mei 1, 2024, akiwa na umri wa miaka 88.

subscribe to our newsletter!

Ni mara chache sana kwa mtu kukumbuka siku ya kwanza na ya mwisho alizowahi kuzungumza na mtu fulani. Imekuwa hivyo kwangu mimi na mzee wetu, Amir Sudi Andanenga, almaarufu kama Sauti ya Kiza. 

Alizaliwa Kilwa mnamo Oktoba 2, 1936. Alianza kufahamika kama mshairi kwenye miaka ya 1950 na kufahamika zaidi alipohamia Dar es Salaam miaka ya 1960. Andanenga alifariki Mei 1, 2024, akiwa na umri wa miaka 88.

Zawadi kubwa aliyonipa Andanenga ni mazungumzo tuliyoyafanya Novemba 26, 2021 – siku ya kwanza niliyokutana naye. Tulikuwa katika eneo la Nafasi Arts Space, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya tukio lililokuwa limeandaliwa la Nafasi pamoja na Picha Time lililoitwa ‘Poetry and Jazz.’ 

Mimi nilikuwa hapo kufanya mazungumzo mubashara na Profesa Mugyabuso Mulokozi, na rafiki yangu na mshairi Neema Komba alikuwa pale kufanya mazungumzo na Andanenga. Lilikuwa tukio la kihistoria ambapo washairi vijana walifanya mazungumzo na washairi wakongwe katika fani hiyo.

Andanenga alipata upofu utu uzimani baada ya kufanya kazi kwenye idara mbalimbali Serikalini. Alipenda kuitwa ‘kipofu anayeona.’ Hakuona kama kuitwa kipofu ni tusi, lakini ikiwa mtu angemwita ‘asiyeona’ hapo ndipo alipokosea. Alilikumbatia giza, na kusema kuwa alizoea kuishi nalo hata ambapo watu wengine walipata tabu kukaa gizani.

SOMA ZAIDI: Zainab Burhani Anavyouchora Mchango Chanya wa Baba Katika Malezi ya Watoto Kwenye ‘Mali ya Maskini’

Kwa miaka ya hivi karibuni, nimekuwa na tabia ya kutokuchukua sana matukio kwa simu yangu. Pengine kwa sababu nimeona jinsi ambavyo mtu anaweza kutokuwa makini na jambo linaloendelea, au kutokujali mazingira yaliyomzunguka, kwa kujenga hiyo tabia ya kurekodirekodi kila kitu kila saa. 

Jambo la maana

Lakini leo hii, ninaona kuwa nilifanya jambo la maana sana kumrekodi Andanenga kabla ya shughuli kuanza siku ile. Bado ninayo taswira ya uzuri wa meno yake meupe pe na fizi zake nyekundu kichwani mwangu, huku sote tukicheka kwa bashasha. 

Alikuwa ameketi kwenye kiti cha mbele kwenye gari, amevaa kanzu nyeupe, koti jeupe, kofia nyekundu na miwani meusi. Mkononi mwake akiwa ameshika fimbo ya kutembelea.

Katika video hiyo ananipa somo fupi la kutofautisha ubahani, ambayo ni namna ya kupanga maneno ya ushairi; ulaghini na anayefanya kitendo hicho kuwa ni mlaghani – anayetia sauti katika shairi lililotiwa sauti na mbaghani; na akahitimisha kuwa mlaghini anampa mghani aghani. Anamalizia maelezo yake kwa kicheko. Ananiambia anaweza kubaghani, kulaghini si bingwa na kughani ndiyo hawezi kabisa. Tunacheka.

Ananieleza kuwa katika miaka ya nyuma tulikuwa na mghani mahiri aliyeitwa Athumani Khalfani. Kisha ananiimbia shairi lililoandikwa na Kaluta Amri Abeid kuhusu wanawake wa Tanga. Tunacheka, maana nilikuwa nimetoka kumwambia kuwa mimi ni mtu wa Tanga.

SOMA ZAIDI: ‘Mapenzi Bora’ ya Shaaban Robert Inavyochambua Maana Pana ya Dhana ‘Mapenzi’

Andanenga aliniimbia sehemu ya shairi aliloandika wakati alipopokonywa uoni, akiyalilia macho:

Macho ni macho, yenye mboni

Yasomboni, ni ya nini?

Macho ni macho, yenye maono

Yasoona, ni ya nini?

Yote ni yake Maanani

Yaliyopangwa, yakubaliwe.

Hilo ni lile aliloniimbia mimi. Katika Diwani ya Ustadh Andanenda, iliyochapishwa mara ya kwanza mwaka 1993 na Benedictine Publication Ndanda – Peramiho, anasema kwenye shairi lake la Sauti ya Kiza:

Ngakua na mato, ya kuonea

Ngalisana kito, cha kuchezea

Kilicho kizito, cha kuelea

Kikamuenea, akivae.

Makusudi yangu, ngaliandaa

Ngafinyangha chungui, cha mduwaa

Ngatia vitangu, vinavyong’aa

Ili ziwe taa, kwa apikae

Lakini Andanenga hakuwa mtu aliyeruhusu hali yake imzuie kufanya lile aliloweza kulifanya. Hakujiona duni, asiye na sauti, mnyonge. Bali alitumia ushairi kupaza sauti yake na ujumbe wowote ule aliosimamia kama kweli. 

Utajiri

Andanenga ametuachia utajiri mwingi katika fasihi, kama vile mashairi yake kwenye kitabu cha Diwani ya Ustadh Andanenga yalichapishwa mwaka 1993. Katika shairi lake la Awezalo Binadamu, anasema:

SOMA ZAIDI: Tusome ‘Kielezo cha Fasili’ Tujue Jinsi ya Kusoma

Bismillahi kutunga, nisikilizeni kaumu

Ndiye mimi Nadanenga, niliyeshika kalamu

Dhamiri kubwa kupanga, yangu kurasani humu

Awezalo binadamu, tusiseme hatuwezi.

Tusiseme hatuwezi, awezalo binadamu

Liwezwalo kwa ujuzi, kwa kutumia elimu

Nasi tukizama mbizi, lazima tutahitimu

Awezalo binadamu, tusiseme hatuwezi.

Kadhalika, sitasahau mara yangu ya mwisho kuzungumza na Andanenga. Ilikuwa ni siku ya sherehe ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Aprili 13, 2024, katika ukumbi wa The Super Dome, Dar es Salaam. 

Mwisho wa sherehe, aliomba niitwe, nami nikaitika. Akaniuliza, mbona mmewasahau watu wenye ulemavu kama mimi? 

Nikamwambia, hatujawasahahu kwani tunapokea mawasilisho ya Braille. Kweli? Nikamjibu, ndiyo. Akasema, basi nitaleta kazi yangu kwenye awamu ijayo. Sikufahamu kuwa ilikuwa mara yangu ya mwisho kumuona na kusikia sauti yake akiwa hai.

SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu

Katika Diwani ya Ustadh Andanenga, mashairi yake yanaelezea uzalendo, lugha ya Kiswahili, ushairi wenyewe, malumbano ya mada mbalimbali za kijamii, rai na mawaidha, mapenzi pamoja na mashairi ya majonzi na kuomba heri.

Shairi lake la mwisho kwenye kitabu hiki ni Molina Tupe Nguvuzo, anasema:

Molina tupe nguvuzo, na nguvunimo fahamu

Na fahamu tupazo, ziwezo zenye elimu

Na elimuni hakizo, na mwa haki kuwe hamu

Na pendo hamuni hamu, ziwe za viumbe vyote.

Molina tupe nguvuzo, na nguvunimo nujumu

Na nujumu utupazo, ziwezo zenye hashimu

Na hashimuni pendezo, na mwa pendo muwe kemu

Umoja hamuni hamu, ziwe za viumbe vyote.

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts