The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Barua Kwa Wasanii wa Tanzania: Huwezi Kujiunga na Wawindaji na Kujidai Uko Upande wa Wawindwaji

Muna haki na msimamo wenu, endeleeni nayo, lakini wawindwaji pia wana haki na msimamo wao.

subscribe to our newsletter!

Wapende wasipende, wakati wa migogoro, mapambano au zahama, wasanii, kama watu maarufu wowote wengine – wanasiasa, viongozi wa dini, mainfluenza na wengine – hawawezi kujificha. Inabidi waamue wako upande gani, upande wa wenye mamlaka, au upande wa wasio na mamlaka, yaani upande wa wananchi. 

Na wananchi, wawe wapenzi wa wasanii au la, wataamua wawachukulie vipi wasanii hawa kutokana na maamuzi yao. Siyo Tanzania tu, bali popote duniani. Kwa mfano, huko Marekani, msanii Kanye West alipoteza washabiki wengi alipojitokeza kumwunga mkono Donald Trump. Kinyume chake, Cardi B alipoteza wengi alipomshambulia Trump. Na wengine wametamka waziwazi hawataki nyimbo zao zitumike kwenye kampeni zake.

Hali hii hujitokeza zaidi, kama nilivyosema, wakati kuna zahama au mpasuko ndani ya jamii. Tangu enzi na enzi wasanii wanaweza kugawanyika katika makundi mawili, waimba sifa za watawala, praise singers kwa kimombo au kwa lugha ya siku hizi, wachawa, na watetezi wa jamii au wakosoaji.  

Katika jamii nyingi za kale, watemi/wafalme/watawala walikuwa na watu wao ambao kazi yao ilikuwa kuimba sifa zao, hata kwa kutia chumvi hadi mdalasini na pilipili kichaa. Na wasanii hawa waliishi maisha ya raha mustarehe kwa kufanya hivyo maana walitunzwa na kuzawadiwa na mtawala wao. 

SOMA ZAIDI: Tukiruhusu Ukatili Utawale Tanzania, Tutawezaje Kuwa na Nchi ya Amani?

Mara nyingine walilazimika kutia chumvi hadi mdalasini na pilipili kichaa katika kuonesha kwamba wao ni wachawa kuliko wengine. Mashindano ya uchawa ni sheeedah! Hali hii ilioneshwa vizuri sana katika shairi la Hayati Jwani Mwaikusa, Noisy Praises (Sifa za Kelele) la miaka 50 iliyopita katika kitabu cha Summons.

I shout and scream your praisesCeaseless noisy praisesThat deafens the earsBlind the sight, destroy the brainAnd kill the sensesSo I am not aware of anythingBut song and screamAnd shouts and noisy praisesNapaza sauti na kupiga nyende nikikusifuSifa za kelele zisizoishaZinazofanya masikio yasisikie tenaMacho yasione, ubongo uharibikeNa hisi ziuliweHivyo sitambui kitu chochoteZaidi ya kuimba na kupiga nyendeNa kupaza sauti na sifa zenye kelele

Mwaikusa alitunga shairi hili miaka 50 iliyopita, lakini bado lina maana leo. Ili msanii aweze kukubalika na kumfaidi mtawala inabidi apaze sauti hadi akili yake na mwili wake viharibike na hata kufa. 

Inategemea na mtawala

Hata hivyo, bila shaka inategemea mtawala yukoje, na msanii yukoje pia. Si kila mtawala anapenda kusifiwa hivyo, maana anajua ni danganya toto tu. Na watawala wengine wanakana sifa hizi za kelele kwa kujua ni unafiki, maana hata kama kweli ni mtawala mzuri, yeye ni binadamu kama binadamu wengine, na si mungu mdogo. 

Ajabu ni kwamba watawala wanaokana sifa hizi mara nyingi ni walewale ambao wanastahili sifa zaidi maana kweli wanatawala vizuri na sababu mojawapo ya kutawala vizuri ni kutodanganywa na waimba sifa na badala yake kuwasikiliza wasioimba sifa.

SOMA ZAIDI:Kama Tanzania Ingekuwa Timu ya Mpira Unayoshabikia, Bado Ungeipongeza Hata Kama Inakosea? 

Ndiyo. Utawala mwingine, hata katika enzi za zamani zisizo na demokrasia, ulihakikisha kwamba sifa ziambatane na ukosoaji pia na kuonesha hali halisi inayofichwa na sifa za kelele. Ndiyo maana, kwa mfano, imbongi, waimba sifa wa watemi wa Kizulu, au griots wa Afrika Magharibi, walichanganya sifa na ukosoaji na waliheshimiwa zaidi kwa kufanya hivyo.  

Huko kwingine, watawala walihakikisha kwamba pamoja na waimba sifa, walikuwa na jesters pia: wachekeshaji ambao kazi yao ilikuwa kuonesha udhaifu, au makosa ya watawala, mara nyingine kwa njia ya kuchekesha.  

Na hawa jesters walilindwa hata kama walisema ukweli wa kufichua au kuumiza sana. Bila shaka hapa Tanzania, jamii nyingine zilikuwa na watu wa aina hii na nitashukuru kupewa mifano na wajuzi wa historia!

Namna mbilitatu

Sasa tatizo kwa hawa wanaoimba sifa tu linaonekana kwa namna mbilitatu.  Kwanza, mtawala huyu akianza kuchukiwa, mwimba sifa wake atachukiwa vilevile maana watu watamwona mnafiki anayejali tumbo lake tu badala ya kujali hali ya wananchi wenzao. Labda awe kama mwimba sifa wa Mwaikusa anayemaliza shairi lake hivi.

But take care, my dear noblemanOne day, my chords may fall apartAnd shout not moreThen there will be a resurrection of sensesAnd the whole world shall stareAt the nakedness of the ugly skeletonsIn your noble cupboardsLakini chunga sana lodi wangu mpendwaSiku moja, nyuzi sauti zangu zinaweza kusambaratikaNa kutopaza sauti tenaHapo hisi zitafufukaNa dunia nzima itakodolea machoUtupu wa mifupa ya kutishaKwenye kabati zenu za kilodi

Uchawa usiozingatia hali halisi unaweza kuwa na athari tatu. Moja ni kwamba chawa anachukiwa sawa hata na yule anayemchawia, maana anakuja kutambua kwamba anadanganywa.

SOMA ZAIDI:Watawala Tanzania Wana cha Kujifunza Kwenye Kisa cha Mfalme Henry II wa Uingereza na Askofu Thomas Becket 

Mbili, chawa anaweza kupata kichaa kwa namna fulani maana inabii apambane na nafsi yake inayojua kimoyomoyo kwamba anaimba unafiki. Kwa Kiingereza huitwa cognitive dissonance (hapa naomba msaada wa wataalam wa Kiswahili), yaani korongo kati ya anachoamini, au kusema, na hali halisi anayoiona. Tatu, chawa anaweza kuamka na kuimba zaidi hali halisi.

Upande wa pili, kuna wasanii ambao wanachagua upande wa wananchi na kutumia sauti zao kwa ajili ya wananchi. Katika utawala unaopendwa, inaweza kuendana na kuwasifia watawala pia na bado wananchi watawaona kuwa wako upande wao.  

Lakini kadiri korongo kati ya watawala na watawaliwa inavyozidi kuwa kubwa, msanii huyu anaweza kufurahiwa sana na watawaliwa, lakini kuchukiwa sana na watawala na hata kudhurika, kupotezwa, kunyimwa njia ya kujikimu au kushitakiwa kwa kuchafua sura ya mtawala. 

Lakini kihistoria, wanaodumu na sanaa yao hudumu hata baada ya kufa kwao ni hawa walioko upande wa wananchi maana wanaonekana kusema ukweli zaidi. 

Katikati ndio wako hawa kama imbongi wanaouma na kupuliza. Wanatumia nafasi yao kama waimba sifa kupenyeza ujumbe maalum kwa watawala wao.

Nafasi ya wasanii

Naamini suala la nafasi ya wasanii kihistoria inahusu mjadala uliopo kuhusu nafasi ya wasanii wetu kwa sasa. Wasanii wana haki kabisa ya kuimba sifa za watawala na chama chao na, kwa namna fulani, nawaheshimu zaidi wale wanaodai kwamba hawana haja ya kuomba msamaha, wao ni kijani damudamu na hawaoni kosa.  

SOMA ZAIDI:Kuna Uchaguzi, Uteuzi na Uchafuzi. Hapa Tanzania Tuna Nini? 

Nawaheshimu kuwa na msimamo ingawa nina wasiwasi juu ya cognitive dissonance yao.  Tangu wakijani wao watangaze kwamba “ushindi ni lazima” zaidi ya miaka 10 iliyopita, tumeona tabia ya kujisifia wanademokrasia kweli wakati misingi ya demokrasia inakanyagwa waziwazi na tunashuhudia matumizi ya ukatili na sasa hata uuaji dhidi ya wanaosimamia demokrasia. 

Lakini hawa wengine wananichekesha. Wanasononeeeeka kwa nini wamechukiwa.  Wanajitahii kudai kwamba ni waburudishaji tu, hawamo katika siasa, lakini pale wanapoamua kutumia sanaa zao panaonesha wana siasa gani, na hasa wanapoamua kuwadharau wenye msimamo tofauti.  

Wengine, hata wale wanaoishi maisha ya anasa kupindukia, wanadai kwamba wameimba pale kwa sababu wanahitaji kujikimu. Umwimbie anayekulipia. Na watawala wanakubali kabisa.  Pesa posa. Hivyo kweli wanalipwa lakini methali inasema huwezi kujiunga na wawindaji na kujidai uko upande wa wawindwaji. Haiwezekani.  

Na wawindwaji wakitambua hivi, huwezi kujitetea na kuwalazimisha wakupende au hata kusononeka kwa nini hawapendwi. Una haki na msimamo wako, endelea nayo, lakini wawindwaji pia wana haki na msimamo wao. Ndiyo hali halisi.  

Acheni kulia na amueni mko upande gani. Wakati wa mpasuko hakuna kujificha.

Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi. 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×