The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kama Wananchi, Tunafanyaje Kuzisaidia, Kuzifariji Familia Zilizopoteza Wapendwa Wao Matukio ya Oktoba 29?

Kama jamii, hatujaweza kuwasaidia vya kutosha wale walioondokewa kufanya misiba ya wapendwa wao; misiba kwa maana ya taratibu za kidini, taratibu za kimila, na taratibu za kijamii.

subscribe to our newsletter!

Kwanza, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana The Chanzo, kama chombo cha habari, kwa kutuhabarisha, na kwa wakati. 

Lakini zaidi niwapongeze kwa kuwa jukwaa ambalo Watanzania mbalimbali, nje ya wanahabari, wamekuwa wakilitumia kutoa tafakuri zao, kufanya chambuzi, na pia kutoa maoni yao katika masuala mbalimbali, ikiwemo hili ambalo linaendelea sasa hivi, na katika muktadha huo basi, na mimi naomba nitoe maoni yangu, walau kwa uchache.

Kama ilivyo kwa Watanzania wengine, naendelea kufuatilia kwa kina haya ambayo yametokea katika taifa letu. Hili, kwa hakika, ni jambo ambalo kwa wengi wetu ni geni, na kutokana na huu ugeni wake, inaonekana kuna mambo ambayo tunajifunza huku tunayatekeleza. 

Sasa, kwa mtazamo wangu, na labda wachache watakuwa wameliona pia, katika mambo mengi ambayo tumekuwa tunafanya baada ya ile Oktoba 29, kuna mambo ambayo tumeyaacha, na tumeyaacha kwa sababu mbalimbali. Kuna sababu za kimfumo, lakini pia kuna sababu za hofu, na nyingine hizo za kiuwezo, kwa mfano.

Katika mambo ambayo kwangu mimi naona ni kubwa sana, na hili kama hatutalitafutia ufumbuzi sasa hivi litakuja kusababisha madhara makubwa sana, ni hili suala la kuwafariji waliopoteza wapendwa wao, na kuwasaidia katika kupona.

SOMA ZAIDI: ‘Yale Hayakuwa Maandamano’: Hotuba Kamili ya Rais Samia Akiongea na Wazee wa Dar es Salaam, Disemba 2, Kuhusiana na Matukio ya Okt. 29, 2025

Kwa bahati mbaya sana hili suala lilivyotokea, kwa mazingira yake, watu wengi wamepoteza wapendwa wao, na sisi kama Watanzania, na kwa dini zetu zote, tunajua kabisa, na tumekuzwa kwenye kuamini, na tuna mila, tamaduni nyingi, zinazotufundisha jinsi gani tunatakiwa kufanya pale tunapoondokewa na wapendwa wetu. 

Bahati mbaya ni kwamba mpaka hapa tunavyoongea kuna wenzetu wengi wanashindwa mpaka sasa kufanya misiba yao kwa sababu watu walioondokewa kipindi ambacho watu wako kwenye lockdown, kwa hiyo, watu wamefiwa lakini hawajakaa msiba, kwa mfano, na sisi tunajua kila msiba una mwenyewe. 

Hatuja fanya vya kutosha

Kama taifa tunaweza kuona tu kwamba watu walifiwa, lakini hao waliofariki ni baba labda wa familia fulani, au ni mtoto, au ni mama, au ni shangazi, na hatujaweza, kama jamii, kuwasaidia wale walioondokewa kufanya misiba ya wapendwa wao; misiba kwa maana ya taratibu za kidini, taratibu za kimila, na taratibu za kijamii.

Watu wamefiwa, labda wengine hawajazika, na hata wale ambao wamezika wamefanya hivyo katika mazingira ambayo watu hawajakaa matanga, watu hawajalia, watu hawajasalimiana, watu hawajapeana pole. Watu hawajafanya misa. Watu hawajafanya hitma za wapendwa wao.

Siku chache kutoka sasa tutafikia 40 ya lile janga lililotokea, na katika mila zetu na desturi na dini zetu nyingi tunaamini siku ya 40 ndiyo siku ambayo, kama jamii, mnakaa, mnamaliza misiba, na hili kwa mazingira yaliyopo inaonekana halitakuwepo.

SOMA ZAIDI: ‘Askari Wangu Wamefanya Kitu Kibaya Sana’: Ya Nanjing 1937, Tiananmen Square 1989 na Oktoba 29, 2025 Tanzania

Kwa hiyo, mimi naomba sana sana, kama jamii, tuwape nafasi waliofiwa wafanye misiba ya ndugu zao kwa kuwajali, kuwasapoti, na kuwa nao pamoja pale ambapo inawezekana. Kwa hiyo, kama unamjua mtu amefiwa na mpendwa wake, tafadhali tuungane nao. 

Kama jamii, tusiache hawa waliopotea, hawa ambao wamepata haya madhara, wakaishia kuwa marehemu ambao nafsi zao, au roho zao, hazitasumbua wale tu waliotoa uhai wao, bali hata sisi ambao tumeshindwa kuheshimu kule kuondoka kwao. 

Na sisi, kama nilivyoeleza hapo juu, familia zetu nyingi sana, tumekuwa tuna heshima kubwa sana kwa wale wenzetu ambao wanatutoka, na tunajua kwamba wale wanaotutoka wanahitaji dua zetu, wanahitaji sala zetu, wanahitaji mila zifanyike, wanahitaji taratibu za kidini zifanyike.

Wengine wamezikwa hawajakoshwa, hawajasaliwa; wengine wamezikwa hawajafanyiwa misa kwa wale wenzetu Wakiristo, na kadhalika. Kwa hiyo, tuwape huo ushirikiano wa kufanya hivyo. 

Kukabiliana na kiwewe

Lakini jingine ambalo linahusiana na hilo ni kwamba kuna watu ambao wameondokewa na watu wao, au watu wao bado wako hospitalini, na waliona wakati wanaondokewa. 

SOMA ZAIDI: Oktoba 29, 2025: Tulichoka Hekima na Busara, Tukajaribu Ujinga, Tumeona Matunda Yake 

Msiba wa kuubeba, wa kuuguza, na mtu akafariki ni msiba mzito, na katika tamaduni zetu nyingi tunakuwa nao pamoja na kuwapa moyo wafiwa. Lakini fikiria msiba ambao unauona, labda mtoto wako anapoteza maisha pale kwa kupigwa risasi, au unauona mwisho wake unavyokuwa, na unawaona wale wanaoutoa ule uhai wa mpendwa wako?

Kile kiwewe, au trauma kwa Kiingereza, haitapona na kuisha kwa kufunika kombe. Mimi nilijua, na niliamini, kwamba wenzetu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, watatusaidia kuhakikisha wanatoa wanasaikolojia wengi kadiri inavyowezekana na kuzifikia hizi familia, kuwafikia hawa watoto waliuona mwisho wa wazazi wao, mwisho wa kaka zao, kwa sababu hili jambo limefanyika kwa uwazi, watu wameona, wale walioona tunazisafisha vipi fikra zao? Tunaponya vipi mioyo yao? 

Hili haliwezi likatokea tu kwa bahati mbaya, inabidi lifanywe, na lifanywe kwa dhamira. Kwa hiyo, japokuwa kama hivi tumekuwa mpaka tunafikisha 40 msaada haujatolewa, niwaombe sana wanasaikolojia, niwaombe sana asasi za kijamii, niwaombe sana wananchi wenyewe waziangalie hizi familia kwa sababu tunajua, maumivu yanapozidi mioyo ya binadamu huota kutu, hii kutu itakayoota janga lake ni kubwa zaidi. 

Kwa hiyo, tuwape msaada, tuwasikilize, na kama itawiwa Serikali si aibu kutoa huu msaada. Tunayo wizara ambayo ina maafisa ustawi wa jamii, ambayo ina wanasaikolojia, waende wakawape watu nafuu, wakawape watu ahueni kwa sababu hii ni kutu inajengeka kwenye mioyo ya watu.

Tunaweza tukalimaliza hili kwa miezi hii, lakini ile picha ya mtu kila siku kuona mwisho wa mpendwa wake haitamtoka. Haitamtoka kwa urahisi. Haitamtoka kwa bahati mbaya. Itamtoka pale tu ambapo huyu mtu atasaidiwa. 

Walioko hospitalini

Kwa hiyo, hilo lilikuwa suala la pili, na suala la tatu na la mwisho ni kwa wenzetu ambao mpaka leo wako hospitalini. Hatujuwi ni wengi kiasi gani ambao mpaka sasa wako hospitalini. Hatujui mazingira yao ambayo wako nayo huko hospitalini. Hatujuwi nani analipa gharama za hayo matibabu.

SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani? 

Kwa hiyo, kama kuna ambalo linaweza kufanywa kuhusu wale walioko hospitalini, ukiachia haya mambo ya kifedha, lakini hata pia kuwapa ahueni ya mawazo, kuwapa hiyo huduma ya kisaikolojia, ili hata ule uponyaji wao uwe wa haraka, tutakuwa tumewasaidia sana, sana, sana. 

Hatuwezi tukaendelea tu na maisha wakati kuna majeraha mengi, na majeraha mengi yako mioyoni, na majeraha mengi yako kwenye picha ambazo zimeingia kwenye kumbukumbu za watu. 

Kwa hiyo, hilo lazima lifanyike ili kuweza kuwapa ahueni wale waathirika. Haimaanishi kwamba tutaweza kuondoa machungu yao. Haimaanishi kwamba tutaweza kuwarudisha wapendwa wao waliopotea. Lakini angalau tutawasaidia kukabiliana na hali hizi, na kama jamii, tutaweza kutimiza wajibu wetu pia.

Nina hofu sana, sana, sana endapo kama taifa, kwa mara ya kwanza, tutawaachia waliofikwa na madhila haya, ya kuondokewa na wapendwa wao, kukabiliana na hali hii peke yao. 

Sisi kama Watanzania, kila siku tunasema msiba wa mmoja ni msiba wa wetu, kwamba mtu haalikwi msiba. Basi ni muhimu tuhakikishe kwamba wale waliotutangulia, wanafanya hivyo kwa heshima na kwa taratibu za dini na mila zetu.

Asanteni sana!

Mwandishi wa makala haya ameomba utambulisho wake usiwekwe hadharani. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×