The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ukatili wa Kijinsia, Kimsingi, Ni Tatizo la Wanaume

Wanaume tukiacha leo kuwafanyia ukatili wanawake chini ya visingizio mbalimbali, tatizo litaacha kuwa kubwa kama linavyoonekana hivi sasa.

subscribe to our newsletter!

Kwenye makala yangu ya wiki iliyopita kwenye safu hii nilijenga hoja kwamba historia inaonesha kwamba kila wakati watu walisimama pamoja kutetea maslahi yao, walifanikiwa, nikitahadharisha, hata hivyo, kwamba matokeo hayo yatawezekana endapo tu kama watu hao wataweza kutambua kiini cha tatizo linalowakabili.

Ilikuwa ni bahati kwamba nilichapisha maoni hayo wakati nikishiriki kikao cha siku mbili, Juni 27 na 28, 2024, cha mashauriano kilichoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO kwa ajili ya kuandaa Comprehensive National Action for the Promotion of Media and Information Literacy in Tanzania, unaolenga kuwajengea uwezo wananchi kusoma na kuelewa maudhui ya habari na taariza zingine wanazokutana nazo kila siku.

Kikikutanisha wadau kadhaa kutoka vyombo vya habari, asasi za kiraia na Serikali, kikao hicho kililenga mahususi kabisa kufanikisha utengenezwaji wa mpango huo maalumu utakaokabidhiwa kwa Serikali kusaidia jitihada za kitaifa za kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia, ukiwemo ule unaotokea kwenye mitandao ya kijamii ambao umethibitika kuendelea kushika kasi hapa nchini kwetu.

Nancy Angulo, anayesimamia kitengo cha habari na mawasiliano UNESCO, na mwenyeji wa kikao hicho, alianza wasilisho lake siku ya kwanza ya mkutano kwa kusema kwamba, kama taifa, tuna tatizo, akionesha takwimu zinazoonesha kuendelea kushamiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia licha ya jitihada kubwa zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo zinazolenga kupunguza na kutokomeza kabisa vitendo hivyo nchini.

Baada ya wasilisho lake hilo, Nancy aligawa zoezi kwa washiriki wote ambapo tulitakiwa kujibu maswali matatu yaliyogawanywa kwenye kolamu tatu: tatizo ni nini?; tunajuaje kama hilo ni tatizo?; na tutajuaje kama tumelitatua tatizo husika? Nilitumia fursa hiyo kuwashirikisha wenzangu nini haswa nafikiri ni tatizo linalopelekea kushamiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini kwetu: Wanaume.

Tuelezane ukweli

Ni lazima ifike mahali tuelezane ukweli bila kuoneana aibu, na bila ya kuwa na hofu ya kupewa majina mabaya pamoja na sifa zingine mbaya, kwa kuelezana kuhusu tembo aliyepo chumbani na ambaye kila mmoja wetu anajifanya kama vile hamuoni, kwamba, kwa kiwango kikubwa, sisi wanaume ndiyo chanzo kikubwa cha ukatili wa kijinsia unaoripotiwa hapa nchini.

SOMA ZAIDI: Uhodari wa Mwanamke ni Zaidi ya Siku ya Wanawake Duniani

Hatua hii ya kuelezana ukweli juu ya msingi wa tatizo linalotukabili ni sehemu ya kwanza muhimu kuelekea kwenye mwelekeo sahihi kwani itatusaidia kujua ni kundi gani tunapaswa kulifikia na programu gani zitahitajika kutekelezwa ili kutengeneza jamii ambayo wanaume na wanawake wanaishi pamoja kwa amani bila kuoneana na kufanyiana ukatili.

Tathmini yangu inaniambia kwamba bado hatujafanya vizuri kama taifa kwenye kutambua chanzo cha tatizo, na kwa hiyo jitihada nyingi zinaelekezwa kwenye kundi lisilo sahihi kwenye utatuzi mzima wa suala la ukatili wa kijinsia, kwani tunashughulika zaidi na waathirika wa vitendo hivyo, yaani wanawake, badala ya watekelezaji wa vitendo hivyo, yaani wanaume.

Kama jamii, tunatembea umbali mrefu katika jitihada zetu za kuficha uhusika wa wanaume kwenye kesi za ukatili wa kijinsia, hali ambayo pia inajidhihirisha kwenye namna vyombo vya habari na waandishi wa habari tunavyoandika habari kuhusiana na masuala haya, aina ya uandishi wa habari ambayo naamini huchochea kushamiri kwa vitendo hivi.

Kwa mfano, habari nyingi zinazohusu ukatili wanaofanyiwa wanawake huripotiwa kwa kutumia usemi taarifa badala ya usemi halisi, na hivyo kuficha uhusika wa wanaume kwenye vitendo hivyo. 

Unasoma habari yenye kichwa cha habari kinachosemeka, Mwanamke auawa au Mwanamke apigwa risasi na kujenga dhana kwamba tatizo ni mwanamke wakati, kimsingi, kuna aliyeua na aliyepiga risasi ambao hawapo kwenye kichwa cha habari husika.

SOMA ZAIDI: Polisi Lindi Wadaiwa Kumlinda Askari Anayeshukiwa Kumbaka Binti wa Miaka 13

Picha ya skrini inayoonesha baadhi ya vichwa vya habari vinavyoripoti ukatili waliofanyiwa wanawake bila kuonesha waziwazi uhusika wa mtenda, yaani mwanaume.

Picha ya skrini inayoonesha baadhi ya vichwa vya habari vinavyoripoti ukatili waliofanyiwa wanawake bila kuonesha waziwazi uhusika wa mtenda, yaani mwanaume.

Kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini hili litapaswa kubadilika kwa vyombo vya habari kuanza kutumia usemi halisi badala ya usemi taarifa vinaporipoti masuala haya. Ni lazima uhusika wa mwanaume uonekane waziwazi kwenye kichwa cha habari kwa kubadilisha namna tunavyoandika habari zetu kwa kuacha kujenga dhana kama vile mwanamke ameuawa kwa radi au amepigwa na punda!

Tuwafuate wanaume

Pamoja na hili ni lazima makundi tunayofikia kwa ajili ya kubadilisha tabia na utamaduni yabadilike kwa kuacha kukutana zaidi na wanawake na kuwaambia wasivumilie ukatili na kwamba wanahitaji kuzungumza, na badala yake tukutane na makundi ya wanaume na kuwakumbusha kwamba wana mchango mkubwa kwenye kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Bahati nzuri ni kwamba tayari yapo mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya hivi, ikiwemo lile la Thamani Women Tanzania, ambalo Mkurugenzi Mtendaji wake, Nafue Nyange, alizungumza kwenye kikao kile cha UNESCO limeanza kukutana na makundi haya ya wanaume, kama klabu za mpira wa miguu, kuchochea ushiriki wa wanaume kwenye mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini.

Nikichangia kwenye kikao hicho, niliwashirikisha washiriki maneno kutoka kwenye wimbo wa msanii maarufu wa miundoko ya hip-hop kutoka nchini Marekani, J. Cole, ambaye kwenye wimbo wake wa Love Yourz, unaohusu umuhimu wa mtu kujipenda na kujijali, anazungumzia umuhimu wa kuwa na uhakika wa mwelekeo uliochukua kwenye safari yako.

Kwenye ubeti wa kwanza wa wimbo huo ambao Cole anajiambia yeye mwenyewe, msanii huyo anaimba: Habari njema ni kwamba umetembea umbali mrefu; Habari mbaya ni kwamba umechukua njia isiyokuwa sahihi. Ni hofu yangu kwamba kwenye jitihada zetu za kukabiliana na ukatili wa kijinsia na sisi, kama taifa, tumechukua njia isiyokuwa sahihi.

SOMA ZAIDI: Umalizaji Kesi Kienyeji Unavyochochea Kushamiri kwa Matukio ya Ulawiti, Ubakaji

Maana, kama Morogoro ipo mashariki mwa Tanzania, haijalishi ni umbali kiasi gani utatembea kuelekea kaskazini, au nguvu na rasilimali kiasi gani utakazowekeza kwenye safari hiyo, au madhila utakayopaswa kuyavumilia, huwezi kufika sehemu unayotaka kufika; ni lazima uchukue mwelekeo sahihi, uende mashariki!

Na kwenye hili la kukabiliana na janga la ukatili wa kijinsia nchini ni maoni yangu kwamba mwelekeo sahihi ni kumtambua mwanaume kama tatizo na kuelekeza nguvu na jitihada zetu huko ili ukatili wa kijinsia uweze kukoma. Nafahamu wapo wanaume wanaokabiliwa na ukatili wa kijinsia, lakini tukilinganisha na wanawake wanaokabiliwa na tatizo hilo tutabaini tatizo, kwa kiwango kikubwa, linatoka wapi.

Kukabiliana na tatizo pana na kubwa kama hili la ukatili wa kijinsia, bila shaka, kutahitaji afua nyingi na shirikishi zaidi kuliko nilichopendekeza hapa. Hata hivyo, naamini kwamba endapo kama wanaume tutaamua leo kuacha kuwafanyia ukatili wanawake chini ya visingizio mbalimbali, tatizo litaacha kuwa kubwa kama hivi sasa linavyoonekana.

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *