The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Ziara ya Siku 15 Mikoa Kadhaa ya Tanzania Imenidhihirishia Ukweli Mmoja Mchungu: CCM Imechoka, Hatuna Budi Kuichoka

Umasikini na ufukara ulioenea nchi nzima, ukipoka wananchi utu na heshima zao, unatwambia kitu kimoja tu: CCM haiwezi kutatua tatizo ililolisababisha.

subscribe to our newsletter!

Mwezi Julai 2025, nilifanikiwa kuwa sehemu ya ziara ya kisiasa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Lindi pamoja na Pwani. 

Ziara hii ilikuwa ni sehemu ya ziara kuu ya chama cha ACT Wazalendo, iliyopewa jina Operesheni Majimaji, iliyolenga kuzunguka nchi nzima kuamsha ari ya kisiasa na kuhamasisha na kuhakikisha tunarejesha thamani ya kura, kupitia kampeni ya Oktoba #LindaKura.

Katika ziara hii nilipata wasaa wa kuijua zaidi nchi yetu na kutathmini hali za Watanzania. Mikoa tisa niliyozuru na kukutana na viongozi na wananchi wake, ilinidhihirishia dhahiri kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimechoka na matokeo yake kimewachosha Watanzania. 

Ziara hii ya Operesheni Majimaji imenifungua macho zaidi kuona ni kwa nini tunapaswa kujidhatiti na kushiriki kikamilifu, kuhakikisha tunaikomboa nchi yetu kutoka kwenye uongozi butu, dhaifu, badhilifu na usio na tija, wa chama tawala CCM.

Kwa macho yangu, nimeshuhudia machozi ya wanawake wakilia na kuomboleza kutokana na huduma za kiafya zinazotweza utu wao; nimeshuhudia jasho la vijana likinyonywa na kudhulumiwa kwa sera na utaratibu mbovu wa CCM unaowafukarisha Watanzania; na nimeshuhudia damu ya Watanzania ikimwagika kutokana na unyanyasaji na ukandamizaji wa haki.

Nimeizunguka nchi yangu kwa uchungu mkubwa. Nimewakuta Watanzania wenzangu wakiwa ni wenye kukata tamaa. Nimesikitishwa na umasikini nilioushuhudia. Nimefadhaishwa na gharama kubwa na huduma mbovu za afya. Nimekasirishwa na mipango duni ya kuinusuru elimu na kutokomeza ujinga.

Huduma za afya

Kote tulipopita tumekuta vilio vinavyofanana katika huduma za afya. Wananchi katika mikoa ya Katavi, Rukwa (Nkasi Kaskazini), Mbeya (Rungwe) na Ruvuma (Songea Mjini), wanaulalamikia mfuko wa bima ya afya. 

SOMA ZAIDI: Serikali Imeshindwa Vita Dhidi ya Umasikini. Imeamua Kutangaza Vita Dhidi ya Masikini 

Wananchi wamesisitiza kwamba, Serikali imekuwa ikiwarubuni kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa ahadi kwamba utawahakikishia kupata matibabu bure, pasipo kulazimishwa kulipia tena. 

Hata hivyo, kote tulipopita wananchi wamesisitiza, licha ya kujiunga na mfumo wa bima ya afya, mfuko huo hauwanusuru kwa vyovyote vile na gharama kubwa za matibabu; na badala yake mfumo huo unawalipisha huduma za afya mara tatu.

“Sisi tunalipa kodi kama wenzetu,” mwananchi mmoja alinieleza kwa uchungu. “Tunaambiwa, na tunajua, sehemu ya malipo ya kodi zetu ni kwa ajili ya huduma za afya. Hapo hapo Serikali inakuja na inatulazimisha kukata bima. Tumejikusanya wee… tumetii. 

“Tumekata bima. Ila hizo bima sasa, ukifika tu, kufungua faili tunalipia [Shilingi 3,000], bado kumuona daktari, vipimo, kote huku kunahitaji malipo na ukifika kwenye dawa ndio kabisaaa… hata panado, tunanunua. Hii bima, bima gani ninyi viongozi mtuambie, ambayo sisi tunalazimishwa kulipia mara tatu kama dozi?”

Wananchi wanalia na gharama kubwa za huduma za afya. Kote tulikopita wananchi wamelalamika kwamba hamna madawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali. Hivyo basi, wananchi wanalazimishwa kununua dawa katika maduka binafsi, ambayo mengi yao ni ya watumishi hao hao wa afya; huko napo gharama za madawa ziko juu. 

Pamoja na dawa, wananchi wanakabiliwa na gharama za vitendea kazi kama mipira, nyembe, glovu, na kadhalika, ambavyo wanahitajika kununua kutokana na kukosekana katika zahanati na vituo vya afya.

Wakati nchini kote wananchi wakikabiliana na changamoto hizi katika sekta ya afya, Ripoti ya Mwaka 2023/24 ya Ukaguzi wa TAMISEMI imeainisha upotevu mkubwa wa fedha katika sekta ya afya. Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alibaini upotevu wa zaidi ya Shilingi bilioni 28.12 kutokana na ubadhirifu mkubwa na usimamizi mbovu katika sekta hiyo. 

SOMA ZAIDI: Mazungumzo na Mchimbaji Mdogo wa Madini Kigoma, Tanzania: ‘Bado Hatujatambuliwa Ipasavyo’ 

Katika kiasi hicho kilichopotea, CAG anaeleza kwamba, takribani Shilingi bilioni tano za fedha zilizotengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba zilielekezwa kwa matumizi mwengine. Pamoja na hayo, takribani Shilingi bilioni 18 zilizotengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba hazijatumika na havijatolewa katika bohari ya dawa. Yote haya yanatokea huku wananchi wakiendelea kulia na mateso katika huduma za afya.

Ubadhirifu na upotevu huu wa mali za umma unadhihirisha ni kwa namna gani CCM haishughulishwi wala haiumizwi na machozi ya wananchi katika sekta ya afya. CCM haiumizwi na machozi ya kina mama wanaokabiliana na gharama za uzazi, ambapo mpaka kujifungua wanajikuta wanatumia zaidi ya laki tano kwa ajili ya matibabu tu. 

CCM haihuzunishwi na machozi ya watoto ndio maana imeizika sera ya Toto Afya na badala yake imepitisha muswada wa kulipa mafao wenza wa viongozi wanaonufaika na mamilioni ya fedha za wenza wao; CCM haiumizwi na machozi ya wazee wanaotozwa gharama za matibabu licha ya kujitoa kwa hali na mali katika ujenzi wa taifa letu.

CCM hii imechoka kweli kweli! Haioni aibu, inauza damu; inauza hewa; inauza watoto; na hivi sasa, bila soni, haijali machozi ya wanafamilia wenye majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao, inauza hadi maiti.

Ajira 

Katika ziara yetu, tumeshuhudia ukubwa wa tatizo la ajira nchini. Tumeshuhudia kwa macho yetu uhalisia wa takwimu za Serikali zinazoeleza katika taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa Katika Mwaka 2024, kwamba idadi ya nguvu kazi nchini ni zaidi ya watu milioni 36, hata hivyo ni watu milioni 3.6, sawa na asilimia 10 tu ndio wenye ajira.

Kwa sehemu kubwa, ziara yetu imetukutanisha na sehemu ya Watanzania wanaoangukia kwenye kundi la watu wa zaidi ya milioni 32 ambao hawana ajira kabisa au wako kwenye ajira zisizo rasmi na zisizo na staha. 

Tumeshuhudia namna gani wananchi hawa, wengi wao wakiwa vijana, wakiwa wamechoka, wamechoka wamechakaa (kama alivyoimba msanii 20 Percent). Vijana na Watanzania wenzetu hawajichokei tu kwa kupenda au kwa kudra, hapana, wamechoshwa na Serikali ya CCM; na matokeo yake, udhalili wa maisha ya watu nchini unaonekana dhahiri; uonekana mchana kweupe; unaonekana katika nyuso zao; ugumu wa maisha yao haujifichi hata thumni.

SOMA ZAIDI: Tumezungumza na Vijana Kumi Waliojiajiri Kupata Uzoefu Wao. Hiki Hapa Ndicho Walichotuambia 

Licha ya kutelekezwa na CCM, vijana na Watanzania kwa ujumla hawajabweteka na kujikalia tu kusubiri umauti uwakute. Watanzania wameamua kupambana, kujiajiri, kujishughulisha kwa namna tofauti tofauti katika kujipatia kipato. 

Wameamua kuvuja jasho, wameamua kuchumia juani; hata hivyo, hili nalo Serikali ya CCM haipendezewi nalo. Serikali ya CCM imeamua kuwazonga vijana na Watanzania hawa wakiwa juani wakijitafutia riziki; na vivyo hivyo, imekuwa mwiba kwa Watanzania hawa wakiwa kivulini wakijilia riziki yao.

Wazalishaji wadogo

Tumepita Mtwara na Lindi na kukutana na wananchi wakilalamika kuhusu soko na malipo ya zao lao la korosho. 

Pamoja na Serikali ya CCM kutangaza kwamba bei ya korosho itakuwa Shilingi 4,000 kwa kilo, wananchi katika mikoa hiyo miwili wameishia kulipwa kati ya Shilingi 800 hadi 1,500; huku asilimia kubwa kati ya hao wakiwa hawajalipwa madai yao kwa hadi miezi mitatu na zaidi. Huu ni unyonyaji na ukandamizaji usiokubalika.

Tumekutana na wananchi wa Songea waliokatazwa kusafarisha mahindi yao nje ya wilaya yao katika kutafuta masoko. Tumekutana na wananchi wa Rungwe waliokatazwa kuvuna chai. 

Tumekutana na wavuvi wanaolalamikia Ziwa Tanganyika kufungwa kwa hadi miezi sita, huku Serikali ikilifungua kipindi hiki ili tu kupisha uchaguzi. Tumekutana na wananchi Rukwa na Katavi wanaotozwa ushuru wa hata gunia moja ambalo mtu analitoa shambani kwake na kulipeleka nyumbani kama chakula.

“Mimi, mimi binafsi, nimewahi kukimbizwa na hawa maafisa wa Serikali kwa kuwa nimepita barrier na gunia langu moja bila kulipa ushuru,” mwananchi mmoja alinieleza. “Inashangaza sana, yani gari ya milioni 200 imenikimbiza kwa ajili ya gunia la 80,000. Haya ndio maisha yetu sisi huku vijijini.”

SOMA ZAIDI: Kila Wakati Ambapo Watu Walisimama Pamoja Kutetea Maslahi Yao, Walifanikiwa 

Kwa upande mwingine, tumekutana na malalamiko makubwa ya vijana na wanawake kukosa mitaji ya kuanzisha biashara na kufanya shughuli za kilimo. Wananchi hawa wameeleza kwamba kutokana na hali zao duni ndio maana wengine wanajikuta wakichukua mikopo ya kausha damu

Miko ya halmashauri

Wakati huohuo, wanalalamikia kuhusu upatikanaji wa mikopo ya halmashauri umekuwa ni changamoto kubwa, kwani kigezo kikubwa mtu anapaswa kuwa mwanachama wa CCM na vivyo hivyo, ili kupewa mikopo hiyo lazima uweze kutoa rushwa na kujuana na wakubwa wa halmashauri na CCM. 

Matokeo yake, wanalazimika kuanzisha biashara ndogo kweli kweli, lakini huko huko nako bado serikali inakuja inawawekea vikwazo.

“Yaani sisi kwetu, unajipanga, unakopa, unapata ka-mtaji kako ka 50,000,” mwananchi mmoja alieleza. “Ukianza tu kufanya biashara, na haswa watu wakianza kuja kidogo, na Serikali nao, kama nzi vile, hao. Yaani biashara ya 50,000 unakuta tunalipa sijui tozo, ushuru, sijui kodi hadi laki moja. Sasa kuna biashara tena hapo?”

Wakati wananchi wanakabiliana na changamoto ya mitaji, Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, imebaini kwamba kuna ubadhirifu wa moja kwa moja wa zaidi ya Shilingi bilioni 92 katika utoaji wa mikopo kwa makundi ya vijana, wanawake na wazee. 

Katika taarifa hiyo, CAG anatueleza kwamba Shilingi bilioni 79.76 ya mikopo hii haijarejeshwa kutoka kwenye vikundi.

CAG pia anaeleza kwamba kwa kipindi cha 2020/21 hadi 2022/23, zaidi ya Shilingi bilioni 19 ambazo zimekusanywa, hazijawasilishwa kwenye mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. 

SOMA ZAIDI: Falsafa ya Maendeleo Inayoeleweka kwa Umma ni Msingi Imara wa Ukombozi wa Taifa 

Kitendo hiki kinapelekea kuyanyima makundi haya mikopo na mitaji ambayo ingewawezesha kuanza na kuendeleza shughuli zake. Ubadhirifu na usimamizi mbovu katika mikopo hii ni ishara na ushahidi kwamba Serikali ya CCM haina dhamira njema ya kuwanusuru na kuwakomboa wananchi kutoka kwenye lindi la umasikini.

Ziara yetu imetudhihirishia kuwa, mithili ya kupe wanyonya damu, Serikali ya CCM imejiwekeza kwenye sera za kinyonyaji, kwa kuendekeza na kujihusisha na uvunaji wa jasho la vijana na Watanzania wanaojitafutia riziki kwa shuruba kubwa. Tumeshuhudia namna gani Serikali ya CCM badala ya kuwakomboa Watanzania, hivi sasa imejikita katika ajenda isiyo ya siri tena, ya kuwakomoa wananchi.

Siku za uchungu

Siku 15 za ziara hii zimekuwa ni siku za uchungu sana katika maisha yangu. Si kwamba sifahamu hali za watu wetu, hapana! Ila ni huzuni zaidi kwamba, kadri unavyozunguka nchi yetu, ukitumaini kuona mahali kwenye neema na ahueni, ndio unakutana na madhila na manyanyaso makubwa kuliko ulipotoka; kila jana yenye dhulma inaonekana inanafuu kuliko kila leo yenye dhahama. Hapa ndipo walipotufikisha CCM.

Siku 15 zimekuwa ni siku za Machozi, Jasho na Damu, kama alivyoimba kaka yangu, Profesa Jay, mwaka 2001. Siku 15 zimenijaza hasira na kuniongezea dhamiri ya kusimama kuitetea na kuunganisha nguvu kuikomboa nchi yangu. 

Siku 15 za ziara zimenidhihirishia kwamba CCM hawana dhamira ya kuwa faraja kwa Watanzania; baada ya dhiki ya Watanzania, kwa Serikali ya CCM ni dhihaka. Hili halipaswi kukubalika! Sisi kama vijana, wanawake na wananchi kwa ujumla, kizazi chetu kinajukumu moja tu: kupambana kuikomboa nchi yetu ya Tanzania.

Ninawasihi Watanzania wenzangu, CCM imechoka, na sisi hatuna budi kuichoka.

Kiza Mayeye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma na Waziri Kivuli wa Fedha wa Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia kizamayeyechiefexecutivedirect@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×