The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ado Shaibu: Ninavyomfahamu Richard Mabala, Mwalimu Hodari, Mwanaharakati Machachari

Alikuja Tanzania akidhani atakaa kwa miezi michache tu, akavutiwa kubaki na mpaka kuacha uraia wake wa Uingereza na kuwa Mtanzania kamili.

subscribe to our newsletter!

Makala haya yalichapishwa kwa mara ya kwanza na mwandishi hapo Septemba 1, 2024, kwenye muundo wa uzi katika mtandao wa X, zamani Twitter. The Chanzo inayachapisha tena hapa kwa ruhusa ya mwandishi. Uhariri umefanyika kuimarisha usomaji mzuri:

Leo nimemkumbuka ndugu yangu, Richard Mabala, Mtanzania aliyeacha alama kwenye sekta ya elimu, hasa kupitia kazi zake za ualimu, uandishi na harakati. Miaka kadhaa nyuma nimewahi kuandika makala kuhusu yeye niliyoiita Masuala 10 Usiyoyajua Kuhusu Richard Mabala. Kwenye thread hii nitayachapisha tena kwa muhtasari.

Jambo moja ambalo baadhi ya wasomaji wa vitabu na makala zake wanaweza wasijue kuhusu yeye, hasa kutokana na anavyokimudu Kiswahili kwa uweledi wa hali ya juu, ni kwamba Richard Mabala ni Mzungu. 

Richard Mabala alikuja nchini mwaka 1973 akiwa miongoni mwa wafanyakazi wa kujitolea chini ya mpango wa wafanyakazi wa kujitolea, au Voluntary Service Oversea (VSO). Yeye alikuwa miongoni mwa Waingereza walioendelea kufanya kazi nchini hata pale Tanzania ilipovunja mahusiano yake ya kidiplomasia na Uingereza. 

Chini ya VSO, utaratibu ulikuwa kwamba wafanyakazi kutoka Uingereza walikuwa wanalipwa mshahara uleule waliokuwa wanalipwa wafanyakazi wa Tanzania. Mabala, ambaye amewahi kufanya kazi kwa muda mrefu mkoani Tabora, hupenda kujiita kwa jina la utani la ‘Mnyamwezi Mkorogo.’

Kuwa ‘Mabala’

Alipofika Tanzania, Richard Mabala anasema jina lake la asili lilikuwa ni Richard Satterthwaite, ambalo ndilo jina lake tokea kwao. Kutokana na kuwawia vigumu wenyeji kulitamka jina hilo, aliamua kubadili jina na kujiita Mabala. Jina hilo Mabala limetoka wapi? Mwenyewe anasema:

SOMA ZAIDI: Richard Mabala: Je, Kupata Nafasi ya Shule Ni Kupata Nafasi ya Elimu?

“Nilijiunga na kwaya ya Ipuli kule Tabora, mwishoni, na baada ya kuzoeana, wanakwaya wenzangu walisema kuwa hawawezi kulitamka jina langu na kwamba watanipa la kwao; Mabala. Nilipowauliza lina maana gani wakasema [ni] ‘eneo kubwa la nje,’ kutoka Uingereza hadi Tabora. 

“Kwa kweli nilianza kulitumia jina hili kwa wasiwasi kidogo, nikiona watu wanaweza kuniona najitia kimbelembele, kulia kuliko mfiwa, lakini kila mtu akalipenda. Kwa hiyo, baada ya kunogewa na kupata uraia [wa Tanzania], nikaliongeza na kuwa jina rasmi.”

Baada ya kuvutiwa na Tanzania, Mabala alikata shauri kuwa raia kamili wa nchi hii adhwimu. Harakati zake za kusaka uraia alizianza rasmi mwaka 1979 ambapo Richard Mabala alipeleka maombi ya uraia kwa mamlaka zinazohusika na hilo, maombi yake hayo yakaridhiwa miaka miwili baadaye na akawa Mtanzania kamili. 

Mabala anasema kuwa hajawahi kamwe kujutia uamuzi wake wa kubadili uraia licha ya kulazimika kupitia mlolongo mrefu wa kuomba viza kila anapotaka kwenda kumjulia hali mama yake mzazi aliyeko Uingereza. Mabala anasema kamwe rangi yake haijawahi kuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli zake mbalimbali hapa nchini.

Mwalimu hodari

Kwa vipindi tofauti, Mabala amefundisha kwenye shule na vyuo mbalimbali nchini. Baadhi ya shule na vyuo alivyofundisha ni Mirambo, Mzumbe, Korogwe, vyuo vya ualimu Chang’ombe na Marangu. Pia, amewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1973 na 1993. 

Mabala analikumbuka zaidi darasa lake la kwanza la Shule ya Sekondari ya Wavulana Mirambo ambalo lilikuwa na wanafunzi ambao sasa ni wanasiasa na wanazuoni nguli. 

SOMA ZAIDI: Vijana wa Siku Hizi ni Zao la Wazee wa Siku Hizi. Tuwe na Akiba ya Maneno Tunapowasimanga

Baadhi yao ni marehemu Profesa Jwani Mwaikusa, aliyekuwa mwanazuoni wa sheria aliyebobea na kuhudumu kama wakili katika Mahakama ya Kimataifa Maalum ya Mashtaka ya Jinai juu ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), iliyoko Arusha; Profesa Abdallah Njozi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro na mwanafasihi mbobezi wa lugha ya Kiingereza; na Dk Harrison Mwakyembe, aliyewahi kuhudumu kama waziri kwa nyakati tofauti.

Baada ya Uhuru, uchapishaji wa vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili ulishika kasi. Uchapishaji wa vitabu kwa lugha ya Kiingereza, hasa vile vya fasihi vilivyoandikwa na waandishi wa Kitanzania ulidorora. 

Kitabu cha Summons: Poems from Tanzania, kilikuwa kati ya diwani za mwanzo kabisa za ushairi wa Kiingereza kuchapishwa nchini baada ya Uhuru. Kazi hii ambayo inajumuisha mashairi ya waandishi mbalimbali wa Kitanzania kama vile Kajubi Mukajanga, Isaac Mruma, Kundi Faraja, Jwani Mwaikusa na Mabala mwenyewe ilikuwa ni zao la ushirikiano wa Mabala na waliokuwa wanafunzi wake wa sekondari. 

Mabala anasema kuwa wanafunzi wake walikuwa wakimpatia changamoto ya kuandika kazi zake mwenyewe badala ya kuishia kuchambua na kuzikosoa kazi za wengine. Mabala anasema: 

“Kajubi Mukajanga [ambaye ni Katibu Mtendaji mstaafu wa Baraza la Habari Tanzania – MCT] ndiye aliyenishawishi kuandika mashairi wakati yeye alikuwa mwanafunzi na mimi nilikuwa mwalimu wake. Eti kazi yangu ilikuwa kukosoa wengine kwa nini na mimi nisiandike ili nao wapate nafasi ya kunikosoa?” 

Mabala aliifanyia kazi rai ya wanafunzi wake na kuandika mashairi na vitabu vingine vya hadithi!

Mwanaharakati machachari

Baada ya miaka mingi ya ualimu, Mabala aliamua kujikita kwenye harakati, akishiriki kikamilifu kwenye shughuli za Asasi za Kiraia (AZAKI). Yeye ni miongoni mwa wanachama waanzilishi wa AZAKI maarufu kama vile HakiElimu na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), na mwishowe, kwa kushirikiana na vijana, akaanzisha asasi ya TAMASHA yenye makao makuu jijini Arusha. Mabala anasema: 

SOMA ZAIDI: Shule, Vyuo Vikuu Viwaelimishe Wanafunzi Badala ya Kuwatahinisha

“Nillifundisha Mirambo, Mzumbe, Chang’ombe TTC, Marangu TTC, Kibosho Girls na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kisha nikatambua kwamba mimi ni mwanaharakati kuliko mwanataaluma, ndiyo maana nikaingia AZAKI kwa lengo la kuwawezesha vijana. Nimeanzisha TAMASHA [Taasisi ya Maendeleo Shirikishi], tukihimiza vijana wapate nafasi yao katika jamii.”

Kati ya mwaka 1999 hadi 2007, Mabala alifanya kazi kwenye shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwenye programu ya kuwakomboa vijana wasio shuleni. Mabala alifanya kazi na UNICEF kama mwandishi wa mfululizo wa vitabu vya sera ambavyo vilitafsiriwa kwa Kiswahili. 

Vitabu vilivyowahi kutolewa katika mfululizo huo ni pamoja na The Special Gift au Zawadi Maalum; Daughter of Lioness au Binti Simba; The Empty Compound, na Who is the Thief?

Vitabu vingi vya Mabala vinahusu watoto na vijana. Mabala anasema kuwa watoto ni kundi lililosahauliwa na kwamba kamwe haiwezekani kujenga utamaduni wa kupenda kujisomea vitabu kama jitihada hazielekezwi kwa watoto wadogo; anaamini kwamba watoto hawawezi kuwa na ari ya kupenda kujisomea wakiwa ukubwani.

Mdau wa Kiswahili

Licha ya kuwa kazi zake nyingi zimeandikwa kwa Kiingereza, Mabala ni miongoni mwa watu wanaopigia chapuo kutumika kwa Kiswahili kama lugha ya kufundishia tangu shule ya msingi hadi chuo kikuu. Mabala anasema: 

“Kama mwalimu, moyo unaumia sana kuingia darasani siku ambayo wanafunzi wamebahatika kupata mwalimu na kukuta sura zilizofadhaika maana hawaelewi wanachofundishwa. 

SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiasi Gani Mitaala Yetu Inawawezesha Wanafunzi Kutafakari?

“Au fanya jaribio la kufundisha kwa Kiingereza lakini uwape kazi ya kujadili katika vikundi. Angalia watakavyochangamkia mada na kujadili kwa kina kwa Kiswahili, lakini huku wakitumia neno la Kiingereza hapa na pale, hasa ya istilahi na wataelewana vizuri sana.” 

Mabala anaongeza juu ya hayo kwa kusema:

“Msingi wa elimu ni ubunifu na uelewa, ndiyo maana nchi nyingi sana duniani wanahakikisha kwamba wanafundisha watoto wao kwa lugha wanayoielewa. Waholanzi, Waswidi na wengineo wana uwezo wa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, lakini hawafanyi hivyo maana wanajua kwamba msingi wa elimu na ubunifu, ni uelewa. Na wanajua pia kwamba mara nyingi wanasayansi ndiyo wabovu kabisa katika kujifunza lugha.” 

Kisha anaendelea kusema kuwa: 

“Iwapo tunatengeneza mazingira yanayofaa watoto wetu wanaweza kujua Kiingereza vizuri sana pamoja na kuwa na uelewa wa mambo yote muhimu katika elimu. Mimi nilikuwa sijui Kihispania kabisa, lakini kwa muda wa miaka miwili tu, ndani ya shule tu, niliweza kupata ‘B’ katika A Level. Kwa sababu ya ufundishaji vizuri, mipango makini na pia juhudi yangu. Kwa hiyo, hakuna linaloshindikana. Elimu kwanza si lugha kwanza.”

Mabala anasema wingi wa shughuli za Asasi za Kiraia na zile za uandishi kamwe haujawahi kumletea matatizo kwenye familia kwa sababu mkewe anamuunga mkono kwenye kazi zake. Anasema kwa utani:

“Mke wangu ni muelewa sana kwa sababu kazi zangu za kuandika nazifanya kati ya saa tisa usiku na saa kumi na mbili asubuhi. Ananiunga mkono sana isipokuwa pale kitanda kinapokuwa cha baridi sana.”
Ado Shaibu ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo. Unaweza kumpata kupitia adoado75@hotmail.com au X kama @AdoShaibu. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ado Shaibu nimesoma makala ya Richard Mabala huyo mzungu mimi na mfahamu tumekuwa tukihudhuria vikao hapo Unicef enzi hizo nikiwa wizara ya Afya. Nina machapisho kama 120 ya makala za kiswahili kuhusu Afya. Natafuta kampuni ambayo inaweza kuchapisha makala hizo katika mfumo wa kitabu au series of books. Utanisaidia au utanielkeza nini kifanyike.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *