The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali, Wadau Waongeze Nguvu Kukabiliana na Tatizo la Sumukuvu Tanzania

Ugonjwa wa sumukuvu siyo tu unaathiri wakulima kwa kukosa masoko kwa mazao yao bali pia afya na ustawi wa Watanzania kwa ujumla.

subscribe to our newsletter!

Miezi hii ya Mei, Juni, Julai na hata Agosti ni miezi ya mavuno hapa nchini kwetu Tanzania. 

Haijalishi uwe mkulima mdogo, wa kati, ama mkubwa, hiki ni kipindi cha kuvuna ulichokipanda; ndicho kipindi pia cha mafuta kujitenga na maji kwa maana kwamba mkulima anajua shughuli yake ya kilimo imemnufaisha vipi ukilinganisha na uwekezaji alioufanya.

Hata hivyo, ni wakati huu ambapo baadhi ya wakulima hufahamu kwamba mazao waliyovuna hayatafaa kwa ajili ya kuuzwa sokoni kwa ajili ya kuliwa na binadamu kwani yameshambuliwa na sumukuvu, au mycotoxin kwa kimombo, kutokana na kutokuhifadhiwa vizuri, pamoja sababu nyingine mbalimbali.

Ripoti mbalimbali zimeonesha namna sumukuvu ilivyo tatizo kwa maelfu ya wakulima nchini Tanzania, hali ambayo siyo tu inahatarisha vipato na ustawi wao, bali pia maendeleo ya taifa zima na watu wake. Hii inatokana na madhara yanayotokana na utumiaji wa mazao yaliyothibitika kuwa yameathiriwa na sumukuvu.

Kubaini sumukuvu katika mazao ni pale unapoona ukungu wa kijani, ama njano, ama mweusi, umezunguka kwenye mazao kama vile karanga, mihogo, viazi, mahindi, nyanya, matunda, pamoja na mazao mengine mbalimbali.

SOMA ZAIDI: Bajeti Wizara ya Kilimo Inaakisi Umuhimu wa Kilimo Tanzania?

Ukosefu wa elimu ya utunzaji wa udongo miongoni mwa wakulima wetu hupelekea kilimo holela chenye kuathiri afya ya udongo na hivyo kupelekea udongo kuwa mgonjwa na kusababisha mazao kupata ugonjwa kama huo, lakini pia mazao kuwa hafifu kwa maana ya mavuno duni.

Wakulima wetu wengi wamekuwa hawapatiwi elimu mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi, hali inayopelekea ukulima holela na kujaza mifugo, ama mazao, yasiyo na viwango, ama ubora wa kushindana katika masoko ya kikanda na kidunia.

Kama wananchi, tumekuwa tukila hizi sumukuvu kwa muda mrefu kidogokidogo, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza nchini mwetu, kama vile saratani za figo na ini.

Mazao ambayo yameathiriwa na sumukuvu yanapoliwa na wanyama, ndege na hata samaki, kisha binadamu akaja kula nyama, maziwa, ama mayai ya viumbe hao, basi hula na ile sumu waliyokula wanyama hao, tafiti mbalimbali zimeonesha.

Madhara ya sumukuvu kwenye mwili wa binadamu ni mengi, ikiwemo saratani, ini kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi pamoja na figo na hatimaye kifo. Viumbe hai wengine kama wanyama wanapokula sumukuvu hufa, na vifo huweza kuwa vya ghafla ama vya taratibu.

SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Yatajwa Kuathiri Kilimo cha Korosho Lindi, Mtwara

Bidhaa zetu kwa muda mrefu sana zimekuwa zikishindwa kushindana kwenye masoko ya kimataifa na hata ya kikanda kwa kukosa ubora. Tatizo hili linaonesha limekosa muarobaini, hali inayoonekana kutokana na kutokuwepo kwa utashi wa kisiasa miongoni mwa wale waliokabidhiwa uongozi wa umma.

Nitoe rai kwa mamlaka husika – Wizara ya Kilimo, Wizara ya Afya, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), halmashauri zote nchini na wadau wengine – kuhakikisha wanakuwa na mpango, ama chombo, maalumu cha kuratibu utekelezaji wa mipango madhubuti itakayohakikisha usalama wa chakula na lishe wanayopata Watanzania.

Wizara ziache kufanya kazi kwa mazoea, ziende porini kwa wakulima na kujionea wenyewe, zikae na wakulima wakati wa kuandaa mipango mikakati kuliko kujifungia ofisini.

Elimu kwa wakulima wetu iwe ni jambo jumuishi. Serikali inaweza kufanya kazi na wadau wa maendeleo, kama vile mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi. Hii itasaidia sana kulinda afya zetu, afya za wanyama pamoja na viumbe walioko ardhini na ambao ni muhimu sana kwa rutuba na afya ya udongo. 

Kwa pamoja tunaweza kukabiliana na tatizo la sumukuvu miongoni mwa wakulima wetu!

Dahlia Majid ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT-Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia majiddahlia935@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ujumbe Mzuri Sana Kwa Tahazali
    Na Usalama wa Chakula Ili Kulinda
    Afya za Wananchi
    Ni Muhimu sana Ujumbe huu
    Ukafanyiwa Kazi na Mamlaka Husika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *