Siku ya Ijumaa, Novemba 29, 2024, siku mbili baada ya kuhitimishwa kwa zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, niliwahutubia wananchi wa Ujiji, Kigoma Mjini, mkoani Kigoma, nikitahadharisha madhara ya kuruhusu vyombo vya dola kuingilia michakato ya kidemokrasia. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo niliyoitoa kwenye viwanja vya Kawawa:
Wananchi wa Ujiji, wananchi wa Kigoma, umati huu wa watu ambao mmekusanyika leo katika uwanja huu wa Kawawa ni ishara dhahiri sisi ndiyo washindi kwenye uchaguzi huu uliomalizika wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Kama [chama tawala, Chama cha Mapinduzi] CCM wanaamini wao kuwa ni washindi waje wathubutu kutujibu kwa mkutano kama huu hapa Kawawa.
Sisi ndiyo wenye mjii huu, na leo tumewaonesha kwamba sisi ndiyo wenye mji huu. Mtu aliyeshindwa hawezi kuwa na furaha hii tuliyonayo; mtu aliyeshindwa hawezi kukusanyika hapa kufanya mkutano kama huu ambao tunaoufanya.
Watu wa Kigoma Mjini, napenda kuwashukuru sana kwa kazi kubwa ambayo mliifanya kwa nidhamu kubwa, na kwa ushiriki mzuri kabisa wa uchaguzi ambao umekwisha. Nataka niwapongeze wagombea wetu wote, wale ambao walifanikiwa kuwa kwenye karatasi za kura na hata wale walioenguliwa kwa kuonewa na watendaji ambao wanaipendelea CCM.
Wote nawapongeza sana kwa kazi kubwa mliyofanya kwenye kampeni, kujenga hoja, kuelezea sera zetu na ilani yetu. Mungu awabariki, na nyinyi ndiyo washindi halali wa mitaa yenu mliyogombea.
Inawezekana kwamba waliotangazwa kushinda wakakalia viti kwenye ofisi zetu za Serikali za Mitaa, lakini hawana watu, wenye watu ni sisi. Na sisi tutawaongoza watu kwa namna tunayotaka sisi. Hatutatii Mwenyekiti yoyote ambaye hakuchaguliwa na watu, akatangazwa na tume ya uchaguzi.
Tunawaambia watu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kuanzia leo hii msitoe ushirikiano wowote kwa Mwenyekiti yoyote wa Mtaa ambaye amejipachika, hakuchaguliwa na amewekwa pale kwa nguvu ya kura za bandia.
SOMA ZAIDI: Dorothy Semu: Kwa nini ACT-Wazalendo Tumeandaa Ilani ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa?
Tunatangaza kuwasusia ofisi zao, tunatangaza kutowapa ushirikiano, tunatangaza kutokushiriki kwenye shughuli zao zozote mpaka uchaguzi utakaofanyika upya chini ya tume mpya ya uchaguzi, chini ya sheria mpya ya uchaguzi, ili tuweze kuchagua watu ambao wananchi wanawataka na sio kuchagua watu ambao wanawekwa na vyombo vya dola.
Kura za bandia
Nyinyi ni mashuhuda, mlishuhudia kura za bandia zilivyozagaa mitaani. Unakuta kura ya bandia anayo mgombea wa CCM, anayo balozi wa nyumba 10 wa CCM hata masanduku ya kura hayajafunguliwa. Uchaguzi umepoteza maana kabisa, uchaguzi haukuwa na credibility yoyote.
Unawezaje kuwa na uchaguzi ambapo maafisa wa Halmashauri na maafisa wa Manispaa wanatoa kura za bandia wanawapa watu waingize kwenye masanduku ya kura? Uchaguzi wa namna gani huu? Utumishi gani wa umma huu ambao unapoteza maana kabisa ya kura?
Tumefanya chaguzi nyingi sana kwenye nchi hii, katika jambo ambalo halikuwahi kutokea ni kuona kura barabarani. Tumeanza kuona kura bandia mwaka 2020, tukadhani kwamba chini ya Serikali ya awamu ya sita angalau tutarudi kwenye mazingira yale tuliyokuwa nayo kabla, lakini na wao ni yaleyale ya 2020. Aibu kubwa, unawezaje kuwa na kura za bandia mtaani?
Tumekamata watu wengi sana, vijana wamefanya kazi nzuri sana, tuliweza kudhibiti vizuri sana, kura nyingi zimekamatwa mtaani. Kuna kijana mmoja mtaa pale Tanganyika kanionesha amekamata kura 400, mtu mmoja kwenye mtaa mmoja!
Kule Mwandiga mliona video imezagaa mtu amekamatwa, ni mgombea, na kura 800 peke yake, watu wenyewe wamejiandikisha kwenye mtaa wake hawafiki 250. Na ndiyo maana vituo vingi wametangaza matokeo idadi ya wapiga kura na matokeo waliyotangaza idadi ya kura walizowapa CCM haviingiliani kabisa kwa sababu ya kura bandia
Kuna kijana wetu mmoja wa Mtaa wa Mji Mwema anaitwa Jerome, watu wa CCM walimteka halafu wakawapelekea polisi, polisi wakampiga sana yule kijana, wakamkanyaga kanyaga mgongoni anaumwa sana sasa hivi huyo kijana. Analazimishwa eti aseme ni ACT Wazalendo ilimpa kura bandia.
Kura zenyewe zimewekewa tiki ya CCM, sasa mtu wa ACT Wazalendo atakuwaje na kura za bandia ambazo zina tiki ya CCM? Na wanaoshiriki vitendo hivi ni askari wetu. Watu wa polisi ambao wanaishi kwa kodi zetu, wanavalishwa kwa kodi zetu, wanafanya kila kitu kwa kodi zetu, wanashiriki kipumbavu kabisa katika kunajisi mchakato wa uchaguzi.
Polisi kushiriki uhalifu
Afisa wa polisi ana nyota tatu amefika kwenye kituo ameweka kura za bandia mfukoni na kwenye soksi, sasa sijui ni yule ngamia, kura zikamwagika ndani ya kituo. Mgombea wetu pale akamkamata yule polisi, wakazingira kituo mpaka Mkurugenzi na OCD wakafika pale.
Mgombea wetu yule akavuruga yale masanduku ya kura kwa sababu tayari yameshanajisiwa. Jana usiku polisi wamevamia nyumbani kwa yule kijana wetu wameenda, wamevunja vyombo, wamefanya kila kitu, WAPUMBAVU HAWANA AIBU POLISI HAWA.
Nilitegemea kuona yule inspekta wa polisi anashtakiwa kijeshi kwa kufanya jambo la aibu kwa jeshi, lakini polisi ndiyo wanaandaa watu, wanaenda wanasumbua watu, wanavunja nyumba za watu.
Nataka nimwambie IGP Kamanda Wambura kwamba Afisa wako wa polisi/Inspekta, ana nyota tatu, anakamatwa anaweka kura kwenye sanduku na Mkurugenzi kaona, OCD kaona. Kwa nini anayenyanyaswa, na kutafutwa ili apigwe, ni mgombea wetu na si yule polisi kukamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za Jeshi la Polisi?
Sheria gani za jeshi la polisi zinaruhusu afisa wa polisi kubeba kura na kuziingiza katika sanduku? Tunaposema Taifa la Wote, Maslahi ya Wote tuna maana Polisi wa Wote, Maslahi ya Wote!
Polisi mshahara wake sio kodi ya wanaCCM peke yake; polisi mshahara wake ni kodi zetu wote. Mmewahi kusikia shamba la polisi? Mmewahi kusikia kiwanda cha polisi? Ila shamba la Magereza mmesikia, shamba la JKT mmesikia. Ni kwa nini mnadhani hamjasikia shamba la polisi?
SOMA ZAIDI: CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi
Ni kwa sababu Katiba yetu na sheria zetu zimeelekeza kazi ya polisi ni moja tu, ni kutulinda sisi, sio kutuonea, sio kutupiga, sio kutuua. Ndiyo maana polisi na Idara ya Usalama wa Taifa ndiyo vyombo pekee vya kijeshi hapa Tanzania ambavyo havishiriki kwenye shughuli za uzalishaji, kwa sababu kazi zao hazihitaji wao kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji.
Wao tunawalisha, tunawavisha, tunasomesha watoto wao, tunawapa makazi yao kwa sababu ya kutulinda sisi. Hatufanyi hivyo ili wawalinde CCM peke yao. Kama CCM imekataliwa kwenye mji huu, kwa nini wang’ang’anie kuwaingiza CCM madarakani?
Na sisi tumeshaamua hatutoi ushirikiano kwa Mwenyekiti yoyote aliyechaguliwa, na haya ndiyo maagizo ya chama chetu. Na hapa Kigoma Mjini tumeamua na ndiyo maelekezo ya Kamati ya Uongozi ya Jimbo, kwamba mitaa yote 67 ambayo CCM wameipora tunakwenda mahakamani.
Tunafungua kesi 67, tunamshtaki Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa, tunamshtaki Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, tunamshtaki huyo waliyomtangaza kushinda. Tunataka kuhakikisha hatulalamiki tu, bali tunachukuwa hatua za kuwarudishia haki zenu.
Huu ni uchaguzi wa kawaida kabisa, uchaguzi wa mtaani, uchaguzi wa kwenye kitongoji, uchaguzi wa kwenye kijiji. Iweje uchaguzi kama huu vyama vya upinzani badala ya kushindana na CCM vishindane na vyombo vya dola? Kwa sababu hapa Kigoma sisi hatukushindana na CCM; CCM walipotea kabisa, hawakuwepo. Walifanya mkutano mmoja tu, wakatafuta vijana wa jogging huko wakawapeleka, hawakuwa na watu.
Sisi mikutano yetu imefanywa na viongozi wetu wa ngazi ya Jimbo na ilikuwa inajaza watu. Mkutano wetu wa kufunga pale center watu wamenyeshewa na hawakuondoka kwa ajili ya kuonesha chama kilivyo imara. Juzi wametunyang’anya ushindi, leo tunakutana Kawawa hapa. Na walitaka kusema uwanja wao tusije, tukawaambia tunakuja fanyeni mnachotaka. Huu ni mji wetu, tunaweza kufanya chochote, na hawana cha kutufanya chochote.
Angalizo kwa Rais
Kwa hiyo, uchaguzi wa ngazi hii unaweza kufanya vyama vya upinzani vishindane na vyombo vya dola. Nataka niwaambie CCM, nataka nimwambie Mwenyekiti wa Taifa CCM, Samia Suluhu Hassan, kama kuna kosa ambalo Chama cha Mapinduzi wanafanya ni kuiachia siasa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
SOMA ZAIDI: ‘Kidole Kimoja Hakivunji Chawa’: Uchaguzi Mkuu wa Nigeria 2023 na Mambo Makuu ya Kujifunza Tanzania
Vyombo vya ulinzi na usalama vikishaonja madaraka ya kisiasa kama hivi wanavyofanya watakaofuata kushughulikiwa ni CCM wenyewe, watawafuata kuwaondoa CCM madarakani.
Tunayoyaona yakitokea Angola, tunayoyaona yakitokea Mozambique, ni makosa ya FRELIMO na MPLA kuiachia siasa kwa vyombo vya dola. Ndio maana muda wote niliokuwa Mbunge, katika jambo nilikuwa nalipigania kwa nguvu zangu zote ni kuiondoa Idara ya Usalama wa Taifa kwenye makucha ya CCM.
Nikapigania mageuzi ya Idara ya Usalama wa Taifa, au TISS, kwa sababu ni kosa kubwa sana kuiondoa nchi kwenye democracy na kuipelekea kwenye securocracy. Securocracy ni nchi inaendeshwa na vyombo vya dola. Democracy ni nchi inaendeshwa na watu kupitia vyama vyao vya siasa.
Kosa kubwa wanalofanya CCM, na kosa hili namueleza Rais Samia alitazame kwa makini, namuelekeza Katibu Mkuu [wa CCM, Emmanuel] Nchimbi alitazame kwa makini. Kinachotokea Mozambique, kinachotokea Angola, kitatokea Tanzania. Na sisi tulikuwa tumeshavuka hatua hiyo, tulikuwa tushatenganisha vyombo vyetu.
Hii nchi yetu ni ya kikatiba. Katiba yetu, pamoja na ubovu wake, imeweka mipaka kuhusu chombo gani kinafanya nini. Kazi ya siasa ni kazi ya vyama vya siasa, na kazi ya siasa ni kazi ya ushawishi. Chama cha siasa ambacho kinashindwa kushawishi halafu kinategemea dola siku kinaondoka hakitajua, na kudondoka kwake kutakuwa ni kudondoka kwa mshindo mkubwa sana.
Ndiyo maana [Rais Benjamin] Mkapa na [Rais Jakaya] Kikwete walifanya makusudi kutenganisha vyombo vya dola na siasa. Sio kwamba walikuwa ni wajinga, wao walifanya makusudi, wakijua kwamba huko tunakokwenda watu wataichoka CCM, watachagua chama kingine.
Watu wasichoke CCM wakachoka na vyombo vya dola. Sasa hivi vyombo vya dola viwili vimeshakuwa politicised, [Jeshi la] Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa, totally politicised. Limebaki Jeshi [la Wananchi] tu halijawa politicized, na siku mkiona na jeshi linakuwa politicized, nchi haitokuwa salama.
Tuachwe tufanye siasa
Kwa hiyo, badala ya kuelekea huko, juhudi zinapaswa kufanyika kuviondoa vyombo vya dola kwenye shughuli za kisiasa ili siasa ifanywe na wanasiasa. Wanasiasa tubishane kwa hoja kama tulivyokuwa tunabishana kabla.
SOMA ZAIDI: Ado Shaibu: Hivi Ndivyo Tanzania Inaweza Kupata Tume Huru ya Uchaguzi
Tujenge hoja zetu, watu waamue kama ilivyokuwa kabla, mbona tulikuwa sawa tu, mbona uchumi wa nchi ulikuwa unakua kwa kasi sana tu? Hakuna nyakati ambayo uchumi wa taifa hili umekua kwa kasi kama wakati wa Mzee Mkapa na wakati wa Mzee Kikwete. Na kulikuwa na democracy, watu walikuwa wanachaguliwa.
Hawa kina Mambo wamechaguliwa uchaguzi wa kwanza wa madiwani wa kwanza kufanyika nchini 1994. Yaani, mara ya kwanza tunafanya uchaguzi wa madiwani wa vyama vingi, tumetoa madiwani hapa hawa kina Mzee Mambo, nini kiliharibika?
Ruagwa pale tuna Mameya wa upinzani, nini kiliharibika? Lakini ndiyo nyakati ambayo mji wetu ulipata hamasa kubwa ya kimaendeleo. Watu wa Kigoma walikuwa hawajui Halmashauri zinaweza kuwa na mabasi ya kubeba wanafunzi, tulianza kuyaona wakati Mzee Mambo, ndiye Meya wa Mji huu.
Mnaweza mkaona namna gani democracy ni tamu, kwa nini watuharibie democracy? Kwa nini wahangaike na Mwenyekiti wa Mtaa, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Mwenyekiti wa Kijiji?
Kule Kagunda leo wameenda polisi zaidi ya 200 kwenda kuumiza watu. Watu wamechagua Mwenyekiti wao, aliyeshindwa wa CCM kakiri nimeshindwa, mtangaze huyo wa ACT Wazalendo aliyeshinda. Mtendaji akakataa, wananchi wakachukua hatua. Sasa wewe polisi inakuhusu nini?
Maamuzi ya ACT Wazalendo
Mambo mawili makubwa ambayo yameamuliwa na chama chetu, moja limesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini. Leo, Kiongozi wetu Taifa wa chama, Dorothy Semu, ametoa tamko la awali la chama kuhusu Uchaguzi Serikali za Mitaa. Mambo mawili makubwa ya kuzingatia kwa watu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.
La kwanza, ametamka uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Chama tulikaa jana usiku, ya kwamba hatuyatambui matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na tunataka uchaguzi urudiwe.
SOMA ZAIDI: Uandikishaji Serikali za Mtaa: Takwimu za Kihistoria au Hamasa ya Kihistoria?
Lakini kabla ya kurudiwa, Sheria ya Uchaguzi iandikwe upya, mchakato wa Katiba Mpya uanze ili tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia huo uchaguzi utakaorudiwa.
Na kwa ajili hii, Kiongozi wetu wa chama, Dorothy Semu, ametangaza chama chetu kinaanza zoezi la kuwasiliana na vyama vingine makini vya upinzani kwa ajili ya kujadiliana namna gani ya kuhakikisha kwamba tunaanza mchakato wa Katiba Mpya na Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ili kuja kusimamia huu uchaguzi.
La pili, Kiongozi wa chama ametangaza kwa wakati huu mpaka hapo chama kitakapotoa maelekezo mengine hatutatoa ushirikiano kwa Wenyeviti wa CCM waliotangazwa kuchukuwa Mitaa yetu, Vijiji vyetu na Vitongoji vyetu. Hayo ndiyo maamuzi makubwa ambayo chama chetu kimeyatoa na kimeyatangaza rasmi kwenye vyombo vya habari.
Na kwa hapa Kigoma Mjini na sehemu zingine za Tanzania, kila mtaa tunakwenda mahakamani. Kwa hiyo, wananchi wa Kigoma Mjini tujiandae na mchakato wa mahakamani. Tumeshazungumza na wanasheria, wanasheria wapo tayari kuanzia kesho kesi zinaanza kuandikwa, tunaenda kuwashitaki wote ili chaguzi zote zirudiwe, tuzifanye chini ya mazingira mapya.
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama mstaafu wa chama cha upinzani ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia zittokabwe@gmail.com au X kama @zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.