The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uchambuzi: Bajeti ya Wizara ya Kilimo 2024/25 Inaakisi Umuhimu wa Sekta ya Kilimo?

Bunge la Tanzania lilipitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo kiasi cha shilingi trilioni 1.249 kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 siku ya Mei 3, 2024.

subscribe to our newsletter!

Bunge la Tanzania lilipitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo kiasi cha shilingi trilioni 1.249 kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 siku ya Mei 3, 2024. Kiwango hiki ni sawa na asilimia 2 ya bajeti nzima ya Serikali inayopangwa kutumika kwa mwaka 2024/25.

Wizara hii ndio inayosimamia Sekta ya Kilimo kwa upande wa mazao, sekta inayotegemewa na wananchi takribani asilimia 65. Sekta hii kwa mwaka 2023 imeendelea kukua kwa asilimia 4.2 mwaka 2023 kutoka asilimia 2.7 mwaka 2022. Pia imechangia asilimia 16.1 ya pato la taifa.

Tumefanya uchambuzi wa bajeti hii na kuangalia maeneo kadhaa kama vile fedha zinazopokelewa na Wizara ukilinganisha na bajeti ambayo imekuwa ikipitishwa, mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi na uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji nchini.

Licha ya bajeti hii ya Wizara ya Kilimo kuonekana ndogo sana ukilinganisha na bajeti nzima ya Serikali kwa mwaka 2024/25, bado kiwango hiki ni ongezeko la takribani shilingi  bilioni 278 ukilinganisha na bajeti ya 2023/24. 

Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka bilioni 229.8 mwaka 2020/21 mpaka trilioni 1.2 mwaka 2024/25. Ongezeko kubwa limetokea kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 kipindi ambacho Serikali ya awamu ya sita iliingia madarakani.

SOMA ZAIDI: Uchambuzi: Bajeti ya Wizara Ya Nishati 2024/25 Ni Ndogo Zaidi Kutokea Katika Kipindi Cha Miaka Mitano. Hiki Ndicho Kilichosababisha

Jambo hili ni jema, ikizingatia kwamba sekta hii ni muhimu kwa ustawi wa maisha ya wananchi wengi, lakini pia wadau wengi wamekuwa wakishauri bajeti ya kilimo kwa ujumla, yaani ustawishaji mazao, mifugo na uvuvi walau itengewe asilimia 10 ya bajeti nzima ya Serikali.

Waswahili husema “mipango sio matumizi”, hii ina maana kuwa pamoja na ongezeko hili la bajeti kwa upande wa Serikali bado kumekuwepo na changamoto kubwa sana ya kuipelekea Wizara fedha zilizotengwa kwenye bajeti, ukiacha mwaka 2021/22 ambapo Wizara ya Kilimo ilipokea asilimia 161 ya bajeti iliyopitishwa Juni 2021. Hii ilitokana na mkopo wa Shirika la Fedha la Kimataifa wa kukabiliana na  UVIKO-19, ambapo Wizara kadhaa ziliweza kupata fedha juu ya kiwango cha bajeti.

SOMA ZAIDI: Uchambuzi Bajeti ya TAMISEMI 2024/25

Mwaka 2022/23 fedha zilizopelekwa ni asilimia 64 tu ya bajeti. Lakini kwa mwaka 2023/24 mpaka kufika Aprili ambapo inabakia miezi miwili kukamilisha mwaka wa fedha, ni asilimia 54% ya fedha za bajeti zilipokelewa na Wizara. Mwenendo huu unatia shaka kama kweli Serikali inauchukulia uzito Wizara hii kama ambavyo imekuwa ikijinasibu.

Mapato ya mauzo ya mazao nje

Katika taarifa ya Wizara ya Kilimo bungeni inaonesha kwamba mauzo ya mazao ya kilimo kwenda nje ya nchi yameongezeka kutoka shilingi trilioni 4.9 mwaka 2020/21 mpaka shilingi trilioni 5.7 mwaka 2022/23. 

Jambo moja kubwa muhimu ni kwamba zao lisilo asilia la biashara ndio limeongoza kwa mauzo ya trilioni 1.3 ikifuatiwa na zao la mahindi mauzo ya bilioni 629.0. Ukiangalia haya ni moja ya mazao ambayo sehemu ya wakulima wake walipatiwa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo katika mwaka husika.

Katika mwelekeo huo, Katika bajeti ya hii Serikali imeahidi kuendelea kupeleka ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima, pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa kutosha wa mbolea za viwandani nchini.

SOMA ZAIDI: Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara

Lakini pia ili kuhakikisha mapato haya yanawanufaisha wakulima ni muhimu sana Serikali kuzingatia maoni ya wadau juu ya mzigo mkubwa wa tozo mbalimbali zinazotozwa kisheria na kikanuni na mamlaka mbalimbali za Serikali kwa wakulima. 

Kilimo cha Umwagiliaji

Katika jambo lingine lilojitokeza katika bajeti hii ni ongezeko la bajeti ya umwagiliaji kutoka bilioni 373.5 mpaka bilioni 403.8. Katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita imeonesha msisitizo wake kwenye kilimo cha umwagiliaji amabpo imedhihirika kupitia bajeti ambazo zimekuwa zikitengwa.

Kwa mujibu wa Wizara miradi ya umwagiliaji iliyopangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka 3 ya kifedha 2022/23, 2023/24 na 2024/25 ikikamilika itaongeza eneo la kilimo la umwagiliaji la hekari 543,366.46 hivyo kufanya eneo la umwagiliaji kutoka hekari 727,280.6  mpaka hekari 1,270,647.1.

Changamoto kubwa katika kufikia hili lengo, yaani miradi yote ya umwagiliaji iliyopangwa iweze kumalizika ni fedha zinazopelekwa katika kutekeleza miradi hiyo. Mwaka 2022/23 kati ya bajeti ya shilingi bilioni 366.8 ni shilingi bilioni 107.8 tu sawa na asilimia 29% ya fedha ndizo zilitolewa.

Hii inaonesha kwamba kwa muda uliobaki ni ngumu sana kwa Tanzania kufikia hekta milioni 1.2 za kilimo cha umwagiliaji. Ni safari ndefu sana inayohitaji mipango na utekelezaji wa kweli, ikizingatia kuwa Tanzania kwa ujumla ina eneo la hekta milioni 29.4 linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo mpaka hivi sasa ni  hekta 727,280.6 tu sawa na asilimia 2.5 ndizo ambazo zinatumika katika kilimo cha umwagiliaji.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ndugu zanguni mie naona pamoja na jitihada zote za BBT zenye nia njema lkn kwa utekelezaji huu wa 54% ya bajeti na hapo bado CAG hajaonyesha kwenye hiyo 54% mafisadi wamekula ngapi .
    Bado hatujaamka bado ni kiza .

    Kwa nini tusianze na kidogo tunachokiweza ikisha mwakani inshallah tukaongeza tena kidogo hivo hivo tukafikia lengo? .
    MF:Leo lima robo, msimu ujao lima nusu, msimu wa tatu lima nusu na robo alafu msimu wa nne lima hekari nzima?
    Ebu tujaribu kujikuna mkono unapofika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *