Niliweka wazi kwamba ninamuunga mkono Tundu Antiphas Mughwai Lissu katika safari yake ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Niliongeza pia kwamba, ashinde ama asishinde, tangu atangaze nia, mambo mengi yanayotutazamisha upya juu ya safari yetu ya ukombozi wa pili wa taifa letu yamejitokeza.
Niliongeza, Lissu ametuonesha ukurasa mbaya zaidi katika mbadala uliopo sasa wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM). Hii ni kutokana na mwitikio wa wafuasi wa CHADEMA wasiomuunga mkono, ambao waliona hatua yake kama vita iliyotangazwa dhidi ya mwenyekiti wa sasa wa chama, na mgombea wao kwenye kinyang’anyiro, Freeman Aikael Mbowe.
Imedaiwa Lissu amemtukana Mbowe na kuvujisha siri za chama. Nilisikiliza hotuba ya Lissu akitangaza nia ya kugombea. Hotuba iliwekwa pia katika ukurasa rasmi wa CHADEMA kule X, zamani Twitter. Hotuba ya Lissu, kwa maoni yangu, haina matusi, si tu kwa Mbowe, bali pia kwa taasisi anayokusudia kuiongoza. Sidhani pia kama CHADEMA kingeafiki kuweka matusi katika ukurasa wao rasmi wa chama.
Lissu ameeleza atakavyoiongoza CHADEMA. Ametaja vipaumbele – akionesha udhaifu uliopo, na atakachofanya. Lissu analazimika kufanya hivi – jambo ambalo si mwiko, ili kushawishi wajumbe kuhusu mwanzo mpya. Kwa hiyo, Lissu hajavunja mwiko wowote.
Hata hivyo, kama kukemea rushwa ni kutoa siri za chama, ninamsihi Lissu aendelee kutufungua macho. Rushwa ni adui wa haki.
Kuhusu rushwa
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, Machi 19, 2021, alikuwa na machaguo angalau matatu dhidi ya wapinzani wake. Mosi ni kuwaalika wamuunge mkono kwa hongo ya vyeo au mali. Baadhi waliitikia mwito huo na kupewa ‘ulaji.’
Pili, ni kutumia mabavu ya dola kuwashughulikia wapinzani na wakosoaji wake. Nyenzo hii ni pamoja na kuwapa kesi, utekaji, mauaji, kuwafilisi, na kujenga hofu kwa wakosoaji, kwa lengo la kuogofya. Tuna idadi kubwa ya vijana waliopotezwa, akiwemo Deusdedith Soka na wenzake. Kuna walioteswa, akiwemo Mdude Nyagali, Edgar “Sativa” Mwakalebela na wengine. Mauwaji ya Ali Mohamed Kibao ni tukio jingine lenye taswira hiyo.
Tatu, ni kufanya biashara na ‘wakosoaji’ waliopo, ili kutengeneza geresha kwamba kuna upinzani. Yaani, upinzani unatumika kupooza upinzani, kama utapenda. Katika hili, si tu vyama vya upinzani vilivyofikiwa, bali pia vyombo vya habari, asasi za kiraia, viongozi wa kidini, wanazuoni, na baadhi ya wanaharakati.
Chaguo la tatu limetekelezwa ‘kwa wivu mkubwa,’ kama wasemavyo wahafidhina katika mageuzi. Dola ilikusudia kunyumbulisha upinzani na kuua sauti zinazosikika zaidi.
Ili kufikia malengo hayo ovu, baadhi ya wakosoaji wenye misimamo walipewa majina fulani fulani. Aah, yule ni ‘msema hovyo, hana busara, mropokaji, hana staha’ na zaidi. Si tu ndani ya CHADEMA, hata asasi za kiraia zilikutwa na biashara hii. Baadhi ya wanaharakati jeuri wameendelea kukutana na cancel culture.
Asasi zilibadili gia angani zikijinasibu ‘kufanya kazi na Serikali.’ Mtakumbuka, hata Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) pia kiliendeshwa kwa dhana dhaifu ya constructive engagement.
Biashara hii haramu dhidi ya mageuzi imedhoofisha jitihada za kudai mageuzi. Mtakumbuka, kwa mfano, kuna vitu vya ajabu ajabu vilianzishwa ili kuahirisha masuala makubwa ya kimageuzi. Mojawapo ni kikosi kazi cha Rais kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala. Ulaghai wa kikosi kazi ulileta ahirisho la kuandika Katiba Mpya. Hadi sasa tunasuasua!
Kikosi kazi kilileta marekebisho duni katika sheria za uchaguzi na vyama vya siasa. Uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, hata baada ya ‘marekebisho’ ya sheria, umekuwa wa hovyo kama lilivyo neno hovyo lenyewe. Faida ya kikosi kazi haionekani popote isipokuwa kwa Rais aliyepata unafuu wa kisiasa.
Ninafahamu jamii yetu haiko tayari kupokea taarifa fulani fulani kuhusu wapendwa wao. Ndio maana, labda, Lissu anazungumza kuhusu rushwa kwa kituo. Lakini orodha ya watu wanaotajwa kuhongwa kwa lengo la kumsaidia Rais kutawala bila ukosoaji ni ndefu.
Masuala haya ya biashara isiyo na afya kwa demokrasia kati ya wanamageuzi na dola, haitatokea uyasikie katika vyombo maarufu vya habari. Hayatachunguzwa na TAKUKURU kwa kuwa, kama tujuavyo, meno ya mbwa hayaumani!
Faida za maridhiano
Lengo la kalamu hii ni kujadilia masuala machache yaliyojitokeza katika hotuba ya Mbowe wakati akitangaza nia ya kugombea tena nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, na moja kati ya suala lililochukua nafasi kubwa kwenye hotuba hiyo ndefu kwelikweli ni kile Mbowe alikitaja kama “faida za maridhiano.”
Kwanza, nieleweke wazi kwamba ninaheshimu sana mchango wa Mbowe katika harakati na vuguvugu za mageuzi ya kisiasa na mengine muhimu sana nchini kwetu. Mbowe, ukweli usemwe, amefanya kazi kubwa kama kiongozi, akilipia gharama ambayo baadhi yetu hatungefikiri kuibeba hata kwa sekunde moja. Kwa dhati ya moyo wangu, ninampa maua yake.
Lakini kwenye hili la maridhiano, naomba niseme bila kupepesa macho kwamba CHADEMA haikuwahi kufanya maridhiano na CCM. Kilichofanyika, iwe Mbowe alijua au vinginevyo, ilikuwa mbinu ya kumtengenezea Samia unafuu wa kisiasa, political convenience kwa kimombo, ili Rais asikutane na ukosoaji halisi. Ndio maana hakuna matokeo makubwa kando ya ahueni ya kisiasa kwa Rais.
Mbowe alitaja kama faida nne za maridhiano CHADEMA kupewa ruzuku baada ya maridhiano. Hoja hii ni dhaifu kuliko maridhiano yenyewe, kwani awali CHADEMA ilikataa kupokea ruzuku kwa utashi wao. Hakukuwa na kikwazo ambacho Rais, au maridhiano, yalikiondoa. CHADEMA ilibadili kauli na kuitambua Serikali, na kudai wapewe ruzuku.
Hoja kwamba ruzuku imesaidia kununua ofisi mpya za chama ni dhaifu vilevile. Ilikuwa lazima fedha za ruzuku zitumike. Fedha zimetumika kwa madhumuni mbalimbali. Kutumia suala hili kama matokeo muhimu ya maridhiano ni kuongeza uzito katika udhaifu wa maridhiano yenyewe.
Pili, kwamba maridhiano yamesaidia kufuta kesi na kutoa watu magerezani. Ni kweli, makada maarufu walifutiwa kesi. Mwenyekiti Mbowe alidai zimesalia kesi mbili, kule Njombe na Kibaha, kati ya mia nne. Takwimu hizi zina walakini kwa kuwa kuna makada wengine bado wako jela.
Mathalani, kada na kiongozi mstaafu wa BAVICHA, Mohamed Issa Simon, anashikiliwa kisiasa mahabusu ya Segerea tangu mwaka 2019. Simon ana mke na mtoto mdogo ambaye, kwa miaka mitano, hamjui baba! Je, Simon alihitaji maridhiano tofauti?
Vilevile, mahabusu zina maelfu ya Watanzania waliobambikiwa kesi. Kama maslahi ni kuanza upya, sifa na utukufu kwa Rais kwa kuwafutia baadhi ya makada maarufu kesi walizowapa hazitoshi. Haki ya huyu bila ya yule ni sawa na ubaguzi wa kiitikadi – kwa kuwa sio kweli kwamba makada wa CHADEMA pekee ndio waliokuwa jela kwa kesi za kisiasa.
SOMA ZAIDI: CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi
Kutangaza neema za maridhiano wakati Mzee Ali Mohamed Kibao ameuwawa kikatili miezi michache iliyopita ni kuibua upya vilio katika familia yake. Mbwana Kombo ametoka jela hivi karibuni baada ya kutekwa, kupotezwa na kuteswa jela kwa mwezi miezi kadhaa kwa kesi ya uongo. Maridhiano hayakusaidia kulinda haki ya Kombo!
Soka na wenzake, Shadrack Chaula na Dioniz Kipanya, walitekwa na dola na kupotezwa sababu ya kumkosoa Rais. Imepita zaidi ya siku 100 wakiwa mateka. Kivyovyote, hakuna nafuu katika mifumo ya haki jinai bila kuirekebisha. Sifa na utukufu kwa Rais kwa kufuta kesi za watu maarufu zilifaa kuwa na kiasi.
George Sanga anaozea jela kwa kesi ya mauaji ya uongo aliyopewa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Kauli ya Mbowe kwamba “mtoto atafurahi kusikia baba amefutiwa kesi ya mauaji sababu ya maridhiano” ina nafasi kwa watoto wa Sanga?
Tatu, kwamba maridhiano yamerejesha shughuli za kisiasa. Hii danganya toto haikudumu. Ilikuwa ni turufu ya Rais kuwaonesha marafiki wa Tanzania kuhusu mwanzo mpya kisiasa. Ndio maana katika miezi miwili, Agasti na Septemba mwaka huu, viongozi wote wakuu wa CHADEMA na mamia ya wafuasi walikamatwa zaidi ya mara moja, kupigwa na kuteswa kwa kosa la kufanya mikutano au maandamano.
Viongozi na wanachama waliumizwa sana. Licha ya uharibifu huo, CHADEMA iliahidi kufungua kesi dhidi ya Jeshi la Polisi, ambayo hadi leo hakuna mrejesho kwa umma.
Kwa hiyo, kudai maridhiano yamerejesha shughuli za kisiasa ni sawa na kufumba macho ili watu wasikuone. Na kimsingi, shughuli halali za kisiasa hazipaswi kuegemezwa katika dhana ya maridhiano. Ni haki isiyopaswa kutegemezwa katika utashi wa mtu au dola.
Kanuni za maridhiano
Maridhiano yana kanuni zake. Ni tofauti sana na ‘wakubwa’ kukutana na kuafikiana kuwatuliza ‘waropokaji’ kwa ahadi ya kupewa nafuu za kiuchumi.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Imefeli?
Kabla ya yote, ilibidi utengenezwe mwafaka wa kitaifa. Serikali ikiri udhaifu na kubainisha madhara yaliyotokea kwa umma na kwa mtu mmoja mmoja. Iombe radhi na kuhakikisha uharibifu hautajirudia. Nafuu makhsusi zingeelekezwa kwa watu mmoja mmoja kwa kadri wanavyostahili.
Serikali ilipaswa kuhakikisha haitarudia kuahirisha ufurahiwaji wa haki kwa sababu zenye uholela, jambo ambalo limeendelea hata wakati wa maridhiano. Ilitakiwa mwafaka uelekeze nini kinafanyika na nani wanashiriki. Umma unastahili kupewa ripoti ya kilichojiri, gharama na hata matokeo, kama wanavyodai!
Maridhiano yalipaswa kuleta matokeo makubwa yahusuyo mwanzo mpya katika ujenzi wa taasisi za kidemokrasia, mageuzi ya kisheria na kikatiba, na ushiriki wa kina wa wananchi katika uendeshaji wa nchi yao. Taasisi kama Bunge na Mahakama zinaendelea kuwa butu, na zinatumika kuwaumiza wananchi kabla, wakati, na baada ya maridhiano.
Nasisitiza, maridhiano yalikuwa ahueni ya kisiasa kwa Rais na Serikali yake. Ndio maana matokeo yake ni ya kuokoteza. Kutoa sifa kwa suala ambalo halikutimilika ni sawa na kujipakaa mafuta mwilini bila kuoga.
Wenye busara watusaidie
Lakini licha ya kuchukua msimamo huu, pengine mimi ndiyo mkosefu. Ni kwa msingi huu, kwa hiyo, ndiyo naomba wenye kipimo cha busara watusaidie pia kutofautisha biashara ya kisiasa na mageuzi ya kisiasa.
Sisi waropokaji tungependa kushiriki kwa kina katika uendeshaji wa nchi yetu, ambayo siyo mali ya CCM na Serikali yake, ikiwemo kuzungumza na wezi wa uchaguzi wanaofuja mali za umma, kwa lugha wasiyozipenda.
Wanufaika wa dola wamejitokeza kipindi hiki kuzungumzia suala la busara bila kuonesha athari zake katika vuguvugu la kupigania mabadiliko tunayoyataka. Na sio kwamba wana busara. Bali wanatumia kauli hiyo kushambulia kundi wanalodhani limenyooka kuliko wao. Hii inajumuisha wahafidhina ndani ya CHADEMA, vijana wanaotumika na dola na watu wanaopewa upendeleo fulani fulani na Serikali yetu dhalimu.
SOMA ZAIDI: Maswali Fikirishi Kuhusu Falsafa ya 4R ya Rais Samia
Tunahitaji kuhamasika kudai haki zetu zaidi kuliko kufikiria kuketi na watawala. Hatuwezi kutelekeza mamlaka na haki zetu kwa mtu na baadaye kwenda kumdai atupatie tuzitumie. Siasa za mazungumzo ni muhimu, lakini hazina ufanisi kama hatuheshimiani.
Mamia ya watu waliouwawa wakishiriki shughuli za kisiasa wangejua mwisho wa madai ya mageuzi ya kisiasa ni watawala kuwapa ahueni za kiuchumi baadhi ya wapiganaji vinara, pengine wasingejihusisha na siasa hata kidogo.
Sehemu ya vijana wa rika langu wanadhani ni salama zaidi kushirikiana na wanyonyaji kuliko kuungana na mawakala wao, ambao wamehakikishiwa upendeleo fulani fulani.
Maana katika upande huu usio salama, unaumia wewe na familia yako. Hili somo lipo kwa kila anayependa kujifunza. Tufanye harakati kwa kuamini katika maono, maana safari ina ndumilakuwili chungu nzima.
Naam! Pia, tukumbushane, kama nilivyowahi kusema kwengineko, demokrasia ni mwafaka wa wengi, hata kama ni wajinga, wamenunuliwa au hawajui walitendalo.
Mapambano Yaendelee!
Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.