Katika mizani ya kisiasa, miaka 10 ya mwanzo ya chama cha siasa ni miaka ya utoto na ukinda. Miaka 10 ya mwanzo ni miaka ya ujenzi wa chama. Katika kipindi hiki, na katika mazingira ya kisiasa na kiutawala kama ya kwetu, ni hali ya kawaida na “kimkakati,” katika miaka ya mwanzo, chama kujiendesha na kujishughulisha kwa tahadhari.
Tahadhari hii ni dhidi ya wajasiria-siasa, uhasama na propaganda zinazoendeshwa na vyama vingine pamoja na dhulma ya dola. Katika kipindi hiki, msisitizo mkubwa wa chama ambacho kina matumaini makubwa ya kukua na kutandaa nchini kote ni kujiendesha kwa tahadhari ya kutokuteketezwa.
Kutokuteketezwa na siasa za ndani; kutokuteketezwa kwa mitazamo na propaganda zinazoendeshwa na vyama vingine vya siasa ambavyo hukiona chama kipya kama adui au mhasimu; na kutokuteketezwa na dola na vyombo vyake ambavyo havifurahishwi na utamaduni na desturi ya kidemokrasia.
Ikiwa mazingira ya kuanzishwa kwa chama cha ACT Wazalendo yametokana na uasi na minyukano ya ndani ya CHADEMA, miongoni mwa wanachama na baadhi ya viongozi waandamizi; hivyo si ajabu uhasama na ukinzani mkali dhidi ya ACT Wazalendo kutoka kwa CHADEMA na wanachama na wafuasi wake. Bila shaka upinzani, au ukinzani, huo umekuwa ukijielekeza – ama kwa dhahiri au siri – kuhakikisha kudumaa, kushindwa au kutokomea kwa ACT Wazalendo.
Wakati adui wa kwanza akidhihirisha dhahiri uhasama wake, ACT walibaki kujitathmini namna gani itashughulika na maadui wawili waliobaki – Dola na Siasa za Kitaasisi. Licha ya kwamba adui wa ndani, yaani siasa za kitaasisi, kuwa ni adui hatari, adui huyu, hata hivyo, hazingatiwi sana nje na kwenye kadamnasi ya siasa; hivyo, ndio maana, pamoja na ACT kuweza kushughulika na kuhakikisha kuwepo kwa hali ya utulivu na mshikamano miongoni mwa wanachama na viongozi, hili sio jambo ambalo linatumika kukipamba chama hicho.
SOMA ZAIDI: Hatimaye ACT-Wazalendo Wanatoka Mafichoni?
Sasa, adui aliyebaki kumuangazia katika hali na hatua hii ni adui Dola! Kuangazia mahusiano kati ya adui Dola na ACT ni muhimu kuzingatia na kutafakari miaka 11 iliyopita ya kisiasa.
Miaka hii 11 imekuwa, kwa lugha nyepesi na isiyo na kona kona, miaka ya kuzikwa kwa haki na kutanda kwa giza la demokrasia. Katika miaka hii, dola limejiendesha kwa mabavu yasiyoelezeka. Miaka hii 11 imekuwa ni miaka ya hadaa ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Hivyo si ajabu, kutokana na mazingira haya na uchambuzi wangu kwamba ACT katika miaka yake ya mwanzo, ilikuwa na jukumu la kuamua ama kulikabili dola kimzobe mzobe au kuikabili dola kikobe kobe.
ACT walikuwa na chaguo la kufanya ama siasa za masuala au siasa za misala. Ili kukabiliana na ufedhuli mkubwa wa dola na kuilinda azma yao ya kubaki kuwa chama hai, ACT wakaamua, wala sio kulazimika, kuchagua siasa za masuala; na vivyo hivyo chama kikajinasibu kama chama cha masuala.
Maridhiano hadi mapambano
Katika tathmini ya Chama baada ya madhila ya Uchaguzi, au Uchafuzi, wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, ACT Wazalendo walifanya tathmini ya kwamba Miaka 10 ya kuongozwa na mtazamo na muenendo wa maridhiano umetosha. Dhulma iliyofanyika katika chaguzi, au chafuzi, za 2019, 2020 na 2024 zilikuwa ni kielelezo tosha kuwa chama hakiwezi tena kujihusisha na siasa za maridhiano.
SOMA ZAIDI: Kwetu Sisi ACT Wazalendo, Mahakama ni Ulingo Mwingine wa Mapambano, Tutaitumia Ipasavyo
Tathmini ya Chama ilibaini kwamba ACT haiwezi kuendelea kuridhiana na “mhuni” Dola. Tathmini hii ilisisitiza kwamba hamna sababu yeyote ya kuendelea kuwa na mahusiano ya heri na “mhuni” Dola. Tathmini ilibaini kwamba hivi sasa chama kimefanikiwa kukua na kujenga misingi inayojiridhisha, na hivyo haihataji fadhila ya dola ili kuweza kubaki kuwa hai na kujijenga.
Tathmini ya chama ilitamka kwamba, kutokana na mazingira, au muktadha wa kisiasa, tunayo kazi moja tu – Kupambana! Maamuzi haya ya kimapambano yamekitaka chama kukacha siasa za “maridhiano.” Chama kimetamka kwamba, “Sababu za kupambana tunazo; nia ya kupambana tunayo; na uwezo wa kupambana tunao!”
Sababu ya kupambana ni kutokana na CCM kuwa sikio la kufa dhidi ya madai ya wananchi na kupuuza na kupora misingi ya haki na demokrasia. Nia ya kupambana ni kulikomboa taifa dhidi ya uozo wa kiuongozi, kisera, kiprogramu na kiutendaji wa CCM.
Uwezo wa kupambana unatokana na uimara wa mitandao ya chama na uwepo wa azma ya kweli na misingi ya mshikamano wa watu na wadau katika jamii, waliochoshwa kufukarishwa, kufedheheshwa, kunyonywa, kukandamizwa na kubezwa na CCM.
Tumjue adui yetu
Desturi ya Mapambano ni kufanya kila namna; kutumia silaha zako zote kushinda. Utaratibu wa Mapambano ni kuunganisha nguvu dhidi ya adui na kumbana katika kila pembe ili kutokumpa nafasi ya kupumua na kukushinda. Silaha ya kimapambano ni dhamira ya kweli na watu imara.
Mbinu ya kimapambano ni kujiamini na kutobabaika. Msingi wa kimapambano ni kumjua adui yako. Na kwa hatua ya sasa, sharti tumjue na tukubaliane kwamba adui wetu ni CCM na mfumo kichefuchefu uliowekwa na unaolelewa na CCM.
SOMA ZAIDI: Dorothy Semu: Kwa nini ACT-Wazalendo Tumeandaa Ilani ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa?
Sharti tutambue kwamba, Mapambano haya si ya ACT pekee. ACT, wala yeyote yule, sio mmiliki, wala muasisi, wa Mapambano haya, haya ni Mapambano yetu, ni Mapambano ya UMMA! Ni Mapambano ya kujinusuru na kurejesha thamani ya utu wetu.
Katika kuadhimisha Miaka 11 ya ACT Wazalendo, ninawatakia Watanzania wote wenye nia njema na nchi yetu Mapambano mema. Ninasisitiza kwamba, uchaguzi ni sehemu ya mapambano na kushiriki uchaguzi ni kupambana.
Tupambane!
Jasper “Kido” Sabuni ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na mwanachama wa chama cha ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia kidojasper@gmail.com au X kama @JasperKido. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.