The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Wadau Wamshukia Makalla Kwa Madai Yake Kuwa CHADEMA inapanga Kusambaza Virusi vya Ebola Kuzuia Uchaguzi: ‘Maneno ya Hovyo’

Amos Makalla, Katibu wa Itikadi, Uenezi, na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yuko matatani kwa kudai kwamba chama cha upinzani, CHADEMA, kinakusanya fedha ili ‘kikanunue’ virusi vya Mpox na Ebola kwa ajili ya shambulio la kibaiolojia ili kuvuruga uchaguzi nchini.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi, na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amekosolewa vikali baada ya kudai kwamba chama cha upinzani cha CHADEMA kinakusanya fedha ili ‘kikanunue’ virusi vya Mpox na Ebola kwa ajili ya shambulio la kibaiolojia ili kuvuruga uchaguzi nchini.

Kauli hiyo aliitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Simiyu, Jumamosi ya Machi 22, 2025, ambapo ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuibua hisia kali miongoni mwa wafuatilia wa siasa za upinzani hapa nchini.

“CHADEMA wanakusanya fedha kwa kisingizio cha kuandaa umma ili wakatae uchaguzi, ili wasimamishe uchaguzi,” alisema Makalla. Lakini kuna ajenda ya siri, hawa watu, na hasa viongozi waandamizi ambao familia zao hazipo Tanzania, wanataka kutumia michango inayochangishwa ya tone tone eti ikifika wakati wakanunue virusi vya Ebola na Mpox, ili wavilete visambae Tanzania na uchaguzi usifanyike.”

“Huu ni mpango wa siri ambao wanauratibu, na kwamba huko wanakopita au wanachofanya ni kukusanya pesa, wameshakutana na watu, wanunue hivyo virusi, eti ikifika wakati wa uchaguzi, miezi ikikaribia, sisi hapa tuugue Ebola na Mpox hapa Tanzania. tayari wamekutana na baadhi ya watu, na harambee wanayoifanya inalenga kupata virusi hivi.”

“Hili ni jambo hatari sana. Ninyi mnaochangia tone tone mnachangia ununuzi wa virusi vya Ebola ili viletwe Tanzania,” Makalla alisisitiza.

Makalla alikuwa akielezea kuhusu kampeni ya tone tone ya CHADEMA iliyoanzishwa na chama hicho Februari 28, 2025, ikilenga kuhakikisha kuwa wanachama na wafuasi wa chama wanakifadhili, hasa katika ajenda yake ya ‘no reforms, no election.’ Kupitia ajenda hiyo CHADEMA inasisitiza kuwa itazuia uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 2025, kutokana na mazingira yasiyo ya haki ya uchaguzi na ukatili wa mara kwa mara dhidi ya wanachama wake.

CHADEMA, kupitia Makamu Mwenyekiti na Naibu Katibu Mkuu, imejibu madai ya Makalla katika  mkutano wa hadhara uliofanyka jijini Mbeya Jumapili, Machi 23, 2025.

“Amos Makalla umeongea maneno ya hovyo sana na anapaswa kuwajibika kwa maneno yako uliyoyasema. Aibu kwako. Tafakari juu ya haya na uyafute maneno yako ndani ya siku saba,” alisema Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.

“Amos Makalla anadai kwamba tunakwenda kununua virusi, lakini hajaambia Watanzania ni duka gani linauza virusi hivi na kwa bei gani ili tuwajulishe Shirika la Afya Duniani (WHO) wakaviangamize kule vinakouzwa. Haya yanaitwa mashambulizi ya kibaiolojia, yeye ni mhujumu uchumi,” alisema John Heche, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.

Aliendelea kusema, “huyu ni mtu mjinga na chama cha aina hiyo kimejaa watu wa hovyo wanaofikiri Watanzania hawawezi kufikiri. Gazeti la serikali, Habari Leo, limetangaza habari hiyo. Nakuomba wewe Mheshimiwa Mwenyekiti, uwaagize wanasheria wetu wawafungulie kesi hawa watu.”

Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amesema chama kitamwandikia rasmi Msajili wa Vyama ili achukue hatua kutokana na kauli hiyo.

“Ili kuweka mambo sawa, ACT Wazalendo kitamwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa, kikitaka hatua ichukuliwe kulingana na Sheria ya Vyama vya Siasa kuhusiana na kauli ya uongo na kifashisti aliyoitoa Katibu wa Uenezi wa CCM, Amos Makalla, dhidi ya CHADEMA,” alisema Shaibu.

“Kauli hii siyo tu shambulio dhidi ya CHADEMA bali pia ni shambulio dhidi ya demokrasia na taifa. Ni kauli ya kizembe ambayo haipaswi kuvumiliwa,” aliongeza.

Kauli hiyo imeibua mjadala mkubwa mtandaoni, ambapo watu wengi wameendelea kumkosoa vikali Makalla.  “Kuna tatizo kubwa Tanzania. Maswali kwa Makalla; Nani anafuga virusi vya EBOLA? Na huyu mtu yuko nchi gani? Anaviuza kwa bei gani? Kwa nini Serikali haijaijulisha WHO? Makalla ni msomi na kiongozi. Kudai CHADEMA wanapanga shambulio la kibaiolojia dhidi ya Watanzania bila ushahidi siyo siasa,” aliandika kwenye ukurasa wake binafsi wa mtandao wa X mwanasheria, Fatma Karume.

Kufuatia maoni makali mtandaoni, gazeti la Serikali la Habari Leo, liliiondoa habari hiyo kutoka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Tumeamua kuiondoa kutokana na kutokuwepo kwa majibu kutoka upande wa pili pamoja na maoni na wasiwasi uliotolewa na baadhi ya watazamaji wetu,” ilisema taarifa iliyotolewa na gazeti hilo jana Jumapili. Mwandishi mashuhuri, Absalomu Kibanda ametoa wito kwa Makalla kuwajibika badala ya vyombo vya habari vilivyosambaza taarifa hiyo.

“Makosa yafanywe na Katibu wa Uenezi na Mafunzo wa CCM,halafu vyombo vya habari ndiyo vibebe mzigo wa lawama?,” ameuliza Kibanda kwenye andiko lake X. “Huku ni kuingilia uhuru wa habari kwa gharama za kukwepa uwajibikaji wa viongozi wa umma. CPA Makalla awajibike kwa kauli yake,” aliongeza Kibanda.

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) kimeorodhesha virusi vya ‘Smallpox’ na Ebola kama kundi A la vimelea vinavyoweza kutumika katika mashambulio kibaiolojia. Sababu kubwa inayotajwa juu ya vimelea hivi ni kwa sababu vinaweza kusambazwa kwa urahisi au kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Husababisha viwango vya juu vya vifo na vina uwezo wa kuwa na athari kubwa kwa afya ya umma. Lakini pia, vinaweza kuzua taharuki na kuondoa utulivu.

Mpaka sasa Serikali ya Tanzania haijatoa tamko kuhusiana na kauli iliyotolewa Mwenezi wa CCM. Makala kwa sasa anaendelea na mikutano ya hadhara kuandaa wanachama na wafuasi wa CCM kwa ajili ya uchaguzi ujao.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×