The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tumezungumza na Vijana Kumi Waliojiajiri Kupata Uzoefu Wao. Hiki Hapa Ndicho Walichotuambia

Wanajivunia uamuzi huo wa maisha yao, wakiwasihi vijana wengi kufuata nyayo zao.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Kwenye vijana kumi walioamua kujiajiri ambao The Chanzo imezungumza nao, hakuna hata mmoja aliyezungumza kwa lugha iliyoashiria majuto au kutokuwa na uhakika juu ya kile anachokifanya. 

Vijana wote, ambao wana umri kati ya miaka 20 na 40, wote kutoka hapa makao makuu ya nchi, wanaonekana wakifurahia na kujivunia uamuzi wao huo wa maisha yao, wakiwasihi vijana wenzao wafuate nyayo zao.

Utakumbuka kwamba wito wa vijana kujiajiri umekuwa ukiimbwa sana kwa siku za hivi karibuni, hususani na wanasiasa, ukiambatana na ripoti zinazoitaja Tanzania kama moja ya nchi za Afrika zenye tatizo kubwa la ukosefu wa ajira. 

Serikali – pamoja na wadau wengine – imekiri wazi kwamba wakati inachukua jitihada mbalimbali za kutatua tatizo hilo, ambalo baadhi huliita “bomu linalosubiri kulipuka,” hakuna uwezekano wa wahitimu wote kuajiriwa, ikiwataka wachangamkie fursa kadhaa zilizopo nchini kujiajiri wao wenyewe.

Wito huu, hata hivyo, umekuwa ukiibua hisia tofauti miongoni mwa wadau, huku baadhi wakiitaka Serikali iache “siasa” na kutengeneza ajira zitakazowasaidia vijana. Wengine wamedai kwamba sauti hizo zitakuwa ni sawa na kelele tu endapo kama mazingira ya kisera, kisheria na kikanuni hayatabadilika ili kuwawezesha vijana kujiajiri. 

SOMA ZAIDI: ‘Siyo Uhuni’: Wanawake Jasiri wa Kizanzibar Walioingia Kwenye Sekta ya Uongozaji Watalii

Lakini kwenye mazungumzo yake na vijana mbalimbali waliojiajiri jijini hapa, The Chanzo ilibaini kwamba, wakati changamoto nyingi zinaendelea kuwakabili, wajasiriamali hawa machachari hawajawahi kujutia uamuzi wao wa kujiajiri.

‘Niko huru’

Christopher Magesa ni mwanachama wa Tusumuke Group, kikundi cha vijana kumi wanaojishughulisha na utotoleshaji vifaranga mkoani hapa, kilichonufaika na mkopo wa halmashauri wa Shilingi milioni 30 uliowawezesha kununua mashine za utotoleshaji na kujenga jengo lililowawezesha kufanya biashara zao.

“Vijana wengi tumekuwa na kasumba ya kwamba bila ajira Serikalini, maisha hayawezi kwenda,” alisema Masega, 34, mhitimu wa Mati Uyole, ambacho ni chuo cha Serikali cha kilimo na mifugo, huku akiwa anapanga mayai ya kuku kwenye beseni jeusi. 

“Vijana hatuamini kwenye vitu tunavyofanya,” aliongeza mjasiriamali huyo. “Pia, vijana wengi tumekuwa tukisoma kwa kukariri. Tunakaririshwa shuleni kujibu mitihani, lakini siyo kurudi mtaani kujibu changamoto za kijamii.”

Aziza Athumani Konyo alianzisha BSF Envicare Investiment inayozalisha chakula cha mifugo na mbolea kutoka kwenye takataka baada ya kupoteza siku nyingi za maisha yake akisubiri kuajiriwa. Anazalisha kati ya kilo 30 na 40 za chakula cha mifugo na mbolea kwa siku, na malengo yake ni kuzalisha kati ya tani mbili mpaka tatu kwa siku.

SOMA ZAIDI: Shule, Vyuo Vikuu Viwaelimishe Wanafunzi Badala ya Kuwatahinisha

“Kujiajiri kumeniongezea kipato binafsi,” alisema Aziza kwenye mahojiano yake na The Chanzo. “Lakini pia kumenifanya kuwa mjasiriamali ambaye ninaweza kuwakwamua na wengine kutoka kwenye umasikini na utegemezi.”

Aziza Athumani Konyo akielezea safari yake ya kujiajiri na yale ambayo amefanikisha mpaka sasa kwenye safari yake hiyo wakati wa mahojiano na The Chanzo. PICHA | JACKLINE KUWANDA.

Mwanachama wa kikundi cha Dodoma Youth Power kinachojishughulisha na ufugaji wa kuku wa kienyeji na chotara Ibrahim Juma, 23, anasema kujiajiri kumemsaidia yeye na wanakikundi wenzake kujikwamua kiuchumi na kuisaidia jamii inayowazunguka. Anaeleza: “Tumepiga hatua kubwa. Nakumbuka tulianza bila kuwa na ofisi wakati huo. Lakini kwa sasa tuna ofisi yetu.”

Samwel Mjirima, 29, ni mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na mwenyekiti wa kikundi cha vijana kinachouza na kutengeneza mvinyo wa zabibu mkoani hapa anayejivunia safari yake ya kujiajiri.

“Tumefikia mahala pakubwa,” alisema Samwel akiwa katika hali ya furaha. “Kupitia kujiajiri binafsi nimekuwa napata mahitaji madogomadogo kama vile kulipia kodi. Lakini pia tumejiwezesha kiuchumi.”

Frank Jordan ni mwandishi wa habari na mwanzilishi mwenza wa kampuni ya habari ya Jordan Media iliyopo hapa jijini Dodoma. Anasema kuhusu safari yake ya kujiajiri: “Kujiajiri kumebadilisha maisha yangu. Mwanzo, wakati naanza, nilikuwa najichangachanga. Sasa hivi maisha yangu yanaendeshwa kupitia fani ya uandishi wa habari. Namshukuru Mungu mpaka sasa hapa nilipofikia.”

Mapambano

Simulizi hizi za kuvutia kutoka kwa vijana hawa walioamua kujiajiri hazimaanisha kwamba safari zao zilikuwa rahisi kama vile kutembelea mbugani, la hasha! Vijana hawa waliileza The Chanzo kwamba wanalazimika kukabiliana na changamoto mbalimbali kuhakikisha uhai wa biashara zao. Hata hivyo, hawaruhusu changamoto hizo ziwakatishe tamaa.

SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwawezesha Vijana Kuwekeza Zaidi Kwenye Uchumi wa Buluu

Aisha Msantu ni Mkurugenzi Mtendaji wa Glaring Future Foundation (GFF), shirika lisilo la kiserikali alilolianzisha mwaka 2019 akiwa na wenzake kuwawezesha vijana kiuchumi. Msantu, 27, anasema yeye na wenzake iliwabidi wapambane sana kuhakikisha taasisi yao hiyo inasimama na kufanikisha ndoto walizokuwa nazo.

“Toka taasisi hii isajiliwe, ina miaka mitano, miaka mitatu nyuma haikuwa myepesi,” anakiri Msantu. “Kuna muda nilisema kwa nini nimeanza, si ni bora niache nikafanye kitu kingine? Lakini ule moyo wa kuendelea kupambana kwa hiki tulichochagua tumeona kimeweza kuleta matokeo.”

Aisha Msantu, Mkurugenzi Mtendaji wa GFF, anaamini kuwa na moyo wa mapambano na imani katika kile unachofanya ndiyo msingi wa kufanikiwa kwenye safari ya kujiajiri. PICHA | JACKLINE KUWANDA.

Lucas Sospeter anamiliki na kuendesha duka la nguo, Smart Jeans, akiwalenga zaidi akina dada. Sospeter, 39, aliacha kazi ya kuajiriwa na kuanzisha duka lake hilo, na anakiri kwamba mwanzoni haikuwa rahisi hata kidogo.

“Nakumbuka wakati naanza nilijaribu vitu kadha wa kadha, nikafeli,” anasimulia Sospeter. “Nikaja kujaribu sasa hivi hiki ninachokifanya, nikafanikiwa. Ukifanya kazi kwa bidii, ukautoa muda wako kwa kile kitu ambacho unakifanya, ukakipenda, thamani utaiona. Lakini pia, kumtanguliza Mungu, siku hadi siku, utaona tu unakua. Ninaona kabisa kuna hatua fulani nimeifanya.”

Kwa Festo Thomas, ambaye kampuni yake hufuga na kuuza mazao ya nyuki, kuishi ni kuwa na uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali, akibainisha kwamba kujiajiri au kuajiriwa siyo kibali cha kutokupaswa kukabiliana na changamoto kwani changamoto ndiyo maisha yenyewe.

SOMA ZAIDI: ACT-Wazalendo: Mikopo ya Asilimia Kumi ya Halmashauri Itolewe Kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii

“Nimejifunza kote kuna changamoto – ukiajiriwa na ukijiajiri,” Thomas, 31, alisema kwa kujiamini. “Wewe unachagua tu uvumilie changamoto zipi. Leo nikiangalia wale wenzagu wenye ajira wana changamoto ambazo mimi nikizitafakari naona nina uafadhali.”

Wajibu wa Serikali

Wakati vijana hawa wanaendelea na harakati zao za kujikomboa wao na familia zao kiuchumi, wanaamini kabisa kwamba Serikali ina jukumu kubwa la kufanya siyo tu katika kuwasaidia wao ambao tayari wameshajiajiri, bali pia wale wanaotamani kufanya hivyo.

Lucas Sospeter, aliyejiajiri kwa kuuza suruali za akina dada, anaamini ukifanya kazi kwa bidii, ukautoa muda wako kwa kile kitu ambacho unakifanya, ukakipenda, thamani utaiona. PICHA | JACKLINE KUWANDA.

Baadhi ya mapendekezo yao ni kwa Serikali kuweka taratibu za uanzishwaji wa kampuni zinazoendana na viwango vya uwekezaji unaofanywa na vijana na ambazo vijana wataziona ni rafiki. 

Ukosoaji mkubwa ambao The Chanzo iliusikia kutoka kwa vijana iliozungumza nao ni kwamba mamlaka za Serikali huwachukulia vijana wanaotaka kujiajiri kama zinavyowachukulia wawekezaji wengine wakubwa.

“Tumekuwa tukikumbwa na changamoto kwenye mamlaka [za Serikali],” Mjirima alisema. “Ukienda kule, wanakuchukulia kama mfanyabiashara mkubwa. Ukikutana na zile gharama na vile vigezo ambavyo vinahitajika, mtu unapata changamoto kufikia lengo lako na unaweza kukata hata tamaa ya kuendelea.”

SOMA ZAIDI: Mfumo Wetu Wa Uchumi Na Dhana Ya Ukosefu Wa Ajira

“Naomba tubadilishe mifumo yetu ya elimu, itoke kwenye nadharia waliyonayo vijana kwamba wakihitimu wanapaswa kuajiriwa,” alishauri Msantu. “Tupewe masomo tofauti katika mifumo ya elimu. Hivyo vitawapa uwanja mpana vijana kuweza kujiajiri katika mambo ambayo wataona yanawafaa.”

Kuhusu suala la mtaji, ambalo vijana wengi wamekuwa wakilitaja kama kikwazo nambari moja kwenye mchakato wao wa kujiajiri, Bryson Kitova, anayejihusisha na kilimo cha umwagiliaji cha mbogamboga, anaamini kwamba wakati Serikali inajukumu la kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata mitaji, vijana wanaweza kuanza kwa kutumia kile kidogo walichonacho.

“Mtaji ni muhimu, lakini pia ni muhimu kutotazama mtaji mkubwa kama ndiyo msingi wa kujiajiri,” Kitova, 35, anashauri. “Unaweza ukajiajiri hata kwa mtaji mdogo halafu ukafanikiwa kupata mtaji mkubwa utakaouwekeza kwenye biashara yako.”


Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. Asante Jackline kwa kuendelea kuandika habari za vijana waliojiajiri. tunaamini Serikali yetu sikivu kupitia viongozi wake wataona Maoni yaliotolewa na vijana hao walio jiajiri kupitia makala hizi na kuyafanyia kazi maoni hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts