The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali ya Tanzania Kuiuzia Zambia Tani 650,000 za Mahindi

Tanzania na Zambia zimeingia makubaliano ya mauziano ya tani 650,000 za mahindi yenye thamani ya shilingi bilioni 650

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Tanzania na Zambia zimeingia makubaliano ya mauziano ya tani 650,000 za mahindi meupe yenye thamani ya shilingi bilioni 650, kufuatia hali ya ukame iliyoikumbuka Zambia kupelekea wananchi takribani milioni 7 kuhitaji msaada wa chakula.

Mkataba wa makubaliano hayo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Dkt. Andrew Komba kwa upande wa Tanzania pamoja na Mratibu wa Maafa kitaifa nchini Zambia Dk Gabriel Pollen, katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Dkt. Komba amesema mahindi ambayo yatapelekwa Zambia katika kipindi cha miezi nane kutoka sasa, yatatoka katika maghala mbalimbali ya NFRA yaliyopo: Sumbawanga, Songwe, Makambako na Songea.  

“Haya mahindi yatakayopelekwa kwa wenzetu wa Zambia ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu kama ilivyosemwa, hivyo viwango vya ubora vimezingatiwa kwa mujibu wa nchi zote mbili,” alisema Dk Komba.  

SOMA ZAIDI: Uchambuzi: Bajeti ya Wizara ya Kilimo 2024/25 Inaakisi Umuhimu wa Sekta ya Kilimo?

Ukame ulioikumba Zambia katika msimu unaoelekea kuisha wa kilimo uliipelekea Serikali ya nchi hiyo kutangaza hali ya dharura kwani watu takribani milioni saba wapo kwenye hatari ya kukumbwa na njaa katika kipindi cha ndani ya miezi kumi na mbili tangu sasa.

Kwa upande wa Tanzania, katika msimu uliopita wa kilimo wa mwaka 2022/23 iliweza kujitosheleza kwa uzalishaji wa mahindi kwa asilimia 120, kufuatia uzalishaji wa tani milioni 8.0 huku mahitaji halisi nchini yakiwa tani milioni 6.6.

Uzalishaji huu wa ziada ulienda sambamba na mauzo ya mahindi nje ya nchi kiasi cha tani laki 5.8 kupelekea kuingizia nchi mapato yenye thamani ya shilingi bilioni 629, kutoka mauzo ya tani laki 1.7 yenye thamani ya shilingi bilioni 124 msimu wa mwaka 2020/21.

Hali hii ya kujitosheleza kwa uzalishaji wa mahindi na ongezeko la mauzo ya mahindi nje nchi inatajwa kuchagizwa na hatua kubwa mbili ambazo Serikali imezichukua tangu mwaka 2021, kuongeza ruzuku kwenye kilimo na kufungua mipaka ya nchi kwa biashara ya mazao ya chakula.

SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Waongeze Nguvu Kukabiliana na Tatizo la Sumukuvu Tanzania

Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe ambaye pia alikuwepo katika hafla ya utiaji saini amesema kuwa mauziano ya mahindi baina ya Serikali hizo mbili hayatazuia wafanyabiashara wa ndani kupeleka mahindi Zambia kupitia utaratibu wa kawaida uliopo. 

“Nataka nitumie fursa hii niwaambie Watanzania kwamba haina maana makubaliano ya Serikali kuuza mahindi Zambia yanafunga mipaka ya watu binafsi kuuza mahindi Zambia,” alisema Bashe, “tunachokitaka tu wafanyabiashara wa Tanzania wanaopeleka mahindi Zambia wafuate utaratibu wa Serikali.”

Bashe pia alitumia fursa hiyo kutangaza kuwa Serikali kupitia NFRA itafungua msimu mpya wa kununua mahindi ya wakulima wa 2023/24 kuanzia Julai 10, 2024, ambapo amesema NFRA itatangaza bei na kuwataka wafanyabiashara waliotuma maombi ya kuiuzia mahindi NFRA waonane na Mkurugenzi kwa ajili ya kusaini mikataba.

“Mahindi yatanunuliwa kwenye vituo vya miaka yote vya NFRA,” alisema Bashe, “lengo tulilojiwekea mwaka huu ni kununua wastani wa tani milioni 1.1 kwa sababu tunataka kuuza mahindi tani milioni 1 ukiacha tulichonacho ndani kama akiba.” 

Naye Waziri wa Kilimo wa Zambia, Reuben Mtolo Phiri amewashukuru viongozi wa nchi mbili, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Hakainde Hichilema wa Zambia kwa jitihada zao za pamoja kuhakikisha makubalino ya mauziano ya mahindi  ya nchi hizo mbili yanafanikiwa.

SOMA ZAIDI: Konokono Wanavyowaliza Wakulima Mbeya, Serikali Yatafuta Suluhu ya Kudumu

Waziri Phiri pia amesisitiza umuhimu wa ushiriki mpana wa wadau mbalimbali kwenye ushirikiano huu wa kibiashara kati ya Tanzania na Zambia kwa kuhusisha na sekta binafsi ya Zambia na Tanzania.

“Tumesaini mkataba wa mauziano ya tani 650,000 za mahindi baina ya Serikali na Serikali. Lakini nina uhakika kuna mikataba midogo itakwenda kusainiwa baadae baina ya sekta binafsi kwa sekta binafsi, au sekta binafsi na Serikali ya Tanzania,” alisema Phiri.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *