The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ongezeko la Wafungwa Waliotoka Gerezani Kurudia Makosa, Serikali na Jamii Zanyooshewa Vidole

Kwa mwaka 2022 pekee wafungwa 3,262, walirudia makosa baada ya kutoka gerezani, wengi wao wakiwa ni walioachiwa huru baada ya kutumikia vifungo vifupi.

subscribe to our newsletter!

Kuongezeka kwa idadi ya wafungwa wanaorudia makosa na kurejea magerezani kumewalazimu wadau mbalimbali kutoa wito kwa Serikali kuboresha miundombinu ya Jeshi la mMagereza. Wadau hawa wanasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa wafungwa wanaotoka magerezani wanarejea katika jamii wakiwa na tabia njema na wenye tija, ili kuepuka kutamani kufanya makosa tena.

Wadau hao pia wanapendekeza Jeshi la Magereza liunde mfumo maalumu wa urejevu ambao utatoa mwongozo bora kwa wafungwa, hususan wale waliofanya makosa madogo. Mfumo huu unalenga kuwafanya wafungwa kuwa watu bora zaidi na wenye manufaa kwa jamii.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa Machi, 2023, ongezeko la wafungwa wanaorudia makosa ni kwa wastani wa asilimia 1.5 kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, licha ya kuwepo mipango mbalimbali ya urekebu.

Kati ya mwaka 2019 na 2023, asilimia 59.22 ya wafungwa waliorudia makosa walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha chini ya mwaka mmoja; asilimia 24.65 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitatu.

Ripoti inaonyesha kuwa kiwango cha kurudia makosa kilikuwa hakiendani na muda wa wafungwa gerezani kwani kwa mwaka 2023 pekee, wafungwa 3,262, walirudia makosa baada ya kutoka gerezani, wengi wao wakiwa ni walioachiwa huru baada ya kutumikia vifungo vifupi ikiwa ni ongezeko la wafungwa 10 ukilinganisha na mwaka 2022.

SOMA ZAIDI: Magereza Walivyomuachia Majonzi Mteja Wangu ‘Rasta’ kwa Kumnyoa Nywele Zake

Ripoti hiyo inaonyesha hali hiyo inasababishwa na ukosefu wa mitaala na miongozo ya magereza kwa ajili ya uendelezaji rasmi wa mipango ya urekebu; uainishaji na utengano wa wafungwa kujikita kwenye jinsia na umri pekee; miundombinu isiyotosheleza ya uainishaji; shughuli za msingi za gereza kuamua uainishaji; na ukosefu wa sera na miongozo ya uainishaji wa wafungwa.

Katika mahojiano aliyofanya na The Chanzo, Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Uwazi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Fulgence Massawe ameimbia The Chanzo kuwa mfumo mpya wa magereza unatakiwa kutekelezwa sasa kwani magereza ya Tanzania yanatumia mfumo wa zamani na ambao hauendani na lengo mahsusi la kubadilisha tabia kwa wafungwa.

“Mifumo ya yetu ya majeshi hasa magereza ni ya kikoloni mno, badala ya kumsaidia mtu unaenda kumharibu kule,” anasema Massawe, “kwa mifumo yetu hata kama mtu ana tabia njema, akishakaa kule ndani lazima taharibika tu.” 

“Mtu anarudi uraiani akiwa hajabadilika na wakati mwingine, anakuwa mbaya zaidi kwa sababu kule anakutana na mazingira yanayomfanya kuwa jasiri na siyo muoga tena.” Massawe aliongeza.

Chombo hiki cha Magereza kina historia ndefu nchini Tanzania tangu wakati wa ukoloni.

Dhumuni la kuanzisha magereza wakati wa ukoloni lilikuwa ni kudhibiti na kuadhibu watu waliokuwa wakipinga utawala wa kikoloni. 

SOMA ZAIDI: Rasimu ya Warioba Ina Majibu Yote Samia Anayahitaji Kuhusu Mfumo wa Haki Jinai

Magereza haya yalitumiwa kama chombo cha kuendeleza utawala wa kikoloni kwa kuhakikisha kuwa wale waliokosa kutii sheria au kupinga utawala wanatiishwa na kuondolewa kwenye jamii kwa kuwekwa kizuizini ili kuwatesa na kuwatisha wale waliobaki ili kutii mamlaka za kikoloni.

Aidha yalitumika kuwashikilia na kuwaadhibu wapinzani wa kisiasa wa utawala wa kikoloni, ikiwa ni pamoja na viongozi wa harakati za kupigania uhuru na haki za binadamu. Wafungwa wengi walilazimishwa kufanya kazi ngumu, kama vile ujenzi wa miundombinu, kilimo, na kazi zingine za kijamii ambazo zilinufaisha Serikali ya kikoloni bila kuangalia ustawi wa mfungwa.

Juma Kibela ni askari mstaafu wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania, ametumikia magereza mbalimbali nchini ikiwemo Gereza Kuu la Butimba lilipo Mwanza na lile la Kasulu mkoani Kigoma. Katika mahojiano yake na The Chanzo ameeleza kuwa uanishaji wa wafungwa katika magereza ya Tanzania ni changamoto.

“Tatizo ni kwamba wafungwa wanachanganywa, magereza zetu hazina utaratibu wa kutenga wafungwa zaidi ya kutenga watu kwa jinsia na umri pekee yake,” aliiambia The Chanzo.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?

“Ilitakiwa watu watengwe kulingana na makosa yao, huwezi kumweka mwizi wa kuku pamoja na jambazi aliyetumia silaha, hapo ndipo shida ilipo,” anasisitiza Kibela, “lazima huyu atajiona yeye bado hivyo ataenda kupambana kufanya uhalifu mwingine tena mkubwa zaidi ili aonekane naye anaweza.”

Hoja ya Kibela inaendana na taarifa ya  CAG ambaye alibaini kuwa suala uainishaji wa wafungwa katika magereza saba aliyotembelea unajikita zaidi kwenye jinsia na umri pekee, masuala mengine kama asili ya kosa, historia ya uhalifu na umuhimu wa urekebishaji hayazingatiwi na hii ni kukosekana kwa miundombinu stahiki.

Kibela anafafanua kuwa iwapo magereza yakiboreshwa, kujipanga kuwa na mitaala mizuri ya urekebu, kuwepo kwa utengenisho unaofaa na jamii nzima ikaeleweshwa namna ya kuwapokea wafungwa waliomaliza vifungo vyao, basi tusingekuwa ama tungekuwa na wafungwa wachache sana wanaorudia makosa.

Katika barua iliyosainiwa na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza DCP Luhende D. M. Makwaia aliieleza The Chanzo kuwa miundombinu isiyo Rafiki pamoja na uhaba wa rasilimali fedha ili kuweza kutimiza programu mbalimbali zinazofaa kwa ajili ya urekebu mfano viwanda vidogovidogo ni moja ya changamoto inayolikabili Jeshi hilo kuweza kuhakikisha program za urekebu zinafanikiwa. Aidha anaeleza kuwa kujengwa magereza bora na ya kisasa ambayo yataendana na falsafa ya urekebu yatasaidia kufikia lengo.

Kwa upande wake Bi. Tumaini Rwela, mwanasosholojia, mkufunzi, na mtafiti kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, jijini Dodoma anafafanua kuwa kwa hali ilivyo kwa sasa, kama taifa tunahitaji juhudi za pamoja kukabiliana na suala hili kwani linaongezeka kila kukicha.

SOMA ZAIDI: Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki

“Kwa tafiti ambazo nimefanya, mtiririko unaonyesha kuwa tatizo linaongezeka, hivyo kwa kutumia mtririko huo unaweza kusema kila mwaka watakuwa wanaongezeka,” alisema Rwela katika mahojiano yake na The Chanzo.

“Na tatizo linasababishwa na mambo mengi, jamii inahusika, Serikali, mifumo ya magereza, sera na wafungwa wenyewe, mambo ni mengi kiasi hicho,” anasema.

Aidha Rwela anaeleza kuwa Tanzania inahitaji kujifunza kutoka kwa mataifa mengine kama Uganda ambao wana asilimia 32 pekee ya wanaorudia vifungo. Anaeleza kuwa mbinu zinazotumiwa na mataifa mengine zitaweza kusaidia kwa namna moja ama nyingine ili kuhakikisha kuwa suala hili linapungua ama kuisha kabisa nchini.

“Tafiti nyingi zaidi zinatakiwa, bado kuna maeneo mengi ya kugusa, mengi mno na hakuna tafiti zilizofanywa juu yake. Hivyo tukifanya tafiti nyingi zaidi tutagusa maeneo tofauti tofauti na kuweka mazingira ya jamii zetu kufahamu kwa kina suala hili lipoje.” alifafanua Rwela.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Mipango ya Maendeleo ya Vijijini mwaka 2023, unarejea kuwa Kenya na Tanzania ni moja ya nchi zenye kiwango kikubwa cha wafungwa wanaorudia uhalifu barani afrika zikiwa na asilimia 47 kila moja zikizidiwa na Zambia na Rwanda ambapo hizi zina asilimia 33% na 36% mtawalia,

Utafiti huu unaonyesha kuwa kulikuwa na wafungwa 3,239, 3,384, 3,235, na 4,001 waliorudi magerezani kwa kurudia uhalifu kwa mwaka 2019, 2020, 2021, na 2022, mtawalia. Wengi wa wahalifu wanaojirudia walikuwa vijana tena ambao hawajaoa, kwani hutamani kupata maisha mazuri kupitia njia haramu kitu ambacho huwafanya kurudia uhalifu na hatimaye kurudishwa magerezani. Aidha wengi wao wanatajwa kuwa wana uelewa mdogo; kwa hivyo, polisi wanapata nafasi ya kuwabambikia kesi.

Utafiti ulifanywa katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam nchini Tanzania huku ukilienga Makao Makuu ya Magereza ya Tanzania (Dodoma), gereza la Isanga na gereza la Ukonga (Dar es Salaam) kwa sababu yana wafungwa wengi zaidi kuliko magereza mengine hapa Tanzania. Idadi ya washiriki katika utafiti huu ilikuwa 114, ikijumuisha wafungwa waliourudia makosa na wale wa mara ya kwanza pamoja na maafisa wa jeshi hilo.

SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Kesi Mahakamani Unavyokwamisha Upatikanaji wa Haki

Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa wafungwa wengi wanaorudia vifungo ni wale ambao hawana ajira huku kukiwa na idadi ndogo sana ya wafungwa wenye ajira kurudia uhalifu. Inaripotiwa kuwa kutokuwa na ajira kunaweza kuchangia mtu kujihusisha na shughuli za uhalifu ambazo zinaweza kusababisha kufungwa.

Aidha utafiti huu pia umebaini kwamba wafungwa waliotenda uhalifu mdogo kama vile kuzurura hovyo, wizi, na kujeruhi kwa makusudi ndiyo wanaohukumiwa na vifungo vifupi na hivyo uwezekano wa kufanya makosa tena ni mkubwa kwa sababu shughuli za kuwarekebisha wahalifu wa kipindi kifupi hazitolewi ama hawajihusishi kikamilifu na shughuli za urekebu.

Hoja hii pia inaelezwa na Massawe wa LHRC kuwa ukosefu wa fursa na ajira umekuwa na mchango kwa kiasi fulani kwa wafungwa kurudia makosa yao kwani wanapokuwa wakirudi uraiani wanakutana na maisha magumu yanayowafanya kutamani kurudi magerezani mahali ambapo wanaamini wanakula bure.

Aidha ameeleza kuwa jamii nyingi huwanyanyapaa na kuwatenga watu waliotoka gerezani na hii husababisha wao kutamani kurudi gerezani.

Utafiti unaonyesha kuwa Asilimia 65.9 ya washiriki wameeleza suala la bejeti finyu huzuia kufanya shughuli za urekebu. 

“Shughuli nyingi za urekebu zinahitaji pesa, hivyo bajeti iliyotengwa kwa ajili ya huduma ya urekebu wa wa wafungwa hairidhishi ikilinganishwa na idadi kubwa ya wafungwa” inaeleza ripoti hiyo.

Pia ilibainishwa kwamba kuna uhaba wa rasilimali watu wenye ujuzi katika eneo la urekebu. Maafisa wa jeshi la magereza walifafanua kuwa mtaala ambao haujakamilika pamoja na kukosa masomo kwa vitendo inachangia kutofanikiwa kuwarekebisha tabia wafungwa. 

Mmoja wa washiriki alisema: “Kukosa ufanisi katika utoaji wa shughuli za kurekebisha kunasababishwa na ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi wa kufanya urekebu kwa wafungwa kwa viwango vya kimataifa. Wengi wetu tuna maarifa ya awali tu kuhusiana na urekebishaji kwa mfano, hapa kuna wafanyakazi sita tu wenye vyeti vya sayansi ya urekebishaji kutoka chuo cha taaluma ya urekebishaji Tanzania; wengine, zaidi ya mia moja, wanatumia tu uzoefu wao.”

SOMA ZAIDI: Rais Samia Ataka Kuimarishwa Kwa Mfumo wa Haki Jinai na Madai Nchin

Akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya kozi ya sayansi ya urekebishaji katika chuo cha taaluma ya urekebishaji Tanzania, Disemba 01, 2023 jijini Dar es Salaam Waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alinukuliwa akisema kuna changamoto ya waliokuwa wafungwa kurudi kwenye uhalifu baada ya kumaliza adhabu zao na kusababisha uhalifu kurejea uraiani sambamba na kuwepo kwa idadi kubwa ya wahalifu mitaani.

“Katika jeshi letu la magereza, bado kuna changamoto tunayoendelea kupambana nayo, ni suala zima la urekebu na hii inadhihirishwa na ukweli kwamba hata baadhi ya wafungwa wanaotoka magerezani wakiingia mitaani, wengine hurudia uhalifu” alisema Masauni.

Jambo hili linaungwa mkono na Jeshi la Magereza nchini na kufafanua kuwa tatizo hili lina athari kwa jamii ikiwemo, Jamii kukosa imani kwa serikali yao pamoja na Jeshi la Magereza kwa kuonekana kuwa limeshindwa kutimiza wajibu wake. 

Katika barua ya Jeshi la Magereza kwa The Chanzo kuwa fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya jamii zinatumika kuwalisha wafungwa, mavazi pamoja na matibabu yao badala ya kufanyia shughuli za maendeleo.

Barua hiyo imefafanua kuwa Sera ya utoaji adhabu, miundo mbinu isiyo rafiki pamoja na uhaba wa rasilimali fedha, msongamano wa wafungwa magerezani ambapo hukwamisha zoezi la uainisho na utenganisho kwa wafungwa ndio changamoto kubwa zinazolikabili jeshi hilo na kushindwa kufanya shughuli za urekebu kwa ufanisi.

“Kufanyike marekebisho ya Sheria pamoja na Kanuni zake kuhusiana na suala zima la urekebu ili kuendana na falsafa ya urekebu, pia kuboresha mitaala na mafunzo kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza ili kuendana na falsafa ya urekebu. Jeshi la Magereza litengeneze mifumo ya kushirikiana na jamii mfano kuwa na mfumo wa Magereza na jamii ili kufanya jamii kujua magereza inawajibu gani na jamii pia” inasomeka barua hiyo.

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts