The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Tusiishie Kumshambulia Diamond Plutinumz Tu kwa Kauli Yake ya ‘Fanyeni Kazi.’ Tumtafutie Msaada Stahiki Pia

Mafanikio ya haraka ya kifedha huwasukuma wasanii wengi kupoteza mguso na uhalisia wa jamii wanazotoka. Wengi hupotea wakijaribu kukabiliana na suala hilo, tunaweza kumnusuru Diamond na hatma hiyo.

subscribe to our newsletter!

“Fanyeni kazi” ni kauli inayoweza kutoka tu kwenye mdomo wa mtu aliyepoteza uhusiano, au mguso, na mazingira aliyopo. Hali hii, ambayo kwa lugha ya kawaida, kimsingi, ni kusahau ulipotoka, huwakabili watu wengi waliokuja kupata mafanikio ya kifedha ukubwani, na kuwalazimisha wale na kulala sehemu tofauti na zile zilizowakuza, na kuchanganyika na watu tofauti na wale aliokula nao shida utotoni na ujanani.

Wasanii wa muziki ni moja kati ya makundi makubwa ya watu ambalo halijanusurika na hali hii, wengi wakijikuta mafanikio yao ya kifedha, ambayo mara nyingi huja kwa ghafla sana, yakitokana na vipaji na vipawa vyao, yakiwaweka kwenye mazingira yanayotishia kuwang’oa kwenye mazingira yao ya awali na kuhatarisha kuwabadilishia mitazamo yao kuhusu maisha na hata binadamu wenzao.

J Cole, msanii maarufu wa Marekani, aliwahi kulilalamikia suala hili, akidhihirisha hofu yake kwamba mafanikio ya kifedha aliyoyapata kutokana na muziki wake yanamfanya akose nguvu na ari, au mzuka, kama wasemavyo wenyewe, kufanya muziki unaoakisi uhalisia wa jamii anayotokea, ikiwemo kuyapa jukwaa masaibu ambayo jamii hiyo na watu wake wanapitia kwa wakati husika.

Sakata la Diamond

Nadhani Diamond Platnumz, msanii wetu pendwa hapa Tanzania wa miondoko ya BongoFlava, anapitia hii hali pia, na kwa bahati mbaya sana kwake, ameshindwa kuidhibiti vizuri kiasi ya kwamba imeweza kujidhihirisha mbele ya jamii yake kwa namna ambayo ni hasi kwake, hususan kwenye namna jamii itakavyomchukulia kutoka sasa.

Kwenye video ambayo inaendelea kuzunguka kwenye mitandao ya kijamii, Diamond, akiwa kwenye gari lake la kifahari aina ya Rolls Royce Cullinan ya mwaka 2021, anaonekana akiwafokea Watanzania, akiwaambia “fanyeni kazi,” huku akiwakosoa kwa kuendeleza “lawama” kwa Serikali haijalishi ni nani yuko madarakani. 

SOMA ZAIDI: Simulizi za Watoto Walioachishwa Shule na Wazazi Wao na Kulazimika Kuingia Mitaani Kutafuta Maisha 

Hakuna muktadha kwenye video hiyo fupi, ambao ungetuwezesha kuelewa kwa nini msanii huyo aliamua kusema hicho alichosema na kwa namna hiyo.

Hata hivyo, watu wengi, kwa sababu zinazoeleweka kabisa, wamekasirishwa sana na kauli hizo za msanii huyo, huku kila mmoja akitafuta neno kali zaidi la kuliekeza kwake kwa namna inayoweza kuakisi hasira aliyonayo.

Wakati nawaelewa kabisa watu walioamua kuruka na Diamond, kama tunavyosema huku mtaani, mimi binafsi sina hasira na Diamond, bali namhurumia kwa kushindwa kwake kudhibiti vizuri mzozo wa kisaikolojia unaomkabili, unaotokana na kupoteza kwake mguso na maisha halisi ya kila siku ya Watanzania. 

Ushauri wangu kwake, na watu waliokaribu naye, ni kutafuta msaada wa kitabibu, haraka inavyowezekana, utakaomuwezesha kulikabili suala hili vizuri, ikiwemo kumuepusha na athari zake hasi.

Mbali na jamii kuwa na mtazamo hasi, uwezo mdogo wa msanii kuweza kukabiliana na mzozo huo wa kisaikolojia unaweza kupelekea madhara makubwa zaidi kwa msanii husika, ikiwemo kusumbuliwa na tatizo kubwa la afya ya akili, matumizi makubwa na holela ya madawa ya kulevya, na hata majaribio ya kuchukua maisha yao wenyewe.

SOMA ZAIDI: Wadau Watia Neno Matukio ya Watoto Kujinyonga: ‘Jamii Imetelekeza Wajibu Wake’

Hatua hizo zimebainishwa na tafiti mbalimbali kama njia za kutokea zinazotumiwa na wasanii wengi wanaojaribu, pamoja na mambo mengine, kuzuia mafanikio yao ya haraka ya kifedha yasiwaondolee mguso na jamii walizopo. 

Diamond Platnumz anadhihirisha kushindwa kuyakabili vizuri mapambano haya, na hiyo si habari njema, siyo kwake tu bali kwa mashabiki zake pia wanaofurahia muziki wake.

Tunafanya kazi 

Maana, katika hali ya kawaida, hutegemei mtu ambaye afya yake ya akili iko sawasawa awaambie wananchi wafanye kazi na kwamba waache kuendeleza “lawama” kwa Serikali yao. Ukiangalia kwenye kila pembe ya nchi hii, unaona wananchi wakivuja jasho kujenga chumi zao binafsi na ule wa nchi yao.

Tanzania haionekani, kwa vipimo vyovyote vile, kama nchi ambayo watu wake hawafanyi kazi. Watoto, vijana na wazee, kike kwa kiume, wanaamka kila asubuhi na kurudi nyumbani usiku mkubwa wakijaribu kufanya kazi yoyote iliyopo mbele yao ili waendelee kuishi na kukuza familia zao.

Kwamba Tanzania si nchi ya watu wasiofanya kazi haihitaji kuelezewa sana. Kimsingi, ni kazi za wananchi hawa zinazojenga uchumi wa nchi ambao, kwa kiwango kikubwa, hutegemea kodi ya kipato na ile ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa. Kodi ya kipato huipati kama watu hawafanyi kazi, na kodi ya ongezeko la thamani haipatikani kama watu hawana uwezo wa kununua bidhaa na huduma.

SOMA ZAIDI: Ongezeko la Wafungwa Waliotoka Gerezani Kurudia Makosa, Serikali na Jamii Zanyooshewa Vidole

Na licha ya ukweli huu, kwamba wafanyakazi wa nchi hii ndiyo misingi wa uchumi wake, wananchi hawanufaiki ipasavyo na kodi hizo wanazolipa kwa namna mbalimbali. Huduma za kijamii za umma zimeendelea kuwa duni sana kiasi ya kwamba watu wanalazimika kwenda kwa watoaji huduma binafsi, wakilazimika kuingia gharama kubwa na kutingisha chumi za kaya zao.

Kusema ule ukweli, hakuna uhusiano hapa nchini kwetu kati ya kodi ambazo wananchi – wafanyakazi, wakulima, na wafanyabiashara wadogo – wanalipa na huduma wanazopata kutoka kwa Serikali yao, kiasi ya kwamba baadhi ya watu wanauliza mantiki ya kulipa kodi ni nini haswa kama hata ndugu yake akifa hawezi kutoa mwili wake mochwari bila ya kulipia!

Je, ni sawa kuwaambia wananchi hawa kwamba hawana haki ya kuilaumu Serikali yao? Kama unalipa kodi, na hupaswi kudai huduma bora, au mahusiano bora kati yako na wale waliopo madarakani, mantiki ya kulipa kodi ni ipi haswa? Nini itakuwa maana ya kuwa raia kwenye nchi yako mwenyewe? Nini maana ya kuishi kwenye Jamhuri?

Katika mazingira hayo yote niliyoeleza hapo juu, hatuwezi kuhitimisha, au kutegemea, kwamba mtu ambaye akili yake inafanya kazi sawasawa ajitokeze hadharani, awakaripie wananchi kwa kuwaambia wafanye kazi, na kwamba waache kulaumu Serikali.

Ishara mbaya

Kwamba Diamond Platinumz amefanya hivyo ni ishara mbaya, na ni jukumu letu kama jamii kumsaidia asiangukie kwenye dimbwi zito na baya zaidi. 

SOMA ZAIDI: Changamoto na Haki za Wafanyakazi wa Majumbani 

Ni bahati mbaya kwamba Tanzania imepoteza vipaji vyake vingi kwa madawa ya kulevya, njia ambayo sayansi imethibitisha kuwa moja wapo ya suluhu wasanii huzikimbilia kukabiliana na msongo wa mawazo unaotokana na mapambano ya kiakili wanayopitia, ikiwemo namna wanavyoweza kuendelea kuwa na mguso na jamii zao, huku wakiwa na umaarufu mkubwa na utajiri mwingi wa kifedha.

Kama jamii, tunapaswa kuwa macho na kuweza kutambua pale mmoja wetu anadhihirisha tatizo hili na hivyo kuchukua hatua za haraka na mapema. Ni mara chache sana mtu kudhihirisha waziwazi tatizo hili, na si watu wengi wana utayari na nguvu ya kuieleza jamii yao kwamba nakabiliwa na tatizo fulani, naomba mnisaidie.

Diamond Plutinumz ametuonesha kwamba kuna tatizo mahala, ni wajibu wetu kumsaidia kabla hatujachelewa.

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×