The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

TFF Wagombane na Simba, Yanga Katika Maendeleo, Siyo Kutuhumiana Kuhusu Hujuma

TFF inahitaji kujikita kwenye kuendesha programu za watoto na vijana badala ya kujihusisha na Ligi Kuu ambayo haiishi vitimbi kutoka klabu kongwe za Simba na Yanga.

subscribe to our newsletter!

Kwa mtu anayefuatilia safu hii, au mahojiano yangu na vyombo vya habari, au kutazama vipindi vya Ndani ya Michezo vinavyorushwa na Dimbani Konekti, atakuwa anakutana mara kwa mara na hoja yangu ya soka la watoto na vijana.

Soka la vijana wa umri huo ndio mkombozi wa nchi yoyote duniani inayotaka kupiga hatua ya maendeleo katika mchezo huo maarufu duniani.

Katika soka la kisasa, hakuna nchi iliyowahi kutwaa Kombe la Dunia bila ya kuwa na soka la watoto, au grassroot football kwa kimombo. Tulizoea kuona klabu za Barcelona na Real Madrid zikisumbua barani Ulaya na duniani, lakini nchi yao ya Hispania haikuwa na mafanikio yoyote hadi mwaka 2010 ilipotwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Hiyo ilikuja baada ya soka la watoto kukolea, huku klabu za Barcelona, inayomiliki shule ya mpira wa miguu ya La Macia, ikizalisha nyota kama Lionel Messi ambaye alichukuliwa Argentina akiwa mdogo, Xavi Hernandez and Andrea Iniesta waliotikisa dunia enzi zao, huku La Fabrica ya Real Madrid ikizalisha nyota kama Raul Gonzalez, Iker Casillas na Dani Carvahal. Ukiondoa Messi ambaye ni Muargentina, hawa walikuwemo kwenye kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini.

Hata wapenzi wa soka wa Hispania waliweza kuona kikosi chao cha miaka saba au nane iliyokuwa inakuja wakati huo, kwa ama kuona nyota hao wakicheza katika mashindano ya watoto, au kuwashuhudia katika ligi za vijana na baadaye kuanza kupewa nafasi katika vikosi vya kwanza vya klabu za ligi za juu.

SOMA ZAIDI: Sakata la Simba, Yanga na TFF: Ni Muhimu Serikali Ilinde Mashabiki Kisheria

Si ajabu kwa kizazi kama hicho kuanza kuchezea kikosi cha kwanza cha Barcelona, Real Madrid, Atletico Madrid au Celta vigo wakati vijana hao wakiwa na umri chini ya miaka 17, kama ilivyo kwa sasa kwa wachezaji kama Mbrazili Endrick aliyeanza kucheza klabu za daraja la juu nchini kwake akiwa chini ya miaka 17.

Muda mfupi baada ya msimu huu kumalizika, tutaanza kuona mashindano ya watoto wa Hispania na baadaye kutoka nchi mbalimbali duniani wakipambana katika La Liga FC Futures, mashindano ya watoto walio na umri chini ya miaka 12 yakiendeshwa na La Liga na taasisi ya Jose Ramon de la Morena.

Ni mashindano ambayo yanakupa picha halisi ya soka la Hispania linakoelekea katika muongo mmoja ujao na jinsi timu ya taifa  itakavyokuwa.

Kwa Hispania mashindano ya umri ni Juveniles, ambayo ni kwa ajili ya vijana wenye umri chini ya miaka 19,18 na 17, Cadetes (U16), Infants (U14), Alevines (U12) na Benjamines (U10).

Programu hizo pekee zinatosha kukupa picha ya kwa nini Hispania iko juu katika kuzalisha wachezaji nyota duniani na sasa kuwa tishio, ikiwa ndio bingwa mtetezi wa Kombe la Mataifa ya Ulaya.

READ MORE: Waliovurunda ‘Dabi ya Kariakoo’ Walazimishwe Kuomba Radhi Hadharani

Kuiga siyo vibaya

Kwa Tanzania, kuiga watu hawa si vibaya na kutafuta habari kuhusu mbinu za wenzetu kufikia hapo si mbaya hata kama Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) linaleta programu zake nyingi za kuendeleza vijana kama hii ya sasa ya Talent Development Scheme (TDS).

Pamoja na ukweli kuwa programu hiyo ya TDS inafadhiliwa na FIFA, ni muhimu kwa nchi kama yetu kuwa na njia nyingine ya kukuza mpira wetu kulingana na mazingira, utamaduni na uchumi wetu, kama ilivyo kwa Morocco ambayo imejenga shule za watoto katika kanda, huku wale bora kabisa wakichukuliwa kwenda shule ya shirikisho la soka la nchi, au centre of excellence kama wanavyoiita wenyewe.

Kwa sasa huwezi kuona hata timu ya taifa ya Tanzania ya miaka mitatu ijayo itakuwaje. Wapo wachezaji wanaoibuka ghafla wakiwa tayari katika umri mkubwa na hukuwahi kusikia habari zao wakati wadogo. 

Wachezaji kama Clement Mzize, Yusuf Kagoma, Ladack Chasambi, Ibrahim Bacca au Lameck Lawi wangeweza kuonekana wakiwa wadogo kabisa kama tungekuwa na programu hizo.

Na pengine wangekuwa na ujuzi zaidi ya huu walionao sasa kwa sababu programu kama za kambi zingewawezesha kukutana na wachezaji nyota wa Ligi Kuu wakati wakiwa wadogo pamoja na jopo la makocha bora wa viwango vya juu.

SOMA ZAIDI: Kwa Kuifokea Yanga, Karia Ameonesha Upande Kwenye Sakata Kati ya Klabu Hiyo na Simba

Wakati ule tulikuwa na mashindano ya Copa Coca Cola ambayo yalianzia katika ngazi ya wilaya hadi mkoa na yalianza kwa kushirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17, lakini kutokana na utamaduni wa viongozi na makocha wetu kutaka ushindi zaidi kuliko kufanikisha malengo ya programu wakawa wanachomeka vijana wenye umri mkubwa lakini maumbile madogo. 

Hiyo ilisababisha mashindano hayo yashushwe umri hadi chini ya miaka 15 ili hata kama kutakuwa na kughushi basi iwe katika miaka 17 na 18.

Pamoja na kwamba hayakufanyika kwa ufanisi mkubwa, mashindano yale yalizaa nyota kama Mohamed Hussein Tshabalala, Mudathir Yahya, Farid Mussa na Aishi Manula. 

Kutokuwa na ufanisi kulitokana na watoto kutokutana na makocha wenye mafunzo sahihi kwa kuwa mikoa mingi iliamini zaidi watu iliowafahamu kuliko wale waliopata mafunzo maalum.

Katika ngazi ya klabu za Ligi Kuu ndiko watoto hawa wanaweza kukutana na makocha wenye elimu sahihi na malezi yanayostahili. Huko, mara moja katika mwezi wanaweza kufanya mazoezi na nyota wanaowahusudu kama akina Pacome Zouzoua, Gibril Sillah, Jonathan Sowah, Kagoma, Nassor Saduuni, Mzize, Ellie Mpanzu na wengine wengi.

SOMA ZAIDI: Ni Kupoteza Muda Kujadili Kanuni Sakata la Simba, Yanga

Kazi ya TFF

Shirikisho la Soka (TFF) linahitaji kujikita huko na kama lina nia ya dhati, shughuli hizo za kuendesha programu za watoto na vijana zitawakamata hadi waone ni mzigo kujihusisha na Ligi Kuu ambayo haiishi vitimbi kutoka klabu kongwe za Simba na Yanga.

Watakachosalia nacho ni kuweka masharti kwa klabu hizo za madaraja ya juu kuwa ni lazima ziwe na shule za watoto ili zipate leseni ya kushiriki Ligi Kuu na shule hizo zitaandaliwa mashindano mwishoni mwa msimu.

Kulazimishwa kuwa na shule hizo, au kukataa masharti kama hayo, ni mzozo ambao tungetarajia kuuona baina ya TFF na klabu, hasa za Simba na Yanga, na si katika mambo kama kubadili muda wa mchezo kuanza au kuahirisha mechi kama ilivyokuwa hivi karibuni.

Tunahitaji kuona TFF ikikorofishana na klabu katika mambo ya msingi ya maendeleo na si kutuhumiana kuhusu hujuma.Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×