Sijui kwa nini nakumbuka masomo yangu ya historia leo, lakini labda mtanisaidia maana kuna mengi sana ya kujifunza katika historia. Somo hili linamhusu mfalme na askofu.
Kwa kifupi, Thomas Becket alikuwa rafiki mwandani sana wa Mfalme Henry II huko Uingereza katika karne ya 12. Walikuwa marafiki sana kiasi kwamba Mfalme akamteua Becket ‘Kansela,’ cheo ambacho nadhani kinafanana na waziri au mshauri mkuu wa mfalme, na baadaye akamteua Askofu wa Canterbury, yaani Askofu Mkuu.
Wafalme Bwana! Becket wala hakuwa padre. Ikabidi asimikwe kama padre haraka sana, lakini kabla ya hapo, Becket alimwonya Mfalme kwamba urafiki wao utabadilika maana sasa angewajibika kwanza kwa Kanisa. Henry akapuuza, akijua kwamba sasa atakuwa na askofu chawa ambaye atamsaidia kufanya apendavyo. Hivyo, Becket alisimikwa na kuanza kazi kama Askofu.
Askofu Thomas Becket sasa alianza kutenda kama alivyomtahadharisha Mfalme. Kwa maneno yake mwenyewe, alibadilika. “Badala ya kuwa mfadhili wa waigizaji na mwindaji wa wanyama, akageuka kuwa mchungaji wa roho za watu,” inasimuliwa.
Becket akaanza kuishi kama maskini na kutoa sadaka nyingi kwa walio maskini. Aidha, alijitoa kama Mshauri Mkuu wa Mfalme na kuanza kupingana naye kuhusu mwenendo wake wa madhambi, kodi zake za kupitiliza na uhuru na haki za Kanisa.
SOMA ZAIDI: Kuna Uchaguzi, Uteuzi na Uchafuzi. Hapa Tanzania Tuna Nini?
Mwishoni alilazimika kukimbia nchi na kuishi uhamishoni, lakini baada ya Papa – maana enzi zile Waingereza bado walikuwa Wakatolii – kumtishia. Henry alisalimu amri na Becket alirudi Canterbury na kupokelewa kwa shangwe. Lakini alipoendelea kutetea maskini na Kanisa, Mfalme alikasirika kupita kiasi na kutamka mbele ya watu: “Nani ataniondolea padre huyu mkorofi?”
Becket auwawa
Basi wafuasi wake wanne waliomsikiliza walisafiri na farasi wao hadi Canterbury walipomkuta Becket akiwa kanisani. Baada ya mabishano mengi na kujaribu kumvuta nje ya Kanisa, walifanya kufuru si tu ya kumuua, bali pia ya kumuua ndani ya Kanisa lake, wakiamini kwamba wanatekeleza matakwa ya mfalme wao, kiongozi wao.
Ukatili huu ulishtua Ulaya mzima, au tuseme eneo lote la Ukristo la wakati ule, na mwisho Becket alitangazwa kama Mtakatifu. Kinyume chake, Mfalme Henry, pamoja na hadhi zake zote za ufalme, alilazimika kutubu hadharani mbele ya kaburi la Becket.
Alipigwa mijeledi na watawa na kushinda na kukesha akisali pale. Aidha, alilazimika kukubali kwamba Kanisa lilikuwa na uhuru wake ambao haupaswi kuingiliwa na dola. Hata Mfalme ambaye aliaminika enzi zile kuwa ni chaguo la Mungu alipaswa kutambua mipaka yake, sembuse kiongozi wa kidemokrasia wa siku hizi ili mradi halivunji sheria za haki, na ukosoaji daima si kuvunja sheria.
Kwa kweli, historia hii imenigusa tangu nikiwa mtoto, kwa sababu nyingi.
SOMA ZAIDI: Kama Sera ya Matibabu Bure Haitekelezeki, Basi Serikali Iache Kudanganya Wananchi
Moja ni kwamba ukipewa jukumu la kuongoza taasisi, ni jukumu lako kulinda taasisi ile. Kama huko tayari kufanya hivi, bora ukatae kazi. Becket alimtahadharisha Mfalme kwamba atafanya hivyo, na Mfalme akapuuza. Sasa, naona mara nyingi siku hizi ni kinyume chake.
Watu wanapuuza taasisi wanazopewa, iwe ni mahakama, vyombo vya habari, asasi za kiraia, mashirika ya umma, na kadhalika. Kule kwenye taasisi wanayohamia, wanapuuza misingi yake, historia yake, misimamo yake, na kuendelea kutumikia ‘mfalme.’ Ndiyo maana taasisi zinapoteza hadhi na imani ya watu.
Na taasisi zikipoteza imani ya wananchi, si tu uhuru na haki vitapotea bali hata amani itapotea maana mfalme atazidi kuvimba kichwa na kutawala peke yake. Hii haiondoi ukweli kwamba ukiamua kusimamia taasisi yako, inahatarisha maisha yako, lakini hatimaye inaimarisha hadhi yako na kupendwa kwako na wananchi.
Nguvu ya maneno
Pili, ingawa sikubaliani sana na msemo kwamba kalamu ina nguvu kuliko panga, bado maneno yana nguvu sana. Ndiyo maana ukiwa kiongozi, hata kiongozi wa ngazi ya chini, chunga sana mdomo wako. Mfalme alitamka maneno yake ya “Nani ataniondolea huyu padre mkorofi?” akiwa na hasira sana.
Yawezekana wala hakumaanisha kwamba alitaka yule auawe, lakini maneno yake yalitosha kuwatuma watu wenye nia ovu, au watu wachawa wa enzi zile kumuua mtu. Hali hii imeonekana sehemu nyingi duniani na daima mwisho wake si mzuri.
SOMA ZAIDI: Kinachoendelea CHADEMA ni Matokeo ya Mkinzano wa Kitabaka Ulioshindwa Kutatuliwa Tangu Kuanzishwa Kwake
Watu wanatekwa, wanatoweka, wanakutwa wameuawa, na ingawa wako wengi wanaopenda kuwa kama Pilato na kunawa mikono, damu ile haitoki. Wale waliomsoma mwandishi wa Kiingereza, William Shakespeare, japo kidogo tu, watamkumbuka Lady Macbeth ambaye alimshinikiza mume wake aue ili awe mfalme, mwisho akawehuka, akinawa mikono tena na tena na tena lakini alama ya damu ikabaki palepale mawazoni mwake.
Tukiwa viongozi, ni muhimu sana tukajihadhari na maneno na maneno tunayotoa, hasa kwa wale walio chini yetu, na hasa tukiwa na hasira. Bora kunywa maji kwanza!
Njia nyingi ya matumizi ya hatari ya maneno ni kuwadhalilisha watu, au kusema uongo juu yao. Wanazi huko Ujerumani waliwaita Wayahudi “panya” au “wadudu” ili kuwaondolea utu wao, ubinadamu wao. Si hawa ni panya tu, kuna shida gani kuwaua?
Vivyohivyo huko Rwanda, Watutsi waliitwa “mende.” Ukiona mende, kanyaga. Baada ya hapa ilikuwa rahisi kuwakubalisha watu kuwaua. Huko Marekani, sasa hivi, ili kuwafukuza watu, Rais Donald Trump anadai kwamba wote ni “wabakaji,” “wahalifu,” na majina mengine mabaya kabisa.
Pia, tusisahau kwamba wakoloni kila mahali waliwaita wenyeji waliowakuta kuwa ni savages, au watu makatili wasio na hata chembe ya utu ili kuhalalisha kuwaua, kuwatawala kwa mabavu, na kuwanyonya. Hadi leo, Mazionisti wanawaita Wapalestina human-animals, au binadamu-wanyamana na majani ya kufyekwa, ili kuhalalisha mauaji ya kimbari dhidi yao.
SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’
Aidha, kutumia maneno ya uongo kabisa dhidi ya kundi lingine, ikiwemo kudai eti wote ni “mashoga” au wamedhamiria kuleta magonjwa makusudi nchini, na shutuma nyingine nzito nzito, kunahalalisha matumizi ya nguvu na ukatili mwingine dhidi yao au watu wanashabihiana nao, maana wameshafanywa ni tishio kwa taifa tayari.
Hayo yote, katika nchi ya kidemokrasia, hayatakiwi. Sisemi kwamba hayatumiki. Yanatumika, lakini kwa misingi ya ubuntu, yaani nipo kwa sababu mpo, kwa misingi ya taifa letu la ujamaa, hayatakiwi kutumika. Ndiyo maana wanaoyatumia hupoteza imani ya watu.
Wananchi wanaweza kunyamazishwa kwa uoga wao, lakini wanakereka sana. Na wakisimama watu kupinga mambo hayo, wanashangiliwa kama Becket alivyoshangiliwa. Baada ya mauaji yale, hata Mfalme mwenyewe alilazimika kwenda kutubu na kupewa adhabu ili kurudisha uhalali wake.
Pointi yangu ya tatu inahusiana na umuhimu wa kuheshimu taasisi nyingine, hata kama wana mawazo tofauti na mawazo yako na ya mfumo wako. Nchi yenye haki na amani hutegemea maelewano kati ya taasisi muhimu mbalimbali, ambayo ni pamoja na kukubaliana kutokubaliana, na kushinda kwa nguvu ya hoja na si kwa hoja ya nguvu, au hata nguvu bila hoja kabisa.
Yawezekana Henry alifanya mengine mengi mazuri, lakini historia inamkumbuka kama muuaji wa Becket tu.
Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.