Mbeya. Mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa skimu ya Mbulu Mlowo uliopo kata ya Mahenje, wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe upo hatarini kutoweka kutokana na maji ya mto Mlowo kubomoa kuta za kingo kwenye mfereji wa umwagiliaji, hali iliyowapelekea wakulima wanaoutegemea mradi huo kuomba msaada kwa Serikali ili kunusuru shughuli za kilimo zilizokuwa zikifanyika hapo.
Kwa sasa wakulima takribani 160 wamelazimika kusitisha shughuli zote za kilimo zinazohusisha uzalishaji wa mahindi, viazi mviringo, matunda, mbogamboga pamoja na karoti. Uzalishaji ambao huanza majira ya kiangazi, kuanzia mwezi Julai mpaka mwezi Oktoba kabla ya mvua za masika kuanza kunyesha.
Stephano Mwashambwa ni mmoja kati ya wakulima ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilima kwenye skimu hiyo. Mwashambwa, 52, ameiambia The Chanzo kuwa hali imekuwa mbaya sana kwao kwa mwaka huu, kwani hawajafanikiwa kulima zao lolote hali inayowalazimu kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kufuata mahitaji ya kula.
“Mwaka huu hatuna namna, mpaka mboga za majani tunafuata Mlowo ambapo ni kilomita tisa kutoka hapa,” Mwashambwa anaeleza. “Tulikuwa hatuhangaiki kununua vitu lakini sasa hivi tunahangaika, hali ya maisha imezorota ndiyo maana nasema uchumi umeshuka. Wakina mama walikuwa hata hawatuombi hela maana walikuwa wanajishughulisha na kilimo.”
SOMA ZAIDI: Uchambuzi: Bajeti ya Wizara ya Kilimo 2024/25 Inaakisi Umuhimu wa Sekta ya Kilimo?
“Kiukweli kilimo cha umwagiliaji kilikuwa kinatusaidia sana ndiyo maana natoa wito kwa Serikali kwamba wanapokuwa wanatoa miradi sehemu nyingine na sisi huku watukumbuke. Kitendo cha kufa kwa mradi huu kimetuathiri sehemu kubwa sana, tunaomba na sisi watukumbuke,” Mwashambwa anaiambia The Chanzo kwenye mazungumzo yaliyofanyika kwenye shamba lililopo karibu na maeneo ya umwagiliaji.
The Chanzo ilifika kwenye maeneo hayo ya skimu ya umwagiliaji Oktoba 9, 2024, siku ambayo kulikuwa na ziara ya Serikali iliyolenga kuukagua mradi huo, na kushuhudia jinsi ambavyo mto huo ulivyohama na kubomoa kingo za skimu kisha kurudi katika njia yake ya asili. Lakini pia, mazao yaliyopandwa kama vile viazi pamoja na mbogamboga yalionekana kukauka kwa kukosa maji kwani kipindi hiki ni cha kiangazi na maji hayapo tena kwenye eneo hilo.
Yusufu Asajile naye ni mkulima anayemiliki mashamba kwenye skimu hiyo aliimbia The Chanzo kuwa uzalishaji umepungua sana, kwa wale wanaofanya kilimo cha mbogamboga waliofanikiwa ni wachache sana, nao ni wale waliokuwa na mashine za kuchota maji.
“Lakini tunaotegemea skimu imekuwa ngumu, na wengi waliopanda viazi wameshindwa kumwagilia kutokana na hali hiyo inawezekana hata mbegu wasipate,” amesema Asajile.
SOMA ZAIDI: Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania
Asajile, 40, akionekana kuwa katika hali ya unyonge sana anaendelea kusema “naiomba Serikali itutazame kwa jicho la pili kwa kuturejeshea hali kama ilikuwa kuwa hapo awali. Kwa maana hii skimu ndiyo tunayotegemea kwa mahitaji ya watoto wetu kama vile kuwasomesha, na hata kuendeleza maisha yetu.”
Skimu ya umwagiliaji ya Mbulu Mlowo yenye ukubwa wa takribani hekari 50 ilianzishwa na Serikali mwaka 2002, lengo likiwa ni kuukwamua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, ambapo mwaka 2007 Serikali ilikamilisha ujenzi wa tuta lenye urefu wa mita 150 na kufukia korongo lililokuwa mita za ujazo 1,200.
Skimu hii inategemewa na vijiji vya Mlowo, Mahenge, Nasama, Iyenga, Isansa, Sambewe, Itumbi pamoja na Mpitu, kipindi cha kiangazi wafanyabiashara wadogo wadogo huenda kwenye mashamba ya skimu hiyo kwa ajili ya kununua mazao mbalimbali ambayo baadaye wanakwenda kuyauza na kujipatia kipato.
Hatujui kama watafanyia kazi
Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji ya Mbulu Mlowo, Zawadi Mgala, ameeleza kwamba tatizo la kuta za maji kubomolewa na mto huo lilianza tangu mwaka 2021 na toka kipindi hicho walikuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuzia maji lakini ilipofika mwaka jana hali ikawa mbaya zaidi.
Jitihada hizo ni pamoja na kujaza matope kwenye eneo lililobomolewa lakini kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda tatizo limezidi kuwa kubwa kiasi cha kushindwa kuzuia.
“Na wewe kwa macho yako umeshuhudia hii mifuko tumeweka,” Mgala alimueleza mwandishi huku akimuonyesha baadhi ya mifuko iliyokuwa imewekwa kwenye eneo hilo. “Kwamba tulikuwa tunataka tutandike tupate angalau kuziba ili tuweze kunusuru maji labda yaingie kwenye mfereji lakini imeshindikana.”
Mgala anaendelea kusema: “kwa upande wa uongozi tumefika mpaka kwenye kata, mpaka wilayani, wakawa wanatuahidi tunakuja, tunakuja, lakini leo na wewe umeona kwa macho yako mhandisi amekuja na wataalamu wake ili kuangalia hali halisi, kwa hiyo wamelichukua lakini hatuelewi kama watalifanyia kazi.”
SOMA ZAIDI: Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara
Alipoulizwa Mhandisi wa kilimo cha umwagiliaji mkoa wa Songwe, John Chacha, kwamba wanapanga kuchukua hatua zipi kuhakikisha mradi huo unarejea kwenye hali nzuri, Chacha akaeleza kuwa tatizo hilo wameshaliona na kwa sasa kitakachofanyika ni wao kukaa mezani kuona ni kwa namna gani watejenga eneo hilo ili shughuli za kilimo zirejee kama ilivyokuwa awali.
“Tumeona uharibifu tunaenda kuandika ripoti zetu na kuripoti katika ngazi za juu zaidi ya sisi kwa ajili ya kuangalia namna ya kufanya ukarabati wa maeneo haya. Lakini pia, tunaangalia ni kwa namna gani tutaweza kuwapa elimu wakulima wa eneo hili ili wajue ni kwa namna gani wataweza kupambana na majanga kama haya. ”
“Wito wangu kwa wananchi na wakulima wa skimu hii ni kwamba pale ambapo tutakuja kukarabati skimu yetu wajue wana wajibu wa kuchanga fedha, halafu watatakiwa wajifunze ili endapo hali hii itajitokeza tena wajue namna ya kukabiliana nayo,” Chacha anamalizia kusema.
Modesta Mwambene ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mbeya. Anapatikana kupitia mwambemo@gmail.com