Mwandishi aliwasilisha wasilisho hili kwa mara ya kwanza Zanzibar, Disemba 15, 2024, wakati wa Mkutano wa Nne wa Kukumbuka na Kuenzi Urithi wa Maalim Seif Sharif Hamad. The Chanzo inalichapisha hapa kwa ruhusa ya mwandishi. Uhariri umefanyika kuimarisha usomaji.
Kwa niaba ya wenzangu 18 ambao hisia zetu zimekusanyika kwa njia ya maandishi kwa tungo ambazo zimekusanywa ndani ya diwani ya Ahadi Iliyotimizwa, tunatanguliza shukran kwa Muumba kwa kuuzawadia ulimwengu, Tanzania na visiwa vya Zanzibar mja wake ashrafu Maalim Seif Sharif Hamad.
Kwa namna alivyoishi, ni wazi kuwa alifanikiwa kuzichota nyoyo za wengi na akazifanya zimee kwa mapenzi yake kwao hata naye kuyapata mapenzi ya nyoyo hizo kwake. Ama, pengine shwari na amani ambayo tunaifurahikia sasa katika ardhi hii, ni pamoja na mchango wake mkubwa na mapenzi yake makuu kwa nchi yake na watu wake.
Ni kwa mapenzi hayo, hakutamani kabisa kuona kiza cha kukosekana amani kinatugubika licha ya tafauti za kisiasa na kutokukubaliana katika baadhi ya mambo.
Hakuna asiyefahamu kuwa ushairi wa Kiswahili umebeba hisia, na bila shaka ni hisia za majonzi ndizo zilizoweza kuwasukuma wengi kuandika mashairi ya kumuadhimisha na kumlilia mzee wetu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Sisi watunzi 19 ni wachache katika wengi waliohuzunika, ila tunapenda kumpongeza kaka yetu, Mohammed Khelef Ghassani, kwa juhudi zake kuhakikisha kuwa machache katika mengi ya mashairi yaliyoandikwa anayakusanya na kuyafanya diwani ya pamoja kama alama ya kuzikusanya hisia zile, kuzipa uhai na kutufanya tuendelee kulia na kujiliwaza kwa msiba uliotufika miaka mitatu iliyopita.
SOMA ZAIDI: Tumejifunza Nini Kutoka Mkutano wa Pili wa Urathi wa Maalim Seif?
Nikiizungumzia nafsi yangu, nikiwa mmoja wa watunzi wa diwani hii, nakiri kutokuwa na asili ya Zanzibar, lakini namshukuru Mungu nimeishi ndani Zanzibar kwa miaka isiyopungua mitano mtawalia, na mbali na hapo niliguswa na mengi mazuri ambayo nilipata kuyasikia kupitia masimulizi rasmi na yasiyo rasmi.
Lakini pia nimejaaliwa kuona namna ambavyo hisia za watu, hasa Wazanzibari, ambao ndio wana mafungamano ya moja kwa moja na Maalim. Nilikiri, na ninakiri, kuwa kuna mapenzi, mapenzi ya dhati, mapenzi makuu, mapenzi makali mno ya watu kuwa tayari kuongozwa naye na hata kufanya lolote atalowaamrisha, iwe kwao linaingia akilini au vinginevyo.
Na ithbati ya hili, imepita misiba kadhaa kabla ya kuuka kwa Maalim na baada yake, misiba ya viongozi waliowahi kushika ngazi za juu kabisa katika nchi zetu, wanasiasa nguli, watu maarufu, watu wenye vyao walivyomiliki, lakini hakuna msiba ambao ulikita kwenye nyoyo za wanaMalenga Chipukizi na kudhihirisha hisia zao kama ilivyokuwa kwa kuuka Maalim Seif Sharif Hamad.
Tungo za kumuomboleza, tungo za kuyanadi mazuri yake, tungo za kunadi nafasi yake kwenye nyoyo zao, zilikuwa zikimiminika kwa namna macho yalivyokuwa yakibubujikwa machozi, michirizi michirizi.
Kubwa kabisa ambalo anatuachia sisi vijana, taifa la leo na baadae, ni kutothubutu kuacha kuzipenda nchi zetu za uzawa, kwa hali zote hata kama itakuwa tumedhulumiwa mali na roho zetu.
SOMA ZAIDI: Maajabu ya Maalim Seif Akiwa Hai Yanaendelea Mpaka Akiwa Kaburini?
Kuwa na msimamo thabiti kwa hoja katika tunayoyaamini, lakini bila kuwa na kibri, jeuri na ujivuni. Uzalendo wa kweli, uungwana, busara na hekima vitawale katika kila ambalo ni mbegu bora ya kuifanya ardhi yetu hii imee, ikuwe, iendelee na kuwa mfano mwema wa kuigwa na mataifa mengine.
Mwisho, tunaamini kuwa Maalim Seif Sharif Hamad atasimama kama maktaba ya kusoma kwa viongozi wetu kwa ngazi zote, na kwa hakika ametufunza kuwa uongozi unaoacha alama chanya ni ule wa kutawala nyoyo za waongozwao na si viwiliwili vyao.
Mja mwema alikuwa, alojisahau yeye, siko alikozalika
Ametufunza muruwa, uzalendo utungiye, hata bila mamlaka
Moliwa kamchukuwa, ila hakika tunaye, wanati wa kila rika
Ingawa amefukiwa, haifukiwi gheraye, kwa miaka na mikaka
Ardhi hii kupowa, ili kuu shaukuye, nalo limetimilika
Jukumu tulilopawa, ni kulinda misingiye, bila chembe kumpoka
Na tumuombee duwa, pahala pema akaye, ambapo alipataka
Umfunike uluwa, tabu zisimfikiye, azidi stareheka
Siku ya kufufuliwa, kando yake awe naye, mtume wetu Mmaka
“Allaahumma ghfirlahu warhamhu waskanahu fil Jannah”
Aamiin!
Bashiru Abdallah ni moja kati ya washairi 19 walioshirikiana kuandika kitabu cha mashairi chenye kuenzi maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad, mwanasiasa aliyetoa mchango mkubwa kwenye harakati za kupigania mageuzi ya kisiasa na kiuchumi Tanzania. Kitaby hicho kinachoitwa Ahadi Iliyotimizwa, kilizinduliwa rasmi Disemba 15, 2024, wakati wa Mkutano wa Nne wa Kukumbuka na Kuenzi Urithi wa Maalim Seif Sharif Hamad, uliofanyika katika Hoteli ya Verde, mjini Zanzibar.
2 responses
Ahasante Maalim
Bashiru Abdallah, nami nikiwa ni mmoja miongoni mwa watunzi wa tungo hizo njema kwa Almarhum Maalim Seif, nikupongeze kwa andiko/chapisho lako hili zuri, nadhifu na lenye kusisimua.
Ala kulli haali ahsate sana
Ahsantta Maalim Ali