The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali Kufuatilia Madai ya Ukatili Dhidi ya Wananchi wa Tabora Walio Kwenye Mgogoro na Mamlaka za Hifadhi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aahidi kuchukua hatua hiyo baada ya kupewa taarifa kuhusu kadhia hiyo inayosumbua maelfu ya wananchi Kaliua.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itafuatilia taarifa zinazohusisha askari wa uhifadhi kuwafanyia vitendo vya kikatili wananchi wa Kaliua, mkoani Tabora, ikiwemo vipigo, ubakaji na mauaji, vinavyofanywa kuwaondosha wananchi kwenye maeneo ambayo Serikali imeyageuza kuwa hifadhi ya taifa.

Majaliwa, ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa (Chama cha Mapinduzi – CCM), alitoa ahadi hiyo hapo Mei 21, 2024, alipokuwa akizungumza kwenye kongamano la wanahabari wa mitandao ya kijamii lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya washiriki.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Serikali alitoa ahadi hiyo kufuatia ombi kutoka kwa mhariri wa The Chanzo, Khalifa Said, aliyemuomba Majaliwa aingilie kati na kuchunguza ukweli wa madai hayo ambayo yaliibuliwa kwa mara ya kwanza na chombo hiki cha habari hapo Mei 8, 2024, na kuibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Lile tatizo la Kaliua tutawasiliana na mamlaka za Serikali kule, tujue ni nini kimetokea,” alisema Majaliwa mwishoni mwa hotuba yake iliyodumu kwa takriban masaa mawili. “Sisi tukiona video zenu wapi huko, Simiyu, Busega huko, mwananchi kapigwa inaonekana kuna shida, tunampigia mkuu wa wilaya [tunamuuliza] hii ni nini?” 

“[Tunamwambia] alete taarifa sasa hivi, anazifuata tunapata taarifa. Lipo tukio moja tunaliendesha, hatutaki kulitangaza kwa sasa, huko Mbeya, tunaendelea kufukuzana nalo. 

Nyinyi ndiyo mmetuonesha, tunalifanya kazi. Serikali ipo bize, Jeshi la Polisi lipo kule Mbeya bize linafanya ufuatiliaji wa hilo. Kwa hiyo, haya ni [matokeo ya] mahusiano mazuri kati ya wanahabari na Serikali,” alisema Majaliwa. 

Ukatili

Kwenye ripoti yake hiyo ya kiuchunguzi, The Chanzo ilifichua vitendo vikubwa vinayohusisha ukiukwaji wa sheria za nchi na misingi ya haki za binadamu vinavyofanywa na askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na mgambo dhidi ya wananchi wanaodaiwa kuishi na kufanya shughuli zao kwenye maeneo yanayodaiwa kuwa ni ya hifadhi.

SOMA ZAIDI: Mauaji, Ubakaji na Vipigo: Simulizi za Kutisha za Mamia ya Wananchi Tabora Waliobaki Bila Makazi Baada ya Serikali Kugeuza Ardhi Yao Kuwa Hifadhi

Wananchi walioathirika zaidi ni wale wanaotoka kata za Usinge, Nzugimulole, Usenye, Igagala na Ugunga, katika wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, ambao tangu mwaka 2021 wamekuwa katika mgogoro na TAWA na TFS, kufuatia hatua ya Serikali kutwaa sehemu ya ardhi ya vijiji na kuigeuza kuwa hifadhi, na kuziacha kaya takriban 7,000 bila makazi.

Wananchi waliieleza The Chanzo namna askari wa uhifadhi wanavyowabaka, kuwaua, kupora mali zao pamoja na kuuwa na kupora mifugo yao, ikiwemo kwa kupigwa risasi. Wananchi wanasimulia namna askari wa uhifadhi walivyowaua baadhi ya wananchi wenzao na kuwachoma moto ili kupoteza ushahidi.

Wananchi pia walieleza namna askari wa uhifadhi walivyobomoa nyumba zao kwa kuzichoma moto, wakiharibu pia shule pekee iliyokuwa kwenye eneo hilo, iliyojengwa kwa nguvu za wananchi, kwa kuichoma moto, na kupelekea mamia ya watoto kushindwa kuendelea na masomo.

Lakini licha ya ukweli kwamba The Chanzo ilipatiwa ushahidi wa picha na video zinazothibitisha madai haya, mamlaka za Serikali wilayani Kaliua zimekanusha kutokea kwa matukio hayo, huku mkuu wa wilaya wilayani humo, Rashid Chuachua, akisema hakuna ukiukwaji wowote wa sheria na haki za binadamu unaofanyika katika kuwaondoa wananchi kwenye eneo la hifadhi.

“Sheria iko wazi tu, kwamba wananchi hawaruhusiwi kwenda [hifadhini],” Chuachua aliiambia The Chanzo. “Lakini hakuna mgogoro wowote uliofika mezani kwangu, kwamba kuna mgogoro wowote, sijapata tatizo lolote mezani.”

Chanzo cha mgogoro

Uchunguzi wa The Chanzo umebaini kwamba ardhi iliyotwaliwa na Serikali ilikuwa sehemu ya hifadhi jamii – inayotambulika rasmi kama Igombe and Sagara Wildlife Management Area (ISAWIMA)–iliyoanzishwa mwaka 2007 na vijiji 11 katika tarafa ya Igagala, wilaya ya Kaliua, iliyohusisha kilomita za mraba 1,800, au hekari 1,800,000, za ardhi ya vijiji ili kuzuia matumizi holela ya maeneo ya kila kijiji mshirika.

SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro

Baadaye, Serikali ilitwaa kilomita za mraba 1,300, kutoka katika kilomita za mraba 1,800, kuanzisha hifadhi ya Igombe Game Reserve, na kuwaachia wananchi kilomita za mraba 500 kwa ajili ya matumizi yao.

Hata hivyo, wananchi hawajapata hizo kilomita za mraba 500 na badala yake hifadhi jamii ya ISAWIMA inadaiwa kupora ardhi hiyo. Hifadhi jamii ya ISAWIMA inadaiwa kushirikiana na TAWA kudhulumu ardhi hiyo kwa kutumia mabavu, vipigo, uharibifu wa mazao, faini zisizo halali na ubakaji.

Serikali ya mkoa na ile ya wilaya zimeendelea kuitambua ISAWIMA licha ya ukweli kwamba kwa sasa, kwa mujibu wa GN No. 455 ya 2021, Hifadhi Jamii ya ISAWIMA haina ardhi, ikikalia ardhi ya wananchi, na kupelekea mgogoro kati yake na wanavijiji.

Wananchi wanaitaka Serikali iwapatie kilomita za mraba 500 zilizobaki baada ya Serikali kutwaa eneo la Igombe Game Reserve, ardhi ambayo inashikiliwa na ISAWIMA katika namna ambayo wananchi wanaamini siyo kihalali.Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumfikia kupitia  najomar@live.com. Habari hii imehaririwa na Lukelo Francis.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *