The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nguvu ya Utashi wa Kisiasa Katika Kujenga Upya Jamii Zenye Migogoro Isiyokwisha: Masomo Kutoka kwa Utawala wa Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi

Tofauti na SUK ya 2010-2015 ambapo kambi mbili ndani ya Serikali, chama tawala na upinzani, zilifanya kazi kwa kuhofiana na kutoaminiana, SUK ya Mwinyi imekuwa tofauti kabisa.

subscribe to our newsletter!

Kwa asili, Rais Hussein Mwinyi ni mtu mpole na mtulivu. Bila shaka amechukua haiba hii kutoka kwa baba yake, hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi. Mwinyi, baba, amejiweka katika kumbukumbu ya heshima ya uongozi wa kisiasa hapa nchini Tanzania, licha ya misukosuko ya kipindi cha mpito cha utawala wake. 

Wanahistoria wanaeleza kuwa Rais huyo wa awamu ya pili nchini Tanzania ni miongoni mwa wanasiasa walioiva katika tanuri moto sana. Mwinyi, aliyefariki Februari 29, 2024, anakumbukwa kwa kukabili mabadiliko magumu, huku nchi ikigubikwa na hofu ya mpito kutoka katika siasa za kimapinduzi, kwa upande wa Zanzibar, na kutoka katika siasa za ujamaa, kwa upande wa Tanzania Bara katika miaka ya 1980.

Lipo kundi katika Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar ambalo halifurahishwi na uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), na hivyo kuhubiri waziwazi kwamba wataiondoa kwenye Katiba iwapo watapata nafasi. 

Baadhi wakionesha hawana tatizo sana na SUK lakini hawajiamini kuifanyia kampeni. Ujasiri wa mapema ya Dk Mwinyi kuitetea SUK katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 ilikuwa ishara nzuri kwa uongozi wake wa baadaye katika eneo la maridhiano na umoja wa kitaifa.

Kitendo cha kuanzisha mazungumzo na Upinzani Zanzibar mara maada ya kuapishwa, na hatua ya kuyakubali masharti yote yaliyotolewa na hayati Maalim Seif Sharif Hamad kwa niaba ya upinzani kuwa ni lazima yatimizwe ili waweze kujiunga na Serikali, kilionesha ukomavu wa kiuongozi na kisiasa. 

Masharti

Sharti la kwanza ni kuwaachilia huru kutoka magerezani wafungwa wote wa Uchaguzi Mkuu wa 2020. Sharti la pili ni kuwapatia matibabu waathiriwa wote wa ukatili wa uchaguzi. Sharti la tatu ni kutoa fidia kwa waathirika wa ukatili wa Uchaguzi Mkuu wa 2020. 

Sharti la nne ni marekebisho ya mfumo wa kisheria unaosimamia mchakato wa uchaguzi ili kufanya mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kufanya uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki. Sharti la tano ni kuunda kamati ya uchunguzi kuhusu sababu za machafuko ya uchaguzi wa 2020 na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika.

SOMA ZAIDI: Safari Yangu ya Gerezani Bila Kupitia Polisi Wala Mahakamani

Tofauti na SUK ya 2010 – 2015 ambapo kambi mbili ndani ya Serikali, chama tawala na upinzani, zilifanya kazi kwa kuhofiana na kutoaminiana, SUK ya Dk Mwinyi imekuwa tofauti kabisa. 

Rais Mwinyi amekuwa akijenga ukaribu sana na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi kutoka upinzani. Amekuwa akiwasifu waziwazi mawaziri kutoka upinzani kwa kazi nzuri wanayofanya katika kusaidia Serikali yake kufanya vyema jambo ambalo halikuwezekana katika SUK iliyopita.

Suala la maridhiano katika Serikali ya Mwinyi kamwe haliwezi kutenganishwa na utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa yaliyowekwa kati yake na hayati Maalim Seif. 

Utekelezaji wa sharti la kwanza, yaani, kuachiliwa kwa wafungwa wa uchaguzi, ulianza mara tu baada ya Rais kuingia madarakani huku lile la pili, yaani, kuwatibu waathirika wa ukatili wa uchaguzi lilifuatia baadaye. 

Utekelezaji wa sharti la nne ulianza kwa mafanikio kwa kuundwa kwa Kikosi Kazi Maalum ambacho kilipewa jukumu la kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar. Kikosi Kazi hicho kilikamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti kwa Rais Oktoba 10, 2022.

Kuaminiana 

Wataalamu wanaelezea kwamba maridhiano ya kisiasa yana lengo kuu la asili la kujenga upya, au kuimarisha, kuaminiana kati ya makundi hasimu ya kisiasa. Kuaminiana kisiasa ni ghali zaidi katika upande usio na madaraka. 

SOMA ZAIDI: Kikosi Kazi cha Mwinyi Chataka Mamlaka Zaidi kwa Z’bar Ndani ya Muungano

Kwa wao kunahitajika kiwango cha juu cha uvumilivu na kujitoa. Kuaminiana pia kunahitaji kujiweka katika uhusiano na mazingira magumu na utegemezi wa mtu mwingine usie na mamlaka nae; yaani ikiwa unamwamini mtu kukupeleka kwenye uwanja wa ndege, kwa mfano, huna budi ukubaliane na hatari kwamba anaweza asitokee na hivyo upo uwezekano mkubwa wa kukosa safari yako.

Wanazuoni wanatuambia kuwa uaminifu wa kisiasa unahitaji mazingatio ya kimaadili kutoka kwa pande zote zinazohitaji kuaminiana. Kiwango cha chini kabisa cha maadili haya ni kuheshimiana. Kuheshimiana ni chombo muhimu sana cha kupunguza umbali kati ya masilahi pinzani ya kisiasa. 

Kumekuwa na tatizo kubwa la maadili ya kuaminiana kutoka upande wa upinzani kiasi cha CCM kusikitishwa na tabia ya upinzani ya kumkejeli na kumdhihaki Rais, jambo linalodhaniwa kuwa na mchango katika mkwamo wa maendeleo ya maridhiano.

Mpango wa ‘Sema na Rais’ umekuwa na mafanikio makubwa kudhibiti uwajibikaji hadi umezua hofu miongoni mwa watumishi wa umma ambao kwa sasa angalau wanadhihirisha baadhi ya viwango vya mafanikio ya utekelezaji wa majukumu yao.

Hatua dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma zinazoripotiwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kama vile kufukuzwa kazi na maafisa husika kushitakiwa mahakamani, zimekuwa zikichukuliwa.

Ishara njema ya utawala bora wa Rais Mwinyi, ni hatua ya hivi karibuni yenye utata iliyotangazwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Dimwa kwa niaba ya Sekretarieti ya CCM Zanzibar kuhusu suala la kuongeza muda wa urais, Rais Mwinyi hakusita kubaki kwenye misingi ya utawala bora na utawala wa sheria, kwa kuipuuza na kuikataa katakata hoja hiyo ingawa hoja ilimpendelea Rais.

SOMA ZAIDI: Malalamiko Zaidi ya 7,000 ya Wananchi Yamfikia Mwinyi Kupitia App ya Sema na Rais

Tokea Rais Mwinyi aingie madarakani, kipindi cha miaka mitatu na nusu, hakuna matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu yahusianayo na siasa yaliyorekodiwa, ukiwachia kesi moja maarufu ya Baraka Shamte, kada maarufu wa CCM aliyetekwa nyara na kuteswa na watu wasiojulikana jambo lilihusishwa na mtindo wake usiotarajiwa wa kumsema vibaya Rais.

Ubaguzi na upendeleo

Wataalamu wa mambo wanatueleza kuwa ubaguzi haujawahi kubaki kama ulivyo, bali ni jambo la kubadilika, linalohusishwa na mabadiliko ndani ya jamii. Kwa mfano, kikundi kimoja kinaweza kufurahia hadhi ya juu ya kijamii kwa wakati mmoja, lakini mabadiliko ya kijamii yanapotokea, kikundi hicho kinaweza kupoteza hadhi hiyo na kugeuka kuwa kundi la kutengwa.

Ubaguzi na upendeleo kwa jina la siasa umekuwa tabia iliyotamalaki Zanzibar na hivyo kuiweka jamii katika matabaka yakiwemo rangi, kabila, maeneo ya kijiografia na utambulisho wa historia ya kabla na baada ya Mapinduzi. 

Licha ya baadhi ya viongozi na wanasiasa wa ngazi ya kati na ya chini kujaribu kuendeleza hali iliyopo na hivyo kudhoofisha juhudi za Rais juu ya suala hili, matokeo siyo ya kukatisha tamaa sana. Hata Ikulu ni kawaida kwa sasa kukuta vijana machotara na wenye asili ya Pemba, jambo ambalo lilikuwa mwiko huko nyuma.

Lugha za kibaguzi na dhihaka zilizozoeleka kutoka midomoni mwa wanasiasa wa chama tawala hapo nyuma, na yale mabango ya kibaguzi na propaganda za kibaguzi yaliyokuwa yanalindwa katika maskani mashuhuri za CCM zimekomeshwa kabisa. 

Maskani za CCM za Kachorora na Muembe Kisonge, maeneo muhimu kwa lugha za kibaguzi na dhihaka dhidi ya Wapemba na watu wenye ngozi nyeupe, zimechukua mkondo mpya kwa kuwa vituo vya ujasiriamali.

Katika historia ya tawala zilizopita, tokea zama za Mreno, Sultani, Muingereza na hata baada ya Mapinduzi, Pemba haijawahi kuchukuliwa kwa uzito unaostahiki kama moja ya visiwa viwili ndugu vinavyounda nchi ya Zanzibar. Juhudi za kuleta maendeleeo na ustawi wa watu kisiwa cha Pemba zimekuwa haziendani kabisa na umuhimu wa kisiwa hicho, ukubwa wake na hata idadi ya watu wake.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Imefeli?

Dk Hussein Mwinyi ndiye Rais pekee kutoka CCM aliyeeleza mara kadhaa nia yake ya kukifungua kisiwa hicho kijamii na kiuchumi na hivyo kuipa mazingatio maalum katika miradi na mipango ya kimaendeleo. Maoni ya wananchi kuhusu suala la Pemba kupewa mazingatio maalum na utawala wa Dk Mwinyi, takwimu zinaonyesha mabadiliko chanya.

Katika nadharia ya uhamasishaji, wataalamu wanatufundisha kuwa kuaminiana kisiasa na uwajibikaji wa walioko madarakani ni mambo yanayotegemeana. Ikiwa wale walio na madaraka watazingatia maslahi ya makundi mengine, kuaminiana kisiasa kunaweza kutokea kwa wepesi. 

Rais Mwinyi hana budi kukamilisha utatuzi wa masharti ya makubaliano kati yake na hayati Maalim Seif yaliyosalia ili kurejesha imani ya upinzani kwake. Bado kuna malalamiko juu ya suala la ubaguzi na upendeleo unaoendelea kimyakimya. 

Utowaji wa fursa serikalini unatekwa nyara na watendaji wa kisiasa wanaotaka kuwanufaisha watoto wao, ndugu zao au wafuasi wa chama tawala na hivyo kurejesha nyuma juhudi za Rais.

Ingawa juhudi kubwa za kuiendeleza Pemba zimechukuliwa, maoni yanadokeza kwamba hatua zaidi bado zinahitajika kuchukuliwa. 

Miundombinu muhimu kama vile bandari na uwanja wa ndege wa kisasa inahitaji kutekelezwa; taasisi za kijamii na kiuchumi kama vile hoteli kubwa za kitalii, hospitali za rufaa, vyuo vikuu au matawi yake, viwanda na makao makuu kwa baadhi ya shughuli za Serikali zinahitaji kuanzishwa katika kisiwa cha Pemba ili kisiwa kiweze kuvutia wakaazi na wageni hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Ahmed Omar ni mwanachama wa ACT-Wazalendo ambaye aliwahi kuwa Katibu wa hayati Maalim Seif Sharif Hamad kwa miaka kumi. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia eddyommy@gmail.com au X kama @ahmed_omar80. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *