The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Bila Ushirikishwaji Mpana na Uhalali wa Kijamii, Wananchi Lazima Waione Tume Kama Chombo cha Serikali Badala ya Taifa

subscribe to our newsletter!

Tangazo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuunda tume ya kuchunguza madhila ya Oktoba 29, 2025, lingetarajiwa lipokelewe kama hatua ya kurejesha imani, kuponya majeraha, na kutoa majibu ya haki kwa taifa lililotikiswa na vurugu, vifo, majeruhi, na taharuki ya kitaifa.

Badala yake, wananchi kadhaa wamelipokea tangazo hilo kwa mtazamo wa shaka, lawama, na hisia kwamba tume hii itafanya yaleyale ya miaka yote, na hasa kufunika ukweli wa mambo.

Malalamiko ya wananchi ni mazito. Tume inaundwa na wastaafu, wasomi wa zamani, watu wanaoaminika kuwa wa karibu na chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), watu waliowahi kutumikia mamlaka kwa utii wa kiwango cha juu; huku kukiwa hakuna vijana, hakuna viongozi wa dini, hakuna wanazuoni huru, na—kwa wengi walivyotarajia—hakuna wazee wenye uzito wa kitaifa kama Jaji Joseph Sinde Warioba. 

Kusema hivyo hakumaanishi hao wajumbe hawafai, la hasha! Hawa ni watu sahihi, lakini si kwa nafasi na kazi waliyopewa. Kuachwa kwa Jaji Warioba, ambaye amekuwa ishara ya uadilifu na busara ya kitaifa kwa miongo kadhaa, ni “kosa la kiufundi” linaloipunguzia tume hiyo uhalali kabla haijaanza kazi.

Lakini Tanzania haipo peke yake katika misukosuko ya namna hii. Mataifa mengi yamepitia maumivu makubwa yakahitajika kuundwa tume za ukweli, maridhiano au uchunguzi. Tofauti kati ya tume zilizofanikiwa na zilizoshindwa mara zote imekuwa moja tu, yaani uaminifu wa umma kwa wajumbe wake.

Uzoefu kwengineko

Tume ya Desmond Tutu nchini Afrika Kusini ndiyo mfano bora kutolewa. Iliundwa kwa sura pana—viongozi wa dini, wanaharakati, wanasheria, waathirika, wanasiasa kutoka pande zote, na wataalamu wa haki za binadamu.

SOMA ZAIDI: Hotuba Kamili ya Rais Samia Akizindua Tume ya Uchunguzi Matukio ya Oktoba 29, 2025: ‘Nina Matumaini Makubwa na Tume Hii’

Hakukuwa na shaka juu ya uadilifu wa viongozi wake. Kwa kuitazama tu, taifa liliona uso au nuru ya haki. Ndiyo maana ilikuwa na matokeo makubwa.

Baada ya ghasia za uchaguzi mwaka 2007/2008, Kenya iliunda Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano, au Truth, Justice and Reconciliation Commission (TJRC). Makosa yaliyofanywa kule yanatoa funzo muhimu. 

Wakenya wengi walipoteza imani kwa tume hiyo pale walipoteuliwa watu waliotajwa katika migogoro, au waliokuwa karibu mno na mamlaka. Wananchi waliona tume hiyo kama jaribio la kuisafisha Serikali, na si kuleta ukweli.

Historia inaonyesha kuwa Nigeria ilipounda Oputa Panel kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na utawala wa kijeshi, ilipata ushirikiano wa wananchi kwa sababu Profesa Chukwudifu Oputa alikuwa na heshima ya kitaifa kama Jaji Mkuu mstaafu mwenye msimamo.

Lakini ripoti yake ilipokataliwa na Serikali, uthibitisho ulitolewa kwamba tume isiyopata uungwaji mkono wa kisiasa au wa kijamii huishia kuwa kumbukumbu tu, na si suluhisho. Hapa Oputa wetu ni Jaji Othman Chande!

SOMA ZAIDI: Tume Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, 2025: Serikali Iepuke Vishawishi vya Kutaka Kujistiri na Badala Yake Ijikite Kwenye Kuliponya Taifa

Baada ya mauaji ya kimbari, Rwanda ilikataa kuunda tume ya wataalamu pekee. Walishirikisha wazee wa jadi, viongozi wa jamii, na watu waliokubalika kwa wananchi. Mfumo wa Gacaca ulifanya kazi kwa sababu ulikuwa wa watu, si wa watawala kama tunavyoona hapa kwetu.

Funzo kuu

Funzo kuu hapo ni kwamba bila ushirikishwaji mpana na uhalali wa kijamii, tume huonekana kama chombo cha serikali, si cha taifa.

Nchini Sierra Leone, Tume ya Ukweli na Maridhiano ilisheheni viongozi wa dini kama Askofu Joseph Humper, ikapata heshima na ushawishi. Serikali iliacha mikono huru kabisa, jambo lililojenga imani.

Katika mazingira yetu ya sasa, wananchi wanajiuliza je, tume ya Tanzania iko huru? Je, sura za wajumbe wake zinawapa wananchi sababu ya kuamini hivyo? Tume yenye mjumbe ambaye jana tu alikuwa Waziri wa Ulinzi itaaminika vipi?

Uwepo wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa machafuko kwenye Tume ya Uchunguzi umeleta ukakasi na maswali kuwa atawezaje kuchunguza uwajibikaji na matendo ya vyombo vya ulinzi na usalama wakati yeye mwenyewe alikuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa maafa hayo? 

SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani? 

Tume yenye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) mstaafu, ambaye aliowaacha polisi ndiyo hao wengine wametoa amri ya kuua raia kama vile wanaua kunguni, nani watakuwa na imani naye?

Kwenye mifano yote niliyotoa kuna mambo manne muhimu, yaani wajumbe lazima wawe wanaheshimika kitaifa (si kiutawala tu), wasiwe watu wa upande mmoja wa kisiasa, wawe na uwakilishi mpana (vijana, viongozi wa dini, vyama vya siasa, wanaharakati, waathirika, na wataalamu).

Tume ya sasa inaonekana haina sura ya taifa. Inaonekana kama chombo cha Serikali, na si jukwaa la kitaifa la kuleta majawabu kwa hali iliyotufika. Na hii ndiyo sababu wananchi wana shaka nayo.

Jaji Warioba

Kwa historia ya nchi yetu, Jaji Warioba amekuwa kielelezo cha uadilifu. Amekuwa kiongozi wa Tume ya Rushwa (Warioba Commission), Tume ya Katiba, na mjumbe wa tume na bodi nyingi za kimataifa. Taifa linayo kumbukumbu ya kazi zake nzuri. Huku mitaani mtu pekee anayezungumzwa na rika zote ni Jaji Warioba. 

Mtu ambaye anaweza kukubalika hata akiwaomba jambo vijana, ni Jaji Warioba. Huo ndiyo ukweli tunaokutana nao huku uraiani. Kama wao Serikalini na katika CCM wanamchukia, kwa wananchi ni kinyume. Washauri wamweleze Rais ukweli huu!

SOMA ZAIDI: Oktoba 29, 2025: Tulichoka Hekima na Busara, Tukajaribu Ujinga, Tumeona Matunda Yake

Kumwacha nje ni sawa na kuunda tume ya uchumi bila mchumi mkongwe.

Kwa majeraha ya Oktoba 29, Watanzania wanahitaji “uso wanaouamini.” Jaji Warioba si lazima awe mwenyekiti, bali hata mjumbe ili kuongeza imani ya watu. 

Kwa hali ya taifa letu ilivyo sasa, ni wachache sana wa aina ya Jaji Warioba wanaoweza kusimama mbele ya taifa wakasikilizwa. Kumweka kando ni kosa la kiufundi. Tusije tukamhitaji wakati mambo yamekuwa mabaya zaidi.

Mataifa mengine yametuonyesha kwamba ukweli haupatikani katika vyumba vilivyofungwa, haki haiwezi kutolewa na watu wanaoaminiwa na upande mmoja tu, na majeraha ya taifa hayaponywi kwa tume za watu walioteuliwa kwa utashi wa watawala, bali kwa mioyo ya watawaliwa.

Ikiwa tume hii ya sasa itaendelea bila marekebisho, kuna hatari kubwa kwamba itajadili, itachunguza, itatoa ripoti ambayo haitapokewa vema na umma.

Washauri wa Rais wamweleze ukweli wa hali halisi huku mitaani na kwenye mitandao. Nyambhisa-bhisa obhurweri ekiriro kirambhura.

Manyerere Jackton ni mwanahabari na mhariri mkongwe nchini Tanzania, na mmiliki mwenza wa gazeti la Jamhuri. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia manyerere77@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×