The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Tukiruhusu Ukatili Utawale Tanzania, Tutawezaje Kuwa na Nchi ya Amani?

Mstari kati ya ustaarabu na ukatili ni mwembamba sana, na watu wakipewa amri kuwa katili ni rahisi sana kuingia katika ukatili.

subscribe to our newsletter!

Niliwahi kufundisha shule fulani ambapo, mara mojamoja, mwalimu mkuu wake aliamua kwamba, kutokana na utundu au uzembe fulani, wanafunzi wapewe extra drill.  Ndiyo.  

Sijawahi kuwepo jeshini, lakini walimu wenzangu waliniambia kwamba ni hiyohiyo waliyopitia wengine wakiwa JKT. Lakini baadaye walikiri kwamba baadhi ya adhabu walizotoa zilikuwa zimepigwa marufuku jeshini, hasa kwa wanawake, na hii ilikuwa shule ya wasichana.

Na extra drill sio mchezo. Sikujua. Sasa kwa kuwa walimu wote walitakiwa kushiriki kutoa hiyo extra drill, ikabidi niwemo na mimi. Wanafunzi walikimbizwa, wakaviringishwa kwenye mchanga, na hata kulazimika kulala kwenye mifereji yenye maji baridi sana, wakarushwa hata kichura.

Hadi wanafunzi karibu wote walikuwa wanalia, wengine wanatoa udenda kama vile wanataka kufa, wanashindwa kusimama, lakini wanapigwa viboko hadi wasimame na kuanguka tena.  

Wengine walizimia, wengine walipelekwa zahanati baadaye lakini adhabu iliendelea … iliendelea … iliendelea hadi baada ya masaa, mwalimu mkuu, ambaye ninao uhakika alikuwa anaangalia akiwa nyumbani kwake maana nyumba ilikuwa ndani ya eneo la shule, hadi akatoka.

Dah maigizo!

Alitukimbilia sisi walimu akihema maana hakuwa mwembamba, akiasa: “Jamani walimu, inatosha, inatosha, jamani, maskini wanafunzi inatosha.”

SOMA ZAIDI: Kama Tanzania Ingekuwa Timu ya Mpira Unayoshabikia, Bado Ungeipongeza Hata Kama Inakosea? 

Ni yeye aliyeagiza iwepo extra drill.  Ni yeye aliyeangalia ikifanyika. Na sasa anajidai mwenye huruma sana na kuwasihi walimu waache. “Jamani imezidi,” alitwambia. “Sikujua, basi, basi, basi walimu naomba mwache.”

Halafu anawageukia wanafunzi, akiwaambia: “Poleni, poleni, nendeni mkapumzike.”

Yaani ionekane walimu ndio washenzi, yeye mtakatifu. Sijui wanafunzi wangapi walitambua hilo, lakini mimi binafsi nilisikia kichefuchefu mbele ya unafiki wa aina hii.

Kufuata amri

Na siyo hiyo tu. Niliwashangaa baadhi ya walimu wenzangu, pamoja na kujishangaa mwenyewe. Wengine, kama mimi, tulifuata amri, lakini katika kufuata, tuliagiza vitu ambavyo katika maisha yetu tusingediriki kufanya hata siku moja.  

Na hata mori kupanda kwa kiasi fulani katika kutaka “kutimiza wajibu.” Na zaidi, ilionekana wazi kwamba walimu wengine walifurahia kutoa adhabu ile. Walipata raha kuona wanafunzi wao wanatoa udenda au kuzimia.

SOMA ZAIDI: Watawala Tanzania Wana cha Kujifunza Kwenye Kisa cha Mfalme Henry II wa Uingereza na Askofu Thomas Becket 

Kwa kweli, tukio hili lilinitafakarisha, lilinikera, lilinihuzunisha nikajisikia mchafu sana kwa kushiriki katika hilo. Na tangia hapo nilikataa katakata kushiriki tena. Sasa ajabu ni kwamba mwalimu mkuu yule alikuwa mwalimu mzuri na shule ilikuwa nzuri na nilifurahi kufundisha pale. 

Na walimu nao, kwa ujumla, walikuwa wazuri na walifundisha kwa bidii. Lakini kila virusi ya ukatili iliporuhusiwa kupenya kupitia extra drill, watu tulibadilika, wengine kidogo, wengine sana.  Utadhani wana tabia mbili ambazo hazisikilizani kabisa.  

Hayo yalitokea zaidi ya miaka arobaini iliyopita, nikiwa bado kijanakijana na kuona ni lazima nitii amri iliyotolewa na mwalimu mkuu. Lakini siwezi kusahau hadi leo jinsi wale wanafunzi walivyoteswa, walivyoumia, walivyozimia.  

Najuta kushiriki hadi leo, nilifanya kosa kubwa sana na mwisho ilikuwa sababu mojawapo ya kuhama shule ile pamoja na uzuri wake wote. Siwezi kusahau na nimetafakari tena na tena juu ya tukio lile.

Na katika kutafakari, nimeelewa sababu za misingi fulanifulani ya haki za binadamu na kanuni za maendeleo.  Hasahasa, baada ya Vita Kuu ya Pili, wakati Wanazi wakubwa wengi waliposhitakiwa katika mji wa Nuremberg, kulekule Ujerumani.  

SOMA ZAIDI: Kuna Uchaguzi, Uteuzi na Uchafuzi. Hapa Tanzania Tuna Nini? 

Wengi walijitetea kwamba walikuwa wanafuata amri tu.  Mahakama ikaamua kwamba madai ya kufuata amri tu hayakubaliki kama utetezi.  Ni lazima mtu afuate utu kwanza, haki kwanza. 

Nilifanya kosa kufuata amri kwa kweli na ingawa mahusiano na wanafunzi wangu yaliendelea kuwa mazuri kutokana na kufanya jitihada ya ziada kufundisha, bado kule kufuata amri ile kulitia doa katika maisha yangu.  

Najua kwamba, hapo baadaye hadi leo, kanuni hizi za Nuremberg zimekanyagwa sana na nchi za kibeberu, hivyo wanaokamatwa na kushitakiwa ni wale wasio na uwezo, au wanaotoka nchi zisizo na uwezo.  

Najua wako wengi wanaostahili kushitakiwa na kwamba “nilikuwa nafuata amri tu” si utetezi kwao pia. Ndio unafiki mkubwa sana uliopo tena. Lakini kanuni bado ina umuhimu wake.  Hatuwezi kujificha kwa kudai eti tulikuwa tunafuata amri tu.

Ustaarabu na ukatili

Pili, niligundua kwamba mstari kati ya ustaarabu na ukatili ni mwembamba sana, na watu wakipewa amri kuwa katili, au wakiona kanuni, au desturi fulani zinaruhusu ukatili, ni rahisi sana kuingia katika ukatili ule na kufanya mambo yaliyo kinyume kabisa cha utu, cha ubuntu na kadhalika. 

SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’ 

Ndiyo maana, kila mfumo hauna budi kuweka mipaka madhubuti kuhusu matumizi ya nguvu, nguvu isije ikageuka ukatili, iwe kwenye vyombo vya dola, iwe shuleni, iwe michezoni, mahali popote.  Na siyo kuweka mipaka madhubuti tu, ni kulinda mipaka ile kwa nguvu zote maana virusi ya ukatili ikiingia ni vigumu sana kuitoa. 

Ndiyo maana tunapata hadithi chungu nzima za ukatili shuleni maana sheria haifuatwi.  Ndiyo maana pia tunapata hadithi chungu nzima juu ya mateso na hata vifo upande wa vyombo vya dola.  Ndiyo maana mbele ya dalili yoyote ya kuandamana, lugha inayotumika ni ya kikatili moja kwa moja, mara kuvunja miguu mara nini sijui.  

Yaani hawajifunzi kwa nchi nyingine? Mkitumia ukatili dhidi ya wanaotembea kwa amani, matokeo yake ni nini? Lakini virusi vya ukatili vikiishaingia, inazidi kutafuna watu.

Usidhuru

Tatu, kanuni kuu ya maendeleo ni do no harm.  Usidhuru. Usilete madhara. Ukatili wa aina hii unapingana kabisa na maendeleo na ukatili unapopenya hata mafanikio yale yaliyotarajiwa, yale ya miradi ya maendeleo, yanatiwa doa na hata dosari.

Nne, kama alivyosema mwanazuoni na mwanamapinduzi Frantz Fanon, ambaye alikuwa mshunuzi maarufu pamoja na mpigania uhuru, alilazimika kuwatibu maafisa na maaskari wa kikoloni wa Ufaransa huko Algeria.  

SOMA ZAIDI: Pengine ni Kweli Polisi Hawahusiki na Utekaji. Lakini Mbona Hatuoni Watekaji Wakikamatwa? 

Fanon aligundua kwamba, kimsingi, huwezi kutenga sehemu moja ya tabia kuwa katili na kuwa mstaarabu sehemu zingine. Kwa mfano, alikuwepo afisa mmoja ambaye, baada ya kuwatesa wapigania uhuru, akakuta anarudi nyumbani na kuwatesa mke na watoto vibaya sana. 

Hakupenda kufanya hivyo, alijuta, lakini virusi ya ukatili vilikuwa vimemtawala. Wengine walipata kichaa kabisa. Wengi walikuja kuasi na kukataa kuendelea na ukatili, na wengine walikataa kwamba si ukatili, wakidai wanafanya vizuri, lakini roho ziliwasuta hadi wakalazimisha usugu wa juujuu.

Ndiyo maana ninasema, upande wangu, nilijifunza kutokana na makosa yangu. Najua kwangu mimi pale shuleni ilikuwa rahisi kukataa kufanya ukatili, tena ingawa walimu wengine walinichukia, lakini kwa watu wengine ni vigumu, kuna amri, kuna vitisho, kuna adhabu, kuna kutengwa. 

Lakini tukiruhusu virusi ya ukatili vitutawale, tutawezaje kuwa na nchi ya amani, na ya haki ambayo ni msingi wa amani? 


Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×