The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali Imeshindwa Vita Dhidi ya Umasikini. Imeamua Kutangaza Vita Dhidi ya Masikini

Kuharibu biashara za wananchi ili kupendezesha mji, na kuwafukuza wananchi kutoka kwenye ardhi zao kupisha upanuzi wa hifadhi za taifa ni vita dhidi ya masikini inayopaswa kupingwa na kila Mtanzania.

subscribe to our newsletter!

Tunashauriwa kuwa macho juu ya aina za upendeleo, au privileges kwa kimombo, tumebarikiwa kuwa nazo wakati tukijadili mambo fulani, au kuuliza baadhi ya maswali. Kwa mfano, wanaume wanausiwa sana kukumbuka upendeleo wao wa kuwa wanaume wanapojadili kuhusu mambo ya wanawake. Vilevile, watu wasiyo na ulemavu wanapaswa kuwa makini sana wanapozungumza kuhusu wenzao walio na ulemavu.

Tunakumbushwa kuwa macho kwani ni rahisi sana kwa watu wenye upendeleo fulani kusahau upendeleo huo walionao kwenye maisha yao ya kila siku na hivyo inakuwa rahisi sana kwao kuwa wabaguzi, au prejudiced kwa kimombo. Ubaguzi ndiyo msingi wa matatizo mengi yanayomsumbua mwanadamu hivi sasa, kama vile vita za kikabila na kidini, ukatili wa kijinsia, utumwa, ukoloni, na kadhalika.

Binafsi nilikumbushwa hili na mwandishi mwenzangu wa habari wakati tukiwa tunatoka katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi hivi karibuni. Nilimwambia kwamba nimeambiwa inawezekana kukodi gari kutoka Dar es Salaam mpaka Mikumi, kutembelea hifadhini humo kuangalia wanyama, kulala humo, na kurudi Dar kwa Shilingi milioni moja tu.

“Sikujua kama ni rahisi hivi,” nilimwambia mwenzangu huyo baada ya kurudi kwenye gari letu, nikiamini nampatia habari ambayo ingemvutia. “Rahisi?” aliniuliza mwenzangu kwa mshangao mkubwa. “Rahisi kwako, Khalifa. Unadhani kwa sababu wewe unamudu hiyo gharama, kila Mtanzania anamudu pia, ndiyo maana unasema ni rahisi. Nadhani huo siyo mtazamo sahihi.” 

Upofu

Alikuwa sahihi sana, na aliniacha na tafakuri nzito kwenye safari yetu yote na mpaka leo hii. Tafakuri hii ilinikumbusha matukio ambapo watu kadhaa walidhihirisha upofu wao juu ya aina za upendeleo walizobarikiwa na kutoa kauli ambazo kwenye masikio ya wengi zilikuwa na ukakasi mwingi na zenye harufu ya ubaguzi dhidi ya watu fulani.

SOMA ZAIDI: Ukatili wa Kijinsia, Kimsingi, Ni Tatizo la Wanaume

Hizi ni pamoja na ile ya kiongozi mwandamizi wa CHADEMA, Godbless Lema, aliyewahi kusema kuendesha bodaboda ni kazi ya laana; Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba kuwaambia watu wanaolalamikia utitiri wa kodi nchini wahamie Burundi kama hawaridhiki na hali ya hapa Tanzania; au kauli ya Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, kwamba maisha hayajawahi kuwa rahisi toka Mungu alipoumba dunia, akijibu malalamiko ya kuongezeka kwa gharama za maisha.

Tabia yetu hii ya kutotambua upendeleo tuliobahatika kuwa nao imedhihirika hivi karibuni pia kwenye kauli kutoka kwa baadhi yetu zinazowashambulia Watanzania wanaofurika kwenye ibada zinazoendeshwa na baadhi ya wale wanaojiita manabii na mitume, wanaoahidi kuwafanyia watu miujiza itakayowaondolea dhiki na shida wanazopitia, kama vile magonjwa na umasikini.

Ukizichambua kauli za Watanzania wengi kuhusu wenzao wanaokwenda huko kwa imani kwamba wanaweza kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili nyingi zao ni hasi, zenye kuashiria ubaguzi, huku majina kama vile “wajinga” na “wapumbavu” yakitumika kuwaelezea Watanzania hao wanaohudhuria huduma hizi ambazo mara nyingi huvutia maelfu ya wananchi.

Kiini cha tatizo

Lakini mbali na kauli kama hizi kudhihirisha uwezo wetu finyu wa kutambua upendeleo tuliobarikiwa nao – kama vile afya njema, kuwa na watoto na kuweza kula angalau mara tatu kwa siku– na kutuwezesha kuwahukumu badala ya kuwaelewa wenzetu, pia inawanyima fursa wale wanaozitoa ya kuona kiini cha tatizo husika na badala yake kutumia muda mwingi kujadili matawi, au viashiria, vya tatizo hilo badala ya shina.

Kama kuna ukweli wowote unaoweza kuziunganisha kauli za bodaboda ni kazi ya laana, nenda Burundi kama huwezi kulipa kodi na watu wanaokwenda kwa watu kama Boniface Mwamposa ni wajinga basi utakuwa ni kwamba Serikali ya Tanzania imeshindwa kwenye vita yake dhidi ya umasikini na sasa imeanzisha vita dhidi ya masikini inayohusisha, pamoja na mambo mengine, kuwatelekeza wananchi wake na kuwageuza mawindo ya kila aina ya wawindaji.

SOMA ZAIDI: Ni Wakati Kama Wananchi Tuache Visingizio na Kuanza Kutimiza Wajibu Wetu wa Kiraia

Kupunguzwa kwa gharama Serikali ilikuwa inawekeza kwenye utolewaji wa huduma muhimu za kijamii kama vile afya na elimu; kukipa mgongo kilimo kilichokuwa kikitambulika kama uti wa mgongo wa taifa; ufisadi uliofurutu ada bila kuwepo kwa uwajibishwaji wa aina yoyote; na kushindwa kuwekeza kwenye viwanda ambavyo vingesaidia kutengenezwa kwa ajira nyingi kumechangia kuwaweka Watanzania kwenye mazingira magumu yanayowasukuma kurukia “fursa” yoyote wanayodhani inaweza kuwapatia maisha bora.

Haishangazi, kwa mfano, kuona Watanzania kwa mamilioni wakishiriki kwenye biashara za upatu licha ya baadhi yao kulizwa kila siku na matapeli wanaoendesha biashara hizo. Mamilioni wengine wanakesha kwenye maduka ya michezo ya kubahatisha wakitegemea leo itakuwa siku yao ya “kutoboa” bila kujua wanamtajirisha mtu fulani atakayeamua ni yupi kati ya mamilioni ya wachezaji ampe “ushindi” ili aendelee kuwahadaa wenzake. Hapo hatujazungumzia mamia ya familia zinazosambaratika baada ya kuchukua mikopo ya kausha damu wasiyomudu kuilipa.

Wakati inawezekana siyo kila mtu anayekwenda kwenye huduma za watu kama Mwamposa wana shida, wengi wao wanakwenda baada ya kuhangaika kwa miaka kutafuta tiba za magonjwa yanayowasumbua bila mafanikio au kiu ya kutaka kuuacha ufukara na kuonja raha za dunia, hali inayokwambia kwamba kama ustawi wa watu ungeimarika, nyumba za ibada zingekosa wahudhuriaji, kama ilivyo hivi sasa kwenye nchi nyingi zilizoendelea kiuchumi.

Ukatili

Miongoni mwa wale wanaojihusisha na matendo yanayotupelekea baadhi yetu kuwahukumu kutoka kwenye nafasi zetu za upendeleo wamo pia waathirika wa vitendo vya kikatili vya Serikali kama vile vya kuwafukuza watu kutoka kwenye ardhi zao za makazi, kilimo na malisho kupisha upanuzi wa hifadhi za taifa, au kuharibu biashara za wafanyabiashara wadogowadogo kwa ajili ya kupendezesha mji au ujenzi wa karakana!

Unategemea kutakuwa na matokea gani pale Serikali inapoharibu biashara za maelfu ya watu ili tu kupendezesha mji, au kupora ardhi ya wananchi ili kumpa “mwekezaji” au kupanua hifadhi ya taifa? Hakuna matokeo mengine zaidi ya kuwadidimiza watu kwenye dimbwi la ufukara, na kuwalazimisha kujihusisha na njia nyingine za kujipatia kipato ambazo ni za hatari zaidi kama vile kuendesha bodaboda, kuwa dada poa, kuchukua mikopo kausha damu, na kadhalika.

SOMA ZAIDI: Kila Wakati Ambapo Watu Walisimama Pamoja Kutetea Maslahi Yao, Walifanikiwa

Ifike wakati kama wananchi tuwe na uwezo wa kutambua tatizo liko wapi ili tuelekeze nguvu zetu huko badala ya kushughulika na dalili zake na tuweze kushughulika na mzizi wa tatizo husika. Hatutakuwa tunajitendea haki endapo kama tutasahau upendeleo tuliobarikiwa na kutumia muda mwingi kuwahukumu waathiriwa wa mifumo kandamizi ya uongozi na isiyowajibika kwa wananchi.


Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *