Nilipata fursa ya kuhudhuria Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Dodoma katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center kuanzia Januari 18 hadi 19, 2025, kama mgeni mwalikwa, kwa kuwa sikuwa mjumbe.
Kutokana na hili, nilifanikiwa kushuhudia na kusikia baadhi ya mambo ambayo hayakuweza kuonekana wakati mkutano huo ukirushwa mubashara kupitia vyombo vya habari. Kwa uzoefu huo nilioupata Dodoma ningependa kutoa maoni yangu kama ifuatavyo.
Awali, taarifa za mkutano mkuu huo maalum zilitolewa Januari 7, 2025, na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla. Makalla alieleza kuwa ajenda kuu zitakuwa tatu: kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara; kupokea taarifa ya kazi za chama kuanzia mwaka 2022 hadi 2025; na kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Ajenda ya kwanza, ya kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, iliwasilishwa kwenye mkutano mkuu Januari 18, 2024. Kabla ya siku hii majina yaliyokuwa yakitajwa kujaza nafasi hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, mwanasiasa mkongwe na mwanachama mwandamizi Stephen Wasira, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Mstaafu Abdallah Bulembo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Abdulrahman Rajab, na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi.
Wengi walikuwa wakimuweka Mizengo Pinda na Stephen Wasira katika nafasi hiyo kutokana na historia ya CCM kumchagua Makamu Mwenyekiti Bara mwanachama ambaye ni mwandamizi, mwenye uzoefu mkubwa wa siasa za chama na Serikali, mtu ambaye amemaliza kujitahidi kutafuta vyeo vya juu zaidi.
Hatimaye, jina la Stephen Wasira ndilo lililetwa mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa ajili ya kulithibitisha. Katika mkutano huo, kura 1,921 zilipigwa, ambapo kura halali zilikuwa 1,917. Kura za “HAPANA” zilikuwa saba, na kura za “NDIYO” zilikuwa 1,910, hii ilikuwa sawa na kumpitisha Wasira kwa asilimia 99.42, huku kura nne zikiharibika.
SOMA ZAIDI: Nioneshe Chama Kilichotayari Kurithi Mikoba ya CCM Kama Chama Tawala ‘Tanzania’
Stephen Wasira
Stephen Wasira amekuwa mwanachama wa TANU tangu akiwa na miaka 14. Alikubalika kuwa mbunge mwaka 1970 akiwa na umri wa miaka 25 tu na alihudumu kama Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa kabla hajatimiza miaka 30.
Kuanzia mwaka 1982 hadi 1985 alifanya kazi kama afisa mwandamizi katika ubalozi wa Tanzania nchini Marekani. Pia, amewahi kuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Maji, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Ni muhimu kutambua kwamba Stephen Wasira aliwahi kutofautiana na CCM, jambo lililomfanya kugombea ubunge kupitia NCCR Mageuzi mwaka 1995 baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi. Alirudi CCM mwaka 2005 na kushinda kiti cha ubunge jimbo la Bunda alipotumikia mpaka mwaka 2015.
Hivyo, uzoefu wake katika siasa za CCM, vyama vya upinzani, na Serikali utakuwa muhimu sana katika kutekeleza majukumu yake mapya. Baadhi ya watu wamehoji kuhusu umri wa Stephen Wasira, ambaye mwaka huu anatimiza miaka 80. Wanahoji kama ataweza kustahimili majukumu ya kuwa kiongozi wa pili katika chama tawala.
Mimi binafsi naamini Stephen Wasira kachaguliwa kwa sababu ya busara na uzoefu wake. Hata hivyo, kwa tathmini yangu, CCM itakapofanya uchaguzi wa viongozi wake wa kitaifa mwaka 2027, ni dhahiri kwamba Stephen Wassira ataomba kupisha mtu mwingine achaguliwe katika nafasi hiyo.
Tukio la kihistoria
Baada ya ajenda hiyo ya kwanza, wengi walidhani kwamba ajenda ya Januari 19, 2024, ingejumuisha kupokea ripoti ya utekelezaji wa Serikali na Ilani ya CCM tu. Hata hivyo, ni wachache walioweza kutegemea kuwa hoja ya kupitisha na kuteua wagombea wa CCM kwa nafasi ya urais wa Muungano na urais wa Zanzibar ingeibuka.
SOMA ZAIDI: Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana Ajiuzulu
Hii ilitokea baada ya wajumbe kama Livingstone Lusinde, Adam Kimbisa, Ng’wasi Kamani, na wengine kutoa hoja ya kuwa uteuzi wa wagombea kwa nafasi za Urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu ufanywe na Mkutano Mkuu Maalum huo siku hiyohiyo.
Baada ya maoni hayo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alipewa fursa ya kutoa muongozo. Mzee Kikwete alieleza vifungu vya Katiba ya CCM, ikiwemo mamlaka ya Mkutano Mkuu kuteua mgombea urais kupitia Ibara 101(5)(b). Baada ya ushauri huo, Halmashauri Kuu ya CCM ikaketi na kufanya kikao cha dharura kujadili suala hilo. Hatimaye uliletwa mrejesho na Mkutano Mkuu ulipitisha jina la Rais Samia kuwa mgombea wa CCM kwa kura za ndiyo 1,924 na kura za hapana sifuri.
Ni utamaduni wa CCM kumteua Rais aliye madarakani kugombea muhula wa pili kwa utaratibu uliozoeleka wa mchakato wa uteuzi wa ndani ya chama. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa mwaka huu ambapo uteuzi wa mgombea urais haukufuata utaratibu uliozoeleka.
Kwa kawaida, mwanachama anayehitaji kugombea urais huwasilisha maombi rasmi kwa Katibu Mkuu wa CCM, akijaza fomu maalum na kulipa ada ya uteuzi. Baada ya hapo, Kamati ya Maadili hufanya uhakiki wa wagombea ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vya kikatiba na maadili ya chama.
Wagombea wanaokidhi vigezo hupitishwa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambayo huchagua majina matatu bora ya wagombea. Majina haya hupelekwa kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu, ambapo wajumbe huchagua jina moja la mgombea kwa kura.
Hatua ya mwisho ni Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, ambapo wajumbe hupiga kura ya kuridhia, au kukataa, uteuzi wa mgombea. Mgombea anayepitishwa hutangazwa rasmi na jina lake hupelekwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi mkuu.
SOMA ZAIDI: Mwenezi Khamis Mbeto: CCM Ndiyo Baba wa Demokrasia Tanzania
Kwa kawaida, mchakato huu hutekelezwa kati ya mwezi Mei na Julai, hivyo wengi walitarajia mchakato wa mwaka huu ufuate utaratibu wa kawaida. Hata hivyo, ni wazi kwamba katika siasa, chochote kinaweza kutokea wakati wowote. Ingawa ni vigumu kusema ni sababu gani zilizochochea wajumbe kuharakisha mchakato wa mwaka huu, ni wazi kuwa siasa za ndani za CCM ziliathiri mchakato ule wa kawaida kupelekea hiki kilichotokea.
Kuna methali ya kimombo inayosema, There is no coincidence in politics, ukimaanisha hakuna bahati mbaya kwenye siasa. Hivyo, ni vigumu kuamini kwamba kile kilichotokea kilikuwa bahati mbaya. Huenda hii ilikuwa ni njia ya kipekee ya kuondoa makundi ndani ya chama na kuhakikisha chama kinajitolea kwa uchaguzi mkuu wa baadaye.
Wapo watu ambao walikuwa wamewekeza nguvu zao kisiasa wakati wa Hayati Magufuli, wakijiandaa kugombea urais mwaka 2025. Ujio wa Rais Samia Suluhu Hassan ulizima ndoto hizo, na huenda baadhi ya watu waliona kuwa hawawezi kusubiri hadi mwaka 2030. Ndoto zao sasa zimezimwa rasmi, na ushawishi wao katika siasa za chama na nchi utapungua kwa kiasi kikubwa.
Mwelekeo mpya CCM?
Baada ya zoezi la uteuzi wa mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar siku hiyo, Kamati Kuu ikaketi tena kwa lengo la kumchagua mgombea mwenza. Mara baada ya kikao hicho, Rais Samia alitangaza jina la Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CCM. Hii inaweza kuwa ni ushindi mkubwa kwa vijana waliolelewa kisiasa ndani ya chama tangu chipukizi, vijana hadi kuwa kiongozi mwandamizi wa kitaifa.
Dk Nchimbi anakumbukwa sana hasa kwa tukio la mwaka 2015 ambapo jina la Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Lowassa, lilipokataliwa na Kamati ya Maadili ya chama, ambapo yeye na makada watatu wa CCM, wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, waliokuwa katika timu ya Lowassa — Sophia Simba na Adam Kimbisa – walitoka hadharani na kulaani kitendo hicho.
Hii ilisababisha adhabu mbalimbali kwa makada hao, lakini katika uchaguzi huo pamoja na Dk Emmanuel Nchimbi kuonekana alikuwa mtu wa karibu na Lowasa, hakuhama chama Waziri Mkuu mstaafu huyo alipotimkia CHADEMA. Nchimbi aliendelea kuwa mwana CCM na alishiriki kumpigia kampeni mgombea wa CCM, Hayati John Pombe Magufuli.
Hata hivyo, baada ya uchaguzi, CCM iliwapa adhabu baadhi ya makada wake kwa kile kilichotokea wakati wa uchaguzi, lakini kwa Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa balozi Tanzania nchini Brazil na Rais Magufuli. Kuteuliwa kwa Emmanuel Nchimbi kuwa balozi kulifanya wengi kuamini kuwa alikuwa amemalizwa kisiasa.
Hata hivyo, utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ulimrejesha Nchimbi katika anga za kisiasa kwani kabla ya uteuzi wa Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais, jina la Emmanuel Nchimbi lilitajwa kama mmoja wa watu ambao wangeweza kushika nafasi hiyo. Huenda Emmanuel Nchimbi alikuwa chaguo halisi la Rais Samia kuwa msaidizi wake mkuu, ingawa mazingira ya wakati huo yalisababisha kutokea kilichotokea.
Kwa uteuzi huu wa sasa kuelekea uchaguzi wa mwaka huu, inawezekana kwamba Emmanuel Nchimbi ndiye atakayekuwa mtarajiwa wa kumrithi Rais Samia endapo CCM itashinda uchaguzi wa 2030, jambo linaloshangaza siyo kwa sababu ya uwezo wake, bali kwa jinsi ushawishi wake unavyoongezeka katika siasa za chama na nchi.
Kilicho dhahiri ni kwamba, matokeo ya Mkutano Mkuu, hasa uteuzi wa Emmanuel Nchimbi kama mgombea mwenza, utadilisha hali ya siasa ndani ya chama. Kwa siku za mbeleni kutakua na shauku kubwa ya kuona ni makundi yapi yamepata nguvu na makundi yapi ushawishi wake umepungua au kuisha kabisa.
Matarajio
Ukiacha makundi ya urais ya 2030, natarajia endapo Rais Samia Suluhu Hassan na Emmanuel Nchimbi watafanikiwa kushinda, basi kutakua na sura mpya ndani ya Serikali yao. Mabadiliko ya kwanza itakua kwenye Baraza la Mawaziri. Ninaamini kutakua na sura mpya nyingi ndani ya Baraza la Mawaziri na hiyo ndio itakua kiashiria cha kwanza cha kundi gani lina ushawishi ndani ya chama.
SOMA ZAIDI: Miaka 45 ya CCM: Mapungufu Makuu ya Chama Hicho Tawala Tanzania
Kilicho wazi ni kwamba, matokeo ya Mkutano Mkuu, hasa uteuzi wa Emmanuel Nchimbi kama mgombea mwenza, yameleta mabadiliko makubwa katika siasa za ndani ya chama. Katika siku zijazo, kutakuwa na shauku kubwa kwetu sisi wafuatiliaji wa siasa ya kuona ni makundi gani yamepata nguvu na ambayo ushawishi wake umeathirika au kupotea kabisa.
Japo ajabu moja ya siasa za Tanzania, hatujawahi kuwa na waziri mkuu, au makamu wa rais, aliyefanikiwa kuja kuwa rais wa nchi. Kwa upande wa umakamu wa rais, ni kwa sababu ya muundo wenyewe wa nafasi hiyo ambapo kwetu sisi haina mamlaka ya moja kwa moja ya kiutendaji wa Serikali.
Lakini kama kuna mtu kwenye siasa za Tanzania ambae anaweza badili hali hiyo ya kihistoria basi mmoja wapo ni Emmanuel Nchimbi kwa sababu anajulikana kama mmoja wa wanasiasa wenye uwezo mkubwa wa kupanga mikakati ya kisiasa.
Kwa majina mengine ambayo yatakuwa yakijipanga kwa ajili ya mwaka 2030, ni dhahiri kwamba watajikuta wakikabiliana na mshindani mkubwa atakayekuwa na cheo kinachompa fursa kubwa ya kujidhatiti kwa ajili ya kinyang’anyiro hicho. Sina shaka kwamba kwa sasa yapo makundi ya 2030 ambayo yameanza kutafakari upya mikakati yao ya miaka mitano ijayo.
Hata hivyo, si ndani ya CCM pekee, bali pia ni muhimu kuangalia jinsi uteuzi wa Emmanuel Nchimbi utakavyoathiri siasa za nje ya CCM. Ukizingatia aina ya siasa ambazo amekuwa akizifanya kama Katibu Mkuu wa CCM, naweza kusema Emmanuel Nchimbi ni mwanasiasa ambaye si mhafidhina, anayependelea siasa za ushindani zaidi kuliko siasa za kurushiana maneno.
Hivyo, itakuwa vyema kuona kama atafanikiwa kuwa Makamu wa Rais, jinsi Serikali itakavyounda mahusiano na vyama vya upinzani na makundi mengine ya kijamii.
Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au X kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.